Kikosi cha Yanga cha mwaka 1973 hapa wanaonekana Meneja wa timu Shiraz Sharrif, Kocha Victor Stanculescu (kabla hajaondoka), Hassan Gobbos, Kitwana Manara, Maulid Dilunga, Sunday Manara, Muhidin Fadhil, Boi Iddi 'Eickens', Suleiman Said Sanga 'Totmund Wanzuka', Gibson Sembuli, 'Mwamba' Omar Kapera, Athumani Kilambo na nahodha Andulrahman Juma.
Na DANIEL MBEGA
KWA
ujasiri wake wa kuwabana washambuliaji, wapenzi wake walipendelea kutanguliza
neno 'Mwamba' kila walipomtaja. Si mwingine bali ni Omari Mohammed Kapera,
mzaliwa wa Temeke, mjini Dar es Salaam mwaka 1947, aliyekuwa 'akiushika mkoba'
wa Yanga, yaani beki nambari tano.
Mara yake
ya kwanza kabisa kuonekana akiiwakilisha Young Africans ilikuwa mwaka 1965 huko
Unguja. Huo ulikuwa mchezo wa sherehe za Pasaka baina ya Yanga na wenyeji wao
African Sports ya Zanzibar, timu ambazo zilikuwa na kawaida ya kutembeleana
kila mwaka inapofikia sikukuu ya Pasaka. Siku hiyo aliingia uwanjani akiwa
amevalia jezi nambari 3. Hadi nusu ya kwanza ilipomalizika Yanga walikuwa nyuma
kwa mabao 2-0. Kipindi cha pili kilipoanza kocha Billy Bandawe (wakati huo)
alimbadili Mwamba Kapera kutoka nafasi ya beki nambari 3 hadi nambari 5.
Ilisaidia.
Kwani aliweza kumkabili senta-fowadi wa African Sports aliyesababisha mabao
hayo mawili asilete tena madhara langoni mwa Yanga. Kipenga cha mwisho
kilipopulizwa matokeo yalikuwa African Sports 2 Yanga 2. Tangu wakati huo mpaka
walipostaafu kucheza soka ili kuwapa vijana chipukizi nafasi, jezi nambari 5
haikumbanduka.
Historia
ya Omari Kapera, ambaye baadaye alishika wadhifa wa Afrisa Michezo wilaya ya
Ilala, haitofautiani sana na mwanasoka yeyote yule. Kama kawaida alianza
kucheza chandimu utotoni mwake na watoto wenziwe. Chandimu, kama mnavyofahamu
kila siku wachezavyo watoto mitaani, hutumia mpira wa matambara uliofungwa
fungwa kwa kamba, uwanja usio na kipimo maalum, hasa hutegemea wingi wa
wachezaji, na magoli ya mawe. Wakati mwingine mwamuzi huwa ni giza, au wakati
mwingine huwa ni mwenye mpira, ambaye kama atanyimwa namba, au atakanyagwa ama
atazuiwa asipachike bao, basi atauweka mpira wake kwani na kuondoka nyumbani.
Huo ndio mwisho wa mchezo!
Kadiri
siku zilivyosonga mbele ndivyo Omari Kapera alivyozidi kuupenda mchezo wa
kandanda. Mnamo mwaka 1962 alipotimu miaka 15 na kupata kimo cha kutosha
alianza kucheza mpira wa kikubwa. Alijiunga na timu ya African Temeke, moja ya
timu maarufu jijini Dar es Salaam enzi hizo ambayo ilitoa wanasoka wengi kwenda
Young Africans. Aliichezea African Temeke kwa miaka miwili akiwa beki wa
kutumainiwa sana, ambaye kukosekana kwake kulileta wasiwasi miongoni mwa
wachezaji wenzake na mashabiki wa timu hiyo.
Wapinzani
wakubwa wa African Temeke walikuwa Good Hope pia ya Temeke, ambayo ilitoa
wanasoka wengi kwenda Sunderland enzi hizo. Timu hizo mbili zilikuwa mikondo ya
Young Africans na Sunderland (sasa Simba). Idadi kubwa ya wachezaji waliojiunga
na African Temeke enzi hizo walikuwa wakiandaliwa kujiunga na Young Africans na
wale wa Good Hope walikuwa wakiandaliwa kujiunga na Sunderland.
Mwaka 1964
Omari Kapera aliihama African Temeke na kujiunga na African Boys iliyokuwa timu
B ya Young Africans. Baada ya mwaka mmoja uongozi wa Young Africans kwa kutilia
maani maendeleo mazuri ya mwanasoka huyo, uliamua kumsajili kwenye kikosi
kamili cha Yanga. Mchezo uliochezwa kati ya Young Africans na African Sports ya
Zanzibar mjini Unguja wakati wa sikukuu ya Pasaka mwaka 1965 ulikuwa wa
majaribio kwake.
Aliwasifu
sana makocha Patrick Mandawa, Billy Bandawe, Maalim Tumu na Profesa Victor
Stanculescu wa Romania ambao walimfundisha katika nyakati mbalimbali enzi zake,
ambapo alisema kwamba, bila wao asingeweza kupata mafanikio kama aliyoyapata.
Mwaka 1966
ulikuwa wa mafanikio makubwa kwa Omari Kapera katika ulimwengu wa kandanda.
Kwanza alipata uthibitisho wa kuwa mchezaji wa kudumu wa Young Africans, timu
aliyoichezea hadi mwaka 1975 ulipotokea mgawanyiko mkubwa. Kuanzia mwaka huo
alichaguliwa katika timu ya Kombaini ya Dar es Salaam na timu ya Taifa
alizozichezea mfululizo hadi mwaka 1973 akivalia jezi yake ya kawaida nambari
5.
Akitoa
maoni yake kuhusiana na kushindwa mara kwa mara kwa timu ya taifa, Taifa Stars,
mwanasoka huyo wa zamani alisema kuwa iko haja ya kuweka msingi bora wa soka
toka mashuleni na kuwahamasisha vijana chipukizi ambao ndio nyota wa baadaye.
Alisema kwamba zamani kulikuwa na michuano ya kila mwaka kwa shule za msingi na
sekondari, ambayo inaendelea mpaka sasa. lakini tofauti na zamani ambapo
viongozi husika walikuwa wakitilia maani sana vipaji vya wachezaji katika
mashindano hayo, hivi sasa mashindano hayo yametelekezwa ambapo hakuna shule
hata moja yenye vifaa vya michezo na hivyo mashindano yenyewe kukosa msisimko.
Baadhi ya
wachezaji walioanzia kwenye mashindano ya mashule na kuja kuwa nyota wa taifa
baadaye aliwataja kuwa ni kipa wa zamani wa Sunderland Mbaraka Salum Magembe,
Maulid Dilunga, Abdulrahman Juma, Hassan Gobbos, Kitenge Baraka na wengineo
wengi.
Michezo
ambayo haijafutika katika kumbukumbu zake ni ule Yanga ilipowaadhibu watani wao
wa jadi Sunderland kwa mabao 5-0 Juni Mosi, 1968; Kipigo walichokipata Taifa Stars
mbele ya Uganda Cranes cha mabao 4-1 katika michuano ya Kombe la Chalenji kwa
nchi za Afrika Mashariki na Kati mwaka 1970 huko Zanzibar; na Yanga ilipotoka
suluhu na Enugu Rangers mjini Lagos, Nigeria kabla ya kutoka sare ya bao 1-1
mjini Dar es Salaam katika mchezo wa Klabu Bingwa Afrika mwaka 1975.
Kwa
wachezaji wa enzi zake aliwasifu Gilbert Mahinya 'Mashine' na Leodgar Tenga
ambao alisema kwamba walimsaidia sana kiuchezaji. "Gilbert nilimhusudu
kutoka na uwezo wake wa kucheza idara zote kwa nguvu moja, na Tenga alinipa
raha hasa tulipokuwa tukitumia mtindo wa 'double centre-half'," alisema
Mwamba Kapera.
Kwa
wachezaji waliotamba hadi miaka ya 1980 alimsifu sana Mohammed 'Adolf' Rishard
aliyeanzia Young African Kids chini ya kocha Victor Stanculescu akapanda hadi
kikosi cha kwanza cha Yanga akicheza na Kapera mwenyewe na kisha kuichezea Pan
Africans pamoja na timu ya Taifa, Taifa Stars, Tanzania Bara na timu ya mkoa wa
Dar es Salaam (Mzizima United).
Nchi
ambazo mwanasoka huyo aliwahi kuzitembelea enzi zake akiwa mchezaji ni pamoja
na Kenya, Uganda, Ghana, Nigeria, Guinea, Sierra Leone, Somalia, Madagascar,
Seychelles, Sudan, Misri, Brazil na Romania.
WASILIANA
NAME SIMU/WHATSAPP/TELEGRAM 0656 331974
No comments:
Post a Comment