Wataalam wa Uhifadhi wakiongozwa
na Dk. Alfred Kikoti (wa kwanza kulia) wakiendelea na zoezi la uwekaji kola
maalum kwa tembo zinazosaidia kudhibiti mienendo ya tembo ndani nan je ya
hifadhi ya Mfumo wa Ikolojia wa Ruaha Rungwa.
Zoezi la uvalishaji wa kola
maalum kwa tembo katika hifadhi ya Ruaha likiendelea.
Helikopta maalum inayotumiwa na
madaktari kwa ajili ya kutambua na kupiga dawa ya usingizi kwa tembo kabla ya
uvalishaji wa kola maalum.
Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Allan
Kijazi (mwenye kofia) akishuhudia zoezi la uvalishaji kola maalum kwa tembo
katika Hifadhi ya Ruaha.
Daktari wa Wanyamapori kutoka
Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori (TAWIRI) akijiandaa kumdunga sindano ya
kumzindua tembo baada ya kukamilika kwa zoezi la kumvalisha kola maalum.
Picha ya pamoja ya wahifadhi
walioshiriki zoezi la uzinduzi wa program maalum ya uvalishaji kola kwa tembo
katika Hifadhi ya Ruaha.
Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Allan
Kijazi (kulia) akiongea na Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Iringa
wakati wa zoezi la uvalishaji kola kwa tembo katika Hifadhi ya Ruaha.
Na Jovina Bujulu-MAELEZO
Utalii ni
miongoni mwa sekta muhimu zinazoliingizia Taifa pato hasa fedha za kigeni
zinazotolewa na watalii wanaofika nchini kwa shughuli mbali mbali ikiwemo kuangalia
wanyama na vivutio vilivyopo katika hifadhi za taifa.
Sekta hii
ya utalii inakumbana na tatizo kubwa la ujangili ambalo linaripotiwa kuiingizia
taifa hasara kubwa kutokana na idadi kubwa ya wanyama pori hasa tembo kuuawa
kila mwaka.
Hivi
karibuni Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA) limezindua programu maalam ya kuwavalisha
tembo kifaa maalumu kijulikanacho kama “kola” au king’amuzi maalum shingoni mwa
tembo hao kinachong’amua na kurekodi mienendo yao kwa kutumia mawasiliano ya
satelaiti.
Program
hiyo inatekelezwa katika mfumo wa ikolojia wa Ruaha Rungwa ambapo tembo 30
wanaoongoza makundi 30 wamevalishwa kola hizo.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi wa program hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Bwana Allan
Kijazi alisema kuwa inalenga kuimarisha ulinzi wa tembo nchini. “Lengo kuu la
program hii ni kupata taarifa za kina juu ya mienendo ya tembo katika mfumo wa
ikolojia wa Ruaha Rungwe zitakazosaidia kubainisha maeneo shorobo (njia za
wanyama) na mitawanyiko yao kwa ajili ya ulinzi wa tembo” alisema Bwana Kijazi.
Aliendelea
kusema kuwa teknolojia hiyo inawawezesha kujua mwenendo wa tembo ndani na nje
ya hifadhi, kujua walipo, wanapopita, kasi yao, sehemu wanazojificha,
wanapokunywa maji, ikiwa wamejeruhiwa, wanapopumzika, maeneo wanayokaa muda
mrefu, kama wamekufa, kama wamehama hifadhi
moja hadi nyingine na taarifa nyingine nyingi, hivyo itakuwa rahisi kwa askari
wa wanyamapori kufuatilia usalama wa tembo hao.
Akizungumzia
uanzishwaji wa program hiyo, Bwana Kijazi alisema kuwa inafadhiliwa na taasisi
ya Global Government Facility pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la
Maendeleo (UNDP); ambapo UNDP kwa kushirikiana na TANAPA na SPANET wametoa
kandarasi ya kufanya kazi hiyo ya kufunga “kola” kwenye tembo kwa kituo cha
kimataifa cha utafiti wa Tembo “WORLD ELEPHANT CENTRE “ kilichopo mkoani Arusha.
Bwana
Kijazi aliendelea kusema kuwa, pamoja na shughuli ya kuweka “kola” kwenye
tembo, pia kituo hicho kina jukumu la kuongeza hali ya usalama wa tembo katika
hifadhi za Taifa.
Kwa
upande Mkurugenzi wa Kituo cha World Elephant Centre Dkt. Alfred Kikoti ambaye
pia ni mtafiti wa tembo aliyebobea kwenye sayansi za wanyama hao alisema kuwa
kituo hicho kilianza kazi ya kufunga “kola” kwenye tembo kuanzia mwaka 2005 ambapo
hadi sasa wamekwisha fanya kazi hiyo maeneo ya ukanda wa kaskazini kuanzia Serengeti,
Loliondo, Manyara, na Tarangire.
Maeneo
mengine ni Wami Mbiki mkoani Morogoro, Mashariki mwa Serengeti, Ziwa Natron,
Kilimanjaro Magharibi na Amboseli upande wa Kenya.
Dkt.
Kikoti alisema kuwa sehemu zote walizofanya kazi ya kufunga kola kwenye tembo,
kifaa hicho kinafanya kazi vizuri ya
kufuatilia mienendo ya tembo kwa tija na ufanisi mkubwa.
Akizungumzia
jinsi kifaa hicho kinavyofanya kazi, Dkt Kikoti alisema kuwa, kifaa hicho kina uzito
wa kilogramu 5 ambacho huvalishwa kwenye shingo ya tembo na kinarekodi mwenendo
wa tembo kwa njia ya satelaiti.
“Kituo
kinafuatilia mienendo ya tembo kwa kutumia kompyuta maalum ambazo zimeunganishwa
na kifaa hicho, hivyo tembo wanaonekana
kwenye kompyuta hizo, na kila wanapokwenda na wanachofanya kinarekodiwa.”
Alisema Dkt Kikoti.
Aidha, Dkt.
Kikoti alisema kuwa kifaa hicho kinatumia betri maalum ambayo ina uwezo wa
kukaa kwa miaka 3 hadi 5, kabla ya kuweka betri nyingine.
Alipoulizwa
jinsi namna wanavyowavalisha tembo kola hiyo, Dkt Kikoti alisema kuwa wanatumia
helikopta ambayo inakuwa umbali wa mita 30 hadi 40 kutoka ardhini kulingana na
ukubwa wa pori walipo tembo hao, na kuongeza kuwa wanachagua tembo mmoja kutoka
kwenye kundi la tembo wanayeona anafaa kufungwa kola hiyo.
“Tembo
anayechaguliwa ni yule ambaye anaonekana ni kijana mwenye umri wa miaka 20 hadi
35, na asiye na mtoto,wala majukumu, hapo daktari wa wanyama anamchoma sindano
kutoka kwenye helikopta ambayo inamfanya alale usingizi na tembo wengine kwenye
kundi wanakimbia kutokana na mlio na kelele za helikopta na baada ya hapo
wanateremka kwenye helikopta na
kumvalisha kola hiyo” alisema Dkt Kikoti.
Aliendelea
kusema tembo huyo baada ya kuzinduka huwafuata tembo wenzake na waliokuwa naye
kwenye kundi na hapo kifaa hicho huanza kuratibu na kufuatilia mwenendo wa
kundi hilo la tembo.
Akizungumzia
kupungua kwa idadi ya tembo katika hifadhi za taifa, Dkt. Kikoti alisema kuwa
kwa sasa hali si nzuri kwani kwa kawaida
makundi ya tembo huwa na tembo 150 hadi 300 lakini kwa sasa makundi yaliyofungwa
kola ni yenye tembo 15 kwa kundi dogo na 300 kwa kundi kubwa.
Katika
kuendeleza jitihada za kulinda tembo, Dkt. Kikoti alisema kuwa kwa sasa kituo
cha World Elephant Centre kinaandaa ujenzi wa kituo kikubwa zaidi cha kimataifa
kitakachoonesha taarifa za tembo dunia nzima ikiwa ni kumuenzi hayati Mwalimu
Nyerere.
Naye
Meneja Mawasiliano wa TANAPA Bwana Paschal Shelulete alisema kuwa zoezi la kuwafunga
kola tembo litasaidia kudhibiti mienendo ya tembo na hivyo kujua walipo ili
kuimarisha ulinzi dhidi ya majangili.
Dkt.
Kikoti alizungumzia mafanikio ya program hiyo kuwa ni pamoja na kutoa elimu kwa
maaskari wa wanyamapori kwani wanaelewa wanyama walipo na kuimarisha doria
sehemu hizo.
Mafanikio
mengine ni idara ya wanyamapori kufahamu mienendo ya tembo na hivyo kuwaelekeza
watalii sehemu ambazo tembo wanakuwepo kwa wakati huo.
Aidha
matumizi ya ardhi yameboreshwa kwani kutokana na satelaiti kola kutoa taarifa
tembo walipo, watu wamefahamu sehemu zinazofaaa kwa wao kuishi na kuendesha
shughuli za kilimo. Pia kutokana na kuwepo kwa ufuatiliaji wa taarifa za
mienendo ya tembo, migongano isiyo ya lazima kati ya tembo na binadamu imepunguzwa.
Pamoja na
jitihada za serikali za kulinda tembo, wadau mbalimbali wa wanyamapori wameunga
mkono suala hilo kwa kuanzisha kampeni ya “OKOA TEMBO WA TANZANIA.” ambayo ina
lengo la kuhamasisha watanzania kuhifadhi tembo.
Akizungumzia
sababu za kuanzisha kampeni hiyo, Mratibu wa kampeni hiyo Bwana Shubeti Mwarabu
alisema kuwa walihamasika kutokana na takwimu za sensa ya tembo zilizotolewa na
Taasisi ya Wanyamapori (TAWIRI) inayoonesha kuwa tembo wamepungua kwa asilimia
60% kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
“Mwaka
2009 idadi ya tembo ilikuwa 109,000 na ilipofika 2014 takwimu hizo zilionesha
tembo wamebaki 43,000 kwa nchi nzima” alisema Bwana Shubeti.
Bwana Shubeti
aliendelea kusema kuwa kampeni hiyo imefanikiwa kutoa elimu iliyotolewa kwa
Umma kwa njia mbalimbali kama vile ushiriki wa maonesho mbalimbali na matamasha
ambapo husambaza vipeperushi vinavyoonesha madhara ya kuua tembo, kufanya
matamasha mbalimbali yenye lengo la kuzuia kuua tembo.
Programu
ya kufunga kola tembo itaendeshwa kwa miaka mitatu, na inawashirikisha wadau
mbali mbali wakiwemo, World Elephant Centre, TANAPA, Taasisi ya utafiti wa
wanyamapori (TAWIRI), Wizara ya Maliasili na Utalii, Idara ya wanyamapori, na
askari wa hifadhi ya taifa.
No comments:
Post a Comment