Na Mwandishi Wetu
YANGA
inajitupa uwanjani leo hii kukabiliana na mabingwa wa Rwanda, APR, katika mechi
ya marudiano ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa ambayo inaonekana kama ni
vita.
Mechi hiyo
itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ina mvuto wa aina yake
kutokana na rekodi baina ya timu ikichangiwa pia na matokeo yaliyopita.
Katika mechi
yao ya kwanza jijini Kigali, Yanga ilishinda mabao 2-1 Jumamosi iliyopita,
matokeo ambayo yamewaweka katika nafasi nzuri zaidi kwa kuwa sasa inahitaji
sare tu ili isonge mbele.
Blogu ya brotherdanny.com inafahamu kwamba,
endapo Yanga itavuka hatua ya sasa, itakutana na Al Ahly ya Misri ambayo nayo
inapigana leo Ijumaa kutaka ivuke ikihitaji ushindi dhidi ya CRD Libolo ya
Angola baada ya kutoka suluhu mjini Luanda.
Lakini Azam
FC, ambayo inaiwakilisha Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho, nayo iko kwenye
nafasi kubwa ya kufuzu baada ya kuichapa Bidvest Wits ya Afrika Kusini kwa
mabao 3-0.
Azam itacheza
Jumapili hii na ikivuka hapo itakutana na Esperance de Tunis ya Tunisia ambayo
leo hii iko nyumbani kucheza na Renaissance ya Chad ikiwa na ushindi wa mabao
2-0 mkononi.
Wawakilishi
wa Zanzibar, JKU hawana uhakika wa kuonyesha maajabu baada ya kufungwa mabao 4-0
jijini Kampala na SC Villa.
Uhakika wa
kufanya vizuri kwa klabu za Afrika Mashariki umebaki kwa Yanga, Azam na Polisi
ya Rwanda na Villa ya Uganda, ingawa APR nayo ina uwezo wa kuyageuza matokeo
yake na Yanga.
Polisi
Rwanda ilitoka suluhu ugenini kwa Vita Club Mokanda ya Congo na inapocheza
nyumbani wikiendi hii inahitaji kuutumia vyema uwanja wa nyumbani kupata
ushindi.
Mabingwa wa
Burundi, Vital’O walikubali kipigo cha mabao 5-1 mjini Aba, Nigeria mbele ya
Enyimba na sasa wana kazi ngumu ya kupata ushindi wa mabao 4-0 mjini Kigali.
Kwenye Kombe
la Shirikisho, Atletico Olympic ya Burundi haina matumaini makubwa baada ya kufungwa
nyumbani mabao 2-0 na CF Mounana ya Gabon.
Katika
matokeo mengine, St. Georges ya
Ethiopia inaweza kufanya maajabu ikiwa itaitoa bingwa mtetezi TP Mazembe ya
Congo DR baada ya kufungana mabao 2-2 Addis Ababa.
Al-Merreikh
ya Sudan ilishinda ugenini 1-0 dhidi ya Warri ya Nigeria, na inahitaji sare au
ushindi nyumbani ili isonge mbele, matokeo ambayo hata Zamalek ya Misri inayahitaji
baada ya 1-0 ugenini kwa Union Douala ya Cameroon.
Ferroviario
Maputo ya Misri, ambayo ilipita moja kwa moja kwenye raundi ya kwanza, ina
kibarua ya kushinda kwa zaidi ya bao 1-0 dhidi ya AS Vita Cub ya Congo DR baada
ya kufungwa bao 1-0 mwishoni mwa wiki.
ZESCO ya
Zambia inakwenda Conakry, Guinea kutafuta hata sare tu dhidi ya Horoya baada ya
kushinda 4-1 nyumbani kama ilivyo kwa Wydad Casablanca ya Morocco ambayo
iliikung’uta CNaPS ya Madagascar mabao 5-1.
Mamelodi
Sundowns ya Afrika Kusini ilishinda 2-0 dhidi ya Leopard ya Congo Brazzaville
na wikiendi hii inahitai kukomaa ugenini ili isonge mbele kama ilivyo kwa Stade
Malien ya Mali ambayo ilipata ushindi kama huo nyumbani dhidi ya Cottonsport
Garoua ya Cameroon.
Ushindani
mkubwa uko katika klabu nne; Olympique Khouribga ya Morocco dhidi ya Etoile
Sahel ya Tunisia; na Etoile du Congo dhidi ya Etente Sportif de Setif ya
Algeria. Matokeo ya mechi zote hizo wiki iliyopita yalikuwa 1-1.
Kaizer
Chiefs ya Afrika Kusini ilipoteza nafasi nyumbani iliporuhusu bao 1-0 mbele ya
ASEC Mimosas ya Ivory Coast, sasa inahitaji kukaza buti ugenini wikiendi hii.
Ingawa
ilishinda 1-0 nyumbani, lakini Club Africain ya Tunisia inahitaji kugagamala
ugenini kwa MO Bejaia ya Algeria kama ilivyo kwa Al Ahly Tripoli ya Libya
iliyopata ushindi kama huo nyumbani na sasa itakuwa ugenini kukabiliana na Al-Hilal
ya mjini Omdurman, Sudan.
Katika Kombe
la Shirikisho kunaonekana kuwa na kazi kubwa licha ya ukweli kwamba hakuna timu
zilizotoka sare mwishoni mwa wiki.
MC Oran ya
Algeria ilishinda 2-0 nyumbani dhidi ya Sporting Gagnoa ya Ivory Coast kama
ilivyofanya ENPPI ya Misri, ambayo hata hivyo yenyewe ilishinda ugenini kwa Africa
Sports huko Abidjan.
Don Bosco ya
Congo DR inahitaji ushindi wa mabao 2-0 kusonga mbele baada ya kufungwa 3-1
ugenini kwa Misr Elmaqasah ya Misri.
Al-Ittihad
ya Libya ilishinda 1-0 dhidi ya Medeama ya Ghana, Nasarawa ya Nigeria ilipata
ushindi kama huo dhidi ya Constantine ya Algeria, Sagrada ya Angola nayo
ikapata ushindi huo huo dhidi ya LD Maputo ya Msumbiji na sasa timu hizo
zinatakiwa kufanya jitihada vinginevyo vibao vinaweza kugeuka zitakaocheza
ugenini mwishoni mwa wiki.
Zanaco ya
Zambia ina nafasi nzuri kwa ushindi wake wa ugenini wa mabao 2-1 dhidi ya
jirani zao Harare City ya Zimbabwe, lakini Kawkab Marrakech ya Morocco wao
wanakwenda kifua mbele kwani walishinda 3-0 nyumbani didi ya Barrack Young
Controllers II ya Libya.
St Eloi
Lupopo ya Congo DR ilishinda 2-1 dhidi ya Ahli Shendi ya Sudan, Stade Gabesien
ya Tunisia nayo ikaifunga Kaloum Star ya Guinea 2-1 nyumbani, matokeo ambayo
yanawaweka katika hatari ikiwa wataruhusu bao 1-0 watakapocheza ugenini.
No comments:
Post a Comment