Dar es Salaam. Giza nene limeendelea kutanda ndani ya
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), baada ya juzi kulazimika kuongeza
muda wa kikao cha Kamati Kuu kusubiri uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu aliyekuwa
Naibu Katibu Mkuu wake Zitto Kabwe.
Kikao
hicho kiliendelea jana kikimhoji aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama
hicho, Dk Kitila Mkumbo, huku taarifa nyingine zikieleza kuwa Zitto Kabwe
ameendelea na msimamo wake akituhumu chama hicho kuongozwa kwa ubabe.
Habari
kutoka ndani ya kikao hicho kinachofanyika Hoteli ya Mbezi Garden jijini Dar es
Salaam zinaeleza kuwa mkutano huo ulianza saa 4:00 asubuhi kwa kujadili ajenda
zilizoshindwa kujadiliwa juzi, ambapo Dk Kitila alianza kuhojiwa saa 7:00
mchana.
Hata
hivyo, taarifa hizo zinaeleza kuwa baada ya Dk Kitila kuingia kuhojiwa,
aliwaomba wajumbe amwite mwanasheria
wake, ambaye anazifahamu vyema taratibu na sheria za chama ili amsaidie kujibu
hoja.
Kazi hiyo
ya Dk Kitila kutafuta mwanasheria ilichukua muda mrefu na akapatikana saa 11;00
jioni ndipo kikao kilipoanza.
Hata
hivyo, kabla ya kuingia katika ukumbi huo wa mkutano, Dk Kitila aliliambia
gazeti hili kuwa atatoa ufafanuzi wa msimamo wake baada ya kutoka ndani ya
kikao hicho.
Hata
hivyo, hadi saa 1:00 jioni jana alikuwa bado ndani ya chumba cha mkutano
akihojiwa, huku taarifa zaidi zikieleza kuwa wajumbe wengi walikuwa wakimsihi
Dk Kitila aombe radhi ili asamehewe, yaishe.
Baada ya
kumaliza kuhojiwa saa 1:40 usiku, Dk Kitila alimwambia mwandishi amemaliza kazi yake na anauachia uongozi
kutoa uamuzi wake.
Mnyika
Awali
akitoa taarifa ya kikao hicho, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa chama
hicho, John Mnyika alisema kuwa Kamati Kuu ilishindwa kuwahoji Dk Kitila na
aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba baada ya
kuondoka mapema eneo la mkutano bila ya kuaga na kuzima simu zao. Alisema kwa
sababu Chadema ni chama kinachoamini katika demokrasia, waliamua kuwatafuta kwa
namna nyingine na kufanikiwa kuwapata jana asubuhi.
Mnyika
alisema kuwa kama mmoja wa watu hao hatafika kuhojiwa mbele ya Kamati Kuu, basi
chama kitachukua uamuzi kitakachoona unafaa dhidi yake.
Mjumbe wa Kamati Kuu apigwa
Katika
hali isiyokuwa ya kawaida, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Shaaban Mwamba,
juzi usiku alipata kipigo kutoka kwa maofisa wa
kikundi cha ulinzi cha chama hicho waliokuwa katika eneo ambalo mkutano
wa Kamati Kuu ulifanyika, baada ya kutuhumiwa alikuwa akiwasiliana na wafuasi
wa Zitto.
Taarifa
kutoka kwa mjumbe mmoja ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini, ilisema
kuwa mtu huyo alikuwa akichunguzwa na maofisa wa ulinzi wa chama hicho muda
mrefu, kutokana na nyendo alizokuwa akizionyesha zilizotia shaka.
Mwandishi
wa habari hizi ambaye alikuwa katika eneo hilo, alishuhudia kiongozi huyo
akibebwa juu juu na maofisa hao, huku akiulizwa aliyekuwa akiwasiliana naye ni
nani, kabla ya vijana wengine wa chama kumkamata na kumweka chini ya ulinzi,
wakimtaka atoe ufafanuzi wa alichokuwa anakifanya.
Baada ya
mahojiano ya muda mfupi, kiongozi huyo alionekana akiinuka na kwenda kunawa kwenye bomba la maji, huku akitokwa
damu mdomoni.
Taarifa
zilizopatikana baadaye zilidai kuwa kiongozi huyo alikuwa akiwasiliana na mama
yake Zitto na Katibu wa Zitto, Dk Alex na kwamba pia simu yake ilikutwa na
ujumbe mfupi aliokuwa amewaandikia watu hao.
Gazeti
hili lilijaribu kumtafuta kiongozi huyo ili kueleza sababu ya kupigwa kwake,
lakini hakupatikana eneo la mkutano kwa madai kuwa alikwenda hospitali kupata huduma
ya kwanza, lakini hakurudi.
Wakati
suala la Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe na uongozi wa chama chake
likiendelea kuwasumbua vichwa wapenzi wa chama hicho, inadaiwa kuwa baadhi wa
wabunge, viongozi na wazee wa Chadema, wanataka suala hilo liishe mapema.
Habari
ambazo gazeti hili lilizipata jana, zilisema kuwa baadhi ya viongozi hao
walitaka Zitto aende Halmashauri Kuu ya Chadema na kuomba msamaha ili mambo
yaishe.
“Walimfuata
Kitila (Dk Kitila Mkumbo) wakamwambia amshawishi Zitto ili mambo yaishe nje ya
mahakama, wanataka aende kwenye Halmashauri Kuu kuomba radhi. Kitila akawaambia
kuomba radhi kwa kosa gani?” kiilisema chanzo hicho.
Zitto azungumza
Hata
hivyo, Zitto aliliambia gazeti hili jana kuwa kumekuwa na jitihada mbalimbali za wazee kutaka kukiepusha chama
hicho na migogoro na kuwa amekuwa tayari kwa suala hilo. “Wazee walikuwa na
wajibu wa kuhakikisha hatufiki hapa tulipofika. Sijui kama fursa hiyo bado
ipo,” alisema Zitto.
Kuhusu
uamuzi wake wa kwenda mahakamani alisema: “Nimekwenda mahakamani kutaka haki
itendeke. Chama cha kidemokrasia kinanyima vipi mwanachama fursa ya kukata
rufaa?
“Nisingekwenda
mahakamani kama ningeona haki ikitendeka. Tatizo kubwa la chama chetu sasa
kinaongozwa na mawazo ya kihuni na yeyote mwenye mawazo ya kujenga anaonekana
msaliti.”
No comments:
Post a Comment