Mh. Katibu MKuu, Chama Cha Demokrasia Na Mendeleo HSE NO 170,
UFIPA STREET, KINONDONI
S. L. P 31191
Dar es Salaam – Tanzania.
YAH: MASHATAKA YA UKIUKWAJI WA KATIBA, KANUNI NA MWONGOZO WA CHAMA.
Rejea
barua yako ya tarehe 26 Novemba 2013 yenye kumbukumbu no
C/HQ/ADM/KK/08/31 Iliyoelezea maamuzi yaliyofikiwa na kikao cha Kamati
Kuu ya Chama cha tarehe 20-22 Novemba 2013, kiliazimia kwamba niachishwe
nafasi zote za uongozi ninazoshikilia katika chama na kwamba Kamati Kuu
iliazimia kwamba hatua zaidi za kinidhamu za kuachishwa ama kufukuzwa
uanachama zichukuliwe dhidi yangu kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za
Uendeshaji za 6.5.2(d), ningependa kuwasilisha majibu ya mashtaka hayo
kama ifuatavyo;
1.0 MAELEZO YA AWALI; Napenda
kuwasilisha utetezi wangu huku nikiwa napinga utaratibu uliotumika
kuandaa na kunifikishia mashtaka husika (Defence Under Protest) kwa
sababu zifuatazo;
1.1. Hatua za kinidhamu
ambazo kimsingi ni adhabu zimeshachukuliwa na Kamati Kuu kwa mashtaka
haya haya ambayo nimepatiwa. Kama barua yako inavyosema na nanukuu
maneno yako “Kamati Kuu kwa kutumia mamlaka yake kwa mujibu wa Kanuni ya
6.5.2(d) ya Kanuni za Uendeshaji Shughuli za Chama (‘Kanuni za
Uendeshaji’), iliazimia kwamba muachishwe nafasi zote za uongozi
mnazoshikilia katika Chama…” (msisitizo ni wangu). Mheshimiwa Katibu
Mkuu; Ni wazi kabisa kwamba adhabu ya kuachishwa nafasi zote za uongozi
imeshatekelezwa. Kamati Kuu imeshanitia hatiani kwa makosa haya haya
ambayo sasa hivi natakiwa nijitetee. Binafsi siamini kwamba kwa
utaratibu huu haki itatendeka na inaonekana kutendeka. Ni vigumu sana
kusema kwamba haki yangu ya msingi ya kusikilizwa na kujitetea imelindwa
wakati tayari adhabu imeshatolewa na chombo kile kile ninachotakiwa
kujitetea mbele yake.
1.2. Kama kiongozi ambaye nimeadhibiwa na Kamati Kuu ninayo haki ya kukata rufaa Baraza Kuu dhidi ya haya yafuatayo;
1.2.1. utaratibu uliotumika na Kamati Kuu kunivua nyadhifa zote za uongozi.
1.2.2. sababu zilizotumika kunivua nyadhifa zote za uongozi.
Mheshimiwa Katibu Mkuu;
Katiba ya Chama pamoja na Kanuni za Uendeshaji zinatoa HAKI hii ya msingi na UTARATIBU kwa maneno haya;
Ibara
6.3.6(d) ya Katiba ya Chama; “Kiongozi aliyechukuliwa hatua za
kinidhamu na mamlaka yake ya nidhamu anayo haki ya kukata rufaa ngazi ya
juu ya ile mamlaka yake ya nidhamu na uamuzi wa ngazi hiyo utakuwa wa
mwisho”.
Ibara 6.3.6(e) ya Katiba ya Chama;
“Rufaa yoyote lazima ifanyike katika muda wa siku thelathini tangu
tarehe ya kupokea rasmi kwa maandishi maamuzi ya mamlaka iliyotoa
adhabu”. Mheshimiwa Katibu Mkuu; Kanuni za Uendeshaji zinatoa UTARATIBU
ambao unatakiwa ufuatwe ili kiongozi aliyeadhibiwa aweze kutumia HAKI
yake ya kukata rufani kwa maneno haya; Kanuni ya 6.5.8 ya Kanuni za
Uendeshaji; “Kiongozi aliyeadhibiwa atapewa taarifa ya msingi wa maamuzi
ya mamlaka ya nidhamu ili kumuwezesha kuamua kukata rufani au la”
Kanuni
ya 6.5.9 ya Kanuni za Uendeshaji; “Mwadhibiwa atakayeamua kukata rufani
atatakiwa kufanya hivyo katika muda wa siku thelathini baada ya
kuarifiwa uamuzi wa adhabu” Kanuni ya 6.5.10 ya Kanuni za Uendeshaji;
“Baada ya kutoa uamuzi kikao husika kinalazimika kuandaa taarifa kamili
ya mwenendo wa shauri na kuwasilisha ngazi ya juu. Taarifa hiyo lazima
ifike katika muda wa siku kumi na nne baada ya kikao cha mamuzi”
Mheshimiwa Katibu Mkuu;
Mpaka
tarehe 01/12/2013 siku ambayo nimepokea barua yako ya mashtaka dhidi
yangu sijapokea taarifa ya msingi wa maamuzi ya mamlaka ya nidhamu na
pia taarifa kamili ya mwenendo wa shauri langu haujawasilishwa Baraza
Kuu. Wakati hayo yote hayajafanyika natakiwa kutoa utetezi wangu wa
maandishi kwa mujibu wa Kanuni ya 6.5.2(a) ikisomwa pamoja na Kanuni ya
6.5.6 ya Kanuni za Uendeshaji kwa makosa yaleyale ambayo tayari
nimeshaadhibiwa na Kamati Kuu. Ni wazi kabisa kwamba barua yako ya
mashtaka ni muendelezo wa hatua au maazimio ya Kamati Kuu kama
ilivyoandikwa “Aidha Kamati Kuu iliazimia kwamba hatua zaidi za
kinidhamu za kuachishwa ama kufukuzwa uanachama zichukuliwe….”
Mheshimiwa Katibu Mkuu;
Utaratibu
uliotumika na Kamati Kuu sio wa HAKI na ni ukiukaji wa Katiba na Kanuni
za Uendeshaji. Nalazimika kutoa utetezi wangu nikiwa napinga (under
protest) kwa sababu kwa Chama ambacho kinasifika kwa kupigania misingi
ya utawala bora na utawala wa sheria ni lazima kiheshimu haki za
wanachama na viongozi wake pamoja na kufuata utaratibu kilichojiwekea
wakati wa kuchukua hatua za kinidhamu. 1.3. Baadhi ya wajumbe wa Kamati
Kuu kwa nyakati mbalimbali wametoa matamko kwamba tumefukuzwa uongozi na
hatua zaidi zitachukuliwa dhidi yetu kabla hata ya ofisi yako kutoa
Mashtaka dhidi yetu. Mheshimiwa Tundu Lissu na Mheshimiwa John Mnyika
walitoa matamko hayo wakati wakiongea na Waandishi wa Habari.
Mheshimiwa Katibu Mkuu;
Kitendo
cha wajumbe hao kutoa misimamo kwa niaba ya Chama au Kamati Kuu ni
ukiukwaji wa haki yangu ya msingi ya kusikilizwa. Ni wazi kabisa kwamba
tayari hukumu dhidi yangu imeshapitishwa kabla sijasikilizwa. Sina imani
na wajumbe ambao tayari wameonyesha waziwazi misimamo yao kuhusu tuhuma
dhidi yangu.
Mheshimiwa Katibu Mkuu;
Kutokana
na hayo yote ambayo nimeyataja hapo juu naomba ofisi yako isitishe
utekelazaji wa maamuzi au maazimio ya Kamati Kuu mpaka pale ambapo
nitakuwa nimepatiwa taarifa ya msingi wa maamuzi ya Kamati Kuu na kuweza
kukata rufaa ngazi ya juu kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Uendeshaji.
Hatua zozote za Kamati Kuu zitaendelea kukiuka Katiba na Kanuni za
Uendeshaji.
Bila kuathiri hayo niliyoyasema;
1
UTETEZI WANGU DHIDI YA MASHTAKA Mheshimiwa Katibu Mkuu; Kwa ujumla
nakanusha na kukataa kuhusu tuhuma zinazoelekezwa kwangu kuhusu
kinachoelezwa kwamba niliandaa mkakati wa mabadiliko 2013, mimi binafsi
sijawahi kushiriki, kuhusika kuandaa au kufahamu kwa namna yoyote ile
kinachoitwa waraka wa Mkakati wa Mabadiliko 2013 kama ulivyoainisha
kwenye barua yako.
KOSA LA KWANZA
Kukashifu
Chama kiongozi au mwanachama yeyote wa chama kinyume na masharti ya
10.1(xii) ya Kanuni za Uendeshaji. Mheshimiwa Katibu Mkuu;
1.
Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba
na Mtu mwingine ambaye hajajulikana niliandaa waraka ulioitwa Mkakati wa
Mabadiliko 2013.
2. Sijawahi kushiriki kwa
njia yoyote kuandaa waraka huo peke yangu au nikiwa na mtu mwingine
yeyote. Nakanusha kumkashifu Mwenyekiti wa Chama Taifa kwa njia yoyote
ile.
3. Kuhusu kutoa kashfa kwa Katibu Katibu
Mkuu wa Chama na Mbunge wa Arusha Mjini Mh. Godbles Lema kama
ulivyoainisha kwenye barua yako mimi binafsi sijawahi kutoa kashfa hizo
na wala kuhusika kwa namna yoyote ile kwenye maandalizi ya mkakati huo
wa mabadiliko.
KOSA LA PILI
Kutokuwa
wakweli na wawazi wakati wote na kushirikiana na vikundi vya majungu na
wadanganyifu (rumour mongers) Kinyume na Kanuni ya Uendeshaji 10.1
(vii) ya Kanuni za Uendeshaji. Mheshimiwa Katibu Mkuu;
1.
Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba
na Mtu mwingine ambaye hajajulikana nilianzisha mtandao wa siri ulioitwa
“Mtandao wa Ushindi’ ili kuniwezesha mimi kutwaa madaraka ya Mwenyekiti
wa Chama Taifa kwa njia zilizo kinyume na Katiba, Kanuni za Uendeshaji
na Kanuni za Kusimamia Shughuli, Mwenendo na Maadili ya Wabunge wa
CHADEMA na Mwongozo wa Kutangaza Kusudio la Kuwania Nafasi za Uongozi
Kwenye Chama, Mabaraza na Serikali 2012.
2. Nakanusha kuanzisha, kushiriki uanzishwaji au kuufahamu unaoitwa mtandao wa ushindi kama ilivyoelezwa na barua yako.
3.
Siku zote nimekuwa mkweli muwazi kwa yale ninayoyaamini na katika
kutekeleza majukumu yangu kama kiongozi na mwanachama mtiifu wa CHADEMA.
Pia sijashirikiana na kikundi chochote cha majungu au wadanganyifu kama
iliyoainishwa kwenye barua yako.
KOSA LA TATU
Kutoa
tuhuma juu ya viongozi wenzenu pasipo kupitia vikao halali na
kuzingatia taratibu na ngazi zilizowekwa kwenye Kanuni kinyume na Kanuni
ya 10.1(x) ya Kanuni za Uendeshaji. Mheshimiwa Katibu Mkuu;
1.
Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba
na Mtu mwingine ambaye hajajulikana nilitoa tuhuma nzito na za uongo
dhidi ya viongozi wakuu wa Chama, yaani Mwenyekiti wa Chama Taifa na
Katibu Mkuu pasipo kupitia vikao halali na bila kuzingatia taratibu na
ngazi zilizowekwa na Kanuni za Uendeshaji.
2. Sijawahi
kushiriki kwa njia yoyote kuandaa waraka huo peke yangu au nikiwa na mtu
mwingine yeyote. Nakanusha kwamba nilitoa tuhuma nzito na za uongo
dhidi ya viongozi wakuu wa Chama, yaani Mwenyekiti wa Chama Taifa n
Katibu Mkuu pasipo kupitia vikao halali na bila kuzingatia taratibu na
ngazi zilizowekwa na Kanuni za Uendeshaji.
KOSA LA NNE
Kujihusisha
na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini, au ukanda ambavyo vina
makusudi ya kubaguana ndani ya chama na miongoni mwa jamii kisiasa au
kijamii na Kanuni ya 10.1(iv) ya Kanuni za Uendeshaji. Mheshimiwa Katibu
Mkuu;
1. Nakanusha kwamba nimejihusisha
katika kuanzisha, kushiriki uanzishwaji au kufahamu kikundi chochote
chenye misingi ya ukabila, udini, au ukanda ambacho kina makusudi ya
kubaguana ndani ya chama na miongoni mwa jamii kisiasa au kijamii kwa
kutumia waraka unaosemekana kuandaliwa nami.
2. Mimi binafsi sio mdini, mkabila au mkanda na sijawahi kujihusisha na kikundi au mtu yeyote mwenye tabia hizo.
KOSA LA TANO
Kujihusisha
na vikundi na vitendo vya kuchonganisha au kuzua migogoro ndani ya
uongozi wa chama au wanachama wake na kinyume na Kanuni ya 10.1 (x) ya
Kanuni za Uendeshaji. Mheshimiwa Katibu Mkuu;
1.
Nakanusha kwamba nimejihusisha na vikundi na vitendo vya kuchonganisha
au kuzua migogoro ndani ya uongozi wa chama au wanachama wake.
2. Mimi binafsi sikifahamu kikundi chochote ambacho nashutumiwa kujihusisha nacho.
KOSA LA SITA
Kutekeleza
mpango wa kusudio la kugombea nafasi ya mwenyekiti wa Chama Taifa bila
kutangaza kusudio la kugombea nafasi hiyo kinyume na kifungu cha 2(g)
cha Mwongozo wa Kutangaza Kusudio la Kuwania Nafasi za Uongozi Kwenye
Chama, Mabaraza na Serikali 2012. Mheshimiwa Katibu Mkuu;
1.
Nakanusha kwamba nimetekeleza au kuhusika katika utekelezaji wa mpango
wa kusudio la kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa bila
kutangaza kusudio la kugombea nafasi hiyo.
2.
Sijatangaza sehemu yeyote kwamba nitagombea nafasi hiyo na pia vile vile
sijatekeleza mpango wowote kama ilivyoelezwa kwenye barua yako.
KOSA LA SABA
Kutengeneza
makundi au mitandao ya kuwania uongozi ndani ya chama kwa nia ya
kujihakikisha ushindi kinyume nakifungu cha 2(d) cha mwongozo wa kuwania
uongozi. Mheshimiwa Katibu Mkuu;
1. Nakanusha
kwamba nimejihusisha katika kutengeneza, kuanzisha, kushiriki
uanzishwaji au kufahamu kikundi chochote kwa ajili ya kuniwezesha
kuwania uongozi ndani ya chama na kujihakikishia ushindi kutwaa
Uenyekiti wa Chama Taifa kinyume na taratibu.
KOSA LA NANE
Kuwachafua
viongozi na wanachama wengine wenye kusudio/nia ya kutaka kugombea
nafasi ya Uenyekiti wa Chama Taifa kinyume nakifungu cha 2(e) cha
Mwongozo wa Kuwania Uongozi. Mheshimiwa Katibu Mkuu;
1.
Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba
na Mtu mwingine ambaye hajajulikana niliandaa waraka ulioitwa Mkakati wa
Mabadiliko 2013.
2. Sijawahi kushiriki kwa
njia yoyote kuandaa waraka huo peke yangu au nikiwa na mtu mwingine
yeyote. Nakanusha kumkashifu Mwenyekiti wa Chama Taifa, kiongozi
mwenzangu au mwanachama yeyote Yule.
KOSA LA TISA
Kujihusisha
na upinzani dhidi ya Chama na makundi ya majungu ya kugonganisha
viongozi na wanachama wakati wa Uchaguzi wa Chama kinyume na Kanuni ya
10.3(4) ya Kanuni za Uendeshaji. Mheshimiwa Katibu Mkuu;
1.
Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba
na Mtu mwingine ambaye hajajulikana niliandaa mkakati wa kugonganisha
viongozi na wanachama wakati wa Uchaguzi wa Chama kwa kuwachafua
viongozi wakuu wa Chama yaani Mwenyekiti wa Chama Taifa na Katibu Mkuu
kwa tuhuma nzito za uongo na kunipamba mimi.
2. Sijawahi kushiriki kwa njia yoyote kuandaa waraka huo peke yangu au nikiwa na mtu mwingine yeyote.
KOSA LA KUMI
Kukashifu
Chama au Kiongozi wa Chama nje ya Bunge kinyume na Kanuni 2(b) ikisomwa
pamoja na Kanuni 3(b) ya Kanuni za Mwenendo na Maadili ya Wabunge.
Mheshimiwa Katibu Mkuu;
1. Nakanusha kwamba
mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba na Mtu mwingine
ambaye hajajulikana kwa kuandaa na kutumia waraka uitwao Mkakati wa
Mabadiliko 2013 nilitengeneza mtandao haramu ndani ya Chama na nilitoa
kashfa, matusi na uzushi dhidi ya Chama na viongozi wake wakuu kwa lengo
la kuchochea mgawanyiko ndani ya Chama.
2. ambao ulikashifu Chama na/au viongozi wake wakuu nikiwa Mbunge wa CHADEMA na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni.
3.
Sijawahi kushiriki kwa njia yoyote kuandaa waraka huo peke yangu au
nikiwa na mtu mwingine yeyote. Nakanusha kwamba nimekashifu Chama au
viongozi wake wakuu nikiwa Mbunge wa CHADEMA na Naibu Kiongozi wa
Upinzani Bungeni kwa njia yoyote ile.
KOSA LA KUMI NA MOJA
Kuchochea
mgawanyiko ndani ya Chama kinyume na Kanuni ya 3(f) ya Kanuni za
mwenendo na maadili ya Wabunge. Mheshimiwa Katibu Mkuu;
1.
Mimi kama kiongozi wa Kitaifa sijawahi kutengeneza mtandao haramu ndani
ya Chama wala kutoa lugha ya matusi na uzushi dhidi ya Chama na
viongozi wake wakuu kwa lengo la kuchochea mgawanyiko ndani ya Chama.
HITIMISHO:
Mheshimiwa Katibu Mkuu;
a)
Nakanusha kila tuhuma mojamoja na kwa ujumla wake dhidi yangu. Mashtaka
yote dhidi yangu sio kweli na sijavunja Katiba au Kanuni za Chama.
b)
Naiomba Kamati Kuu ijiridhishe kwa kiasi kinachostahili kuhusu mashtaka
yote niliyoshtakiwa nayo kwa kuangalia ushahidi wote uliotolewa au
utakaotolewa dhidi yangu.
c) Utetezi wangu umetolewa bila
kupewa nakala ya Waraka unaosemekana nimeuandaa ilhali kukiwa na maelezo
kwamba kuna waraka ‘feki’ na waraka ‘original’ ambao umetumika na
Kamati Kuu kufikia maamuzi yake.
d) Ndugu Kitila Mkumbo na
Samson Mwigamba kwa maneno yao wenyewe wametamka kwamba
hawakunishirikisa na sikushiriki kwenye uandaaji wa waraka ambao ndio
msingi wa mashtaka haya. Kamati Kuu inao ushahidi huo.
Wako katika ujenzi wa Chama,
.............................. ......................
Mh. Zitto Zuberi Kabwe (MB).
No comments:
Post a Comment