MABINGWA wa
soka Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, wameondoka leo Jumatano Machi 9, 2016
kwenda Afrika Kusini huku mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga, nao wakitarajiwa
kuondoka Alhamisi Machi 10, 2016 kwenda Kigali katika harakati za kuwania
ushindi kwenye michuano ya klabu Afrika.
Yanga,
ambayo imecheza mechi saba mfululizo bila kufungwa – zikiwemo tano za Ligi Kuu –
inaondoka kwenda kuivaa APR Jumamosi Machi 12, katika mchezo wa kwanza wa
mzunguko wa kwanza ikiwa na ushindi mnono wa mabao 5-0 ilioupata Jumanne, Machi
8, 2016 dhidi ya African Sports kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hali hiyo
inawapa jeuri vijana wa Hans van der Pluijim, ambao wanaonekana kuimarika na
kueleza kwamba wana uhakika mkubwa wa kuibuka na ushindi ugenini kwa APR,
ambayo hivi karibuni ilimuajiri kimya kimya Nizar Khanfir, aliyewahi kuwa kocha
wa timu ya Taifa ya Tunisia pamoja na klabu za Stade Gabasien, Club African,
Esperance na Sfaxien.
Khanfir
amechukua mikoba ya kocha wa muda, Emmanuel Rubona, ambaye ndiye ameiongoza
vyema APR tangu Septemba 2015. Rubona sasa atarejea kwenye nafasi yake ya awali
ya kocha msaidizi, wakati kipa mkongwe Jean Claude Ndoli ataendelea kuwa kocha
wa makipa.
Yanga imecheza mechi tano za
ligi bila kupoteza ambapo ilitoka sare ya 2-2 na Prisons, ikaifunga JKT Ruvu
4-0, ikaifunga Simba 2-0 kabla ya kubanwa mbavu na Azam kwa sare ya 2-2, lakini
ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya ‘Wana Kimanumanu’ African Sports ni chachu ya
kiwango cha juu kuweza kuchochea kufanya vizuri dhidi ya APR.
Mechi
nyingine mbili za Yanga zilikuwa za raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa, ambapo
kwanza iliifunga Cercle de Joachim 1-0 ugenini kabla ya kuichapa 2-0 jijini Dar
es Salaam na kusonga mbele.
APR, ambayo
inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Rwanda, imecheza mechi
tisa mfululizo bila kupoteza, hii ni tangu ilipofungwa na Mukura Victory mabao
2-0 Septemba 22, 2015.
Baada ya
hapo, ikiwa chini ya Rubona, imetoka sare mara mbili na imeshinda mechi saba,
ikiwemo ya Machi 3, 2016 dhidi ya Amagaju ambayo Wajeda hao walishinda 2-1.
Japokuwa ilifungwa
mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Mbabane Swallows ugenini, lakini
ilizinduka nyumbani na kuishindilia timu hiyo ya Swaziland mabao 4-1.
Kwa upande
wa Azam, wao wameondoka leo Jumatano kwenda kuvaana na Bitvest Wits ya Afrika
Kusini katika mchezo wa kwanza wa mzunguko wa kwanza wa Kombe la Shirikisho,
lakini wakiwaahidi Watanzania kwamba watawarejeshea furaha ya ushindi.
Mchezo ambao
utafanyika kwenye Uwanja wa Bidvest jijini Johannesburg, Jumamosi Machi 12
kuanzia saa 1.00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, utachezeshwa na waamuzi
kutoka Madagascar wakiongozwa na Andofetra Avombitana Rakotojaona atakayepuliza
kipyenga, akisaidiwa na Pierre Jean Eric Andrivoavonjy na Lionel Hasinjarasoa
Andrianantenaina.
Azam
imeanzia moja kwa moja raundi ya kwanza, lakini Bidvest Wits imefika hatua hiyo
baada ya kuiondoa Light Stars ya Seychelles kwenye raundi ya awali kwa ushindi
wa jumla wa mabao 9-0, ikianza kwa kushinda ugenini 3-0 kabla ya kuichapa tena
6-0 nyumbani.
Bidvest,
ambayo leo Jumatano iko ugenini kwa Polokwane, haijapoteza mechi tangu
ilipofungwa 1-0 nyumbani na Kaizer Chief Fevruari 9, 2016. Baada ya hapo
iliifunga Pretoria University 2-1 na ikatoa kipigi kama hicho kwa Maritzburg
Februari 24.
Kwa sasa timu
hiyo inashika nafasi ya pili nyuma ya Mamelodi Sundowns ikiwa na pointi 42
baada ya kushuka dimbani mara 21. Sundowns ina pointi 52.
Hata hivyo,
kocha msaidizi wa Azam FC, Mario Marinica, alikaririwa wiki hii akisema
wameiona Bidvest Wits kwenye mechi kadhaa na wanajua mbinu wanazotumia na kuahidi
kwamba wanayo nafasi nzuri ya kuwatoa Wasauzi hao.
Marinica ndiye
aliyekwenda kuipeleleza Bidvest Wits wakati ikiichapa Light Stars ya Seychelles
mabao 3-0 kwenye raundi ya kwanza ya michuano hiyo, akiwa ameongozana na kocha mwingine
msaidizi Dennis Kitambi.
“Tuna kikosi
bora, lakini tatizo kubwa tulilonalo ni kushindwa kutumia vema nafasi
tunazotengeneza za kufunga mabao, vinginevyo naamini tuna nafasi kubwa ya
kufanya vizuri dhidi ya Bidvest kama tukicheza kwa staili yetu tunayocheza hivi
sasa,” alisema kocha huyo raia wa Romania.
CREDIT: FIKRAPEVU
No comments:
Post a Comment