Na Hastin
Liumba,Usinge
MBUNGE wa viti maalumu chama cha wananchi (CUF) Magdalena
Sakaya amesema atachukua fomu kugombea jimbo la Urambo Magharibi wilayani
Kaliua mkoa wa Tabora.
Kauli hiyo aliitoa kwenye mkutano wa hadhara wakati akiongea
na wananchi wa kata ya Usinge wilayani Kaliua.
Sakaya alisema kikubwa kinachomsukuma kugombea ubunge wa
jimbo hilo kunatokana na hali mbaya kiuchumi na huduma za kijamii ambazo
kimsingi anaona wananchi wametelekezwa.
Aidha kingine kilichomsukuma ni unyanyasaji unaofanywa kwa
wananchi jamii ya wafugaji na kusema baadhi ya viongozi wamekuwa wakitumia
wafugaji kama mtaji wao huku wakiwatukana wafugaji kuwa ni ‘Manyani’.
Alisema licha ya hayo bado huduma za maji na afya ni mbovu
kwa kiasi kikubwa na zaidi kinamama wajawazito wamekuwa wakipoteza maisha kwa
kukosa huduma nzuri za afya ikiwemo upungufu wa watalaamu wa afya.
Sakaya alisema kwa wilaya ya Kaliua kuna zahanati na vituo
vya afya 34 na watalamu wa afya wako 44 tu hali ambayo inatia uchungu na zaidi
kina mama wajawazito wamekuwa wakitamka wakifikia hatua ya kujifungua wanapata
mawazo kwa kukosa huduma.
Alisema kingine ni hali mbaya waliyonayo wakulima hasa wa
tumbaku na kuongeza wengi wao hadi sasa hawajalipwa malipo yao na kufikia hatua
mabenki wameshindwa kuwakopesha kwa kukosa sifa.
Mbunge huyo anasema licha matatizo hayo bado kumekuwa na
viongozi ambao wanawagawa wananchi kwa ukabila na udini.
Alisema kiwango cha kugawa wananchi kwa ukabila na udini
kimekuwa kwa kiasi kikubwa na kuahidi endapo atapata nafasi ya kuwa mbunge
ataondoa dhana hiyo ikiwemo kutatua kero zinazokabili wananchi wa jimbo hilo.
“Ndugu zangu mimi ni mwanamke lakini pamoja na hilo siogopi
vitisho vyovyote vile wala siogopi hata nguvu za giza kwani jimbo la Kaliua
siyo la mtu binafsi…..nitagombea na nitashinda tu.’alisema.
Alisema wananchi mmenyanyasika kwa muda mrefu hivyo muda wa
kuifuta CCM madarakani umefika na silaha ya kuiondoa ni kwenda kujiandikisha
muda ukifika ili shetani CCM ang`oke.
Aidha Sakaya alisema hali ya kiuchumi ni mbaya kwani
tunategemea wahisani kutekeleza miradi ya maendeleo kwa asilimia 70 na hili ni
hatari kwa ustawi wa nchi na wananchi wake.
No comments:
Post a Comment