Rais Jakaya Kikwete
SALAMU ZA MWAKA MPYA ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE KWA WATANZANIA,
TAREHE 31 DESEMBA, 2013
Utangulizi
Ndugu zangu;
Watanzania Wenzangu;
Niruhusuni
nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujalia
uzima mpaka kufika na kuiona siku hii ya leo ya kuuaga mwaka 2013 na
kuukaribisha mwaka 2014. Wapo ndugu, jamaa na marafiki zetu wengi ambao
hawakupata bahati tuliyoipata sisi kwa vile wametangulia mbele ya haki.
Tuendelee kumwomba Mola wetu awape mapumziko mema na azilaze roho zao
mahali pema peponi. Ameen.
Hali ya Usalama
Ndugu Wananchi;
Tunaumaliza
mwaka 2013 nchi yetu ikiwa salama na tulivu. Mipaka iko salama na ile
hali ya wasiwasi tuliyokuwa nayo kwa nyakati fulani mwaka huu sasa haipo
tena. Uhusiano wetu na majirani ni mzuri na tutaendelea kufanya kila
tuwezalo kuhakikisha kuwa hali inaendelea kuwa hivyo au hata kuwa bora
zaidi mwaka 2014 na daima dumu.
Hali ya
usalama wa ndani ya nchi nayo ni nzuri. Hali ya wasiwasi tuliyokuwa nayo
mwaka wa jana na mwanzoni mwa mwaka huu kuhusu uhusiano baina ya
Wakristo na Waislamu haipo. Ni matumaini yangu kuwa haitajirudia tena.
Pepo mbaya amepita tuombe atokomee kabisa.
Ndugu zangu;
Watanzania wenzangu;
Napenda
kurudia kuwasihi kuwa tuchague kuendelea kuishi pamoja kwa upendo,
umoja, kuvumiliana na kushirikiana. Tuepuke kugeuza tofauti zetu za
kisiasa, kidini, rangi, kabila au maeneo tutokayo kuwa chanzo cha uadui
na mifarakano. Kwa sasa tuna mwelekeo mzuri nawaomba tuudumishe. “Mjenga
nchi ni mwananchi na mbomoa nchi ni mwananchi”. Tuchague kuijenga nchi
yetu badala ya kuibomoa. Tusiwasikilize watu hasidi wanaochochea uadui
na mifarakano miongoni mwetu. Watatuvurugia nchi yetu nzuri.
Uhalifu
Ndugu Wananchi;
Katika
mwaka 2013 vyombo vya dola vikishirikiana na wananchi viliendelea
kupambana na vitendo vya uhalifu. Mafanikio ya kutia moyo yameendelea
kupatikana ingawaje bado kuna kazi kubwa ya kuendelea kufanya mwaka 2014
na miaka ijayo.
Dawa za Kulevya
Ndugu Wananchi;
Kati
ya Januari na Desemba 2013, kilo 1,261 za heroin, kilo 3 za cocaine na
kilo 89,293 za bangi zimekamatwa na watuhumiwa 1,631 wametiwa mbaroni.
Tatizo la biashara na matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa na mapambano
yanazidi kuwa makali. Mafanikio yanaendelea kupatikana ingawaje bado
tuna kazi kubwa na ngumu ya kufanya mbele yetu. Ni makusudio yetu
kuongeza maradufu nguvu ya kupambana dhidi ya uhalifu huu.
Tupo
hatua nzuri katika matayarisho ya kuanzisha Kikosi Maalum cha Kupambana
na Dawa za Kulevya katika mwaka wa fedha 2014/15. Pia tutaitazama upya
sheria ya adhabu kwa makosa ya kufanya biashara ya dawa za kulevya ili
kuifanya iwe na meno makali zaidi. Vilevile, tutaongeza uwekezaji katika
vituo vya tiba na kuwarekebisha watu wanaotumia dawa za kulevya.
Mafanikio yanayopatikana Muhimbili na Mwananyamala yanatupa moyo wa
kufanya zaidi.
Ujambazi
Ndugu wananchi;
Jeshi
la Polisi limeendelea kupambana na ujambazi wa kutumia silaha na
mafanikio yameendelea kupatikana. Matukio ya ujambazi yemepungua mwaka
2013 ukilinganisha na mwaka 2012. Takwimu zifuatazo zinathibitisha
ukweli huo. Mwaka 2012 matukio ya ujambazi yaliyoripotiwa yalikuwa 6,872
na kwa mwaka 2013 yameripotiwa matukio 6,409. Mwezi Julai mwaka huu,
niliamua kulihusisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania katika
kupambana na ujambazi wa kutumia silaha na utekaji wa magari katika
Mikoa ya Geita, Kagera na Kigoma. Katika Mikoa hiyo tatizo la ujambazi
lilikuwa limefikia kiasi cha kulazimisha watu kusindikizwa na Polisi
kutoka Ngara kwenda Karagwe, Biharamulo kwenda Muleba na kutoka
Nyakanazi hadi Kakonko. Hali hii haikubaliki na hatuwezi kuiacha
iendelee.
Ndugu Wananchi;
Uamuzi
wangu huo ndiyo ulioanzisha Operesheni Kimbunga ambayo imekuwa na
mafanikio ya kutia moyo. Hali ya usalama katika Mikoa hiyo inaelekea
kuimarika ingawaje ni mapema mno kusema tatizo limedhibitiwa. Silaha
nyepesi na nzito zipatazo 650 zikiwemo za kijeshi na za kiraia pamoja na
mabomu ya kutupwa kwa mkono 11 zilikamatwa kwenye operesheni hiyo.
Aidha, watu 31,203 waliokuwa wanaishi nchini kinyume cha sheria walirudi
makwao. Kati yao, watu 21,758 walirudi kwa hiari na 9,445 walirudishwa
wakati wa Operesheni.
Ndugu Wananchi;
Nimepata
minong’ono kuwa baadhi ya watu walioondoka wanarudi kinyemela. Napenda
kuwatahadharisha kuwa wasifanye hivyo. Wanajisumbua bure. Hawatadumu.
Ushauri wangu kwao ni kuwa kama wanapenda kuishi Tanzania wafuate njia
halali za kufanya hivyo.
Ujangili wa Wanyamapori
Ndugu Wananchi;
Mwaka
huu tuliongeza nguvu katika kupambana na ujangili wa wanyamapori na
uvunaji haramu wa rasilimali za misitu. Hili ni tatizo la siku nyingi
lakini katika miaka ya hivi karibuni limekuwa kubwa mno na kuwazidi
nguvu Askari wa Wanyamapori na Maafisa Misitu.
Kwa
nia ya kuwaongezea nguvu, mwaka 2010 niliagiza Jeshi la Polisi lisaidie
Idara ya Wanyamapori na Idara ya Misitu katika kupambana na uhalifu
huo. Operesheni kadhaa ziliendeshwa maeneo mbalimbali nchini na
mafanikio ya kutia moyo yalipatikana. Lakini, kwa kutambua ukubwa wa
tatizo na hasa kwa upande wa aina ya silaha na mbinu zinazotumiwa na
majangili niliamua kuhusisha vyombo vingine vya usalama likiwemo Jeshi
la Ulinzi. Nia ni kuongeza nguvu ya mapambano. Ndipo ilipoanzishwa
“OPERESHENI TOKOMEZA”.
Ndugu Wananchi;
Kazi
nzuri imefanyika chini ya Operesheni hiyo. Mafanikio ya kuleta
matumaini yameweza kupatikana. Mitandao ya ujangili imeweza kutambulika
na wahusika wake kadhaa wametiwa nguvuni. Mitandao hiyo inahusisha watu
wa aina mbalimbali. Wamo raia wa kawaida, wapo watu maarufu, wapo
watumishi wa idara mbalimbali za Serikali wakiwamo wa Idara za
Wanyamapori na Misitu. Watu 1,030 walikamatwa pamoja na silaha za
kijeshi 18, za kiraia 1,579 na shehena kubwa za meno ya ndovu na nyara
nyingine navyo vilikamatwa.Watu kadhaa tayari wameshafikishwa
mahakamani.
Ndugu Wananchi;
Wahenga
wamesema “kwenye wengi pana mengi”. Katika utekelezaji wa Operesheni hii
kumekuwepo na taarifa za kufanyika makosa kinyume na malengo na
madhumuni ya Operesheni. Niliagiza baada ya kumalizika kwa awamu ya
kwanza, zoezi lisitishwe kwa muda ili uchunguzi ufanyike, kasoro
zitambuliwe na waliofanya makosa wachukuliwe hatua zipasazo. Wakati kazi
hiyo inafanyika suala hilo lilijadiliwa Bungeni na Kamati Teule
kuundwa. Matokeo yake sote tunayajua. Mawaziri wanne wamewajibika
kisiasa.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kutumia nafasi hii kuwapa pole Mawaziri wetu hao kwa matatizo
yaliyowakuta. Nawapongeza kwa uamuzi wa kukubali kuwajibika kwa makosa
yaliyofanywa na maofisa wa chini yao. Wameonesha ukomavu wa kisiasa na
kiuongozi wa hali ya juu na moyo wa uzalendo.
Kama
mlivyosikia nitaunda Kamisheni ya Uchunguzi itakayoongozwa na Jaji wa
Mahakama Kuu. Uchunguzi wa kina utafanywa kuhusu kadhia yote hiyo.
Makosa yaliyofanyika yataainishwa na waliofanya kutambuliwa ili
wachukuliwe hatua zipasazo kwa mujibu wa sheria na kwa mujibu wa kanuni
za utumishi wa umma.
Ndugu Wananchi;
Ni
muhimu kufanya hivi ili haki itendeke ipasavyo. Mtindo wa mzigo wa
makosa ya watumishi wa umma kubebwa na viongozi wa kisiasa pekee, tena
wasiokuwa na hatia ya moja kwa moja, siyo sahihi. Lazima kila mtu abebe
mzigo wake inavyostahili. Ni matumaini yangu pia kwamba katika siku za
usoni kunapotokea matatizo ya namna hii uchunguzi uwe wa kina ili wale
hasa waliohusika na kutenda makosa wawajibishwe. Uwajibikaji wa
wana-siasa peke yao hautoshi, kwani huwaacha waharibifu waendelee na
kazi isivyostahili. Mtindo huu utawafanya watumishi wasione umuhimu wa
kutokurudia makosa. Hata hivyo, pale kwenye ushahidi wa wazi kwamba
kiongozi wa kisiasa angeweza kuchukua hatua za kuzuia madhara lakini
hakufanya hivyo lazima kiongozi huyo awajibike.
Ndugu Wananchi;
Tunakamilisha
matayarisho ya kuanza awamu ya pili ya Operesheni Tokomeza. Ni muhimu
kuendelea nayo kwani tusipofanya hivyo majangili wataendelea na vitendo
vyao viovu. Hali ni mbaya sana kwa upande wa uwindaji wa ndovu.
Nilipolihutubia Bunge tarehe 7 Novemba, 2013, nilieleza kuwa tutafanya
sensa ya ndovu katika Pori la Hifadhi la Selous. Sensa hiyo imekamilika
lakini taarifa yake inatisha. Kuna ndovu 13,084 tu wakati mwaka 1976
walikuwa 109,419. Tusipoendelea na Operesheni hii baada ya miaka
michache ijayo hakutakuwa na ndovu hata mmoja. Halikadhalika, zoezi la
kuondoa mifugo katika mapori ya hifadhi ya taifa litaendelea. Katika
awamu ya pili ya Operesheni hii, washiriki watasisitizwa kutokutenda
maovu yaliyofanyika katika awamu ya kwanza.
Mchakato wa Kuunda Katiba
Ndugu wananchi;
Tumefika
mahala pazuri katika mchakato wetu wa kutayarisha Katiba Mpya ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jana Mwenyekiti wa Tume, Mheshimiwa
Jaji Joseph Warioba, alitukabidhi Rasimu ya Pili ya Katiba, mimi na Rais
wa Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein. Kama nilivyosema jana
kinachofuata sasa ni kuitangaza Rasimu hiyo katika Gazeti la Serikali
kwa kila mtu na hasa Wajumbe wa Bunge la Katiba, kuiona na kuisoma.
Baada ya hapo kitafuata kitendo cha kuifikisha Rasimu kwenye Bunge
Maalum la Katiba kwa ajili ya kujadiliwa na hatimaye kupatikana Rasimu
ya Mwisho itakayofikishwa kwa wananchi kupigiwa kura.
Ndugu Wananchi;
Mchakato
wa kupata Wajumbe 201 watakaoungana na Wabunge na Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi kuunda Bunge Maalum la Katiba umeanza. Ni matarajio yetu
kuwa katika wiki ya tatu ya Januari, 2014, uteuzi utakamilika. Siku 21
baada ya hapo Bunge la Katiba litaanza. Hii ni kwa nia ya kuwapa nafasi
Wajumbe hao kusoma Rasimu ya Katiba. Baada ya Bunge la Katiba kumaliza
kazi yake, utaanza mchakato wa Kura ya Maoni itakayopigwa na wananchi
ndani ya siku 74 baada ya Rasimu ya Katiba kupitishwa na Bunge Maalum na
kukabidhiwa kwa Rais.
Iwapo Rasimu itakubaliwa
na wananchi hapo tutakuwa tumepata Katiba Mpya. Lakini, iwapo Rasimu
itakataliwa ina maana kuwa Katiba ya sasa itaendelea kutumika mpaka hapo
mchakato mwingine utakapoanzishwa na Katiba mpya kupatikana. Ni
matumaini yangu na, ni maombi yangu na rai yangu kuwa Rasimu hiyo
itakubalika ili nchi yetu isonge mbele.
Pongezi
Ndugu Wananchi;
Niruhusuni
nitoe pongezi zangu za dhati kwa Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Tume kwa
kazi kubwa na nzuri waliyoifanya. Najua haikuwa kazi rahisi hata kidogo
lakini wameweza. Kwa namna ya pekee nawashukuru wananchi kwa ushiriki
wao mzuri uliowezesha zoezi la mabadiliko ya Katiba kufikia hatua
tuliyofikia sasa.
Ndugu Wananchi;
Ni
matumaini yangu na ndiyo matumaini ya Watanzania wote kuwa Wajumbe wa
Bunge Maalum la Katiba wataijadili Rasimu ya Katiba kwa makini na
kufanya kila wawezalo kuiwezesha nchi yetu kupata Katiba nzuri
itakayoimarisha na kudumisha Muungano wetu. Katiba itakayoendeleza
umoja, upendo, udugu, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa wananchi wa
Tanzania. Katiba itakayoihakikishia nchi yetu amani, utulivu na ustawi
wa kiuchumi na kijamii.
Ni imani yangu na ya
Watanzania wote kuwa Wajumbe wa Bunge la Katiba wataweka mbele maslahi
mapana ya taifa na watu wake. Wasiweke mbele maslahi yao binafsi au ya
vikundi vyao vya kisiasa au kijamii. Wakifanya vinginevyo kuna hatari ya
kupata Katiba isiyokidhi haja na itakuwa hasara kubwa kwa taifa letu na
kwao pia.
Uchumi
Ndugu wananchi;
Katika
mwaka tunaoumaliza leo, Tanzania iliendelea kupata mafanikio katika
nyanja mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Jambo la
kufurahisha ni kuwa mafanikio hayo yamepatikana licha ya kuwepo
changamoto kadhaa hapa nchini na hali ya uchumi wa dunia kuwa bado
haijatengemaa vya kutosha.
Pato la taifa
limekua kwa asilimia 7.1 ukilinganisha na asilimia 6.9 mwaka jana.
Tunategemea kuwa mwaka 2014 pato la taifa litakua kwa asilimia 7.3.
Mfumuko wa bei umeshuka kutoka asilimia 12.1, Desemba, 2012 hadi
asilimia 6.2, Novemba 2013. Lengo letu ni kufikia asilimia 5 mwezi Juni,
2014.
Ndugu Wananchi;
Hadi Novemba,
2013, Tanzania ilikuwa imeuza nje bidhaa na huduma zenye thamani ya
dola za Marekani milioni 7,720.8 ukilinganisha na dola milioni 7,916.6
za mwaka ulioishia Novemba 30, 2012. Kushuka kwa bei za kahawa, pamba,
katani, chai, karafuu na dhahabu ndiko kulisababisha kupungua kwa mapato
yetu ya fedha za kigeni. Hali hii inatukumbusha umuhimu na uharaka wa
kuendeleza viwanda vya kuongeza thamani mazao na bidhaa zetu tunazouza
nje. Jambo hili tutalipa msukumo maalum mwaka 2014 na kuendelea.
Pamoja
na kushuka kidogo kwa mapato ya mauzo yetu ya nje akiba yetu ya fedha
za kigeni iliendelea kuwa nzuri. Hadi Novemba 30, 2013 akiba yetu
ilikuwa dola za Marekani 4,538 milioni. Hata hivyo, akiba hiyo
inatuwezesha kuagiza bidhaa toka nje wa miezi 4.4 ni chini ya lengo letu
la miezi 4.5. Sina wasiwasi kuwa mwaka 2014 tutaliziba pengo hilo.
Ndugu Wananachi;
Sekta
zilizochangia sana katika kasi ya ukuaji wa uchumi mwaka 2013 ni pamoja
na mawasiliano asilimia 20.6, huduma ya fedha asilimia 13.2, uzalishaji
viwandani asilimia 8.2, madini asilimia 7.8, ujenzi asilimia 7.8,
biashara asilimia 7.7 na uchukuzi asilimia 7.1. Bado kasi ya ukuaji wa
sekta ya kilimo ilikuwa ndogo kwani ilikuwa asilimia 4.3.
Pamoja
na hayo, kilimo kinaendelea kutoa mchango mkubwa kwa ustawi wa uchumi
wa Tanzania na watu wake. Kilimo kinachangia asilimia 24.7 ya pato la
taifa na asilimia 10.7 ya mapato ya fedha za kigeni. Kilimo kimeiwezesha
nchi yetu kujitosheleza kwa chakula na kuvipatia viwanda malighafi. Kwa
upande wa mazao ya chakula, kwa mfano, mwaka huu uzalishaji ulikuwa
tani 14,383,845. Ukilinganisha na mahitaji yetu ya chakula ya tani
12,149,120 hivyo tunajitosheleza na kuwa na ziada kidogo. Ziada hii ni
kidogo mno hivyo inatulazimu mwaka ujao tuongeze maradufu juhudi na
uwekezaji katika kutekeleza shabaha na malengo ya kilimo.
Ndugu Wananchi;
Kwa
ajili ya uzalishaji wa chakula kuwa mzuri, mwaka huu Wakala wa Taifa wa
Hifadhi ya Chakula wameweza kununua tani 233,689.8 za nafaka hadi
kufikia Desemba 27, 2013 kiasi ambacho hakijawahi kufikiwa miaka ya
nyuma. Mwaka 2012 wakati kama huu Wakala ilikuwa na kiasi cha tani
93,047.8 tu na kutulazimisha kutafuta chakula nje ya nchi. Kwa ajili
hiyo tulilazimika kuruhusu wafanyabiashara kuagiza mahindi, mchele na
sukari kutoka nje kwa nafuu ya kodi. Uamuzi huo umesaidia nchi kuwa na
chakula cha kutosha na kuuzwa kwa bei nafuu kwa walaji.
Ndugu Wananchi;
Ni
matarajio yangu, na ndiyo hasa dhamira yetu, kwamba mwaka 2014 tutapata
mafanikio makubwa zaidi kwa upande wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Naamini tutaweza kwa vile tumejipanga vizuri. Tunayo miradi ya
kimkakati iliyoainishwa vizuri katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka
Mitano na chini ya Utaratibu wa Matokeo Makubwa Sasa. Miradi hiyo kama
itatekelezwa kama ilivyopangwa uchumi utakua kwa kasi kubwa zaidi, ajira
nyingi zitapatikana na huduma za kiuchumi na kijamii zitaboreka sana.
Bahati
nzuri tumeweka utaratibu mpya na mzuri wa kufuatilia utekelezaji wa
mipango, miradi na shughuli za Serikali. Katika Ofisi ya Rais
kumeanzishwa Ofisi maalum ya ufuatiliaji ijulikanayo kama Presidential
Delivery Bureau. Na, kila Wizara ina kitengo cha namna hiyo
kijulikanacho kama Ministerial Delivery Unit. Kwa ajili hiyo utekelezaji
wa miradi ya kimkakati na shughuli za Serikali utakuwa mzuri zaidi.
Mazingira ya Uwekezaji
Ndugu Wananchi;
Ni
makusudio yetu kuwa kuanzia sasa tutaihusisha sekta binafsi kwa nguvu
zaidi katika utekelezaji wa miradi na shughuli za maendeleo. Nimeagiza
Presidential Delivery Bureau ishughulikie suala la uboreshaji wa
mazingira ya uwekezaji nchini. Sifa ya nchi yetu kuhusu mazingira ya
uwekezaji siyo nzuri. Kwa mujibu wa tathmini inayofanywa kila mwaka na
Benki ya Dunia, mwaka 2007 nchi yetu ilikuwa kati ya nchi 10 bora
duniani kwa kufanya mageuzi makubwa ya kupunguza gharama za kufanya
biashara. Mwaka huo tulikuwa nchi ya 142 kati ya nchi 175. Mwaka 2008
tukapanda na kuwa wa 130 kati ya nchi 176, mwaka 2012 tulikuwa wa 134
kati ya nchi 185 na sasa ni wa 145 kati ya nchi 185. Hali hii si nzuri
hata kidogo kwa uchumi unaokusudiwa kujengwa kwa kutegemea uwekezaji wa
sekta binafsi. Tunategemea PDB itatupa ushauri mzuri wa nini kifanyike
kurekebisha mambo.
Ndugu Wananchi;
Utekelezaji
wa miradi ya Big Result Now (BRN) katika kilimo, umeme, reli, barabara,
bandari, maji, elimu na kuongeza mapato ya Serikali umeanza kwa kasi
inayoleta matumaini. Kama upande wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali
utakwenda inavyotarajiwa tutegemee mambo mengi mazuri kufanyika kuanzia
mwaka 2014 mpaka 2016.
Mpaka sasa hali ya
ukusanyaji wa mapato ya Serikali si mbaya. Wastani kwa mwezi unakaribia
shilingi bilioni 700 kuelekea shilingi bilioni 800. Makusanyo ya mapato
ya Serikali kwa miezi ya Julai hadi Novemba yaliongezeka kutoka shilingi
bilioni 3,008.1 kipindi kama hicho mwaka 2012 hadi shilingi bilioni
3,555.5 mwaka 2013. Hata hivyo makusanyo ya Julai hadi Novemba, 2013 ni
asilimia 88.1 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 4,036.8. Lengo
halijafikiwa kwa sababu ya kuchelewa kutekelezwa kwa baadhi ya
marekebisho ya mfumo wa kodi, hususan tozo ya simcard, kodi za mishahara
kutokana na kutokupandishwa kwa kima cha chini katika sekta binafsi na
ya uhawilisho wa fedha (money transfer). Pia kuendelea kwa mvutano baina
ya TRA na wafanyabiashara kuhusu bei za mashine za kodi. Ni matumaini
yangu matatizo hayo yatashughulikiwa na kumalizwa mapema iwezekanavyo
ili tuweze kupata mafanikio makubwa zaidi katika ukusanyaji wa mapato ya
Serikali mwaka 2014.
Elimu
Ndugu Wananchi;
Kwa
upande wa elimu tumeendelea kupata mafanikio katika kupunguza tatizo la
upungufu wa walimu wa shule za msingi na sekondari. Mwaka huu tuliajiri
walimu 28,666. Kwa ajili hiyo upungufu wa walimu ni 57,755 kati yao
20,625 wa shule za msingi na 37,130 wa shule za Sekondari. Mapema mwaka
ujao tutaajiri walimu wapya 36,100 kati yao 18,100 wa shule za msingi na
18,000 wa sekondari. Kufanya hivyo kutafanya pengo lililopo liwe dogo
zaidi.
Kwa upande wa shule za sekondari,
tatizo la walimu wa masomo ya sanaa tunakaribia kulimaliza. Changamoto
yetu kubwa itakuwa kwa walimu wa masomo ya sayansi. Upungufu ni walimu
26,998 na uwezo wa vyuo vyetu ni kutoa walimu wa sayansi 2,300 kwa
mwaka. Mapema mwaka 2014 tutakutana na wadau wa elimu nchini kujadiliana
juu ya mkakati wa haraka wa kulikabili tatizo hili. Nilipanga tufanye
hivyo mwaka huu lakini mambo yaliingiliana sana hatukuweza.
Ndugu Wananchi,
Tumeendelea
kupunguza tatizo la uhaba wa vitabu na vifaa vya kujifunzia na
kufundishia. Tuliongeza fedha katika bajeti ya elimu kwa ajili ya
vitabu. Hivi sasa usambazaji wa vitabu vyenye thamani ya shilingi
bilioni 76 za bajeti ya mwaka 2012/13 unaendelea. Kwa sababu hiyo hivi
sasa upungufu wa vitabu umeshuka na kufikia kitabu kimoja kwa wanafunzi
3. Naamini shilingi bilioni 49 zilizotengwa katika bajeti ya mwaka huu
wa fedha kwa ajili ya vitabu itafanya mambo kuwa nafuu zaidi.
Tukiendelea kuwekeza kama tufanyavyo sasa shabaha yetu ya kila
mwanafunzi wa msingi na sekondari kuwa na kitabu chake kwa masomo yote
ifikapo 2016 itatimia.
Ndugu Wananchi;
Mwaka
huu tumeanza utekelezaji wa mpango mkubwa wa kujenga nyumba za walimu.
Kwa kuanzia tumetenga shilingi milioni 500 kwa kila Halmashauri.
Tumeanza na Halmashauri 40, mwaka ujao na miaka inayofuata tutaongeza
fedha zinazotengwa na kuzifikia Halmashauri zote. Kwa upande wa ujenzi
wa maabara katika sekondari za kata napenda kuwakumbusha Wakuu wa Mikoa
na Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Miji, kuwa kila
mmoja ahakikishe kuwa ifikapo Novemba, 2014 malengo yanatimia.
Wasisubiri kuulizwa.
Maji
Ndugu Wananchi;
Kwa
kutambua umuhimu wa maji kwa maisha ya wanadamu na uchumi katika bajeti
ya mwaka huu wa fedha sekta ya maji imepewa upendeleo katika mgao wa
fedha. Tutaendelea kuongeza fedha katika bajeti mbili zinazofuata ili
watu wengi zaidi mijini na vijijini wapate maji safi na salama. Kama
fedha zitapatikana kama ilivyopangwa na utekelezaji ukasimamiwa vizuri
tunatarajia kuwa katika mwaka 2013/14 watu milioni 7.1 watapata maji.
Katika mwaka ujao wa fedha 2014/15 tumepanga kuwapatia maji watu wengine
milioni 7 na mwaka utaofuata (2015/16) tutaongeza tena huduma hiyo kwa
watu milioni 1.3 na kufanya tufikie asilimia 74 ya Watanzania wanaopata
maji safi na salama ifikapo 2015/2016.
Afya
Ndugu wananchi;
Tumeendelea
kupata mafanikio katika kuendeleza upatikanaji wa huduma ya afya kwa
wananchi wa Tanzania. Zahanati, vituo vya afya na hospitali zimeendelea
kujengwa kote nchini. Aidha, hospitali za wilaya, mikoa, kanda na
Hospitali ya Taifa Muhimbili zimeendelea kuboreshwa. Kwa ajili hiyo
idadi ya Watanzania wanaoweza kupata huduma ya afya iliyo bora inazidi
kuongezeka. Hali kadhalika, wataalamu wa afya wa fani mbalimbali
wameongezeka na hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba imezidi
kuboreshwa. Pamoja na yote hayo bado kuna kazi kubwa ya kufanya mbele
yetu. Kufanya hayo ndiyo dhamira yetu kuu kwa mwaka 2014.
Ndugu wananchi;
Tumeendelea
kupata ushindi katika mapambano dhidi ya magonjwa yanayoua watu wengi
nchini. Kwa upande wa malaria, kwa mfano, maambukizi ya ugonjwa huo kwa
watoto na mama wajawazito yamepungua kutoka asilimia 18 hadi 9.5.
Tutaendelea kugawa vyandarua kwa wajawazito na watoto kwa kutumia hati
punguzo pamoja na kusisitiza matumizi ya dawa mseto na kupulizia dawa ya
kuua mbu majumbani. Aidha, tunatarajia kupata mafanikio zaidi miaka
ijayo kiwanda cha kuzalisha viuadudu vya kuua viluilui vya mbu
wanaoeneza malaria kitapoanza kazi.
Ndugu Wananchi;
Mambukizi
ya UKIMWI yameshuka hadi asilimia 5.1. Inaleta faraja kuona watu wengi
wamejitokeza kupima afya zao kwa hiari. Mpaka sasa watu milioni 18
wamepima. Tunao watu 1,298,402 walioorodheshwa kwa ajili ya kupata
huduma ya tiba na kati yao 485,715 wanapata dawa. Waliosalia watapata
wakati wao ukifika.
Mpaka sasa vituo 4,603
vinavyotoa huduma ya kuzuia maambukizi ya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda
kwa mtoto vimeanzishwa nchini kote tangu mpango huo uzinduliwe tarehe 1
Desemba, 2012. Idadi yake inaendelea kuongezeka. Ni dhamira yetu
kuendeleza jitihada za kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa
Watanzania. Mafanikio ya kampeni hii pamoja na ile dhidi ya malaria
ndiyo chachu ya mafanikio tuliyopata katika kupunguza vifo vya watoto
nchini na kufikia lengo la Milenia mwaka huu.
Magonjwa ya Moyo
Ndugu Wananchi;
Katika
mwaka 2013 tunaoumaliza leo, tumeshuhudia mambo kadhaa mazuri
yakifanyika yanayoelezea mafanikio tunayoendelea kuyapata katika
jitihada zetu za kujenga uwezo wa tiba kwa maradhi tunayopeleka wagonjwa
nje ya nchi. Niruhusuni niyataje baadhi yake. La kwanza, ni kuanza kazi
kwa Kituo cha Tiba na Mafunzo ya Magonjwa ya Moyo katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili. Hiki ni kituo kikubwa na cha aina yake cha matibabu
ya maradhi ya moyo hapa nchini. Huduma za kisasa za uchunguzi na
matibabu ya maradhi ya moyo ambazo zamani zilikuwa zinapatikana nje ya
nchi sasa zinaweza kupatikana hapa hapa nchini. Kwa kuwa na vitanda 100
vya kulaza wagonjwa, Watanzania wengi wataweza kuhudumiwa na maisha yao
kuokolewa.
Ndugu Wananchi;
Katika
kituo hiki watu wanaweza kufanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo (open heart
surgery), uwekaji wa mashine ya kuongezea nguvu kwenye moyo (pacemaker),
uwekaji wa vyuma vidogo katika mishipa ya damu ya moyo ambayo imebanana
(stent). Tangu kituo kianze kazi rasmi tarehe 30 Aprili, 2013 mpaka
sasa watu 347 wamefanyiwa upasuaji wa moyo na watu watatu wamewekewa
pacemaker tangu huduma hiyo ianze Novemba, 2013. Mapema mwakani kituo
kinatarajiwa kuanza huduma ya kuweka stent.
Kituo
hiki ni kipya hivyo katika mwaka 2014 tutaendelea kukijengea uwezo wa
vifaa tiba, wataalamu na mahitaji mengine muhimu ili kulipunguzia taifa
mzigo wa kupeleka wagonjwa nchi za nje. Serikali, pia itaendeleza
ushirikiano wake na uongozi wa Hospitali ya Kanda ya Bugando kuboresha
huduma ya upasuaji mkubwa wa moyo katika hospitali hiyo. Huduma hiyo
ilizinduliwa tarehe 26 Oktoba, 2013 na Makamu wa Rais Mheshimiwa Daktari
Mohamed Ghalib Bilal.
Saratani
Ndugu Wananchi;
Kwa
upande wa maradhi ya saratani, Februari, 2013 jengo jipya la kulaza
wagonjwa 170 lilifunguliwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.
Kufunguliwa kwa jengo hilo kumeongeza uwezo wa taasisi yetu hiyo kulaza
wagonjwa 290 badala ya 120 tu kabla ya hapo. Ujenzi wa jengo hili jipya
umesaidia sana watu wengi zaidi kuhudumiwa na kupunguza msongamano
mkubwa wa wagonjwa uliokuwepo.
Figo
Ndugu Wananchi;
Kuhusu
maradhi ya figo mwaka huu pia tumeshuhudia huduma ya usafishaji wa figo
zenye matatizo ikipanuliwa. Huduma hiyo imeanzishwa tena katika
Hospitali ya Kanda ya Mbeya na imeanzishwa kwa mara ya kwanza katika
Chuo cha Tiba katika Chuo Kikuu cha Dodoma. Pale Mbeya tayari wagonjwa
93 wamehudumiwa mwaka huu na kuwapa matumaini mapya ya maisha yao. Kwa
pale Chuo Kikuu cha Dodoma, ujenzi wa kituo kikubwa kitakachobobea kwa
magonjwa ya figo unaendelea na unategemewa kukamilika mapema mwaka 2014.
Mafunzo
Ndugu Wananchi;
Katika
mwaka 2013 tumefungua ukurasa mpya katika jitihada zetu za kuongeza
wataalamu wa afya nchini. Chuo cha Sayansi ya Tiba katika Chuo Kikuu cha
Dodoma kimefanya mahafali yake ya kwanza ambapo wanafunzi 50 wa Shahada
ya Uuguzi walihitimu. Tunatarajia kuanza kupata madaktari kuanzia mwaka
2014.
Kwa upande wa mchakato wa kujenga
makazi mapya ya Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili
kule Mloganzila mchakato umeanza. Ujenzi wa miundombinu ya barabara,
maji na umeme unaendelea hivi sasa. Mwaka 2014 ujenzi wa Hospitali ya
kisasa ya kufundishia yenye vitanda 650 utaanza. Ujenzi wa Mlonganzila
ukikamilika Chuo Kikuu cha Muhimbili kitaweza kuchukua wanafunzi 15,000
wa fani zote ukilinganisha na 3,060 wa sasa. Hatua hiyo itaongeza sana
uwezo na kasi yetu ya kupunguza uhaba wa Madaktari, Wauguzi na wataalam
wengine wa afya.
Nyumba
Ndugu Wananchi;
Katika
mwaka 2013 ujenzi wa nyumba 35 za kuishi watumishi wa afya katika mikoa
ya Mtwara (5), Rukwa (20) na Singida (10) umekamilika. Ujenzi wa nyumba
100 unaendelea. Nyumba hizo ni sehemu ya mpango wa ujenzi wa nyumba 580
zinazojengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na Global Fund kwa awamu
mbili. Awamu ya kwanza zinajengwa nyumba 310 ambapo taasisi ya Benjamin
William Mkapa Foundation ndiyo mtekelezaji wa ujenzi huo. Napenda
kutumia nafasi hii kutoa shukrani za dhati kwa Rais Mstaafu Mheshimiwa
Benjamin Mkapa kwa mchango wake mkubwa alioutoa na anaoendelea kutoa kwa
maendeleo ya nchi yetu na watu wake.
Ujenzi wa Miundombinu
Ndugu wananchi;
Katika
mwaka 2013, tumeendelea kupata mafanikio makubwa katika kuboresha
miundombinu ya usafiri wa ardhini, majini na angani. Kasi ya ujenzi wa
barabara imeendelea kufanyika kote nchini. Kazi ya ujenzi ingekuwa nzuri
zaidi kama mtiririko wa malipo kwa Wakandarasi ungekuwa mzuri. Tatizo
hili tutalitafutia ufumbuzi mwaka 2014 ili kasi ya ujenzi wa barabara za
lami nchini iwe nzuri zaidi.
Pamoja na hayo
mwaka huu kilomita 877 za barabara zimekamilika. Ujenzi wa daraja la
Malagarasi nao umekamilika kinachosubiriwa ni sherehe za uzinduzi.
Ujenzi wa daraja la Kilombero umeanza na ule wa daraja la Kigamboni
unaendelea vizuri. Tunatarajia kuwa mwakani tutaongeza zaidi kasi ya
ujenzi wa barabara zilizosalia ikiwa ni pamoja na kujenga baadhi ya
barabara kwa ubia na sekta binafsi. Kwa kasi na mwenendo tunaoendelea
nao sasa naamini ifikapo mwaka 2015 tutakuwa tumefikia hatua ya juu sana
katika shabaha yetu ya kuunganisha mikoa yote nchini kwa barabara za
lami.
Ndugu Wananchi;
Jitihada za
kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam zimeendelea
kutekelezwa. Barabara kadhaa zilipanuliwa na kazi inaendelea. Ujenzi wa
njia ya kupita mabasi yaendayo haraka umeendelea kwa kasi ya kuridhisha.
Mchakato wa ujenzi wa barabara za juu ya nyingine katika njia panda za
TAZARA na Ubungo umeshaanza. Mwaka ujao huduma ya usafiri wa treni
kusafirisha abiria Dar es Salaam itaongezwa ili watu wengi zaidi
wanufaike.
Ndugu wananchi;
Mwaka
huu, kwa upande wa reli ya kati, kazi ya kuboresha njia ya reli
imeendelea kufanyika na itaendelea mwaka 2014. Mwakani (2014) Shirika la
Reli litapokea injini mpya 13, mabehewa ya mizigo 274 na breki 34 hivyo
kuboresha sana huduma katika reli ya kati. Kuhusu ujenzi wa reli mpya
ya upana wa kimataifa ni matarajio yetu kuwa kama kila kitu kitaenda
sawa mchakato wa ujenzi utaanza katika nusu ya pili ya mwaka 2014.
Ndugu Wananchi;
Tumetoa
kipaumbele cha juu katika kuboresha huduma ya usafiri wa anga nchini.
Mwaka huu, tumeendelea na ukarabati, upanuzi na ujenzi wa viwanja vya
ndege vya Mikoa ya Kilimanjaro, Kigoma, Tabora, Mwanza, Arusha, Mtwara
na Kagera. Ni jambo la kufurahisha kuona Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Songwe ukianza kutumika. Hatimaye ndoto imetimia. Mwaka wa 2014 ujenzi
wa majengo mengine ya kuhudumia abiria, mizigo na ndege utaendelea
katika uwanja huo.
Pia ni furaha iliyoje kwamba upanuzi wa
Uwanja wa Ndege wa Mafia na ujenzi wa gati la Kilindoni vimekamilika.
Kero ya miaka mingi imepatiwa ufumbuzi. Kazi ya ujenzi wa jengo jipya la
abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere itaanza
rasmi mwaka 2014.
Nishati
Ndugu wananchi;
Dhamira
yetu ya kutaka Tanzania iwe na umeme wa uhakika na unaonufaisha watu
wengi imepata sura na mwelekeo mzuri mwaka huu 2013. Ujenzi wa bomba la
gesi kutoka Mtwara na Songosongo kuja Dar es Salaam umeanza na
utekelezaji unakwenda vizuri. Kama ujenzi wa bomba utakamilika kama
inavyotarajiwa na ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme Kinyerezi utaenda
kama ilivyopangwa, ifikapo mwaka 2015 Tanzania itafikia lengo la
kuzalisha megawati 3,000 za umeme.
Ndugu Wananchi;
Bahati
nzuri mwaka huu, kufuatia kuongezewa fedha za bajeti, kasi ya
usambazaji umeme imekuwa nzuri. Tunaumaliza mwaka huku idadi ya
Watanzania waliounganishiwa umeme ikiwa imefikia asilimia 24
ukilinganisha na asilimia 21 mwaka 2012 na asilimia 10 mwaka 2005. Haya
si mafanikio madogo. Kwa mwelekeo huu, kufikia lengo la asilimia 30 ya
Watanzania kupata umeme mwaka 2015 ni jambo la uhakika kabisa sasa. Tena
kuna uwezekano mkubwa wa kulivuka lengo hilo.
Ushirikiano wa Kanda
Watanzania Wenzangu;
Katika
mwaka 2013, nchi yetu imeendelea kushiriki vizuri katika shughuli za
Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC) ambazo sisi ni wanachama. Mwezi wa Agosti, 2013
tulikabidhi Uenyekiti wa chombo cha SADC kinachoshughulikia Siasa,
Ulinzi na Usalama kwa Namibia. Tulikuwa tumemaliza kipindi chetu cha
mwaka mmoja.
Katika kipindi chetu cha uongozi
tulishiriki kwa ukamilifu kutafuta suluhu kwa mizozo na migogoro ya
kisiasa na kiusalama nchini Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
na Madagascar. Tunafurahi kuona kwamba mambo katika nchi zote hizo sasa
yanakwenda vizuri. Nchini Zimbabwe utulivu umerejea baada ya kufanyika
kwa uchaguzi mwezi Julai, 2013. Nchi ya Madagascar nayo imemaliza duru
ya pili ya uchaguzi wa Rais kwa usalama. Matokeo yanatarajiwa kutangazwa
tarehe 7 Januari, 2014. Ni matumaini yetu kuwa watu wa nchi hiyo
watayapokea matokeo hayo na wataelekeza nguvu zao katika kujenga umoja
na maridhiano ili wajenge upya uchumi wa nchi yao.
Kwa
upande wa Mashariki ya Kongo, tishio kubwa la usalama kutokana na
vitendo vya kundi la waasi la M23 limezimwa na Jeshi la Kongo kwa
kushirikiana na Jeshi la Umoja wa Mataifa. Kama mjuavyo Tanzania ni moja
ya nchi zinazochangia maafisa na askari wa Jeshi hilo.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kutumia nafasi hii, kwa mara nyingine tena kutoa pongezi zangu za dhati
kwa wanajeshi wetu kwa kazi yao nzuri na iliyotukuka waliyoifanya huko
Mashariki ya Kongo. Pia nawapongeza wanajeshi wetu walioko Darfur na
Lebanon kwa kazi yao njema waifanyayo. Wote nawaomba waendelee kudumisha
nidhamu na weledi, mambo yaliyowafanya wapewe sifa nyingi na
kuheshimiwa. Wameiletea nchi yetu heshima kubwa.
Bahati
mbaya, katika kutimiza wajibu wao huo wa kimataifa tumepoteza vijana
wetu 10, saba Darfur na watatu Kongo. Narudia kutoa pole kwa Jeshi letu
na familia za marehemu kwa msiba mkubwa uliowakuta. Napenda
kuwahakikishia kuwa daima tutauthamini na kuuenzi mchango wao. Wanajeshi
wote tunawatakia heri na fanaka tele katika mwaka 2014.
Jumuiya ya Afrika Mashariki
Ndugu Wananchi;
Mwaka
huu, ushiriki wetu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki umepita katika
mtihani kidogo kufuatia ndugu zetu wa Uganda, Rwanda na Kenya kufanya
mambo ambayo yalijenga hisia ya kuwepo mifarakano. Pia yalileta hofu
kuwa hata uhai wa Jumuiya yenyewe ulikuwa mashakani. Katika mkutano
uliopita wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya uliofanyika tarehe 30
Novemba, 2013 mambo hayo tuliyazungumza kwa uwazi na kidugu. Tumeelewana
kuwa yaliyopita si ndwele tugange yajayo.
Ndugu Wananchi;
Katika
mkutano wa Kampala tuliamua mambo matatu makubwa na muhimu katika
kuendeleza agenda ya utangamano wa Afrika Mashariki. La kwanza,
tulikubaliana kuhusu Itifaki ya kuanzisha Umoja wa Fedha wa Afrika
Mashariki na kutia saini. Hii ndiyo hatua ya juu ya utangamano wa
kiuchumi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Tumekuwa tunashirikiana
katika kuwianisha sera za uchumi, fedha na bajeti, kwa uamuzi huu sasa
tunaelekea kwenye kuwa na sera moja ya fedha na bajeti kwa mambo hayo na
hatimaye sarafu moja. Baada ya hatua hii, inayofuata ni ile ya
utangamano wa kisiasa, yaani Shirikisho la Kisiasa. Katika mkutano wetu
wa Kampala tulikubaliana kuwa nchi wanachama ambazo hazijakamilisha
kutoa maoni yao, zifanye hivyo kisha baada ya hapo tuzungumzie jambo
hilo na kulipa mwelekeo.
Ndugu Wananchi;
Vilevile
katika kikao chetu cha Kampala, tuliridhia mpango wa utekelezaji wa
uamuzi wetu wa awali wa kuanzisha Himaya Moja ya Forodha ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki. Lengo la mfumo au utaratibu huu ni kufanikisha
utekelezaji wa malengo na madhumuni ya Umoja wa Forodha wa Afrika
Mashariki. Utaratibu huu utarahisisha na kuharakisha uingizaji na utoaji
wa bidhaa katika bandari na mipaka ya nchi za Afrika Mashariki. Pia,
utaondoa vikwazo visivyokuwa vya kodi katika uingizaji na usafirishaji
wa bidhaa kutoka nchi wanachama kwenda nchi nyingine. Kwa jumla, Himaya
Moja ya Forodha itasaidia biashara kukua na hivyo uchumi wa nchi
wanachama kukua na kuboresha ustawi wa wananchi wa Afrika Mashariki.
Narudia
kuwakumbusha wenzetu wa Wizara ya Afrika Mashariki na Wizara ya Fedha
kutengeneza utaratibu mzuri wa kuelimisha jamii kuhusu Umoja wa Fedha na
Himaya Moja ya Forodha. Nawataka Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda na
Biashara, Wizara ya Afrika Mashariki, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara
ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi, Mamlaka ya Bandari, Mamlaka ya Mapato na
Jeshi la Polisi, kuhakikisha kuwa taratibu zote husika kuhusu Himaya
Moja ya Forodha zinakamilishwa mapema. Nia yangu na yetu sote ni kuona
utekelezaji unaanza mara moja. Hili ni jambo lenye maslahi makubwa kwa
nchi yetu.
Medani za Kimataifa
Ndugu Wananchi;
Katika
medani za kimataifa, mwaka 2013 ulikuwa mzuri kwa Tanzania. Nyota ya
nchi yetu iliendelea kuangaza vizuri. Tumeendelea kuwa na uhusiano mwema
na mataifa yote duniani na hakuna nchi ambayo tuna uadui nayo. Pia tuna
uhusiano mzuri na mashirika ya kimataifa na kikanda yanayoshughulikia
masula ya siasa, fedha na maendeleo. Vile vile, tuna uhusiano mzuri na
watu mashuhuri na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanayoshughulikia
masuala ya maendeleo na ya kibinadamu.
Kwa
sababu hiyo tumepata misaada mingi ya maendeleo na ya kibinadamu
iliyochangia katika mafanikio tuliyoyapata katika maendeleo ya kiuchumi
na kijamii mwaka 2013. Napenda kwa niaba yenu nitumie nafasi hii kutoa
shukrani zangu za dhati kwa nchi, mashirika na watu waliochangia katika
maendeleo ya nchi yetu mwaka huu. Wakati tukiwashukuru, napenda
kuwakumbusha kuwa misaada yao bado tunaihitaji mwaka ujao (2014) na
miaka inayofuatia.
Ndugu Wananchi;
Kwa
upande wa wageni, mwaka huu ulikuwa wa baraka sana kwa Tanzania.
Tumepata heshima ya aina yake ya kutembelewa na Rais wa China,
Mheshimiwa Xi Jiping tarehe 24 – 25 Machi, 2013 na Rais wa Marekani
Mheshimiwa Barack Obama tarehe 01 - 02 Julai, 2013. Pia tulitembelewa na
Rais wa Sri Lanka Mheshimiwa Mahinda Rajapaksa tarehe 26 – 27 Juni,
2013. Waziri Mkuu wa Thailand, Mheshimiwa Yingluck Shinawatra tarehe 30
Julai mpaka Agosti 1, 2013 Pamoja na hao, tulipokea Wakuu wa Nchi na
Serikali 19 waliokuja kushiriki mkutano wa Smart Partnership Dialogue
uliofanyika Dar es Salaam tarehe 28 Juni, 2013.
Ndugu Wananchi;
Vilevile,
tulitembelewa na Marais Wastaafu wa Marekani, Mheshimiwa Bill Clinton
na Mheshimiwa George W. Bush. Nchi yetu inanufaika na misaada
inayotolewa na mashirika yao katika nyanja za afya na kilimo. Napenda
kutumia nafasi hii kuwashukuru wageni wetu wote hao kwa uamuzi wao wa
kuja kututembelea. Wameipa nchi yetu heshima kubwa. Ni matumaini yetu
kuwa mwaka 2014 utaendelea kuwa wa baraka kama huu tunaoumaliza leo. Pia
nawashukuru sana Watanzania wenzangu kwa kuwapokea vizuri wageni wetu.
Wameondoka nchini wakiwa na furaha kubwa na kumbukumbu nzuri kuhusu nchi
yetu.
Licha ya kutembelewa, mimi na viongozi
wenzangu Wakuu wa Nchi yetu tulialikwa na kufanya ziara katika nchi
mbalimbali duniani. Pia tumeshirikishwa katika mikutano mbalimbali ya
kimataifa. Ziara hizo zimekuwa na manufaa makubwa kwa nchi yetu.
Ndugu Wananchi;
Katika
kikao cha Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika kilichofanyia mwezi Januari,
2013 nilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Nchi za Afrika
ya kushughulikia masuala ya mabadiliko ya tabia nchi. Mwenyekiti wa
Kamati hiyo ndiye huwa mwakilishi na msemaji wa Bara la Afrika katika
majukwaa ya kimataifa ambapo masuala hayo yanazungumzwa au
kushughulikiwa.
Kwa ajili hiyo nilikwenda
Warsaw, Poland kuhudhuria Mkutano Mkuu wa 19 wa Mabadiliko ya Tabia Nchi
uliofanyika tarehe 11 – 22 Novemba, 2013. Katika mkutano huo
hatukufanikiwa vya kutosha. Hivi sasa matumaini yetu yapo katika mkutano
wa mwakani (2014) nchini Peru. Iwapo tutafanikiwa tutakuwa tumejenga
msingi mzuri utakaowezesha Mkutano wa Paris mwaka 2015 kufanikiwa
kupatikana Mkataba wa Kimataifa unaozifanya nchi ziwajibike kisheria kwa
masuala yahusuyo kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Ikishindikana Peru na kama mataifa yataendelea kukaidi katika mkutano wa
Paris, hatma ya dunia yetu itakuwa mashakani kwani hali si nzuri hata
kidogo.
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu
tunaoumaliza nchi za SADC tumepoteza mmoja wa viongozi wetu mashuhuri,
shujaa Nelson Mandela. Nilipata nafasi ya kuwawakilisha katika sala ya
kitaifa, kutoa heshima za mwisho na mazishi yake. Kule Qunu, nilipewa
nafasi ya kuzungumza ambayo niliitumia kuelezea uhusiano wetu na shujaa
Mandela, ANC na mchango wa Tanzania kwa ukombozi wa kusini mwa Afrika.
Hotuba yetu ilipokelewa vizuri sana na wenyeji kwani niliwaelezea baadhi
ya mambo ambayo walikuwa hawayajui. Watu wengi wa Afrika Kusini na
duniani kwa jumla sasa wanaufahamu vizuri mchango mkubwa wa nchi yetu
kwa ukombozi wa Afrika Kusini. Tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze
mahala pema, peponi roho ya shujaa Nelson Mandela.
Miaka 50 ya Mapinduzi na Muungano
Ndugu Wananchi;
Mwaka
ujao (2014) ni wa aina yake katika historia ya nchi yetu. Ni mwaka
ambao tunatimiza miaka 50 tangu Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya
Januari 12,1964 na miaka 50 ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya
Tanganyika ziungane na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Aprili
26, 1964. Ni mwaka wa kutambua na kusheherekea mafanikio tuliyoyapata.
Lakini, ni mwaka wa kuweka nadhiri ya kupata mafanikio makubwa zaidi
miaka 50 ijayo na kuendelea. Tutakiane heri katika kusheherekea siku
hizo adhimu.
Shukurani
Ndugu Wananchi;
Napenda
kuchukua nafasi hii adhimu kuwashukuru kwa dhati Makamu wa Rais,
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu,
Mheshimiwa Mizengo Pinda, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,
Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idd. Viongozi Wakuu wenzangu hao
nawashukuru kwa msaada mkubwa walionipa na wanaoendelea kunipa katika
kuiongoza nchi yetu mwaka 2013. Naomba tuendelee hivyo mwaka 2014 kwa
maslahi ya nchi yetu na watu wake.
Nawashukuru
pia Mawaziri na viongozi wengine wa Serikali zetu mbili kwa kazi nzuri
waliyofanya ya kuongoza na kusimamia utekelezaji wa miradi na shughuli
mbalimbali za Serikali. Kazi yao nzuri ndiyo iliyotupatia mafanikio
tunaojivunia leo. Naomba sote tutambue kuwa bado zipo mbele yetu kazi
nyingi na changamoto kubwa na nzito za kushughulikia katika jitihada
zetu za kuwaletea wananchi na nchi yetu maendeleo. Tunao wajibu wa
kudumisha umoja, mshikamano, amani na utulivu wa nchi yetu. Hatuna budi
kuendelea kushirikiana na kusaidiana pamoja na kufanya kazi kwa bidii
zaidi mwaka ujao 2014 kwa niaba na kwa maslahi ya watu waliotuchagua.
Ndugu Wananchi;
Kwa
namna ya pekee nawashukuru sana Watanzania wote po pote pale walipo kwa
kuunga mkono juhudi za Serikali na kufanya kazi kwa bidii na maarifa
kujiletea maendeleo. Hali kadhalika nawapongeza kwa uelewa wenu
ulioiwezesha nchi yetu kuendelea kuwa kisiwa cha amani. Nawaomba
tuendelee na moyo huo wa kuipenda nchi yetu na kujitolea kwa ajili ya
utulivu wake na maendeleo yake na yetu sote.
Naomba
pia nimalize kwa kuwashukuru viongozi wetu wa dini wa madhehebu
mbalimbali pamoja na waumini wao kwa sala na maombi katika kipindi chote
cha mwaka unaoisha leo. Sala zao na maombi yao yametupa nguvu na faraja
katika vipindi vigumu ambavyo tumevipitia. Naomba muendelee kuliombea
taifa letu ili lipate baraka na neema ya Mwenyezi Mungu.
Mwisho
Ndugu Wananchi;
Naomba
tuzidi kuombeana heri ili mwaka ujao uwe wa baraka na mafanikio makubwa
zaidi. Twendeni tukasherehekee mwaka mpya kwa amani na utulivu.
Nawatakia heri na fanaka tele katika mwaka mpya wa 2014.
Mungu Ibariki Tanzania,
Mungu Ibariki Afrika.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment