Masanja Mwinamila (44) mara baada ya kufikishwa katika kituo cha Polisi Wilaya ya Nzega Juni 15, 2015.
Mtoto Margreth Hamisi Machiya (6) aliyenusurika kuuzwa akiwa hai na mjomba wake.
Mtoto Margreth baada ya kufikishwa Kituo cha Polisi Wilaya ya Nzega usiku wa manane.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, ACP Juma Bwire akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo Juni 16, 2015.
Na Daniel
Mbega, Nzega
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi ya Wilaya ya Nzega leo hii
imemhukumu Masanja Mwinamila (44), mkazi wa Kitongoji cha Kona Nne, Kijiji cha
Ugembe II, Kata ya Mwakashanhala, Tarafa ya Puge wilayani Nzega katika Mkoa wa
Tabora kwenda jela miaka 10 kwa kosa la kuteka mtoto mwenye albinism, Margreth
Hamisi (6).
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Saraphine Nsana,
alitoa hukumu hiyo baada ya mshtakiwa kusomewa shtaka na kukiri kutenda kosa
hilo.
Ilielezwa mahakamani hapo kwamba, mnamo Juni 15, 2015
majira ya saa 3:00 usiku katika Kijiji cha Ugembe II, Kata ya Mwakashanhala
wilayani Nzega, mtuhumiwa alimteka binti huyo kwa lengo la kwenda ‘kumuuza’ ili
ajipatie fedha (kiasi kimehifadhiwa).
Hii ni mara ya kwanza kwa kesi inayohusisha utekaji
nyara, kujeruhi na mauaji dhidi ya watu wenye albinism kuchukua muda mfupi
zaidi, kwani ndiyo kwanza kesi hiyo ya Jinai Namba 116/2015 imefikishwa
mahakamani kwa mara ya kwanza na kutolewa hukumu.
Jitihada za
Polisi
Mafanikio ya kukamatwa kwa Masanja Mwinamila akiwa katika
harakati za kutaka kumuuza mtoto Margreth Hamisi, ambaye ni mpwa wake,
yametokana na umakini wa Jeshi la Polisi nchini ambapo maofisa wake wa Kikosi Kazi cha Taifa waliweka
mtego na kufanikiwa kumnasa mtuhumiwa kabla hajamdhuru mateka wake.
Tukio hilo limefanikisha kuubomoa mtandao hatari wa
mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kwani ni takriban wiki tatu tu
tangu maofisa usalama walipofanikiwa kuwanasa watu wengine sita wakiwa katika
harakati za kuuza mifupa inayodhaniwa kuwa ya binadamu (albino) mjini Kahama Mei
22, 2015 ambapo tayari wamekwishafikishwa mahakamani pamoja na wengine watatu
waliokamatwa baadaye.
Matukio hayo mawili makubwa yaliyotokea katika kipindi
hicho yamedhihirisha namna serikali kupitia jeshi hilo na vyombo vingine vya
usalama inavyoshughulikia mitandao hiyo hatari usiku na mchana ili kuhakikisha
Watanzania wote wanaishi kwa amani na usalama.
Kukamatwa na hatimaye kuhukimiwa kwa Masanja Mwinamila kumedhihirisha
kwamba matukio mengi ya kuuawa au kujeruhiwa kwa watu wenye albinism yanapangwa
na kufanikishwa na wanandugu wenyewe kwa sababu ya mawazo potofu ya kutafuta
utajiri kwa njia za mkato.
Kama alivyoeleza Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora,
ACP. Juma Bwire, Juni 16, 2015, Masanja alithubutu kwenda kumnyakua mtoto huyo
Margret Hamisi (6) majira ya saa 3 usiku na kukimbia naye gizani akiwa na lengo
la kumuuza ajipatie utajiri.
Lakini habari kutoka eneo la tukio zinaeleza kwamba,
haikuwa kazi rahisi kwa wanausalama kumwokoa binti huyo akiwa hai na kumtia
mbaroni mtuhumiwa, kwani walilazimika kujifanya ‘wanunuzi’ ili kuweka mtego wa
kumkamata mtuhumiwa na kumwokoa mateka.
Taarifa za uchunguzi zinaeleza kwamba, mtuhumiwa huyo
alianza mchakato wa kutafuta ‘soko’ la kumuuza mtoto wa dada yake mapema mwezi
Juni 2015, lakini wasamaria wema wakawaarifu wanausalama kuhusu kinachotaka
kutokea katika eneo hilo.
Ilibidi maofisa wawili wa usalama wapangiwe kazi ambapo
mmoja alijifanya mnunuzi na mwingine mganga wa jadi anayeambatana na ‘tajiri’
huyo feki ambao walikutanishwa na mtuhumiwa huyo aliyewaeleza kwamba ‘dili la
albino lipo’.
“Alisema kuna dada yake mwenye albinism ambaye ana watoto
wawili – wa kiume na wa kike – ambaonao wana albinism, huyo dada ni mtoto wa
baba yake mdogo ambaye alifariki mwaka jana (2014), hivyo nyumbani hakuna mtu
wa kiume wa kuleta upinzani.
“Akasema kwamba biashara hiyo ingefanyika sana, kwani
alipanga kuanza kumuuza mtoto wa kike, halafu angemuuza yule wa kiume na
hatimaye kummalizia dada yake!” kilisema chanzo cha ndani kutoka eneo la tukio.
Kwa kawaida asilimia kubwa ya wakazi wa Kanda ya Ziwa ni
wapagani na wanawaamini waganga wa jadi kuliko mtu yeyote, hiyo alipokutanishwa
na watu hao wawili, mtuhumiwa Masanja Mwinamila aliamini kila alichoambiwa na
‘mganga’.
Mganga huyo feki, mbali ya kumpigia ramli na kumwogesha
dawa kwenye njiapanda, alimtaka mtuhumiwa kuleta mtoto huyo akiwa hai kwa
maelezo kwamba inabidi ‘afanye tambiko ili dawa zifanye kazi’, lakini lengo
likiwa kumzuia mtuhumiwa asimdhuru mtoto na hivyo kupata nafasi ya kumwokoa.
Akiwa na shauku kubwa ya kupata mamilioni ya fedha, baada
ya kukubali masharti ya mganga, Masanja alimuomba ‘tajiri’ atafute bunduki ili
wakati yeye atakapomnyakua mtoto, wafyatue risasi hewani kuwatisha watu
watakaokimbilia eneo la tukio mara yowe litakapopigwa.
Taarifa zinasema, wanausalama waliposikia kauli hiyo
wakahisi mtuhumiwa angeweza kwenda hata na panga na kuwajeruhi watu
atakaowakuta eneo la tukio ili amchukue mtoto, hivyo mganga huyo akatoa
masharti kwamba hata kama bunduki itapatikana, lakini asingependa kuona damu
inamwagika kwa yeyote huku akimwaminisha kwamba dawa atakazoogeshwa zitamfanya
awe ‘kiza’ asionekane na mtu yeyote.
Takriban mara tatu zoezi hilo liliahirishwa kwa kuangalia
mazingira ya kiusalama, lakini baada ya wanausalama kujipanga vyema, ndipo Juni
15, 2015 wakafanikisha mtego huo na kumkamata mtuhumiwa akiwa amembeba mtoto
ambaye alinyakuliwa akiwa usingizini.
“Ilikuwa ni kazi ngumu, lakini kama siyo imani kwa
mganga, ingekuwa hatari sana hata kwa wanausalama wenyewe. Jamaa alipewa masharti
kwamba, mtoto huyo anayeuzwa anatakiwa afikishwe kwa mganga akiwa hai bila
kujeruhiwa mahali popote; Familia itakayovamiwa pia isimwage damu; Fedha za
manunuzi kabla ya kukabidhiwa mlengwa lazima zifanyiwe tambiko na masharti ya
matumizi; hakutakiwa kufanya zianaa siku nne kabla ya tukio; na lazima
kuogeshwa dawa wale wote watakaokwenda kwenye tukio,” kilifafanua chanzo
kingine.
Bi. Joyce Mwandu Nkimbui (33), ambaye ni mama wa Margret,
anasema siku tatu mfululizo kabla ya tukio, mtuhumiwa huyo ambaye ni kaka yake
anayeishi jirani na hapo alikuwa akija asubuhi na jioni akijifanya kuja
kusalimia na wakati mwingine hata kupikiwa chakula.
Hata hivyo, alishangaa kukuta kwamba ndiye aliyevamia
nyumbani kwao usiku wa Juni 15, 2015 na kumwamuru asikimbie kabla yeye
hajaingia ndani na kumkwapua mtoto.
“Walikuja usiku, sijui walikuwa wangapi, lakini
wakanilazimisha ‘wewe mama tulia’, nikaogopa na kukimbilia kwenye majani,
nikaanguka kwa sababu sioni vizuri usiku, nikakutana na mwenyekiti wa
kitongoji, ambaye tulikwenda naye nyumbani na kukuta tayari mtoto hayupo,”
Joyce alisema kwa masikitiko.
Matukio mbalimbali
Tangu mwaka 2006 serikali imekuwa ikipambana na matukio
ya kuuawa na kujeruhiwa kwa watu wenye albinism nchini, ambapo tayari watu zaidi
ya 10 wamehukumiwa kunyongwa, wengine kesi zao ziko mahakamani na watuhumiwa
wengine wanaendelea kusakwa kwa kuhusika na matukio hayo ya kutisha.
Wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya wenye
albinism duniani jijini Arusha Juni 13, 2015, Rais Jakaya Kikwete alisisitiza kuwa kati ya watu 13 waliohukumiwa
kunyongwa wawili kesi zao zipo katika hatua ya mwisho kufikishwa kwake na
kuahidi zitakapofika mezani kwake atazitendea haki stahiki.
"Lakini mwaka 2014 hadi 2015
serikali tumepambana na watu wakatili dhidi ya walemavu kwa kuwakamata watu
25 kati yao sita kesi zao zipo mahakamani, huku watano upelelezi
unaendelea na 11 wameachiwa huru kwa kutopatikana na hatia," alisema.
Rais Kikwete pia aliwahakikishia wenye
albinism kupatiwa vifaa vya kupambana na kansa ya ngozi bure kwenye hospitali
za serikali.
Mwaka 2009, Waziri Mkuu Mizengo Pinda
aliangua kilio bungeni kuonyesha uchungu alionao dhidi ya vitendo vya mauaji ya
kikatili ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), na machozi yake yakayeyusha
hoja ya wabunge wa upinzani waliokuwa wamepania kumbana, ili ajiuzulu kwa madai
kwamba, alitoa amri ya kuua wauaji ambayo ni kinyume na katiba ya nchi.
No comments:
Post a Comment