NI kwa utuki au kwa mikakati maalum, nafasi kadhaa za juu katika Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) zinashikiliwa na viongozi wenye asili ya mkoa wa Kagera.Wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa TFF, Oktoba 27, 2013 kwenye ukumbi wa NSSF Waterfront, walimchagua kwa kura nyingi Jamal Emil Malinzi kuwa Rais mpya kurithi kiti kilichoachwa na Leodegar Tenga aliyeachia ngazi. Malinzi ana asili ya Kagera.
Baada ya wajumbe
wa Kamati ya Utendaji, kupangwa katika kamati ndogondogo, wiki hii
Malinzi amemtangaza aliyekuwa Katibu Mkuu wa klabu ya Yanga, Mwesigwa
Selestine kuwa Katibu Mkuu wa TFF akichukuwa nafasi ya Angetile Osiah
aliyesitishiwa mkataba wake kwa kupewa likizo ya malipo hadi mwezi huu.
Mwesigwa ana asili ya Kagera.
Aidha, Malinzi
alimtangaza Katibu Mkuu wa klabu ya Simba, Evodius Mtawala kuwa
Mkurugenzi wa Vyama, Wanachama na Masuala ya Sheria. Mtawala ambaye
kitaaluma ni mwanasheria, pia anatoka Kagera.
Tofauti
na Malinzi na katika kujali misingi ya utawala bora uongozi uliopita wa
Tenga uliiteua kampuni moja ya kimataifa kufanya usaili wa watu
walioomba nafasi mbalimbali za uongozi. Lakini Malinzi ‘aliunda’ kamati
ya kufikirika iliyopokea maombi na kufanya mchujo kwa kuzingatia sifa
mbalimbali ikiwemo ya elimu.
Baadaye majina
yaliyopitishwa yalipigiwa kura na Kamati ya Utendaji. Lakini habari
kutoka ndani ya TFF zinasema Rais ndiye alikuwa anapokea maombi hayo.
Vilevile,
Malinzi amemteua Pelegrinius Rutayuga kuwa mshauri wake wa masuala ya
Ufundi. Mshauri huyu ni mwakilishi wa mkutano mkuu kutoka mkoa wa
Kagera.
Mwenyekiti wa Kamati ndogo ya Kamati ya
Mashindano itakayoshughulikia mpira wa ufukweni ni Ahmed Mgoyi, mjumbe
wa TFF kutoka Kigoma, lakini makamu mwenyekiti ni Shaffih Dauda ambaye
pia anatoka mkoani Kagera.
Akihisi kwamba watu
wanaweza kumpigia kelele kuhusu uteuzi wa viongozi watokao eneo moja,
Malinzi aliwaambia waandishi wa habari Jumanne, “Mimi sijali kwamba
waombaji ni dini gani na wanatoka wapi bali najali sifa na utendaji
kazi.”
Kauli hiyo ya utetezi imeanza kukosolewa
na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambao wameidokeza MAWIO kuwa
hiyo ni dosari kubwa kwa uongozi wa Malinzi.
Malinzi
alisema kuwa mchakato wa upatikanaji wa ajira hizo ulipitia taratibu
walizoziweka na hao ndio wameonekana kuwa wanafaa kuendana na malengo na
sera za TFF.
Alisema mchakato huo ulianza kwa
watu mbalimbali kuomba nafasi hizo na baada ya kamati ya ajira, ambayo
hakutaka kuiweka wazi kwa madai kuwa ni kamati ya ndani ya TFF, kupitia
majina ya waombaji yalipelekwa katika Kamati ya Utendaji ya TFF ambayo
ilipata washindi.
Akifafanua, Malinzi alisema
TFF ina malengo yake na Mtawala na Mwesigwa ndio walioonekana kuendana
na matakwa na hakuna kitu kingine zaidi ya uwezo wao na uzoefu wao
uliowashawishi wajumbe kuwapa ajira hizo.
Uteuzi
mwingine wenye harufu ya asili ya Kagera ni wa wakili Julius Lugaziya
ambaye anakuwa mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa ya TFF. Malinzi amemteua
Melchesedeck Lutema aliyekuwa wakili wa Malinzi katika kesi mbalimbali
wakati anafanya kazi kwenye kampuni ya mwanasheria maarufu marehemu
Julius Ndyanabo kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi.
Halafu
Malinzi ameondoa masalia yote ya uongozi wa Tenga isipokuwa Ofisa
Habari wa TFF, Boniface Wambura. Nafasi ya Mkurugenzi wa Mashindano
iliyokuwa chini ya Sadi Kawemba kwa sasa inakaimiwa na Idd Mshangama
ambaye ni ofisa wa itifaki.
Sunday Kayuni,
aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi, ameondolewa na nafasi yake inakaimiwa na
Salum Madadi, huku Danny Msangi akishikilia kwa muda nafasi ya
Mkurugenzi wa Fedha.
Nafasi zinazokaimiwa ni
kutokana na walioomba kutokuwa na sifa zinazohitajika na Malinzi amesema
zitajazwa baadaye isipokuwa wote walioomba awali wasijisumbue kuomba
tena.
Rais huyo wa TFF amesema waajiriwa wote mikataba yao itaanza rasmi Januari Mosi 2014 na itakoma baada ya miaka miwili.
Chanzo gazeti la Mawio toleo la wiki iliyopita
No comments:
Post a Comment