TIMU ya soka ya KCC ya Uganda imeanza vyema michuano ya Kombe la Mapinduzi, baada ya kuwafunga mabingwa wa Zanzibar, timu ya KMKM mabao 3-2, katika mchezo uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Amaan, mjini hapa. KMKM walikuwa wa kwanza kuliona lango la KCC katika dakika ya 7 kwa bao lililofungwa na Khamis Ali katika mechi hiyo ya ufunguzi.
Kuingia kwa bao hilo kulisababisha KCC kuongeza mashambulizi langoni mwa KMKM na kufanikiwa kusawazisha bao hilo katika dakika ya 10, kwa bao lililofungwa na Herman Waswa.
Kikosi cha timu ya KCC kikiongozwa na Kocha Mkuu George Msimbi, kilijipatia bao la pili katika dakika ya 20 lililowekwa wavuni na Tony Odour.
KMKM walisawazisha bao la pili katika dakika ya 79, kupitia kwa Maulid Ibrahim Kapenta, baada ya kuunganisha krosi ya Juma Mbwana.
KCC walikuja juu na kujipatia bao la tatu katika dakika ya 82, lililofungwa na William Waoro, baada ya kutokea vuta nikuvute katika lango la KMKM.
Hadi dakika 90 za mchezo huo zinamalizika, KCC ilitoka uwanjani kifua mbele kwa ushindi huo wa mabao 3-2.
Nayo timu ya Mbeya City imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya timu ya kombaini ya Pemba ‘Clove Stars’, katika mechi iliyochezwa katika Uwanja wa Gombani, kisiwani Pemba.
Bao la Mbeya City lilifungwa katika dakika ya 13 na Deus Kaseke, wakati bao la Clove Stars lilifungwa na Mohamed Juma Mtwango katika dakika ya 24.
CHANZO: Mtanzania
No comments:
Post a Comment