Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akiteta jambo la Edward Lowassa
Na Daniel Mbega
KIMBUNGA
cha kisiasa kinatarajiwa kuanza kuonekana wiki hii Ukawa watakaporihia kwamba
Edward Lowassa ndiye awe mgombea pekee wa urais kutoka umoja huo, akipitia
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Na
kimbunga hicho kitakuwa kikubwa zaidi wakati Lowassa atakapochukua rasmi fomu
ya kugombea urais katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi, hali ambayo italeta
mafuriko makubwa.
Natabiri
kwamba mafuriko hayo yanaweza kugeuka kuwa gharika pindi Lowassa atakapoanza
kutambulishwa nchi nzima, kabla ya kuanza rasmi kwa kampeni za uchaguzi.
Sina
uhakika kama Chama cha Mapinduzi (CCM) kina Mkakati B wa kukabiliana na gharika
hiyo ingawa Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi, Nape Moses Nnauye,
alitamba mjini Dodoma kwamba walifanikiwa kuzuia mafuriko kwa mikono.
Siku
kadhaa zilizopita, CCM ilitaja sababu tano zilizokilazimu kuengua jina la
Lowassa kati ya wagombea 38 wa urais huku chama hicho kikisisitiza kwamba
taratibu zote zilifuatwa, ingawa Lowassa mwenyewe amekuwa akizungumza nje ya
chama kwamba hakutendewa haki ndiyo maana ameamua kuhama.
Sababu
zinazotajwa ni pamoja na; 1. Kukiuka taratibu za chama kwaani alionekana
kufanya kampeni badala ya kutafuta wadhamini; 2. Kutoa rushwa kwa wanachama
mbalimbali hivyo kukigawa chama na kama angepishwa kuwa mgombea CCM ilikuwa
katika hatari ya kuwekewa pingamizi mahakamani lakini pia angeweka watu wake
kwenye utawala kuwalipa fadhira; 3. Edward Lowasa aliwahonga wajumbe katika
uchaguzi wa wajumbe NEC uliofanyika miaka iliyopita ili kupata watu wake ndani
ya NEC; 4. Kuanza kampeni kabla ya wakati, alikuwa akisafirisha watu mbalimbali
na kuwalipa fedha nyingi kisha kutoa taarifa kuwa walikuwa wakimtaka kugombea
Urais, hii ni hadaa na hatari kwa chama; na 5. Kuwa na kashfa nyingi za
ufisadi.
“Msemea
sikioni siyo majinuni”, yawezekana kabisa CCM wanajua wanachokisema na ndiyo
maana wao leo ndio wanaosema ‘Lowassa ni fisadi’ wakati Chadema alikokimbilia
wanasema ‘Lowassa siyo fisadi’ japokuwa ni Chadema hao hao waliomwanika
hadharani kwamba ni miongoni mwa mafisadi 11 wanaoiangamiza Tanzania katika ile
‘Orodha ya Aibu’ (List of Shame) pale Mwembeyanga Jumamosi ya Septemba 15,
2007.
Chadema,
ambao siku zote walidai kwamba wana ushahidi na wakaitaka Serikali imfikishe
Lowassa mahakamani, leo hii wamegeuka, wamebadilika na kusema kwamba mwanasiasa
huyo ‘ni msafi’.
Kama
tuhuma za kwamba wamepewa Shs. 10 bilioni ili kumkaribisha mwanasiasa huyo
zitakuwa na ukweli wowote, basi nachelea kusema kwamba hakuna Mtanzania mwenye
ujasiri wa kukemea ufisadi na kilichopo ni mazingaombwe tu ya watu wachache
kutumia hoja za ufisadi ili waende Ikulu ya Magogoni.
Nakubaliana
na maneno ya Mwalimu Ndimara Tegambwage aliyoyabandika wiki iliyopita kwenye
mtandao wa kijamii wa facebook kwamba “Siasa haijawahi kuwa mchezo mchafu… Bali
kuna watu wachafu kwenye siasa – na vyamavya siasa.”
Naam.
Fedha inaweza kununua kila kitu: inaweza kununua nafasi katika Ukawa na mwenye
tuhuma za ufisadi akateuliwa kugombea nafasi yoyote bila hata kufuata
utaratibu.
Nataka
kushawishika na maelezo ya mwanasiasa machachari mdogo wangu Zitto Zuberi Kabwe
aliyoyatoa Januari 5, 2014 kuhusu tuhuma dhidi ya Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe, akijibu mapigo ya Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu
aliyeanza kumtuhumu yeye kwamba alihongwa magari mawili na Wakili Nimrod Mkono.
Zitto
alisema, kama Mkono ndiye aliyemweleza Lissu kwamba alimhonga yeye Zitto
magari, basi atakuwa alimweleza pia kwamba mwaka 2005 Mkono huyo huyo alimpa
Freeman Aikaeli Mbowe Shs. 40 milioni ili Mbowe asifanye kampeni Musoma
Vijijini; Atakuwa pia alimwambia kwamba mwaka 2008 (baada ya orodha ya mafisadi
kutangazwa 2007) Mkono alimpa Mbowe Shs. 20 milioni za uchaguzi wa Tarime
ambazo Mbowe alisema kwenye chama ametoa mkopo na akalipwa.
Zitto
akaendelea kusema kwamba, kama Mkono alimwambia Lissu kuhusu kumhonga yeye
magari, pia atakuwa alimwambia kwamba mwaka 2010 Mkono huyo huyo alimpa Mbowe
Shs. 200 milioni za kampeni ya Dk. Slaa na hakusahau kumwambia kuwa Rostam Aziz
(fisadi) pia alimpa Mbowe Shs. 100 milioni za kampeni bila kusahau kwamba
gazeti la Tanzania Daima lilianzishwa na fedha kutoka chama cha Conservative
cha Uingereza.
Akamtaka
Lissu amuulize Mbowe aliingia deal (mkataba) gani na (Abdulrahman) Kinana na
(Frederick) Sumaye mwaka 2005 kufuatia deni lake NSSF bila kusahau kuweka wazi
mkataba kati yake na NHC kuhusu nyumba ya umma ilipo Club Bilicanas.
Naam. Hizo
ndizo siasa na hiyo ndiyo michezo inayoendelea ndani yake. Sishangai kuona leo
Chadema wamemuona yule yule waliyemwita fisadi, amekuwa muadilifu wa kutupwa.
Kinachonishangaza
tu ni kitu kimoja, nani kati ya Lowassa na Chadema atakayeweza kumbadilisha
mwenzake? Kama wamemwita ‘mtakatifu’ aliyekuwa ‘mwenye dhambi’, watawezaje
kumbadilisha atakapokuwa madarakani hasa ikizingatiwa kwamba hata alipokuwa
madarakani, Lowassa hajawahi kupinga hadharani vitendo vya rushwa na ufisadi na
mafisadi wenyewe, ambao karibu wote waliotajwa na Chadema ni maswahiba zake?
Kimsingi,
Chadema haitakuwa na jeuri wala uwezo wa kumbadili Lowassa kwa sababu tayari
amekwishasema mapema kabisa kwamba yeye ‘anachukia umaskinina hawachukii
matajiri’ ambao Chadema imewatangaza miaka mingi kwamba ni mafisadi. Kwa hili,
kamwe Chadema haitaweza.
Lakini
Lowassa yeye ameweza kuibadilisha Chadema vile atakavyo. Nguvu zake kisiasa na
kifedha zimebadili mambo mengi ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani kwa sasa.
Kwanza;
Lowassa kafanikiwa kubadili ratiba ya uchaguzi ya Chadema. Wakati ambapo tarehe
ya mwisho ya kuchukua na kurejesha fomu za kugombea urais kupitia chama hicho
ilikuwa saa 10 jioni Jumamosi, Julai 25, 2015, Chadema iliamua kusogeza mbele
ratiba kutokana na kuendelea vikao vya siri vya kumshawishi Lowassa akiunge
nacho.
Pili;
Lowassa amefanikiwa kumbadili mgombea kipenzi wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa,
ambaye tangu kutua kwa Lowassa ndani ya chama hicho, kumekuwepo na hadithi
nyingi kwamba huenda daktari huyo wa theolojia amejiengua ndani ya chama na
siasa kwa ujumla. Chadema walijipimana kuona hakuna mtu ndani yao wala ndani ya
Ukawa ambaye alikuwa na ubavu wa kukabiliana na mgombea wa CCM, Dk. John
Magufuli, isipokuwa Lowassa.
Tatu;
Lowassa ameibadilisha bajeti ya uchaguzi ya Chadema. Kwa fedha alizonazo, ni
dhahiri kwamba bajeti ya kampeni za uchaguzi wa chama itapaa sana, japokuwa
wanapaswa kuwa makini na Sheria ya Gharama za Uchaguzi.
Nne;
Lowassa amebadilisha kauli zao za ufisadi dhidi yake. Kama nilivyosema hapo
juu, viongozi wengi, kama si wote, wa Chadema na hata Ukawa, wanaamini Lowassa
‘siyo fisadi tena’ kwa kutumia fomula ya namba hasi ikitoka kushoto kwenda
upande wa kulia wa alama ya sawa sawa lazima itakuwa namba chanya! Watamnadi
kwa kumtakasa kwa nguvu zote na ole wake atokee mtu akasema Lowassa fisadi,
watapambana naye kila kona!
Tano;
Lowassa kabadilisha Ilani ya Uchaguzi ya Chadema. Hivi sasa wataalam wachama
hicho wamejichimbia kubadili vipengele mbalimbali vya ilani hiyo, hasa kwa kuzingatia
kwamba sera za Lowassa ni kutowatupa matajiri ambao chama hicho kinawaita ni
mafisadi. Nguvu zaidi ya kumkaribisha Lowassa inatajwa kutoka kwa Mbowe, ambaye
huenda anajua maslahi yaliyo nyuma ya ujio wa Lowassa.
Kwa
misingi hiyo basi, siyo rahisi Chadema – chama chenye haiba ya kupinga ufisadi
nchini – kikambadili Lowassa kirahisi rahisi hivyo kama wengi wanavyodhani,
bali ni wimbi jingine la ‘ufiadi’ ambalo litaingia Ikulu ikiwa Lowassa
atashinda Oktoba 25, 2015.
Na endapo
Ukawa itashindwa uchaguzi, hili ndilo litakalokuwa ‘anguko kuu’ la upinzani
nchini.
Haya ndiyo
niyaonayo.
0656-331974
No comments:
Post a Comment