Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Kigwangalla akitoa hotuba yake katika semina hiyo. Kushoto ni Mwasisi wa Taasisi ya Millen Magese, Millen Happiness Magese. (Picha na Video na Andrew Chale,Modewjiblog).
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imesema kuwa ipo tayari kushirikiana na wadau mbalimbali akiwemo Mwanadada Millen Magese na Taasisi yake katika mapambano ya ugonjwa na athari za Endometriosis ambao unawapata wanawake wengi hapa nchini.
Kauli hiyo imetolewa mapema leo Machi 30.2016 na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Kigwangalla wakati wa kufungua rasmi semina maalum kwa vijana wapatao 500 wa shule za Sekondari zikiwemo za Turiani Sekondari, Makurumla na zinginezo za Manispaa ya Kinondoni pamoja na walezi na walimu, ambapo katika mkutano huo, Dk. Kigwangalla amebainisha kuwa, juhudi zinazofanywa na Mwanadada Millen Magese ni za kuungwa mkono hivyo wataendelea kushirikiana naye bega kwa bega.