Edward Lowassa - Ukawa
Dk. John Magufuli - CCM
Na Daniel Mbega wa brotherdannyblog
TUME ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekwishawatangaza wagombea urais wa mwaka huu 2015
ambapo idadi imepungua kuliko ilivyokuwa mwaka 2005.
Jumla yao
wapo nane waliokidhi vigezo, huku wanne wengine wakienguliwa kwa kushindwa
kutimiza vigezo vinavyotakiwa.
Waliotemwa
na NEC ni Mchungaji Christopher Mtikila wa DP, Godfrey Malisa wa CCK na John
Lifa Chipaka wa Ada-Tadea ambao fomu zao zilikuwa na kasoro, wakati ambapo mgombea
wa chama cha AFP, Omari Sombi, yeye hakurudisha kabisa fomu.
Waliopitishwa,
kwa mujibu wa Mwenyekiti wa NEC Jaji mstaafu Damian Lubuva, ambao sasa tutaanza
kushuhudia sarakasi zao majukwaani ni mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk.
John Pombe Joseph Magufuli, mgombea wa Ukawa Edward Ngoyayi Lowassa, Fahmi
Nassoro Dovutwa wa UPDP, Macmillan Lyimo wa TLP, Chifu Lutasola Yemba wa ADC,
Anna Mghwira wa ACT-Wazalendo, Hashimu Rungwe wa Chauma na Malik Kasambala wa
NRA.
Ufuatao ni
wasifu wa wagombea hao:
FAHMI NASSORO DOVUTWA (UPDP)
Fahmi Dovutwa akiwa na fomu za urais
Huyu ni
Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha United Peoples Democratic Party (UPDP).
Alizaliwa Kisarawe mkoani Pwani Februari 27, 1957. Rekodi zake za elimu
zinaoneysha kwamba alianza elimu yake ya msingi mwaka 1967 katika shule ya
msingi Zanaki hadi alipohitimu mwaka 1974 na kuendelea na masomo ya sekondari
katika shule ya Azania jijini Dar es Salaam ambako alihitimu mwaka 1977.
Mwaka
2014, alikuwa miongoni mwa Watanzania waliopata fursa ya kuteuliwa na Rais wa
Tanzania kupitia kundi la vyama vya siasa, na kuwa mjumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba lililofanya kazi yake mjini Dodoma na kukamilisha Katiba Inayopendekezwa.
Hakuna
rekodi zozote zinazoonyesha harakati zake za siasa hasa kwa kipindi cha miaka
10 kushuka chini, lakini itakumbukwa kwamba mwaka 2010 alijitosa katika mbio za
urais kupitia chama chake cha UPDP.
Siku chache
kabla ya uchaguzi, Dovutwa alitangaza kujitoa kwenye kinyang’anyiro hicho,
lakini licha ya kujitoa huku jina lake likiwa limekosewa, bado aliweza kupigiwa
kura na Watanzania na akashika nafasi ya mwisho kati ya wagombea saba
waliojitokeza akipata asilimia 0.16 ya kura zote. Wagombea wengine walikuwa Jakaya
Mrisho Kikwete wa CCM (asilimia 62.83), Willibroad Slaa wa Chadema (asilimia
27.5), Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF (asilimia 8.28), Peter Kuga Mziray wa
APPT (asilimia 1.15), Hashim Rungwe wa NCCR (asilimia 0.31), na Mutamwega Bhatt
wa TLP (asilimia 0.21).
Mwanasiasa
huyu ana mikogo ya aina yake; kuanzia uvaaji wake ambao humtofautisha na
wagombea wengine. Lakini tatizo kubwa ni kwamba, anapenda kudandia hoja ambazo
hazina mashiko. Halafu ameshindwa kabisa kukitapa uhai chama chake ambacho kipo
kama hakipo tu.
Ni
miongoni mwa wagombea ambao wataleta nakshi kwenye kampeni za mwaka huu
kutokana na mbwembwe zake, ingawa ana changamoto kubwa sana katika siasa za
mageuzi.
EDWARD NGOYAI LOWASSA (UKAWA)
Lowassa alipokabidhiwa fomu za urais Chadema
Alizaliwa
Agosti 26, 1953 katika Kijiji cha Ngarash, Monduli na ndiye mtoto mkubwa wa kiume
kwa Mzee Ngoyai Lowassa. Alianza kusoma katika Shule ya Msingi Monduli kati ya
mwaka 1961–1967. Akaendelea kwenye Shule ya Sekondari Arusha kwa kidato cha
kwanza mpaka cha nne kati ya mwaka 1968 - 1971, baadaye akaenda Shule ya
Sekondari Milambo mkoani Tabora alikohitimu
kidato cha sita katika mwaka 1972–1973.
Alijiunga
na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1974–1977 na kuhitimu Shahada ya Sanaa
katika Elimu (B.A Education) na baadaye Chuo Kikuu cha Bath, Uingereza kwa
Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Maendeleo (mwaka 1983–1984).
Baada ya
kumaliza chuo kikuu, Lowassa alifanya kazi ndani ya CCM akiwa ofisa wa ngazi ya
juu kuanzia wilaya, mkoa na baadaye makao makuu kati ya mwaka 1977–1989.
Aliajiriwa
kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC),
mwaka 1989–1990.
Lowassa
amemuoa Regina na wana watoto watano, wasichana wawili na wavulana watatu.
Watoto hao ni Fredrick, Pamella, Adda, Robert na Richard.
Lowassa
alichaguliwa kuwa Mbunge kupitia kundi la Vijana ndani ya CCM na akashikilia
nafasi hiyo kati ya mwaka 1990 hadi 1995. Mwaka 1993 aliteuliwa kuwa Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais (Haki na Mambo ya Bunge),
kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Ardhi na Makazi akiwa Waziri mwaka 1993–1995.
Mwaka 1995
wakatiwa Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi, Lowassa alishinda ubunge kwa
asilimia 87.3. Alikaa bila uteuzi wowote kwa miaka miwili. Mwaka 1997–2000,
Rais Benjamin Mkapa alimteua kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais
(Mazingira na Kuondoa Umasikini).
Kwenye
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 aligombea tena ubunge wa Monduli na kushinda kwa
mara ya tatu. Rais Mkapa akamteua kuwa Waziri wa Maji na Mifugo hadi mwaka
2005.
Kwenye
Uchaguzi Mkuu wa 2005, aligombea ubunge na kushinda kwa asilimia 95.6. Rais
Jakaya Kikwete alimteua kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na Bunge likamthibitisha
kwa kura 312.
Uwaziri
mkuu wa Lowassa ulikoma Februari 8, 2008, alipojiuzulu kutokana na kashfa ya
Richmond. Kamati Maalumu ya Bunge ya watu watano iliyoongozwa na Dk Harrison
Mwakyembe ilisisitiza kuwa wizara ya Nishati na Madini na Ofisi ya Waziri Mkuu
ndizo zinazopaswa kubeba lawama ya uingiaji wa mkataba mbovu na Richmond,
kampuni ambayo uchunguzi ulionyesha kuwa ni ya mfukoni mwa watu huku Serikali
ikilazimika kulipa mabilioni ya fedha katika mkataba ambao una upungufu
makubwa.
Baada ya
kujiuzulu, Lowassa aligombea ubunge kwa mara nyingine Monduli (mwaka 2010) na
kupata asilimia 90.93 ya kura zote na hadi sasa ndiye mbunge wa jimbo hili
japokuwa amekwishaaga kwamba hatagombea tena kiti hicho.
Lowassa alikuwa
miongoni mwa wana CCM 17 waliochukua fomu kuwania urais mwaka 1995 lakini
aliyepitishwa ni Mkapa. Mwaka 2005, hakugombea urais ila alikuwa na mipango ya
muda mrefu ya kumsaidia rafiki yake, Kikwete na inadaiwa kuwa makubaliano ya
Kikwete na Lowassa yalikuwa kwamba mwenzake akishaongoza nchi kwa miaka 10
(yaani 2005 – 2015) atamtengenezea njia 2015 – 2025.
Katika
kampeni za ndani ya CCM mwaka huu alikuwa miongoni mwa wanachama 42 waliochukua
fomu, lakini akaenguliwa katika hatua za mwanzo tu na kushindwa kuingia tano
bora. Ndipo akaamua kujiunga na Chadema na sasa ndiye anaakilisha Ukawa kwenye
mbio za urais.
Umaarufu
wake na nguvu ya fedha ndivyo vinavyomfanya awe na wafuasi wengi hata kwenye
mikutano yake.
Udhaifu wa
kwanza wa Lowassa ni kuwa karibu mno na watu wenye majina yenye taswira zinazotia
shaka, ndiyo maana anahusishwa na tuhuma za ufisadi hata kama hakuna ushahidi
wa moja kwa moja wa kuhusika kwake. Waingereza wanasema; Ndege wenye mabawa
yanayofanana, huruka pamoja. Marafiki wakubwa wa Lowassa ni watu wenye pesa na
matajiri, hilo linaweza kumkwamisha katika harakati zake.
Ndiyo
maana jamii imegawanyika mno juu yake, wengine wakimuona kama mtu mwenye
mipango mingi ya kifedha na mfanyabiashara zaidi kuliko kiongozi wa nchi huku
wengine wakimuona kama kiongozi anayethubutu.
Lakini
udhaifu wake mwingine ni kwamba hana uwezo wa kuendesha mapambano dhidi ya
rushwa na ufisadi kwa sababu wengi kati ya rafiki zake ndio hao wanaotuhumiwa
pamoja naye. Atawezaje kuwanyooshea kidole huku akitangaza hadharani kwamba
anawapenda?
JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI (CCM)
Magufuli alipoteuliwa na CCM
Alizaliwa
tarehe Oktoba 29, 1959 huko wilayani Chato mkoani Kagera (sasa ni wilaya ndani
ya Mkoa wa Geita). Alianza elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Chato mwaka
1967 na akahitimu mwaka 1974. Alifaulu na kujiunga na Shule ya Seminari Katoke,
Biharamulo ambako alisoma Kidato cha Kwanza na cha Pili mwaka 1975 - 1977,
akahamishiwa Shule ya Sekondari Lake, Mwanza ambako alisoma kidato cha Tatu na
Nne mwaka 1977 - 1978.
Masomo ya
kidato cha Tano na Sita aliyapata mkoani Iringa katika Shule ya Sekondari
Mkwawa kati ya mwaka 1979 na 1981. Baadaye akarudi Chuo cha Ualimu Mkwawa
kusomea Stashahada ya Elimu ya Sayansi akibobea kwenye masomo ya Kemia,
Hisabati na Elimu; hii ilikuwa mwaka 1981 – 1982.
Baadaye
akaenda kuanza kazi ya ualimu katika Shule ya Sekondari Sengerema, akifundisha
masomo ya Kemia na Hisabati. Ajira hii aliifanya kati ya mwaka 1982 na 1983, kisha
akajiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria akianzia
Makutupora, Dodoma (Julai - Desemba 1983), na kambi ya Makuyuni, Arusha
(Januari hadi Machi 1984) na akamalizia katika kambi ya Mpwapwa mkoani Dodoma
(Machi – Juni 1984).
Mwaka 1985
alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akisomea Shahada ya Sayansi ya Elimu
akibobea kwenye masomo ya Kemia na Hisabati na alihitimu mwaka 1988.
Mwaka 1989
- 1995 alifanya kazi katika kiwanda cha Nyanza Cooperative Union (Ltd.) akiwa
mkemia na wakati huohuo alianza masomo ya shahada ya uzamili ya Sayansi katika
Chuo Kikuu cha Salford nchini Uingereza, kikishirikiana na Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam ambako alisoma kati ya mwaka 1991 na 1994.
Magufuli
aliendelea na elimu ya juu zaidi kwa maana ya Shahada ya Uzamivu ya Kemia
kuanzia mwaka 2000 hadi 2009 ambayo aliihitimu katika Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam na kuwa mhitimu wa shahada ya udaktari. Dk Magufuli ana mke, watoto na
familia imara.
Dk.
Magufuli alianza mbio za ubunge mwaka 1995, alipojitosa katika jimbo la Chato
kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kushinda wakati akiwa na miaka 36.
Rais Benjamin Mkapa akamteua kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Miundombinu.
Uchaguzi
wa mwaka 2000 ulipoitishwa, Dk. Magufuli aligombea na kushinda kwa mara ya
pili. Rais Mkapa akamteua kuwa Waziri wa Wizara ya Miundombinu na akakaa hapo
hadi kipindi cha uongozi wa Mkapa kilipomalizika.
Mwaka 2005
aligombea jimboni kwake na akaingia
kwenye orodha ya wabunge waliopita bila kupingwa. Rais Jakaya Kikwete akamteua
kuongoza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hadi mwaka 2008
alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambayo aliiongoza hadi mwaka 2010.
Mwaka 2010
wana CCM wa Chato hawakuchoka kumpa ridhaa Dk Magufuli, hii ikiwa mara ya nne.
Mara hii hakupita bila kupingwa, alipambana na mgombea kutoka Chadema,
Rukumbuza Vedastus Albogast ambaye alifanikiwa kumtoa jasho Magufuli.
Katika
uchaguzi ule alipata ushindi wa asilimia 66.39 dhidi ya asilimia 26.55 za
mgombea wa Chadema. Na baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge kwa mara ya nne, Rais
Kikwete akamrudisha katika Wizara ya Ujenzi ambako yuko hadi hivi sasa.
Dk.
Magufuli pamoja na kazi nzuri aliyoifanya akiwa waziri katika wizara
alizoziongoza, lakini si maarufu katika ‘mitandao’ ya CCM na hata uchukuaji na
urejeshaji wa fomu ndani ya chama hicho haukuwa na mbwembwe kama wagombea
wengine. Alipoulizwa na wanahabari, yeye alijibu kwamba anasubiri kuinadi Ilani
ya Uchaguzi ya CCM.
Kushinda kwake
kulikuwa kama ‘ndondokela’ baada ya kukatwa kwa Lowassa na kupitishwa kwa jina
la Bernard Membe – mgombea ambaye alikuwa na ushindani mkubwa na Lowassa. Wajumbe
wa NEC, wengi wakidaiwa kuwa wa upande wa Lowassa, wakampa kura nyingi
zilizomvusha hadi tatu bora na kuwaengua Membe na January Makamba.
Huku akapambana
na wanamama wa shoka, Dk. Asha-Rose Migiro na Balozi Amina Salum Ali, lakini
akashinda kwa ‘mafuriko’.
Magufuli ana
uwezo wake wa kielimu. Lakini jambo lingine linalompa nguvu, ni kukaa kwa muda
mrefu katika wizara zake. Amekuwa Naibu Waziri wa Miundombinu kwa miaka mitano
na pia Waziri wa Miundombinu wakati wa Mkapa; akaongoza wizara ya Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi kwa miaka mitatu kabla ya kuongoza ile ya Uvuvi na
Mifugo kwa miaka miwili. Lakini pia tangu mwaka 2010 hadi hivi leo ameiongoza
Wizara ya Miundombinu bila kuhamishwa. Jambo hili hulikuti kwa mawaziri wengi
sana, hasa katika serikali ya Kikwete. Hii ina maana kwamba anaaminiwa kutokana
na utendaji wake. Anafaa!
Huyu jamaa
ni makini na ana uwezo wa kusoma na kuchambua nyaraka. Yeye husoma kila jambo
na kwamba anatumia muda mwingi sana kusoma kila taarifa na hadi anaweka mistari
na michoro kwenye taarifa.
Mhandisi
mmoja ambaye amewahi kufungiwa leseni na Magufuli anasema kuwa kosa moja kubwa
alilofanya ni kumwandikia Magufuli taarifa ndefu lakini yenye uongo kwenye aya
moja. Anasema kuwa aya hiyo ilikuwa iko ukurasa wa 20 lakini ndani ya muda
mfupi “Magufuli aliibaini na kibarua chake kiliota nyasi”. Utendaji huu wa
kufuatilia hadi vilivyomo kwenye maandishi ndani kabisa, umewashinda wanasiasa
na viongozi wengi, Magufuli anabebwa na jambo hilo.
Tatizo ni
moja tu kwa Dk. Magufuli; kufanya maamuzi ya haraka. Mgombea mwenza wake ni
Samia Suluhu Hassan na endapo CCM itashinda, itakuwa ni mara ya kwanza katika historia
ya Tanzania kuwa na Makamu wa Rais mwanamke.
ANNA MGHWIRA (ACT-WAZALENDO)
Anna Mghwira
Anna
Mghwira ni mwenyekiti wa taifa wa chama cha ACT – Wazalendo. Alizaliwa Januari 23,
1959 katika hospitali ya mkoa wa Singida, Kata ya Mungumaji, Kitongoji cha Irao
Manispaa ya Singida Mjini. Baba yake mzazi alikuwa diwani na kiongozi wa TANU
kabla ya CCM hadi mwaka 1985, mama yake alijishughulisha na kilimo na ufugaji
na wazazi hawa kwa ujumla walijipatia watoto tisa, akiwemo Bi. Anna.
Bi. Anna alianza
safari ya kielimu katika shule ya msingi “Nyerere Road” mwaka 1968 – 1974
akaendelea na elimu ya sekondari kwenye Shule ya Ufundi Ihanja kati ya mwaka
1975 – 1978 kabla ya kuhitimisha masomo ya juu ya Sekondari (Kidato cha V na
VI) Lutheran Junior Seminary kati ya mwaka 1979 – 1981.
Aliendelea
na masomo ya Chuo Kikuu mwaka 1982 baada ya kujiunga Chuo Kikuu cha Theolojia
(Chuo Kikuu cha Tumaini) na kuhitimu shahada ya Theolojia mwaka 1986.
Mwaka
huohuo 1986 alijiunga Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam akitafuta shahada ya Sheria
na akaimaliza na kutunukiwa mwaka 1986.
Kati ya
mwaka 1987 – 1998, Bi Anna aliendelea na shughuli za ujenzi wa Taifa, akifanya
kazi ndani na nje ya nchi na kupata uzoefu mkubwa.
Safari ya
Elimu ya Bi. Anna ilikamilikia Chuo Kikuu cha Essex nchini Uingereza ambako
alianza shahada ya uzamili ya sheria (LLM) mwaka 1999 na kutunukiwa mwaka 2000.
Licha ya
kuwa mwanasheria na mtheologia aliyebobea, pia amefanya kazi za maendeleo kwa
muda mrefu na ana uzoefu katika uendeshaji wa serikali za mitaa, uzoefu wa
utumishi katika mashirika ya kimataifa, kitaifa na mashirika ya dini ambamo
amejihusisha na masuala ya wanawake, watoto, wakimbizi, utawala na haki za
binadamu.
Anna ana
historia ya kupenda siasa, masuala ya jamii na michakato ya maendeleo kama
inavyojidhihirisha katika maandiko yake mbalimbali katika majarida na magazeti
ya hapa ndani ya nchi.
Alianza
siasa tangu wakati wa TANU akiwa ni mwanachama wa Umoja wa Vijana wa Tanu (Tanu
Youth League) na aliwahi kushinda tuzo mbalimbali kutokana na ushiriki wa juu
katika TANU lakini baadaye ilipoanzishwa CCM alipunguza ushiriki wake ili ajipe
muda katika masomo na baadaye ndoa na malezi ya watoto.
Kwa
kipindi kirefu hakuwa anajihusisha na siasa hadi alivyoamua kujiunga na Chadema
mwaka 2009 ambako alishika nafasi mbili tu za Uenyekiti wa Baraza la Wanawake
ngazi ya Wilaya na Katibu wa Baraza la Wanawake Mkoa.
Mwezi
Machi 2015 alijiunga rasmi na chama cha ACT – Wazalendo na katika Mkutano Mkuu
wa kwanza wa chama hicho, yeye ndiye akachaguliwa kuwa mwenyekiti wa kwanza wa
ACT.
Bi. Anna
aliolewa na Shedrack Maghwiya tangu mwaka 1982 na walibahatika kupata watoto 3
wa kiume: Fadhili, Peter na Elisha. Hata hivyo kwa bahati mbaya, mume wake hivi
sasa ni marehemu.
Bi. Anna
Mghwira alijitosa katika mbio za ubunge kwa mara ya kwanza mwezi Januari 2012
baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutangaza uchaguzi mdogo katika Jimbo la
Arumeru Mashariki baada ya kifo cha Solomon Sumari.
Anna
alishiriki kura ya maoni ndani ya Chadema akihitaji kupewa ridhaa, hata hivyo
chama hicho kilimpitisha Joshua Nassari na Bi. Anna alikuwa na kazi ya
kuendelea kumuunga mkono hadi ushindi ulipotangazwa kwa chama hicho.
Pia,
amewahi kugombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki, kupitia Chadema japokuwa
hakuchaguliwa kushikilia wadhifa huo.
Ndiye
mwanamke pekee anayegombea urais safari hii na mgombea mwenza wake ni Hamad
Mussa Yusuph. Hata hivyo, mgombea mwenza wa CCM pia ni mwanamke, Samia Suluhu
Hassan.
HASHIM RUNGWE SPUNDA (CHAUMA)
Hashim Rungwe
Hashim
Rungweni Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania akifanya kazi zake kama wakili
binafsi. Alizaliwa Januari Mosi, 1949 katika eneo la Ujiji, mkoani Kigoma.
Alianza
elimu ya msingi katika shule ya msingi Kipampa iliyoko mkoani Kigoma kati ya
mwaka 1959 – 1966 na akajiunga na masomo ya sekondari katika Shule ya Sekondari
ya Chuo Kikuu cha Cambridge kati ya mwaka 1967 – 1969 na kuhitimu kidato cha
nne, kabla ya kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita hapa hapa
Tanzania.
Mwaka 1975
alisoma ngazi ya Cheti katika Taasisi ya Kukuza Mauzo ya Dar es Salaam, mwaka
1977 alisoma Lugha ya Kifaransa kwa ngazi ya cheti katika taasisi ya “Alliance
Francais” ya jijini Dar es Salaam na kisha akasoma lugha ya Kiarabu na elimu ya
dini ya Kiislamu kwa ngazi ya shahada katika Chuo Kikuu cha Mfalme Abdul
kilichoko Saudi Arabia kati ya mwaka 1979 – 1982.
Mwaka 1989
alisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ngazi ya Cheti, akichukua masomo ya
Usimamizi wa Umma lakini pia mwaka 1991 alisoma ngazi ya cheti hapo hapo Chuo
Kikuu, akijikita katika eneo la Historia ya Afrika na Falsafa ya Historia na Masuala
ya Maendeleo.
Hashim
aliendelea zaidi kielimu alipoamua kubobea katika sheria, alijiunga na Chuo
Kikuu Huria Tanzania na kusoma shahada ya sheria kuanzia mwaka 1996 na kuhitimu
mwaka 2003 na mwaka huohuo 2003 akasajiliwa kuwa wakili wa Mahakama Kuu ya
Tanzania.
Kwa upande
wa ajira, Hashim amefanya kazi na mashirika mbalimbali ya ndani ya nchi. Kwa
mfano, kuanzia mwaka 1969 hadi 1973 amekuwa ni Ofisa aliyeajiriwa serikalini na
kufanya kazi katika idara mbalimbali za sekta ya umma.
Pia, mwaka
1982 hadi leo amekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Udalali ya Bahari,
lakini pia kuanzia mwaka 1990 hadi leo amejiajiri katika kampuni ya Bahari
Motors inayojishughuliza na uuzaji wa magari akiwa kama Mkurugenzi Mtendaji
Kisiasa,
Hashim aliwahi kuwa mwanachama imara wa TANU kati ya mwaka 1966- 1977 na kisha
CCM kati ya mwaka 1977 – 1995. Ndiyo kusema kuwa wakati mfumo vyama vingi
unaanzishwa mwaka 1992 yeye alikuwa mwanachama wa CCM kwa miaka mitatu zaidi
kabla ya kuhamia NCCR Mageuzi mwaka 1996.
Alipokuwa
NCCR alishiriki hatua mbalimbali za chama hicho katika kupigania mabadiliko,
lakini alijiondoa NCCR mwaka 2012 na kuanzisha chama cha siasa kinachojulikana
kama Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) na baada ya kuanzisha chama hicho
alichaguliwa kuwa Mwenyekiti mwaka 2014. Ameoa na ana watoto watano.
Mwaka 1995
aligombea ubunge katika Jimbo la Kawe kupitia CCM, lakini akashindwa na
Zainudin Adamjee. Mwaka 1996 akahamia NCCR-Mageuzi na mwaka 2005 akagombea
ubunge Jimbo la Kinondoni na kushindwa na Iddi Azan wa CCM. Mwaka 2010
akagombea urais kupitia NCCR-Mageuzi akashika nafasi ya tano kati ya wagombea
saba na kupata kura 29,638 sawa na asilimia 0.31.
MACMILLAN ELIFATIO LYIMO (TLP)
Macmillan Lyimo
Huyu alizaliwa
Januari 29, 1964 katika kijiji cha Kondeni Matala Wilaya ya Moshi Vijijini,
katika jimbo la Vunjo, akiwa mtoto wa nne kati ya watoto sita wa familia ya Mwalimu
Elifatio Lyimo na mama Elingisongoya.
Alianza
elimu msingi katika shule za msingi Kondeni na Kirua kati ya mwaka 1975 na 1978
(darasa la kwanza hadi la nne). Kisha, mwaka 1978 hadi 1979 alisoma katika
Shule ya Msingi Sanya Juu katika Wilaya ya Hai. Baadaye akajiunga na Shule ya
Msingi Karoro kati ya mwaka 1980 – 1981 alikomalizia darasa la saba.
Macmillan
alikuwa mwanafunzi pekee aliyefaulu kutoka kwenye shule zote za Kata ya Mwika Kusini.
Baada ya ufaulu huo wa “upweke” alichaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari
katika Shule ya Sekondari Same mkoani Kilimanjaro akafanikiwa kuhitimu mwaka
1985 akipata Daraja la Kwanza (Division I) na kuchaguliwa kuendelea na masomo
ya juu ya sekondari katika mchepuo wa ECA (Uchumi, Biashara na Uhasibu). Masomo
haya ya juu ya sekondari (kidato cha tano na cha sita) aliyapata katika Shule
ya Sekondari Umbwe iliyoko Moshi Vijijini (1985 - 1988) ambako nako alipata
daraja la kwanza (Division I).
Baada ya
hapo alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa katika kambi za Mgambo na baadaye
Maramba zote za mkoani Tanga, kisha akahamishiwa makao makuu ya JKT eneo la
Mlalakuwa jijini Dar es Salaam mmwaka 1988 – 1989 kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam kuanzia mwaka 1989 alikohitimu Shahada ya Biashara (BCom)
mwaka 1993. Katika kujiendeleza kitaaluma, Macmillan alijiunga na Chuo Kikuu
Huria cha Tanzania (OUT) mwaka 1999 – 2004 alikosoma na kutunukiwa Shahada ya
Uzamili ya Usimamizi wa Biashara (MBA). Tangu mwaka 2013 amekuwa akiendelea na
masomo ya Shahada ya Uzamivu katika Chuo Kikuu Huria Tanzania na hivi sasa yuko
katika hatua ya utafiti akitarajia kuhitimu shahada hiyo ya falsafa miaka
michache ijayo.
Tangu
ahitimu shahada yake ya Biashara, Macmillan hajawahi kuajiriwa serikalini na
haamini katika “kuajiriwa na serikali”. Amefanya shughuli za biashara ndogo
ndogo kabla ya kufungua kampuni yake binafsi inayojihusisha na masuala ya
madini na raslimali za nchi.
Mwaka 2000
aligombea ubunge katika Jimbo la Temeke, Dar es Salaam na akashindwa na Abbas
Zuberi Mtemvu wa CCM, mwaka 2010 aligombea ubunge Arusha Mjini lakini
akashindwa na Godbless Lema wa Chadema, yeye akishika nafasi ya mwisho akiwa na
kura 179 (0.18%)
Mwaka 2010
aliomba ridhaa ya TLP kugombea urais, lakini akashindwa na kada maarufu wa
chama hicho Muttamwega Bhatt Mganywa ambaye alipitishwa, akagombea urais na
kupata kura 17,482 (0.21%).
Lakini
safari hii bahati ilikuwa yake, kwani Aprili 23, 2015 alipitishwa na TLP kuwa
mgombea Urais na akawa mgombea wa kwanza kutangazwa na chama cha siasa kwa
ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu.
CHIFU LUTASOLA YEMBA (ADC)
Chifu Lutasola Yemba
Huyu
hafahamiki katika siasa za Tanzania, lakini ndiye aliyepitishwa na chama
chaAlliance fo Democratic Change (ADC) kilichoanzishwa na aliyekuwa Mbunge wa
Wawi kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Hamad Rashid Mohammed, ambaye alijitoa
mwaka 2014.
Hamad,
ambaye aliwahi kuwa Kiongozi Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wakati wa
Bunge la Tisa, yeye anagombea Zanzibar akichuana na Maalim Seif Sharrif Hamad
wa CUF na Dk. Ali Mohammed Shein wa CCM.
Hata
hivyo, mgombea mwenza wa Chifu Yemba ni Said Miraji Abdullah, kada maarufu wa
zamani wa CUF aliyejiengua pamoja na Hamad.
JANKEN MALIK KASAMBALA (NRA)
Mwanasiasa huyu si maarufu sana katika siasa za Tanzania, hususan za vyama vingi.
Mwaka 2005 aligombea ubunge katika Jimbo la Ukonga kupitia chama hicho, lakini akashika nafasi ya tano kwa kupata kura 1,186. Mshindi alikuwa Dk. Milton Makongoro Mahanga aliyepata kura 126,955.Lakini chama cha kimemuona anafaa kugombea nafasi ya urais. Tusubiri tuone.
Imeandaliwa
na www.brotherdanny.com kwa msaada wa
makala za Julius Mtatiro zilizochapishwa kwenye gazeti la Mwananchi.
No comments:
Post a Comment