Mshambuliaji wa Yanga raia wa Uganda, Emmanuel Okwi alikuwa mwiba kwa Al Ahly timu hizo zilipocheza jijini Dar es Salaam mwaka 2014.
Na Daniel Mbega
MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga, sasa wanatafuta ‘dawa’
dhidi ya National Al-Ahly kwani ‘mzimu’ wa timu za Misri umeonekana kuleta
upepo mbaya kwa timu hiyo ya Jangwani, mtandao wa www.brotherdanny.com unaripoti.
Na ‘dawa’ hiyo haina budi kupatikana kabla ya Jumamosi, Aprili
9, 2016 wakati timu hizo zitakapopambana jijini Dar es Salaam kwenye mchezo wa
kwanza wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika ili kuwania kufuzu kwa
hatua ya makundi inayoweza kuwafanya wakwa mabilionea.
Wakati Yanga inatafuta nafasi ya kucheza kwa mara ya nne robo
fainali na mara pili hatua ya makundi ya michuano hiyo tangu iliposhiriki mwaka
1998, Al Ahly wao wanausaka ubingwa wao wa tisa na kuzidi kujikita kileleni mwa
timu bora za Afrika.
Yanga imefanikiwa kuitoa APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2
baada ya kufunga 1-1 jijini Dar es Salaam Jumamosi Machi 19, 2016 huku ikiwa
imeshinda 2-1 ugenini wiki moja iliyopita.
Al Ahly wao wameitoa CRD Libolo ya Angola kwa kuwafunga mabao
2-0 jijini cairo baada ya mechi ya kwanza kuwa na matokeo ya sare tasa.
mtandao wa www.brotherdanny.com unatambua kwamba, mara ya mwisho kwa Yanga kukutana uso kwa macho na Al Ahly
ilikuwa mwaka 2014 katika raundi ya kwanza ya michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa
ambapo mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam Machi Mosi, Yanga ilishinda bao
1-0 lililopachikwa na nahodha Nadir Haroub Canavaro katika dakika ya 82, hii ilikuwa
ndiyo mara ya kwanza kabisa kuifunga timu hiyo kutoka Misri.
Hata hivyo, ziliporudiana mjini Alexandria Machi 9, Yanga
ikafungwa 1-0, hali iliyolazimu zipigiane mikwaju ya penalti ambapo Yanga
ikatolewa kwa 4-3. Said Bahanuzi na Mbuyi Twite ndio waliokosa penalti kwa Yanga
na Al Ahly ilikuwa haina haja ya kumalizia penalti yake ya mwisho.
Katika raundi ya awali Yanga ilikuwa imeitoa Komorozione ya
Comoro kwa jumla ya mabao 12-2.
Historia ni mwalimu mzuri, lakini siyo kwa Yanga, hasa
linapokuja suala la kukutana na timu kutoka Misri.
Rekodi ambazo www.brotherdanny.com inazo zinaonyesha kwamba, safari hii itakuwa mara ya nane kupangwa na timu za Misri,
lakini hii itakuwa mara ya tano kwa Yanga kukutanishwa na Al Ahly.
Katika mechi 14 zilizopita dhidi ya timu za huko, Yanga
imeshinda mechi moja tu, imetoka sare tano na kufungwa mechi nane, huku
ikifunga mabao 8 na kupachikwa 29.
Lakini kwa upande wa mechi dhidi ya Al Ahly, Yanga imecheza
mara nane, ikishinda moja, kutoka sare mara mbili tu, zote nyumbani, na
kupoteza mechi tano. Kati ya mechi hizo nane imefungwa mabao 19-5!
Kwa bahati nzuri au mbaya, timu hiyo ya Jangwani imepambana na
timu tatu tu za Misri katika historia yake –Al Ahly, Ismaily na Zamalek.
Imewahi kucheza na Ismaily kwenye Klabu Bingwa Afrika mwaka
1992, lakini ikafungwa nyumbani 2-0 na kulazimisha sare ya 1-1 mjini Ismailia.
Mwaka 2000 Yanga ilifungwa mabao 4-0 kule Cairo na Zamalek baada
ya kuwa imelazimisha sare ya 1-1 mjini Dar es Salaam katika Kombe la Washindi,
na mwaka 2012 ikalazimisha pia sare ya 1-1 mjini Dar es Salaam dhidi ya Zamalek
kabla ya kuchapwa bao 1-0 jijini Cairo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Rekodi za Yanga dhidi ya Al Ahly zinaonyesha kwamba, kwa mara
ya kwanza timu hizo zilikutana mwaka 1982 kwenye Klabu Bingwa Afrika.
Baada ya Yanga kuitoa Textil Pungue ya Msumbiji katika raundi
ya kwanza kwa jumla ya mabao 4-1 (ikishinda 2-1 ugenini na 2-0 nyumbani), ikakabiliana
na al Ahly ambapo ilikubali kipigo cha mabao 5-0 mjini Cairo na ziliporudiana
mjini Dar es Salaam ikatoka sare ya 1-1.
Mwaka huo Al Ahly iliendelea hadi kutwaa ubingwa huo ambapo
kwenye robo fainali iliitoa Green Buffaloes ya Zambia kwa mabao 3-2, katika
nusu fainali ikaifungashia virago Enugu Rangers ya Nigeria kwa jumla ya mabao
4-1 na kwenye fainali ikatandika Asante Kotoko jumla ya mabao 4-1 pia.
Mwaka 1988
Yanga ikakumbana na Al Ahly katika raundi ya kwanza ya michuano hiyo ya Klabu Bingwa
Afrika, ambapo zilitoka suluhu mjini Dar es Salaam na ikafungwa 4-0 Cairo.
Al Ahly
ikaendelea kuifunga Nakivubo Villa SC ya Uganda kwenye raundi ya pili jumla ya
mabao 6-3, kwenye robo fainali ikaitoa Matchedje ya Maputo Msumbiji kwa jumla
ya mabao 2-1 kabla ya kuutema ubingwa wake kwa Entente Setif ya Algeria kwa
mikwaju ya penalti 4-2. Kwanza ilifungwa mabao 2-0 mjini Algeiers, lakini
ikapata ushindi wa mabao 2-0 nyumbani.
Mwaka 2009
Yanga ilipangwa na Al Ahly katika raundi ya kwanza ambapo ilifungwa jumla ya
mabao 4-0. Ilifungwa ugenini 3-0 na ikafungwa 1-0 nyumbani.
Lakini ulikuwa
mwaka mbaya kwa Al Ahly kwani ilitolewa na Kano Pillars ya Nigeria kwa sharia ya
bao la ugenini baada ya matokeo ya jumla kuwa 3-3. Zilitoka sare ya 1-1 mjini
Kano, ziliporudiana zikafungana 2-2.
Katika raundi
ya tatu ya Kombe la Shirikisho ambako iliingia baada ya kutolewa kwenye Ligi ya
Mabingwa, Al Ahly pia ikatolewa kwa penalty 6-5 na Santos FC ya Angola. Kwanza ilishinda
3-0, halafu ikafungwa 3-0 mjini Luanda.
Mara ya nne
kwa Yanga na Al Ahly kukutana ilikuwa mwaka 2014, kama ilivyoelezwa hapo juu,
na sasa mashabiki wanasubiri kuona ni dawa gani inayofaa kuuondoa mzimu wa timu
za Misri kwa Yanga, ambazo zimekuwa kikwazo katika mafanikio kwenye mashindano
hayo ya klabu za Afrika.
Rekodi ya Yanga katika michezo ya kimataifa hairidhishi wala
kufurahisha. Ni mara tatu tu katika historia yake imewahi kufanya vizuri –
mwaka 1969 ilipotolewa na Asante Kotoko kwa shilingi, na mwaka 1970 ilipofungwa
2-0 na Kotoko kwenye Uwanja Huru mjini Addis Ababa baada ya kutoka sare mechi
zote mbili. Mara zote mbili timu hiyo ilitolewa kwenye robo fainali.
Mara ya tatu ilikuwa mwaka 1998 wakati kikosi kilichoundwa na
akina Edibily Lunyamila kilipofanikiwa kufuzu katika hatua ya makundi (robo
fainali) ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ukiacha kiwewe cha kutofanya vizuri kwenye mechi za kimataifa,
Yanga kwa ujumla imekuwa na mkosi mbele ya timu kutoka Afrika ya Kaskazini.
Haina kabisa na siyo suala la ushabiki wala kukosa uzalendo.
Iwe kwenye michuano ya Afrika ama ile ya Afrika Mashariki na
Kati, timu hiyo daima huwa haitambi mbele ya timu kutoka Sudan, Sudan Kusini,
Misri, Tunisia, Libya au Morocco ambazo imewahi kukumbana nazo.
Kati ya mechi 35 ilizocheza na timu kutoka ukanda huo, Yanga
imeshinda mechi sita tu, ikilazimisha sare 14 na kufungwa 15! Katika mechi zote
hizo imefunga mabao 26 huku ikibugizwa mabao 54.
No comments:
Post a Comment