Marehemu William Mgimwa
WAZIRI wa Fedha, Dk. William Mgimwa (63), amefariki dunia katika Hospitali ya Mediclinic Kloff, nchini Afrika Kusini, alikokuwa amelazwa kwa matibabu, huku swali kubwa likibaki nini kimemuua. Tangu alipopelekwa kutibiwa nchini Afrika Kusini, si Serikali wala Ofisi ya Bunge ambayo imewahi kusema Dk. Mgimwa anasumbuliwa na ugonjwa gani.
Taarifa iliyotolewa na Serikali mjini Dar es Salaam jana, ilisema Waziri Mgimwa alifariki dunia jana saa 5:20 asubuhi, wakati akiendelea kupewa matibabu.
“Hivi sasa taratibu za kuleta mwili wa marehemu zinafanywa kati ya Serikali na Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini,” ilisema taarifa hiyo.
Dk. Mgimwa, amelazwa nchini Afrika Kusini karibu mwezi mmoja sasa.
Akizungumza na MTANZANIA kutoka Afrika Kusini, mdogo wa marehemu, Joackim Mgimwa, ambaye siku zote amekuwa akimuuguza kaka yake, alikiri kufariki dunia, lakini hakuwa tayati kusema anasumbuliwa na ugonjwa gani.
“Hivi sasa sina maelezo ya kusema, huu ni wakati mgumu ndugu yangu, tuombe Mungu turudi nyumbani,” alisema Joackim na kukata simu.
Kabla ya taarifa za jana, Waziri Mgimwa aliwahi kuzushiwa kifo Desemba 22, mwaka jana, hali iliyomlazimu mdogo wake aliyekuwa akimuuguza, Joachim kukanusha taarifa hizo.
JK amtembelea
Desemba 10, mwaka jana, Rais Jakaya Kikwete alimtembelea Dk. Mgimwa katika hospitali hiyo, baada ya kumaliza shughuli za mazishi ya Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.
Taarifa ya Ikulu ilisema katika mazungumzo yaliyochukua kiasi dakika 15, Waziri Mgimwa alimwambia Rais Kikwete: “Hali yangu inaendelea vizuri Mheshimiwa Rais na nakushukuru sana kwa kupata muda wa kuja kuniona. Inatia moyo na nguvu sana Mheshimiwa Rais.”
Wakati wa uhai wake, Dk. Mgimwa atakumbukwa kwa mchango mkubwa alioutoa, kwani alikuwa mtaalamu wa mikopo na aliziwezesha benki nyingi nchini kufanikiwa kuanzisha vitengo vya mikopo.
Historia yake:
Dk. Mgimwa, alizaliwa Januari 20, 1950, mkoani Iringa na alipata elimu ya Msingi katika shule za Wasa na Seminari ya Tosa kati ya mwaka 1961 hadi 1967.
Kati ya mwaka 1968 hadi 1971, alijiunga na Shule za Seminari Tosamaganga na Mafinga na kuhitimu kidato cha nne.
Baada ya kuhitimu kidato cha nne, alijiunga na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kati ya mwaka 1975 hadi 1978 na kutunukiwa Stashahada ya Juu kwenye masuala ya benki.
Mwaka 1983 hadi 1984, alijiunga na IFM na kutunukiwa uzamili katika masuala ya fedha.
Kati ya mwaka 1989 hadi 1991, alijiunga na Chuo cha Maendeleo (IDM) Mzumbe, ambacho sasa ni Chuo Kikuu cha Mzumbe na kutunukiwa Shahada ya Uzamili katika masuala ya fedha.
Kabla ya kuchaguliwa kuwa mbunge mwaka 2010, Dk. Mgimwa alifanya kazi Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na Chuo cha Benki Mwanza, kati ya mwaka 1980 hadi 2010.
Akiwa NBC aliajiriwa kama mhasibu wa benki mwaka 1980-1981, Mhadhiri katika chuo cha benki hiyo (1981-1989), Meneja wa benki (1996-1997) na mkurugenzi wa benki hiyo (1997-2000).
Kati ya mwaka 2000 hadi 2010, Dk. Mgimwa alikuwa Mkuu wa Chuo cha Benki mkoani Mwanza.
Katika uchaguzi wa mwaka 2010, alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Kalenga na mwaka jana Rais Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Fedha.
Uzoefu wa kisiasa:
Mwaka 1991-1994, Dk. Mgimwa alikuwa Diwani wa Kata ya Gangilonga.
Mwaka 1994-1995, alikuwa Kamanda Msaidizi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) na mwaka 2008 hadi 2010 alikuwa mlezi wa kata ya Wasa.
WASIRA AMLILIA
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Steven Wasira, alisema Serikali imepata pigo kubwa la kumpoteza Waziri Mgimwa.
“Taifa limepata pigo kubwa la kupoteza mtu muhimu, makini na mweledi mno katika masuala ya fedha, Dk. Mgimwa hakuwa mtu wa papara kufanya uamuzi wa jambo Fulani.
“Pigo hili limegusa mpaka Bunge letu, wananchi wa Kalenga, nashindwa kuamini lakini Mungu amempenda zaidi kumwita mbele ya haki,” alisema Waziri Wassira.
Alisema tangu Dk. Mgimwa alipoteuliwa kwenye baraza la mawaziri, walikuwa wakifanya kazi kama mapacha.
“Tulikuwa tukifanya kazi kama mapacha, tulikuwa tukipanga masuala ya mipango na kupeleka Hazina. Napata shida mno kwa kifo hiki,” alisema Waziri Wassira.
CHANZO: Mtanzania
No comments:
Post a Comment