Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday 4 March 2016

TWIGA STARS SIKIO LA KUFA, YACHAPWA 2-1 NA ZIMBABWE NYUMBANI



TIMU ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) leo imeshindwa kuuvunja mwiko na kuondoa uteja mbele ya Zimbabwe baada ya kukubali kipigo cha nyumbani cha mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza wa kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake zitakazofanyika nchini Cameroon baadaye mwaka huu.
Licha ya kujitahidi na kupata bao la kuongoza dakika ya 18 kupitia Mwanahamisi Omari, Twiga walijikuta wakishangilia bao hilo kwa dakika mbili tu baada ya Majory Nyauwe kuisawazishia Zimbabwe dakika ya 20.
Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa zimetoshana nguvu, lakini kipindi cha pili kilianza kwa mashambulizi kwa timu zote, lakini alikuwa Erina Jeke aliyezima ndoto za Twiga kuibuka na ushindi baada ya kupachika bao la pili kwa wageni katika dakika ya 48 ya mchezo.
Hii maana yake ni kwamba ahadi ya zawadi ya Shs. 300,000 kwa kila mchezaji endapo wangeifunga Zimbabwe imeyeyuka.
Serikali iliahidi kwamba, endapo Twiga itawafunga wadada hao wa Zimbabwe, basi kila mchezaji atapata Shs. 300,000 kama zawadi na wakirudia tena kuwafunga huko Harare wiki mbili baadaye, watapata kiasi kama hicho.
Fedha hizo, kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Anastazia Wambura, zimechangwa na wadau wa soka ambapo jumla zimepatikana Shs. 15 milioni.
Blogu ya brotherdanny.com inatambua kwmaba hicho ni kichekesho cha soka letu la kubabaisha, kwa sababu serikali imekurupuka kukusanya michango ya zawadi kwa ushindi badala ya kukusanya fedha hizo kwa ajili ya maandalizi bora ya timu hiyo, ambayo katika kipindi cha miaka 14 tangu ilipoanza kushiriki mashindano hayo mwenendo wake siyo mzuri.
Kocha wa timu hiyo, Nasra Juma, aliahidi kwamba vijana wake wangefanya vizuri kwenye mchezo huo, lakini kauli hiyo inaonekana ilikuwa ya kisiasa zaidi kutokana na Twiga Stars kushindwa kupewa maandalizi ya kutosha ikiwamo mechi za kujipima nguvu.
Hii ni mara ya tatu kwa Tanzania kukumbana uso kwa macho na Zimbabwe kwenye mashindano hayo, lakini daima Twiga Stars imekuwa haifurukuti mbele ya ‘Watoto wa Mugabe’ ambapo katika mechi tano sasa, ndiyo leo imefanikiwa walau kupachika bao huku ushindi ukiwa ni ndoto za mchana.
Mara ya kwanza zilizokutana kwenye raundi ya pili ya michuano hiyo mwaka 2002, Twiga Stars ilikubali kutandikwa mabao 5-0 jijini Dar es Salaam Septemba 21, na ziliporudiana Harare Oktoba 13, ikapokea kipigo kama hicho pia ingawa katika raundi ya kwanza ilikuwa imeiondoa Eritrea kwa jumla ya mabao 5-4, ikishinda ugenini 3-2 na kutoka sare ya 2-2 nyumbani.
Mwaka 2004, baada ya kuitoa tena Eritrea kwa jumla ya mabao 5-1 (ilishinda 4-0 na kutoka sare ya 1-1 Asmara), Twiga Stars ikaishia mikononi mwa Wazimbabwe kwa kupachikwa jumla ya mabao 7-0, kwanza ikifungwa 3-0 jijini Dar es Salaam na kufungwa 4-0 jijini Harare.
Ingawa takwimu zilizopo, ambazo Fikra Pevu inazo, zinaonyesha kwamba Twiga Stars imecheza mechi nyingi Zaidi kwenye mashindano hayo kuanzia kwenye hatua ya awali hadi michuano ya fainali, lakini Zimbabwe ndiye yenye rekodi nzuri Zaidi.
Zimbabwe, ambayo ilianza kushiriki mashindano hayo mwaka 2000, imefuzu fainali tatu katika miaka ya 2000, 2002 na 2004 na imecheza jumla ya mechi (zikiwemo za hatua ya awali ya kufuzu) 25 ambapo imeshinda 14, imetoka sare mara nne na kupoteza mechi 11, huku ikifunga mabao 51 na kufungwa 44.
Twiga Stars yenyewe, ambayo imeshiriki fainali mara moja tum waka 2010 kule Afrika Kusini ambako ilipoteza mechi zote, imecheza jumla ya mechi 27, ikishinda nane, kutoka sare mara tano na kufungwa 14, wakati imepachika mabao 43 na kuruhusu wavu wake utikiswe mara 58.
Baada ya kuzikosa fainali za Namibia mwaka 2014 iliposhindwa kutamba mbele ya jirani zao wa Zambia kwa kufungwa bao 1-0 katika mechi zote za nyumbani na ugenini, Zimbabwe sasa ina hasira, na inapotambua kwamba Tanzania imekuwa daraja lake la kwenda fainali, basi inaweza kujisahau na hapo ndipo Twiga Stars, wakiwa imara, wanaweza kufanya maajabu.
Katika mashindano yaliyopita, Zambia ndio waliowatoa kwanza Twiga Stars katika raundi ya kwanza kwa kushinda 2-1 Lusaka na kutoka sare ya 1-1 Dar es Salaam kabla ya kukutana na Zimbabwe, ambao walikuwa wamewatoa Botswana kwa mabao 3-0.
Fainali za mwaka huu 2016 zitafanyika nchini Cameroon kati ya Novemba 19 hadi Desemba 3 ambapo katika hatua ya awali hadi fainali jumla ya nchi 23 zinashiriki, 18 kati ya hizo zikianzia raundi ya kwanza.
Endapo Twiga Stars itafuzu, basi itakumbana na mshindi kati ya Zambia na Namibia katika raundi ya pili.


No comments:

Post a Comment