Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (wa pili kulia) akitembea mitaani eneo
la Chake Chake Pemba, Zanzibar kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu usalama wao
katika kipindi cha uchaguzi kisiwani humo. Waziri Kitwanga ameambatana na Mkuu
wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mwanajuma Majid Abdullah (kulia), Mkuu wa Mkoa wa
Kaskazini Pemba, Omari Khamis Othman (wapili kushoto aliyevaa kaunda suti) na
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kusini Pemba, Ahmed Khalid Abdulla (kushoto, aliyevaa
tai. Kitwanga aliridhishwa na juhudi za kuimarisha ulinzi katika kisiwa hicho. Picha
zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga akizungumza na waandishi wa habari
(hawapo pichani) mara baada ya kuuzunguka msitu wa Taifa wa Ngezi, uliopo
Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba ambao baadhi ya watu wasioitakia
mema Zanzibar walisambaza taarifa za uongo kuwa kuna wakimbizi wamejificha
katika msitu huo baada ya kukimbia vurugu kisiwani humo. Hata hivyo hakuna
mkimbizi yeyote aliyekuwepo katika msitu huo na wananchi wapo katika makazi yao
wakiendelea na shughuli zao za kujitafutia kipato. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa
Kaskazini Pemba, Omari Khamis Othman. Kulia ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa
Kaskazini Pemba, Hassan Nasri. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kushoto) akizungumza na wauza nguo wa
Soko Kuu la mjini Chake Chake, Pemba. Wananchi hao walikuwa wanaendelea na
shughuli zao kama kawaida bila wasiwasi wowote. Waziri Kitwanga pia alisikiliza
maoni ya wananchi hao kuhusu uchaguzi mkuu na kuridhishwa na juhudi za kuimarisha
ulinzi katika kisiwa hicho. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (katikati) akizungumza na wajumbe wa
Kamati ya Ulinzi na Usalama, mjini Chake Chake, Pemba, kuhusu masuala
mbalimbali ya uimarishaji ulinzi katika kipindi cha uchaguzi unaotarajiwa kufanyika
Machi 20, 2016. Kushoto meza kuu ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mwanajuma
Majid Abdullah na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omari Khamis Othman.
Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga akimuuliza swali Mkazi wa Wawi, Chake
Chake Pemba, bibi Zabibu Mohamedi, wakati Waziri huyo alipokuwa anatembea
mitaani kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Machi
20, 2016. Hata hivyo wananchi hao walimuahkikishia kujitokeza kwa wingi kupiga
kura katika siku hiyo ya uchaguzi. Kulia
ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omari Khamis Othman. Picha na Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi
Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga akiwahoji wafanyakazi wa Bandari Kuu
ya Pemba kuhusu uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Machi 20, 2016.
Wafanyakazi hao walimuhakikishia kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo na
pia wananchi hao wapo salama na wanaendelea na shughuli zao zakujipatia kipato
za kila siku. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kulia) akiwauliza maswali wananchi wa
mjini Chake Chake, Pemba kuhusu jinsi walivyojiandaa na uchaguzi wa Machi 20,
2016 na kutoa maoni yao kama kuna tatizo lolote. Hata hivyo wananchi hao
walimuambia Waziri Kitwanga wanaendelea na shughuli zao kama kawaida, hakuna
vitisho vyovyote katika eneo lao. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi.
**************************************************************************
Kitwanga atembea mitaani
akichukua maoni ya wananchi Pemba, wananchi wasema hakuna vurugu, wanaendelea
na shughuli zao kama kawaida
Na Felix Mwagara wa MOHA
WAZIRI
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga amewataka wananchi wa Zanzibar
waondoe hofu kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu visiwani humo.
Akizungumza
mara baada ya kufanya mazungumzo na wananchi hao wakati alipokuwa anatembelea
mitaa mbalimbali ya Soko Kuu la mjini Chake Chake, Pemba aliwataka wananchi hao
waendelee na shughuli zao za kujipatia kipato kama kawaida na hakuna mtu
atakayewabughudhi kwani ulinzi umeimarishwa, na waachane na uzushi wa kutokea
vurugu unaoenezwa visiwani humo.
Waziri
Kitwanga alianza matembezi hayo mitaani mara baada ya kufanya mazungumzo na
Kamati ya Ulinzi na Usalama mjini Chake Chake ambapo walimuhakikishia kuwa,
Pemba yote ni salama na ulinzi umeimarishwa na hakuna atakaye fanyiwa vurugu
kwa mtu yeyote atakayefuata sheria.
Waziri
Kitwanga aliwataka wananchi hao kuondoa hofu wanapowaona askari mbalimbali
wakipita mitaani kwani wapo kwa ajili ya kuwalinda wananchi hao pamoja na mali
zao katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Machi 20 mwaka
huu.
“Musiwaogope
askari, na wala msiwe na wasiwasi, mnapowaona shangilieni kwani askari ndio
msaada wako kwa ajili ya usalama wako endapo inapotokea vurugu ya aina yoyote,
mtaenda kupiga kura salama na mtarudi salama, hakuna mtu wa kuwabughudhi,
msitishwe na mtu yeyote,” alisema Waziri Kitwanga na kufafanua;
“Leo
nazunguka mitaa mbalimbali ya hapa Pemba, lengo ni kuchukua maoni yenu pamoja na kuwaondolea
hofu wananchi na kuwahakikishia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimejipanga
vizuri kwa ajili ya kulinda usalama, hivyo jitokezeni kwa wingi siku ya
uchaguzi mkapigie kura kiongozi mnaemtaka.”
Hata
hivyo, Waziri Kitwanga alifanya ziara Mkoa wa Kaskazini Pemba katika msitu wa
Ngezi unaodaiwa kuwa kuna baadhi ya wakimbizi wamejificha katika msitu huo ili
kuokoa maisha yao baada ya kudaiwa kuwa kutatokea na vurugu.
Kitwanga
akiongozana na Wakuu wa Mikoa ya Kusini Pemba na Kaskazini Pemba pamoja na
maafisa wa Jeshi la Polisi Pemba, walienda katika msitu huo na kuukagua na
hawakukutana na mtu hata mmoja aliyejificha msituni humo kama inavyodaiwa na
kusambazwa habari na baadhi ya watu wasioitakia mema Zanzibar.
“Ndugu
waandishi wa habari, tumezunguka kwa pamoja kuungalia msitu huu, kuwatafuta hao
wakimbizi, hatujamuona mtu yeyote, ukisikia propaganda ndio hii, watu
hawaitakii mema Zanzibar na Tanzania kiujumla, mmeona kuwa habari hii ni ya
uongo, hakuna mkimbizi yeyote katika msitu huu kama tulivyoshuhudia wote kwa
ujumla,” alisema Kiwanga.
Aliongeza
kuwa, baadhi ya wananchi ambao wana mipango yao binafsi wanawatia hofu wananchi
kwa kutunga habari za uongo kuwa Zanzibar imechafuka, wakati habari hizo hazina
uhalisia wowote.
Hata
hivyo, wananchi wa Pemba walimuhakikishia Waziri Kitwanga wanafanya shughuli
zao za kuwapatia kipato kama kawaida na pia siku ya uchaguzi wataenda kupiga
kura kama kawaida kwani wanaamini amani itakuwepo kama ilivyokuwa sasa.
Waziri
Kitwanga alifanya ziara Zanzibar katika Kisiwa cha Unguja na kuzungumza na
Maafisa wa Jeshi la Polisi na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, na baadae
kumalizia ziara yake kwa kutembelea katika mikoa yote ya Pemba ikiwa ni hatua
ya kuangalia hali ya usalama visiwani humo katika kipindi hiki cha uchaguzi
mkuu katika maeneo hayo.
No comments:
Post a Comment