Sherehe ya makabidhiano ilifanyika shule ya msingi Kawawa iliyopo Kigogo Luhanga
Machi 22 2016 Dar es Salaam: Kampuni ya Tigo
Tanzania imetoa msaada wa madawati 500 yenye thamani ya shilingi milioni 82.5
kwenye shule kumi za msingi katika mkoa wa Dar es Salaam ikiwa ni mchango wa
kampuni hiyo katika kuisaidia serikali kukabiliana na upungufu wa madawati
katika shule za msingi nchini.
Akizungumza leo katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika
katika Shule ya Msingi Kawawa iliyopo katika kata ya Mabibo katika manispaa ya
Kinondoni, Mkurugenzi Mkuu wa Tigo Diego Gutierrez amesema mchango huo ni
sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya kampuni hiyo ya kuunga mkono jitihada
mbalimbali za kuleta maendeleo nchini.
“Mchango huu ni sehemu ya jitihada mbalimbali
zinazofanywa na Tigo katika kusaidia utekelezaji wa miradi yenye tija kubwa kwa
jamii. Tunaamini kwamba kupitia msaada huu, Tigo inatoa mchango wake katika kujenga
viongozi wa baadaye wa taifa hili na wanataluuma mbalimbali wakiwamo madaktari,
wahandisi na wengineo, "amesema Gutierrez.
Gutierrez amesema mwaka jana Tigo
ilikabidhi msaada kama huo wa madawati katika shule za msingi katika mikoa ya
Shinyanga, Mbeya Iringa na Morogoro na kuongeza kwamba kampuni hiyo itaendelea
kutoa madawati zaidi sehemu mbalimbali nchini siku za zijazo.
Makabidhiano yalihudhuriwa na Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda ambaye alisema madawati hayo 500 yataboresha
mazingira ya kujifunzia kwa watoto katika Mkoa wa Dar es Salaam na kutoa wito
kwa wadau wengine kuunga mkono zoezi hilo.
“Tunapenda
kutoa shukrani zetu za dhati kwa kampuni ya Tigo kwa kuwa mdau muhimu kwetu
katika jitihada zinazoendelea za kujaribu kupunguza tatizo la ukosefu wa
madawati ya kutosha katika shule za msingi za mkoa wetu wa Dar es Salaam. Ni dhahiri
kwamba msaada huu wa madawati 500 yatawawezesha mamia ya wanafunzi wetu kupata
sehemu za kukaa na hivyo kujipatia elimu zao katika mazingira bora zaidi,”
alisema Makonda.
|
No comments:
Post a Comment