Na Daniel
Mbega
MWISHONI mwa wiki
iliyopita, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo) Zitto Kabwe, kupitia mitandao
ya kijamii, alitoa taarifa kwamba Deni la Taifa la Tanzania kwa sasa limefikia
Dola 15 milioni ambazo ni zaidi ya Shs. 30 trilioni.
Kutokana na ukubwa wa deni
hilo, Zitto Kabwe anasema, Tanzania hulipa Huduma ya deni la taifa takriban
Shs. 2.2 trilioni kila mwaka, fedha ambazo ni nyingi kuliko hata bajeti ya
wizara yoyote nchini.
Lakini akasema kwamba, ndani
ya madeni hayo kuna ambayo yamepatikana kwa rushwa na mengine yamechukuliwa kwa
matumizi ya anasa tu, yaani ‘odious debts’.
Deni mojawapo la hovyo ni
la Dola 600 milioni (Shs. 1.2 trilioni) ambalo Tanzania ilikopa kutoka Benki ya
Standard ya Uingereza kupitia Hati Fungani (Bonds), mkopo ambao Taasisi ya
Serious Fraud Office (SFO) ya Uingereza imebainisha kwamba umepatikana kwa
rushwa huku taasisi nyingine ya Corruption Watch ya Uingereza pia ikisema
kwamba Tanzania imepata hasara ya Dola 80 milioni (Shs. 160 bilioni) kwa
kuchukua mkopo huo.
Alhamisi Juni 11, 2015 wakati akiwasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi yam waka 2014
na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2015/2016 bungeni mjini Dodoma, aliyekuwa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Dk. Marry Nagu, alisema
kwamba Deni la Taifa limekua kutoka Shs. 30.6 trilioni hadi kufikia Shs. 35.01
trilioni huku ongezeko hilo likitokana na riba, madeni mapya yaliyokopwa na
Serikali kugharamia ujenzi na ukarabati wa miundombinu hasa ya usafirishaji wa
nishati.
Lakini akasema licha ya deni
hilo kufikia kiasi hicho, utafiti na takwimu unaonyesha kiwango cha umaskini
vijijini kimepungua kwa asilimia 6.1, katika kipindi cha miaka mitano
iliyopita.
Hili linatia mashaka na
kuzua maswali mengi yasiyo na majibu kwa sababu kwa miaka nenda-rudi tumekuwa
tukielezwa kwamba deni la taifa ninaendelea kukua – halipungui.
Wanasiasa na wanaharakati
nchini Tanzania wamekuwa wakilizungumzia sana Deni la Taifa na wengine kwa
miaka kadhaa sasa wamelifanya kuwa mjawao ya agenda zao wanaonadi sera za vyama
vyao.
Ukiangalia ukubwa wa deni
hilo, kama wanavyosema wanasiasa, kwa Watanzania milioni 45 waliopo sasa, maana
yake kila mmoja anadaiwa Shs. 778,000!
Tanzania, kama zilivyo nchi
nyingi za Afrika na zinazoendelea, ni mtumwa wa madeni, lakini hivi ni kweli
tunadaiwa ama tumenyonywa?
Kwa sasa ni jambo la kawaida
kuona kwa nchi ya Kiafrika kuwa na mfadhili, mhisani, mwekezaji ama mdai hata
kama mfadhili ama mwekezaji huyo ndiye chanzo cha matatizo na umaskini kwa nchi
husika.
Kinachoonekana bora zaidi ni
kwa nchi hiyo tu kusifiwa kama mfano wa kuigwa wa mafanikio ya uchumi wa
uliberali mamboleo na hivyo kuendelea kupokea misaada zaidi, mikopo na
makubaliano mabaya katika mikataba ya ‘kimahaba’.
Na kwa kadiri inavyojikuta
imebanwa katika sera za kibepari, nchi hiyo yenye madeni makubwa, tegemezi, na
inayonyonywa kirahisi, itaendelea tu kuwa kipenzi cha Mataifa ya Magharibi!
Tunatambua kwamba dhana ya
deni la taifa inamaanisha idadi yote ya fedha zilizokopwa na Serikali kutoka
kwa wakopeshaji mbalimbali – wawe wakopeshaji wa ndani ama wa nje, wenye
masharti nafuu ama masharti ya kibiashara.
Mikopo hiyo hujazia kwenye
pengo la bajeti na wakati mwingine serikali zinakopa baada ya hao wanaojiita
wahisani kuamua kuchangia bajeti ama kutochangia kwa sababu wanazozijua wenywe,
kama walivyogoma wakati wa sakata la Akaunti ya Escrow. Huwezi kwenda
kuwashikia mtutu wa bunduki wakupe.
Hivi sasa Waafrika, nchi
zote zilizo kusini mwa dunia na watu wote wanapigania na kulilia maisha bora,
haki za kijamii, haki za kibiashara na siyo misaada ya kibiashara.
Hata hivyo, ni mara ngapi
tumewahi kuketi kutafakari na kuchambua mizizi ya matatizo yetu? Tumewahi kuhusisha
madeni haya makubwa na ufukara wetu? Je, tunatambua madhara ya madeni haya
katika maisha yetu kisiasa, kiuchumi na kijamii?
Tumeshawahi kufanya
ukaguzi wa madeni haya tunayodaiwa na kujiridhisha ni akina nani wanaotudai,
wanatudai kiasi gani, kwa ajili gani na kwa masharti gani? Madeni hayo ni ya
muda gani na riba yake ni kiasi gani? Nini siasa ya deni husika? Je, tunatambua
ni wakati gani msaada ama ruzuku inapokuwa deni? Hivi ni kweli tunadaiwa ama
tumenyonywa?
Katika miaka ya 1980 Rais
wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere aligomea mabadiliko ya uchumi
(Structural Adjustment Programme) yaliyohimizwa na Shirika la Kimataifa la
Fedha (IMF) na Benki ya Dunia kwa sababu aliona kile ambacho viongozi wetu wa
sasa hawakioni ama wanajifanya hawakioni.
Kwake yeye, mkakati wa IMF
na WB ulikuwa kutufundisha ubepari na kanuni zake za mchezo wa kukopa na
misaada. Kwa sasa wakubwa hao wanaketi wakiwa wameridhika kwamba mkakati wao
umefanikiwa na hata kama vyombo hivyo vitaondoka leo, havina hofu kwa kuwa bado
wanaye mrithi mwingine mbaya zaidi ambaye anaitwa Shirika la Biashara la Dunia
(WTO) ambalo ndani yake mataifa yote wanachama, makubwa kwa madogo, matajiri
kwa maskini, yanatazamwa kama yako sawa.
Kwa Mwalimu Nyerere,
ilikuwa wazi kwamba IMF na WB ndiyo majeshi mapya ya makabaila chini ya jina
jipya la utandawazi wa kibiashara, majeshi ambayo tofauti na wakati wa ukoloni
yalipotumia bunduki, dhahabu, vito na serikali kumiliki maisha yetu na kuchota
rasilimali zetu, sasa yanazitumia serikali zetu wenyewe na mashirika ya
kimataifa pamoja na mikopo na mitaji kama silaha yao ya kutudhibiti, kutunyonya
na kutukandamiza.
Wakati tunaelezwa kwamba
nchi yetu ina madeni makubwa – mengine yasiyolipika – lakini ni kwa kiasi gani
cha rasilimali ambacho kimechotwa isivyo halali barani Afrika, Tanzania
ikiwemo, kwa miaka yote na bado wanaendelea kutaka kuchota tu rasilimali hizo.
Mabadiliko ya tabia nchi
yaliyosababisha uhalibifu wa mazingira dunia nzima umefanywa na mataifa hayo hayo
makubwa kutokana na uchafuzi unaofanywa na viwanda vyao vinavyotegemea rasimali
zinazochotwa barani Afrika huku sisi tukipatwa na madhara hayo. Kitu gani
ambacho wametulipa kwa kusababisha uharibifu wa mazingira ambao katika sehemu
kubwa umetusababishia ukame na jangwa?
Hivi kwa umaskini
waliotuachia kwa kuchota rasimali zetu badala ya kutuendeleza wenyewe
tusimamie, na kwa madhara mengi waliyotusababishia, bado tunaendelea kusema
kwamba tunadaiwa? Kwamba fedha walizotupatia kama mkopo zinapaswa kuwa fidia kwa
rasilimali zetu walizozichota, wakati mwingine kwa kutumia viongozi wetu, hivyo
tunaweza kusema hatudaiwi!
Mwalimu Nyerere alisema
kwamba hatudaiwi na hatupaswi kulipa. Ndiyo maana alimwambia hata Nelson
Mandela asilipe deni la makaburu wakati alipoingia madarakani, siyo halali. Alimwambia
pia Laurent Kabila asilipe deni la Mobutu Seseseko! Ni makossa kulipa deni
haramu ambalo limewanufaisha wachache.
Wakati wa Mpango wa Kurekebishaji
Uchumi (SAP) mojawapo ya masharti yaliyowekwa na wakubwa wa IMF na WB ilikuwa
ni kuondoa ruzuku kwenye huduma za jamii na kilimo na ndipo gharama za
uchangiaji huduma za elimu, afya na kadhalika zilipoanzishwa.
Mwalimu Nyerere hakuamini
kwamba mikopo na misaada inaweza kutukomboa kiuchumi, badala yake aliona kwamba
ukombozi wa Mwafrika ulikuwa kwenye mawazo yake: kama tutapatiwa elimu katika
fani mbalimbali litakuwa suluhisho la kudumu hata kusimamia rasilimali zetu.
Ikiwa sisi ni maskini
licha ya kuwa na rasilimali zote hizi, basi hiyo inatokana na uwezo kielimu,
lakini pia kimawazo, maana tunaweza kusoma tukajaza makabati kwa shahada zetu,
lakini tusipobadilika kimawazo, bado tutaendelea kuwa wajinga na mwisho wake
tutaogelea katika lindi la utumwa-mamboleo.
Mataifa mengi yanakimbilia
Afrika kuja kuwekeza kwa sababu yanaelewa tunazo rasilimali. Wakubwa hao wako
tayari kutoa misaada hata ya vyandarua na vifaa vya kukusanyia taka kama
geresha tu huku wakichuma rasilimali zetu nyingi ambazo hazina idadi.
Afrika siyo maskini,
lakini imebatizwa jina la umaskini mpaka kwenye fikra zetu ili tuamini kwamba
hatuwezi kufanya jambo lolote kwa sababu ‘sisi ni maskini’.
Ili kuondoka na hilo, ni
vizuri viongozi wa Afrika na Waafrika kwa ujumla tuzinduke. Hao wanaokimbilia
kuja kuwekeza lazima tuwabane tuone sisi kama taifa tunanufaikaje, na kama
wanatupatia msaada, basi usiwe na masharti kwa sababu maendeleo waliyonayo huko
yametokana na rasilimali zetu wakati wao hawakutulipa fidia.
Ni kwa msingi huo ndiyo
maana ninaona kwamba sisi hatudaiwi, bali tumenyonywa vya kutosha na
wakatupumbaza kwamba ‘ni maskini’ ili waendelee kutunyonya huku wakitupatia ‘peremende’
kidogo kufanikisha unyonyaji wao.
Tukatae kuitwa wadaiwa
sugu kwa sababu deni hilo kimsingi hakuna anayelifahamu kwa kina na linazidi
kutufanya tuwe maskini kila siku.
Tunachopaswa kukifanya ili
kuepukana na ‘madeni’ hayo ni kuwajibika. Kwanza lazima serikali ya sasa
iyachunguze madeni yote ambayo Tanzania inadaiwa, kama yalipatikana kihalali
ama siyo kihalali, kama yalilenga kuhudumia wananchi ama kwa anasa za viongozi
kama tulivyoambiwa hapo juu.
Kauli mbiu ya Rais John
Magufuli katika ‘kutumbua majipu’ lazima ijikite huku kwenye deni la taifa kwa
sababu linawatesa wananchi wakati kumbe inawezekana limetokana na uzembe wa
viongozi au hata wamekopa kushibisha matumbo yao tu.
Kushindwa kufanya hivyo
hatari yake ni kwamba hata mapato yote ya ndani yanaweza kuishia kulipa madeni
na utafika wakati ambapo serikali itashindwa kuwahudumia wananchi katika elimu,
afya, maji na miundombinu kwa sababu fedha zote zitakuwa zikilipa madeni ya ‘anasa’.
Baada ya hapo lazima
tuweke mkazo katika kukusanya kodi, wajibu ambao ulisahauliwa na viongozi wetu
kiasi kwamba wapo wafanyabiashara ambao walikuwa kwenye fungate la muda mrefu
huku wakiingiza mabilioni ya fedha na serikali ikikosa mapato.
CREDIT: FIKRAPEVU
No comments:
Post a Comment