Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Tuesday 1 March 2016

APR VS YANGA MARA YA PILI LIGI YA MABINGWA, PAMBANO LA 8 LA DAIMA!


Na Daniel Mbega
MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga, watapambana na mabingwa wa Rwanda, Armée Patriotique Rwandaise (APR), katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufuzu raundi ya awali kwa ushindi wa jumla ya mabao 3-0 dhidi ya Cercle de Joachim ya Mauritius.
APR yenyewe imefuzu hatua ya awali kwa ushindi wa jumla ya mabao 4-2 dhidi ya mabingwa wa Swaziland, Mbabane Swallows. Mechi ya kwanza walifungwa ugenini bao 1-0, lakini Jumamosi, Februari 27, 2016 wakaichabanga timu hiyo mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Amahoro jijini Kigali.
Mechi ya kwanza baina ya APR na Yanga itachezwa mbele ya mashabiki 30,000 kwenye Uwanja wa Amohoro Machi 12, 2016 na inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na rekodi nzuri ya APR ya kufanya vizuri nyumbani.

Kwamba hiyo inaweza kuwa tiketi ya Yanga kubaki ama kuondoka mashindanoni ni suala la kusubiri kutokana na rekodi baina ya timu hizo mbili zenye uzoefu tofauti wa mashindano ya ndani na kimataifa.
Takwimu ambazo Fikra Pevu inazo zinaonyesha kwamba, hii itakuwa mara ya pili kwa timu hizo kupambana katika mashindano ya Afrika, hususan Ligi ya Mabingwa, lakini itakuwa mechi ya nane kuzikutanisha timu hizo katika mashindano yote.
Katika mechi saba zilizopita, timu zote zimeshinda mara tatu kila moja na kutoka sare mara moja.
Zilipokutana kwa mara ya kwanza kabisa kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati jijini Dar es Salaam mwaka 1996, APR ilishinda kwa penalty 4-2 katika hatua ya nusu fainali baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 katika muda wa kawaida.
Wiki mbili baadaye timu hizo zikapambana kwenye raundi ya awali ya Klabu Bingwa Afrika, ambapo mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam Yanga ilishinda kwa bao 1-0, lakini ziliporudiana mjini Kigali, APR ikashinda kwa mabao 3-0 na kusonga mbele. Raundi ya kwanza ilikoing’oa AS Bantous ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa jumla ya mabao 2-1 kabla ya kutolewa na Petro Atletico ya Angola kwa jumla ya mabao 3-2.
Tangu wakati huo timu hizo hazikubahatika kukutana tena hadi mwaka 2007 wakati wa mashindano ya Kombe la Kagame mjini Kigali ambapo zilipangwa Kundi A.
Katika mechi yao ya Januari 10, 2007, Yanga ilikubali kipigo cha bao 1-0 lililofungwa na Mwemere Ngiricodu katika dakika ya 10 ya mchezo.
Aidha, Julai 13, 2008 timu hizo zilikutana tena kwenye Kundi C la michuano ya Kombe la Kagame jijini Dar es Salaam ambapo safari hii zilitoka sare ya 2-2 huku mabao ya Yanga yakifungwa na Mrisho Ngassa (65) na Jerry Tegete (68) wakati ya APR yote yalifungwa na mlinzi Mbuyu Twite dakika za 15 na 77.
Mbuyu Twiye, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, hivi sasa ndiye beki tegemeo wa Yanga baada ya kujiunga na timu hiyo msimu wa 2010/2011.
Mwaka 2012 APR na Yanga zikapambana tena kwenye Kombe la Kagame, zikiwa Kundi C mjini Dar es Salaam, na safari hii Yanga ikashinda kwa mabao 2-0.
Timu hizo zilifanikiwa kufuzu hadi nusu fainali ambapo zilikutana tena uso kwa uso na kwa mara nyingine, Yanga ikashinda kwa bao 1-0 na kusonga mbele hadi kutwaa ubingwa wake wa tano wa Kagame.

Uzoefu
Ukizungumzia uzoefu na ukongwe, Yanga ndiyo kongwe zaidi na yenye mafanikio makubwa kwa ligi ya ndani na mashindano ya kimataifa kulinganisha na APR, ingawa mpira hauangalii umri.
Yanga iliyoanzishwa mwaka 1935 imetwaa ubingwa wa Tanzania mara 20 na ndiyo inayoongoza kwa kutwaa ubingwa huo mara nyingi zaidi kuliko klabu yoyote nchini Tanzania.
Lakini pia imetwaa Kombe la Nyerere (ndilo lililotumika kupata mwakilishi wa Kombe la CAF) mara nne.
Katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), vijana hao wa Jangwani wametwaa mara tano katika miaka ya 1975, 1993, 1999, 2011 na 2012, na mara tatu imeishia fainali katika miaka ya 1976, 1986 na 1992.
Hii ni mara ya 21 kuwania ubingwa wa klabu barani Afrika – mara 11 ilishiriki wakati mashindano hayo yakiitwa Klabu Bingwa Afrika (kati yam waka 1969 na 1996) na mara 10 tangu mashindano hayo yalipobadilishwa na kuitwa Ligi ya Mabingwa Afrika kati yam waka 1997 na sasa.
Katika miaka yote hiyo, hatua ya juu kabisa ambayo Yanga imefikia ni robo fainali mara tatu katika miaka ya 1969, 1970 na 1998, mwaka ambao ilikuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kucheza hatua ya makundi kabla ya Simba kuifikia hatua hiyo mwaka 2003.
Ilishiriki mara mbili Kombe la Washindi Afrika na hatua ya juu kabisa ilikuwa robo fainali mwaka 1995 ambapo uzembe ulisababisha itolewe na Blackpool ya Zimbabwe kwa kufungwa nyumbani mabao 2-0 licha ya kutoka sare ya 2-2 ugenini.
Aidha, ilishiriki mara mbili Kombe la CAF na safari zote iliishia raundi ya kwanza.
Baada ya Kombe la CAF kuunganishwa na Kombe la Washindi na kuitwa Kombe la Shirikisho , Yanga imeshiriki mara tatu na ikaishia hatua ya kati (Intermediate Round) mwaka 2007 ambapo kama ingeshinda ingeweza kushiriki hatua ya makundi (Robo Fainali) ya Kombe la Shirikisho baada ya kuwa imetolewa kwenye raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa ikiwa katika harakati za kutaka kucheza hatua ya makundi kwa mara ya pili.
Kwa upande wake, APR, timu ya Jeshi la Rwanda iliyoanzishwa mwaka 1993 (ina umri wa miaka 33 tu dhidi ya 81 ya Yanga) lakini imeweza kuzifunika timu kongwe kama Mukura Victory Sports iliyoanzishwa mwaka 1963, Kiyovu na Rayon katika mashindano ya ndani.
Maafande hao wametwaa ubingwa wa Rwanda mara 14 tangu mwaka 1995, halafu imetwaa Kombe la Rwanda mara 8.
Katika mashindano ya Kombe la Kagame, imetwaa ubingwa mara tatu katika miaka ya 2004, 2007 na 2010.
Kwa upande wa mashindano ya klabu za Afrika, APR inashiriki mara ya 13 na hatua ya juu Zaidi iliyowahi kuifikia ni raundi ya tatu mwaka 2004 kabla ya kutolewa na Enugu Rangers ya Nigeria kwa jumla ya mabao 3-1.
Mwaka 2003 ilifika nusu fainali ya Kombe la Washindi ambako ilitolewa na Julius Berger ya Nigeria kwa jumla ya mabao 3-2. Ilifungwa 3-0 ugenini, lakini ushindi wake wa mabao 2-0 nyumbani haukuweza kuivusha mbele ya Wanigeria hao ambao nao walishindwa kutwaa ubingwa mbele ya Etoile du Sahel ya Tunisia iliyoshinda kwa jumla ya mabao 3-2.
Katika raundi ya kwanza, APR ilianza kuisambaratisha US Kenya ya Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa jumla ya mabao 9-2, katika raundi ya pili ikaitoa Etoile du Congo ya Brazzaville kwa jumla ya mabao 5-1 na kwenye robo fainali ikaiondoa timu kongwe barani Afrika, Asante Kotoko ya Ghana, kwa faida ya bao la ugenini. Ilifungwa 2-1 ugenini, halafu ikashinda bao 1-0 nyumbani.
APR imeishia raundi ya kwanza mar azote mbili ilizoshiriki Kombe la CAF, na katika Kombe la Shirikisho iliishia raundi ya kati (intermediate) mwaka 2004.

Mabenchi ya ufundi
Linapikua suala la benchi la ufundi, APR imekuwa na rekodi ya kusikitisha ya kuondokewa na makocha, ambapo mwaka jana pekee iliondokewa na makocha wawili mfululizo, huku mmoja wao akiondoka bila kuaga.
Kwanza Ljubomir Ljupko Petrovic raia wa Bosnia aliondoka baada ya kukaa kwa miezi sita tu na nafasi yake ikachukuliwa na raia mwenzake wa Bosnia Dusan Dule Suljagic, ambaye licha ya kuisaidia kutwaa ubingwa, lakini aliondoka bila kuaga.
Lakini tangu aliyekuwa kocha msaidizi wakati huo, Emmanuel Rubona, alipochukua mikoba mwezi Septemba 2015 akisaidiwa na kipa mkongwe Jean Claude Ndoli, ameweza kuiongoza timu hiyo hadi hatua hii iliyofikia.
Timu hiyo inawategemea Zaidi wachezaji kama kipa Olivier Kwizera, walinzi Michael Rusheshangoga, Albert Ngabo, Emery Bayisenge, Ismael Nshutinamagara na viungo Migi Mugiraneza, Yannick, Hegman Ngomirakiza, Jean-Claude Iranzi na wengineo.
Kwa upande wa Yanga, bado inanolewa na Mholanzi Hans van der Pluijm (67) anayesaidiwa na Juma Mwambusi na Juma Pondamali.
Kikosi chake kiko vizuri hata kwenye ligi kikiundwa na wachezaji kama makipa Deogratius Munishi "Dida" na Ally Mustafa, walinzi Oscar Joshua Nkulula, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Vincent Bossou, Juma Abdul, nahodha Nadir Haroub, Salum Telela, Simon Msuva, Issoufou Boubacar Garba, Haruna Niyonzima, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Amissi Tambwe, SHaji Mwinyi, Malimi Busungu, Deus Kaseke, Paul Nonga na wengineo.
Kwa ujumla, mechi baina ya timu hizi ni ngumu kutabiri, ingawa Yanga wanatakiwa kuwa makini Zaidi na APR ambayo huwa haichagui uwanja wa kushinda. Ni kijeshijeshi tu!


CREDIT: FIKRA PEVU



No comments:

Post a Comment