TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI JUU YA KUPOTEA KWA BEN
Leo
Umoja wa Kizazi cha kuhoji Tanzania (UTG) umefanya mkutano na waandishi
wa habari kuelezea suala la kupotea kwa Katibu wao Ndugu Ben Saanane na
suala la kuokotwa kwa miili ya watanzania 7 huko Bagamoyo.
Vyombo vya habari vilivyoshiriki:
1. Televisheni (ITV, StarTV, na Clouds TV)
1. Televisheni (ITV, StarTV, na Clouds TV)
2. Radio (Radio One, East Africa Radio, Wapo Radio, Clouds Fm).
3.
Magazeti (Tz Daima, Mwananchi, HabariLeo, Citizen, The Guardian,
Majira, Mtanzania, Uhuru, Mzalendo, MwanaHalisi, JamboLeo, Nipashe).
Ifuatayo ni sehemu ya taarifa ya UTG kwa vyombo vya habari:
______________________________________________
______________________________________________
UMOJA WA KIZAZI CHA KUHOJI TANZANIA/ THE UNION OF THINKING GENERATION (UTG).
Taarifa kwa vyombo vya habari
_____________________________
_____________________________
Ndugu waandishi wa Habari,
Awali ya yote tunawashukuru kwa kukubali wito wetu na kushiriki mkutano huu ambao utatupa fursa ya kuwasilisha hoja zetu kwa watanzania.
Awali ya yote tunawashukuru kwa kukubali wito wetu na kushiriki mkutano huu ambao utatupa fursa ya kuwasilisha hoja zetu kwa watanzania.
Umoja
wa kizazi cha kuhoji Tanzania (UTG) ni kundi huru la vijana wa
kitanzania kutoka maeneo mbalimbali ya nchi lililoanzishwa kwa malengo
ya kuibua mijadala mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika
mambo yanayolikabili taifa letu. Mijadala hiyo hufanyika kwa njia
mbalimbali ikiwa ni pamoja na mijadala ya wazi (open forums) au kupitia
mitandao ya kijamii.
Ndugu
waandishi wa habari kiini cha mijadala hii ni kutoa fursa kwa watu
mbalimbali hasa vijana kujadili, kuhoji, na kutoa mapendekezo yenye tija
kwa taifa kuhusiana na mambo mbalimbali yanayolikabili taifa.
Asasi
hii haifungamani na chama chochote cha siasa, wala dhehebu lolote la
kidini. Ni kikundi huru chenye wanachama kutoka vyama mbalimbali vya
siasa na wengine wasio na vyama.
Ndugu waandishi wa habari,
Tumewaita hapa ili kuzungumza nanyi juu ya mambo mawili yanayolikabili taifa letu kwa sasa. Mosi ni kuhusu kupotea kwa Katibu wetu wa UTG Tanzania Ndg.Benard Focus Rabiu Saanane, na pili ni kuhusu kuokotwa kwa miili ya watanzania wenzetu katika eneo la mto Ruvu huko Bagamoyo.
Tumewaita hapa ili kuzungumza nanyi juu ya mambo mawili yanayolikabili taifa letu kwa sasa. Mosi ni kuhusu kupotea kwa Katibu wetu wa UTG Tanzania Ndg.Benard Focus Rabiu Saanane, na pili ni kuhusu kuokotwa kwa miili ya watanzania wenzetu katika eneo la mto Ruvu huko Bagamoyo.
1. KUPOTEA KWA KATIBU WA UTG NDG.BEN SAANANE.
Ndugu waandishi wa habari,
Mnamo tarehe 18 November mwaka huu (2016), Katibu wa kundi hili Ndugu Benard Focus Saanane au maarufu kama Ben Saanane aliondoka nyumbani kwake maeneo ya Tabata jijini Dar es Salaam, na tangu siku hiyo hajaonekana tena hadi leo yapata siku 24.
Mnamo tarehe 18 November mwaka huu (2016), Katibu wa kundi hili Ndugu Benard Focus Saanane au maarufu kama Ben Saanane aliondoka nyumbani kwake maeneo ya Tabata jijini Dar es Salaam, na tangu siku hiyo hajaonekana tena hadi leo yapata siku 24.
Tukio
la kupotea kwa Ndugu Saanane lilianza kuibua mijadala kuanzia tarehe 26
November mwaka huu baada ya Ben kutokuonekana nyumbani kwake Tabata, na
katika eneo lake la kazi ambalo ni Makao makuu ya chama cha demokrasia
na maendeo (CHADEMA).
Baada
ya siku kadhaa za kutokujulikana alipo, familia yake ikawasiliana na
watu mbalimbali wa karibu na Ben kujua kama wana taarifa yoyote kuhusu
Ben alipo. Baada ya kukosa taarifa kuhusu Ben alipo familia
ikishirikiana na uongozi wa UTG ilichukua hatua kadhaa kama ifuatavyo:
1.
Kutoa taarifa Makao makuu ya Jeshi la Polisi na katika kituo cha Polisi
Tabata mnamo siku ya jumatatu ya tarehe 05/12/2016 na kupewa RB namba
TBT/RB/8150/2016 ambapo pamoja na mambo mengine Polisi walitoa ruhusa ya
kumtafuta Ben maeneo mbalimbali.
2.
Jumatatu hiyo ya tarehe 05/12/2016 iliundwa kamati maalumu yenye
wajumbe kutoka UTG na baadhi ya wanafamilia na kuanza kumtafuta Ben
maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam ikiwemo Mahospitalini ambapo
ilitembelea hospitali ya Amana, Temeke, Mwananyamala na Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili. Kote huko kamati hiyo ilipewa ushirikiano wa kutosha
na kukagua vyumba vya wagonjwa mahututi, orodha ya wagonjwa waliolazwa
hospitalini humo wasiotambulika (unknown cases) na katika vyumba vya
kuhifadhia maiti lakini hakupatikana.
3.
Baada ya kumkosa Ben katika hospitali hizo kamati ilitoa mrejesho
Polisi na kuomba wawasiliane na vituo vyao ili kujua kama Ben
ameshikiliwa mahabusu katika kituo chochote cha Polisi jijini Dar.
Polisi waliijibu kuwa Ben hajashikiliwa katika kituo chao chochote
jijini Dar.
Kamati
iliomba kujiridhisha kwa kupita katika vituo hivyo na kukagua. Kati ya
tarehe 6 na 7 mwezi huu kamati ilipita na kukagua mahabusu katika vituo
vyote vikubwa vya Polisi jijini Dar vikiwemo Kituo cha Polisi Oysterbay,
Mabatini, Urafiki, Magomeni, Buguruni, Chang'ombe na kituo cha Polisi
Sitaki shari lakini Be hakupatikana katika vituo hivyo, wala hakuwemo
katika orodha ya mahabusu waliowahi kufikishwa katika vituo hivyo.
4.
Baada ya hapo kamati ilipata fursa ya kwenda kuuliza katika magereza
mawili jijini Dar es Salaam yanayohifadhi Mahabusu, (gereza la Segerea
na gereza la Keko) lakini hakupatikana huko pia.
5.
Baada ya kumkosa huko kote kamati ilienda idara ya uhamiaji makao makuu
ili kujua kama Ben amesafiri nje ya nchi, lakini ilionekana kwamba Ben
hajasafiri nje ya nchi kwa kipindi cha mwezi November wala December.
Taarifa
ya Idara ya uhamiaji kuwa Ben hajasafiri nje ya nchi ilitoa tafsiri
kuwa Ben bado yupo nchini. Lakini maswali yanabaki yupo wapi? Yupo
katika hali gani? Je amekufa au yupo hai? Kwanini taarifa zake hazipo
wazi?
6.
Kufuatia sintofahamu hiyo kamati ilienda mamlaka ya mawasiliano nchini
TCRA ili kupata taarifa za mawasiliano ya mwisho ya Ben ambazo
zingesaidia kufumbua kitendawili cha alipo Ben.
TCRA
waliieleza kamati kuwa jukumu hilo ni la kampuni ya simu kupitia jeshi
la Polisi, na hivyo Polisi wanapaswa kuandika barua kwenye kampuni
husika ya simu kuomba taarifa za mawasiliano ya Ben. Polisi walichukua
upya maelezo ya tukio hilo na kuahidi kuandika barua hiyo kwenye kampuni
husika ya simu ili kupata mawasiliano yake.
Lakini
hadi sasa kamati hiyo haijapata mawasiliano hayo kwa madai kuwa bado
kampuni husika ya simu haijawasilisha taarifa hiyo kwa jeshi la Polisi.
7.
Tarehe 08/12/2016 ziliripotiwa taarifa za kuokotwa kwa miili ya watu
huko Bagamoyo eneo la mto Ruvu. Kwa kuwa familia na uongozi wa UTG
zilikua katika taharuki ya kupotea kwa Ben kamati ililazimika kusafiri
kwenda Bagamoyo kujiridhisha kama miili iliyookotwa inahusiana na Ben
kwa namna moja au nyingine.
Kamati
inayofuatilia suala hili ilipofika ilikuta miili yote imeshazikwa bila
kuacha kielelezo chochote. Tarehe 09/12/2016 kamati ikiwa bado Bagamoyo
ilishuhudia maiti nyingine moja ikielea katika mto Ruvu, eneo lilelile
zilipopatikana maiti za awali. Polisi walifika na kuichukua maiti hiyo,
na ilipoikaguliwa iliridhika kuwa sio ya Ndugu Ben Saanane.
*2. KUOKOTWA KWA MIILI YA WATU 7 KATIKA ENEO LA MTO RUVU, KATA YA MAKURUNGE, WILAYANI BAGAMOYO.
Ndugu waandishi wa habari,
Kama tulivyowaeleza hapo awali kuwa iliokotwa miili ya watu 6 siku ya jumatano tarehe 7/12/2016 katika kingo za mto Ruvu kijiji cha Mtoni, kata ya Makurunge na maiti nyingine moja ijumaa ya tarehe 09/12/2016 katika eneo hilohilo na kufanya jumla ya maiti zilizopatikana kuwa 7.
Kama tulivyowaeleza hapo awali kuwa iliokotwa miili ya watu 6 siku ya jumatano tarehe 7/12/2016 katika kingo za mto Ruvu kijiji cha Mtoni, kata ya Makurunge na maiti nyingine moja ijumaa ya tarehe 09/12/2016 katika eneo hilohilo na kufanya jumla ya maiti zilizopatikana kuwa 7.
Taarifa ya kupatikana miili hiyo ni ya kuogofya na kushtua hasa kutokana na namna miili hiyo ilivyookotwa.
Miili
6 ya awali ilikua imewekwa ndani ya mifuko ya sandarusi na ndani
iliwekewa mawe ili isielee, kisha mifuko hiyo kushonwa na kutupwa mtoni.
Mwili mwingine mmoja uliopatikana tarehe 09 haukua ndani ya sandarusi
lakini ulikua umevuliwa shati na kuonekana na majeraha mgongoni na
kwenye ubavu kama vile umejeruhiwa na kitu chenye ncha kali.
Mazingira ya kupatikana kwa maiti hizo na hali ilizokua nazo ni viashiria kuwa sio vifo vya kawaida.
Mazingira
ya maiti hizo yanaashiria vitu viwili. Mosi huenda watu hao waliuawa
kabla ya kutupwa mtoni au walijeruhiwa kabla ya kuwekwa kwenye mifuko
hiyo wakiwa hai na kutupwa katika mto huo na kufia humo.
Sisi
kama Umoja wa Kizazi cha Kuhoji Tanzania tunasikitika sana kuona jambo
hili la vifo vya watanzania wenzetu likipewa uzito mdogo na taasisi
zenye wajibu wa kushughulikia jambo hili.
Ni
ajabu kwamba hadi Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Pwani
haijachukua hatua zinazoridhisha juu ya jambo kubwa kama hili. Taarifa
tuliyoipata kutoka ofisi ya serikali ya kijiji cha Makurunge inaeleza
kuwa hadi kufikia tarehe 10/12/2016 hakuna kiongozi yeyote wa serikali
kuu aliyekua amefika eneo hilo. Si Waziri, Mkuu wa mkoa wa Pwani wala
Mbunge wa eneo husika waliokua wamefika eneo hilo.
Ni
jambo la kustaajabisha kwamba watu 7 wanaweza kupoteza uhai wao katika
mazingira yenye utata na serikali isichukue hatua za kuridhisha wala
Waziri kutoa tamko. Ikumbukwe ni serikali hiihii ambayo mawaziri wake
watatu walitoa tamko kufuatia mwanafunzi mmoja kuadhibiwa huko mkoani
Mbeya na waalimu wa mazoezi kwa madai kuwa ni ukatili, lakini hakuna
Waziri yeyote aliyetoa tamko kuhusiana na suala la miili iliyookotwa
Bagamoyo.
Ikiwa
adhabu kwa mwanafunzi ilipewa uzito na kufanya mawaziri watatu kutoa
tamko, lakini hakuna waziri hata mmoja aliyetoa tamko kwenye suala hili
la Bagamoyo, sisi kama umoja wa kizazi cha kuhoji tunatilia shaka
utendaji wa serikali.
Haiwezekani
adhabu kwa mwanafunzi mmoja iwe na uzito mkubwa kuliko uhai wa
watanzania 7. Serikali inayoona adhabu kwa mwanafunzi mmoja ni ukatili
kuliko vifo vya watanzania 7 ni serikali isiyojali watu wake.
Serikali
imekaa kimya kuhusu maiti 7 zilizookotwa Bagamoyo lakini ipo busy
kufuatilia suala la kupotea kwa Faru mmoja aitwae John katika hifadhi ya
Ngorongoro. Suala la Faru huyo limepewa uzito mkubwa kiasi cha baadhi
ya mawaziri kuhangaika usiku na mchana kujua alipo Faru huyo, lakini
suala la vifo vya watanzania wenzetu na miili yao kutupwa mto Ruvu
halijapewa uzito wowote.
Haiwezekani
katika taifa letu Faru mmoja awe na thamani kuliko maisha ya watanzania
7. Hatumaanishi kuwa suala la Faru lipuuzwe, hapana. Tunamaanisha suala
la Faru lipewe uzito lakini suala la vifo vya watanzania wenzetu lipewe
uzito zaidi. Tunathamini rasilimali za nchi lakini tunapaswa kuthamini
zaidi maisha ya watanzania. Rasilimali zetu hazitufai kitu ikiwa maisha
yetu hayathaminiwi.
Tunaamini
Waziri wa mambo ya Ndani Mhe.Mwigulu Nchemba ni mtendaji mzuri na
anayechukua hatua kwa wakati katika mambo yanayohusu wizara yake. Hata
lilipotokea tulio la mauaji ya askari kule Chamazi (Mbande) Mhe.Mwigulu
alifika eneo la tukio usiku huohuo. Lakini tumeshangazwa na ukimya wake
kwenye suala hili la kuokotwa kwa miili ya watanzania wenzetu huko
Bagamoyo.
Tumesikitishwa
pia na kitendo cha Jeshi la Polisi kuamua kuizika miili hiyo bila
kuacha vielelezo vyovyote huku jeshi hilo likiwa na taarifa ya baadhi ya
watanzania kupotelewa na ndugu zao. Hii si sahihi hata kidogo.
Wapo
watanzania wametoa ripoti za kupotelewa na ndugu zao katika vituo
mbalimbali vya polisi nchini, ikiwemo familia ya Ndugu Ben Saanane, sasa
kwanini polisi waamue kuzika miili hiyo bila kusubiri uchunguzi?
Utetezi
uliotolewa na Polisi kwamba miili hiyo ilikua imeharibika hauna mashiko
kwani tunaamini vingeweza kupatikana vinasaba ambavyo vingewasilishwa
ofisi ya mkemia mkuu wa serikali kwa ajili ya uchunguzi.
Lakini
Polisi kuamua kuizika miili hiyo bila hata kuacha vipande vya nguo za
marehemu ni jambo linalotilia shaka weledi wa jeshi hili.
Pia
eneo ilipokutwa miili hiyo halina doria wala ulinzi wowote nyakati za
usiku. Utafiti ulioufanywa na kamati unaonesha kuwa eneo hilo limekuwa
na historia ya matukio ya kutisha kwa muda mrefu lakini halina ulinzi
wowote.
Pia
kupatikana kwa miili ya watu 6 waliowekwa kwenye mifuko ya sandarusi
iliyojazwa mawe ndani ni kielelezo kuwa maiti hizo hazikutupwa mbali na
eneo hilo. Si rahisi maiti zisafirishwe kwa maji kwa eneo kutoka nje ya
Bagamoyo wakati zina mawe ndani na bila mifuko iliyohifadhia
haijaharibika.
Kama
maiti hizo zilisafirishwa kwa magari kutoka maeneo ya mbali zikiwa
kwenye mifuko na kwenda kutupwa eneo hilo inawezekanaje wakati njiani
kuna askari polisi wanaokagua magari?
Na
ikiwa watu hao walisafirishwa wakiwa hai kama mateka na kwenda kuuawa
eneo la jirani na mto huo na kuwekwa kwenye mifuko ya sandarusi na
kutupwa mtoni, je inawezekanaje watu 7 kusarishwa kama mateka bila
Polisi kujua? Bado maswali ni mengi kuliko majibu.
Vilevile
tunasikitishwa na kitendo cha Idara ya Afya wilaya ya Bagamoyo
kushindwa kuchukua hatua. Baada ya maiti hizo kuonekana eneo hilo la mto
bado watu waliendea kutumia maji ya mto huo katika matumizi mbalimbali.
Kamati
ilifika eneo hilo na kushuhudia maiti zikiwa mtoni na pembezoni kidogo
wananchi wakichota maji ya kunywa, ya kupikia na shughuli zingine. Maana
yake ni kwamba kuna watu walikunywa, na kupikia maji yaliyotokana na
maiti. Hii ni hatari sana kwa afya za wakazi wa kata ya Makurunge na
maeneo jirani kwa sababu inaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa.
Pia
tunasikitishwa na utaratibu uliotumika kuizika miili iliyookotwa, kwa
sababu haikuzikwa kama binadamu, wala haikupewa heshima bali ilifukiwa
katika shimo moja watu wawili. Tunaamini binadamu anastahili kusitiriwa
na kupewa heshima hata anapokua maiti, kwa hiyo haikua busara kuzika
maiti mbili kwenye shimo moja tena kwa kuwafukia tu kwenye mashimo kama
mizoga.
MAPENDEKEZO:
Kutokana
na matukio hayo mawili hapo juu (la kupotea kwa Ndugu Ben Saanane na
kuokotwa kwa miili ya watu 7 huko Bagamoyo, UTG inatoa mapendekezo
yafuatayo:
1.
Vyombo husika kutoa taarifa ya mawasiliano ya Ndugu Ben Saanane kama
yalivyoombwa na familia yake. Tunasikitika sana kwa uhirikiano hafifu
kamati iliopata kutoka Jeshi la Polisi na kampuni husika ya simu ambayo
Ben alikua akitumia mtandao wao.
Tangu
taarifa hiyo imeombwa kumekua na uchelewashwaji bila sababu zozote za
msingi licha ya kukamilisha taratibu zote za kisheria zinazotoa haki ya
kupata mawasiliano hayo.
2.
Vyombo vya habari vitoe uzito kwenye matukio yanayohusu uhai wa
watanzania kuliko matukio mengine yoyote kwa sababu uhai wetu ni muhimu
kuliko jambo jingine lolote. Tumesikitishwa kuona magazeti yote
yaliandika habari ya Faru aliyepotea Ngorongoro lakini ni gazeti moja tu
lililoandika habari za kupotea kwa ndugu Ben Saanane. Pia ni magazeti
machache yaliyoandika habari za maiti zilizopatikana Bagamoyo.
Tunawataka
waandishi wa habari wazingatie weledi katika kuandika. Moja ya mambo
yanayoweza kuipa uzito habari ni suala la ukubwa wa habari yenyewe
(magnitude). Ni ajabu kwamba habari ya kupotea kwa Faru mmoja imeonekana
kubwa kuliko kupotea kwa mtanzania mwenzetu Ndg.Ben Saanane au kuokotwa
kwa miili ya watanzania wenzetu huko Bagamoyo.
3.
Tunakitaka chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) ambayo ndiyo
taasisi Ben Saanane aliyokua akiifanyia kazi, kuchukua hatua za
kiridhisha dhidi ya suala hili. Zipo taarifa kwamba Chadema wanafuatilia
jambo hili na watachukua hatua, lakini sisi kama UTG hatujaridhishwa na
namna chama hicho kinavyochelewa kuchukua hatua. Ben amekua mtumishi wa
Chadema wa muda mrefu, hivyo hatuoni kama ni sahihi kwa chama hicho
kushindwa kutoa tamko lolote hadi leo, ikiwa ni siku 24 sasa tangu
apotee.
4.
Tunazitaka taasisi zote za haki za binadamu zijitokeze hadharani na
kupiga kelele juu ya mambo haya mawili makubwa katika taifa. Zipige
kelele Ben apatikane akiwa hai, na zipige kelele Serikali ichukue hatua
dhidi ya maiti zilizookotwa Bagamoyo.
Ikiwa
Watanzania wanaweza kupotea na wasijulikane walipo, na wengine kuokotwa
wakiwa maiti na wasijulikane walipotoka ni dalili kwamba nchi hii sio
salama. Ziko wapi taasisi kama Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu? Iko
wapi Tume ya Haki za binadamu na Utawala bora? Wanasubiri nini kutoa
tamko juu ya mambo haya yanayotishia usalama wa raia?
5.
Jeshi la Polisi liimarishe doria katika eneo la mto Ruvu mahali
palipokutwa maiti hizo, na maeneo mengine kando ya mto huo yenye
changamoto za kiusalama. Pia Jeshi hilo lifanye uchunguzi na kuchukua
hatua kwa wote watakaobainika kuhusika na matukio hayo.
6.
Tunaitaka serikali kwa kushirikisha taasisi zake kama wizara ya afya,
ofisi ya mkemia mkuu wa serikali, na jeshi la polisi iratibu zoezi la
kufukua miili iliyozikwa ili kupata sampuli zitakazotumika kutambua
ndugu wa marehemu watakapojitokeza.
7.
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Pwani na Kamati ya Ulinzi na
Usalama wilaya ya Bagamoyo zijitathmini kuona kama zinastahili kuendelea
kuwepo madarakani. Ikiwa mkuu wa mkoa wa Pwani hajafika eneo la tukio
siku 4 baada ya maiti hizo kupatikana ajitathmini kama bado anastahili
kuendelea kuongoza mkoa huo.
Mamlaka
yake ya uteuzi pia ifikirie upya juu ya nafasi yake. Wapo wakuu wa
mikoa na wilaya wanaowajibika na kuchukua hatua katika mambo yanayohusu
raia. Tumeshuhudia mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam akishughulikia matatizo
mbalimbali ya wananchi hata katika ngazi ya mtaa, lakini mkuu wa mkoa
wa Pwani ameshindwa hata kutoa tamko tu la kulaani kitendo kilichotokea
mkoani kwake.
8.
Jukumu la kwanza la Jeshi la Polisi ni kulinda usalama wa raia na mali
zao. Ikiwa Polisi mkoa wa Pwani umeshindwa kutimiza jukumu hili, basi
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Pwani na Wilaya ya Bagamoyo wajitathmini
kama bado wanastahili kuendelea kuwepo katika nafasi zao.
9.
Pia kitendo cha Mbunge wa Bagamoyo Prof.Shukuru Kawambwa kushindwa
kufika eneo la tukio hata kutoa pole kwa wakazi wa kijiji cha Mtoni na
Kata ya Makurunge kinatosha kumfanya ajitathmini kama kweli yeye ni
mwakilishi wa wananchi.
10.
Pia idara ya afya wilaya ya Bagamoyo ijitathmini na iwajibike kwa
kushindwa kuchukua hatua kulinda afya za wakazi wa maeneo ilipookotwa
miili hiyo. Ikiwa watu walikunywa, kuoga na kupikia maji yaliyogusana na
maiti za binadamu, na idara ya Afya haikuchukua hatua yoyote basi ina
kila sababu ya kuwajibika.
Mwisho
tuhitimishe kwa kunukuu maneno ya Mwalimu Julius Nyerere aliyosema kuwa
"Binadamu wote ni ndugu, na Afrika ni moja. Ni wajibu wa kila mmoja
wetu kuulinda, kuutetea na kuuthamini utu wa binadamu mwingine". Kwa
maneno hayo ya Nyerere tunataka serikali ichukue hatua ya kumtafuta na
kumpata Ndugu Ben Saanane akiwa hai, na serikali ichukue hatua za
kuridhisha dhidi ya miili ya watanzania wenzetu iliyookotwa huko
Bagamoyo.
Asanteni,
Imetolewa na:
Malisa Godlisten,
M/kiti UTG
M/kiti UTG
Noel Shao
Naibu Katibu UTG.
Naibu Katibu UTG.
No comments:
Post a Comment