Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday 23 January 2014

REGINALD MENGI AWARUKIA VIONGOZI WA DINI


TAARIFA YA DKT. REGINALD A. MENGI, MWENYEKITI MTENDAJI WA IPP LIMITED, KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU OMBI LAKE KWA VIONGOZI WA DINI 


TAREHE 20 JANUARI 2014 

Hivi karibuni kumekuwepo na misimamo tofauti kutoka viongozi wa dini juu ya uchumi wa gesi asilia. 

Ningeomba viongozi wa dini wasitoe uamuzi juu ya watu mbalimbali ambao wametoa maoni yao juu ya ushirikishwaji na uwezeshwaji wa Watanzania, na hasa wazawa, juu ya umiliki wa uchumi wa gesi. 

Nawasihi wanaposhiriki kwenye mikutano ya aina yeyote ile wasikilize maoni ya pande zote mbili kabla ya kutoa maamuzi yao, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwaongoza kutoa msimamo ambao hatimaye unanufaisha Watanzania wote kwa njia impendezayo Mwenyezi Mungu, ili isifike wakati waumini wao wakashindwa kuwaelewa. 

Ni vizuri ikaeleweka kwamba kinachopiganiwa siyo Sekta Binafsi ya Tanzania ichukue nafasi ya Shirika la Mafuta (TPDC), TPDC lazima iendelee kuwakilisha maslahi ya Watanzania. Kinachotakiwa ni Sekta Binafsi ipewe sehemu ya ile fursa wanayopewa wawekezaji wa nje na iwezeshwe kushirikiana na TPDC ili sehemu kubwa ya mapato yanayopatikana kwenye gesi yetu yabaki hapa nchini kuendeleza Taifa letu. 

Hatuna nia ya kutaka vitalu vipewe kwa Watanzania binafsi , ila Serikali ichukue uamuzi wa kuwapa Watanzania ambao wamejiunga kwenye makundi na ambao watapanua wigo wa huo umiliki kuingiza Watanzania wengi kwenye hayo makundi yao. Mtu yeyote anayesema eti kuna mzawa nayetaka kumiliki kitalu cha gesi yeye binafsi anasema uongo mtupu na anastahili atubu kwa Mwenyezi Mungu.

Sisi tunataka vitalu vimilikiwe siyo na mtu mmoja mmoja mzawa, tunataka vimilikiwe na makampuni au vikundi vya Watanzania na hasa wazawa. Makampuni hayo yatauza hisa zake kwa Watanzania ili Watanzania wote wapate fursa ya kushiriki. Hii ndio njia ambayo hata mtu mwenye hali ya chini ataweza kushiriki katika uchumi wa gesi. 

Mimi napinga kwa nguvu zangu zote mtu binafsi au mtu mmoja mmoja kumiliki kitalu cha gesi kwa sababu gesi asilia ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa Watanzania wote, na si kwa Watanzania wachache. 

Hoja kwamba Watanzania hawana mtaji siyo sahihi. Sisi tunaamini kwamba mtaji wa Watanzania ni gesi yenyewe, ambayo thamani yake ni zaidi mara tano ya fedha watakazoleta wageni. Lakini cha kusikitisha zaidi ni kwamba hizo fedha watakazoleta wageni watarudishiwa mara baada ya gesi kuanza kuzalishwa. Kwa maana nyingine hizo fedha ni kama mkopo kwa Watanzania ambao itabidi tuzirudishe mara baada ya uzalishaji wa gesi kuanza.

Ukweli ni kwamba wawekezaji wa nje pia wanatumia vibali wanavyopewa juu ya gesi yetu kuhamasisha wawekezaji wengi wachangie kwenye fedha wanazoleta. Mfano wa karibuni sana, ni kampuni ya nje ambayo imeuza sehemu ya vitalu walivyopewa na kupata zaidi ya dola bilioni moja. Inawezekanaje -mwekezaji wa nje apewe vitalu na auze sehemu ya vitalu hivyo ili kupata fedha ya kuendeleza vitalu vinavyobaki, lakini inaonekana kama ni dhambi -kwa wawekezaji wazawa kufanya hivyo?

Pia ikumbukwe kwamba wanaoleta fedha siyo mtu mmoja mmoja ni watu ambao wamejiunga, wengine wakiwa na hali za kawaida kabisa kama ilivyo Watanzania wengi. Hiki ni kitu ambacho Watanzania tungeweza kufanya, -na -pale ambapo Watanzania watakosa uwezo basi wawezeshwe kama inavyoelekeza sera na sheria ya Taifa ya Uwezeshaji Kiuchumi ya mwaka 2004 na dira ya maendeleo ya Taifa, inayosema kwamba kufikia mwaka 2025, sehemu kubwa ya uchumi wa Tanzania unatarajiwa kumilikiwa na Watanzania wenyewe. 

Ieleweke kwamba jambo linalozungumziwa hapa ni jambo ambalo litaamua mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu kwa vizazi vilivyopo na vizazi vijavyo. Endapo tutakabidhi utafutaji na uzalishaji wote wa gesi asilia (upstream) kwa wawekezaji wa nje tutakuwa tumewanyima Watanzania, hasa wazawa, fursa ya kuchangia na kushiriki katika maendeleo ya taifa hili. Na watabaki kuwa watazamaji tu. 

Mwisho, hivi karibuni Sekta Binafsi ya Tanzania ilifarijika sana kwa mafanikio iliyofikiria yamepatikana kutokana na kikao cha Baraza la Taifa la Biashara chini ya uenyekiti wa Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete na ambacho kiliamua kuwepo kwa kamati itakayochambua na kupeleka mapendekezo yake mwezi Machi 2014 kuhusu utaratibu wa jinsi gani Watanzania watakavyowezeshwa kikamilifu katika kushiriki katika uchumi wa Taifa, ikiwa ni pamoja na uchumi wa gesi. Iliaminika kwamba Wizara zote husika zingengoja ripoti ya kamati hiyo kabla ya kuchukua hatua yeyote ya kuitisha vikao vya kujadili jambo la kuwawezesha Watanzania hasa wazawa. 

Kwa vile Wizara ya Nishati na Madini imeamua kuitisha vikao kinyume na mapendekezo hayo, tunashauri viongozi wa dini wawasikilize lakini pia watafute nafasi kama hiyo kuisikiliza Sekta Binafsi ya Tanzania na wadau wengine ambao hawajashirikishwa kwenye mikutano hiyo.


Dkt. Reginald Mengi

Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment