Jane, mke wa marehemu Mgimwa akilia kwa simanzi
Dar es Salaam. Vilio, simanzi na majonzi,
vilitawala jana katika Uwanja za Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius
Nyerere, wakati mwili wa aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mbunge wa Kalenga
(CCM), Dk William Mgimwa, aliyefariki dunia Afrika Kusini, ulipowasili
nchini.
Mamia ya wananchi wakiwamo viongozi mbalimbali wa
Serikali na wanasiasa, jana walijitokeza uwanjani hapo kuanzia saa 4.30
asubuhi na ilipofika saa 7.45 mchana, ndege ya Shirika la Ndege la
Afrika Kusini (SAA), iliyobeba mwili huo ilitua uwanjani hapo.
Mjane wa marehemu, Jane Mgimwa akiambatana na watoto wake walishuka kutoka ndani ya ndege hiyo na kupokewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi.
Mjane wa marehemu, Jane Mgimwa akiambatana na watoto wake walishuka kutoka ndani ya ndege hiyo na kupokewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi.
Baada ya mwili huo kuwasili , msafara wa magari
ulianza kuelekea nyumbani kwa marehemu Mikocheni B Mtaa wa Ruvu, jijini
Dar es Salaam ambapo ibada fupi ya Misa Takatifu ilifanyika na baadaye
mwili wa Dk Mgimwa ulipelekwa Hospitali ya Jeshi ya Lugalo kuhifadhiwa.
Kwa mujibu wa ratiba ya mazishi, Rais Jakaya
Kikwete ndiye atakayewaongoza viongozi wa Serikali na wananchi kutoa
heshima zao za mwisho kabla mwili haujapelekwa kijijini kwa marehemu,
Magunga mkoani Iringa kesho.
Marehemu Dk Mgimwa, alifariki dunia Januari Mosi
mwaka huu katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic, iliyoko mjini Pretoria,
alikokwenda kwa matibabu, zaidi ya mwezi mmoja na nusu uliopita.
Akizungumza na waandishi wa habari, Januari 2
mwaka huu Waziri Lukuvi alisema, Serikali itaweka wazi chanzo cha kifo
wakati wa kumuaga marehemu kwenye Viwanja vya Karimjee jijini Dar es
Salaam.
“Hatuwezi kusema leo (Alhamisi, Januari 2 mwaka
huu), hapa kwa sababu siyo busara. Hatujapokea hata taarifa ya daktari,
nafikiri siku tutakayokuwa tukimuaga kwenye Viwanja vya Karimjee, ndipo
tutapata nafasi ya kueleza hilo,” Lukuvi alinukuliwa akisema.
Baada ya shughuli ya kuaga mwili huo Viwanja vya
Karimjee, utasafirishwa kwa ndege kwenda kijijini Magunga, kupitia
Iringa mjini ili kuwapa nafasi wananchi kutoa heshima za mwisho, kisha
kwenda kijijini ambako mwili huo utalala, kabla ya maziko
yatakayofanyika kesho.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim alisema kuwa marehemu Dk Mgimwa
atakumbukwa kwa utendaji kazi wake uliotukuka, ambapo kwa muda mfupi
aliweza kuijengea heshima Wizara ya Fedha iliyokuwa imepoteza imani kwa
wananchi.
Mama mzazi
Siku nne baada ya taarifa ya kifo cha aliyekuwa
Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa mama yake mzazi, Consolata Mgovano
amesema kuwa hakupata taarifa kwamba mtoto wake alikuwa amelazwa
hospitalini Afrika Kusini.
Akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake Kijiji cha Magunga,
Kata ya Maboga, Tarafa ya Kiponzero, Wilaya ya Iringa Vijijini jana,
mama huyo alisema hakupata taarifa ya ugonjwa wa mtoto wake hadi
alipovumishiwa kuwa amefariki kwenye taarifa iliyosambaa kwenye vyombo
vya habari.
“Mimi mama yake mzazi, sikuwahi kufahamu, wala
kupata taarifa kama mtoto wangu anaumwa na amepelekwa kutibiwa. Wala
sikuwahi kufahamu anasumbuliwa na ugonjwa gani, badala yake siku za
nyuma nilipata taarifa kupitia vyombo vya habari kuwa amefariki, lakini
taarifa hizo hazikuwa na ukweli,” alisema Consolata.
Alisema taarifa hizo zilimsumbua kwani hakujua tatizo lililosababisha mtoto wake kupoteza maisha.
Mama huyo alisema Marehemu Mgimwa ndiye mwanawe wa kwanza kati ya watoto wanane aliozaa.
“William ndiye aliyekuwa tegemeo langu kubwa, kwa
sababu alikuwa anaisaidia familia pamoja na kuwasomesha watoto hawa wa
marehemu ndugu zake. Sasa hivi sijui ni nani atakayewasaidia na
kuwaendeleza katika kielimu,” alisema mama huyo.
Naye dada wa marehemu, Rosemary Mgimwa alisema
kuwa kaka yao alikuwa nguzo ya familia hivyo, amewaachia pengo kubwa na
hawajui wataliziba vipi.
CHANZO: Mwananchi
CHANZO: Mwananchi
No comments:
Post a Comment