Timu ya Gor Mahia kutoka Kenya imeilaza AL Khartoum ya Sudan 3-1 na kufuzu kwa fainali ya mchuano wa Kagame kwa vilabu vya soka kanda ya Afrika Mashariki na kati CECAFA inayoendelea mjini Dar es Salaam Tanzania.
Al Khartoum iliwatia mashabiki wa Gor wasiwasi baada ya kutangulia kutikisa wavu wa mabingwa hao kutoka Kenya kwa bao la dakika ya kwanza kupitia Ibrahim El Mani.
Mfungaji matata, Michael Olunga alikuwa tegemeo la Gor Mahia kwa mara nyingine baada ya kuisawazishia Ko’galo katika dakika ya 24 kupitia mkwaju wa penalti na kufikisha idadi yake ya magoli hadi matano.
Baadaye mshambulizi huyo alimuandalia pasi safi Innocent Wafula ambaye aliiweka Gor kifua mbele.
Katika dakika ya 55, Meddie Kagere alifunga kwa kichwa baada ya mkuki wa michael Olunga kurejeshwa na mabeki wa Al Khartoum.
Mashabiki wa Gor Mahia waliofurika katika uwanja wa kitaifa wa Dar es Salaam waliinuka kwa shangwe kusherekea uongozi huo wa mabao matatu.
Kocha wa Gor Mahia, Frank Nuttal, alieleza kufurahishwa na matokeo hayo na kufuzu kwa fainali bila kupoteza mechi.
Aiodha aliwapongeza wachezaji wake kwa uhodari wao.
‘’Tumefanya maandalizi mazuri, na tunafurahi sana kufuzu kwa fainali bila kushindwa. Nawapongeza wachezaji wangu,’’ alieleza.
Gor imefuzu kwa fainali hizo kwa mara ya kwanza tangu 1985.
Ingawa pande hizo zilikutana katika mechi ya makundi, zilitoka sare ya bao moja.
Gor, licha ya kuwa katika kundi moja na Yanga na Al Khartoum, ilirekebisha makosa yake ya kuondolewa kutoka hatua hiyo msimu uliopita kwa kumaliza katika nafasi ya kwanza katika kundi lake.
Kabla ya shindano la CECAFA, Gor Mahia ilikumbwa na matatizo ya kifedha huku timu hiyo ikiwategemea wasamaria wema kuhakikisha wamesafiri hadi Dar Es Salaam kushiriki mchuano huu.
CREDIT: BBC
No comments:
Post a Comment