Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Tuesday 29 December 2015

KWA HERI IPTL, VIPI WALE WALIOTUINGIZA MKENGE?

 Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya ufuaji umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), iliyo chini ya Pan Africa Power Solutions (PAP), Bw. Harbinder Sethi (Kushoto), akiwaonyesha waandishi wa habari (hawapo pichani) maboresho yaaliyofanyika katika kiwanda hicho tangu PAP ilipochukua uongozi wa IPTL. Wakishuhudia ni baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya IPTL.

Na Daniel Mbega
ACHANA na Shs. 240 bilioni za akaunti ya Tegeta Escrow, tunazungumzia mabilioni ambayo Serikali imeilipa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kwa miaka 20.
Mkataba wake umekwisha mwaka huu 2015 kwa staili ya aina yake, ukitanguliwa na wakubwa kugawana mabilioni yaliyokuwa yamehifadhiwa kwenye akaunti ya Escrow, huku wengine wakiziita fedha hizo kwamba ni ‘za mboga’.

Jambo linalotia simanzi ni kwamba, licha ya wakubwa hao wakiwemo wa Ikulu, kugawana mabilioni hayo, lakini mkataba wake pia ulikuwa na utata mkubwa tangu awali, huku ukiliingiza taifa katika hasara kubwa kwa miaka yote 20, hali inayowalazimu Watanzania waiombe Serikali ya Awamu ya Tano ipitie ripoti zote za mradi huo na kuwawajibisha wahusika wote kwa sababu wanafahamika.
Taarifa zilisema kwamba, baadhi ya mawaziri waliotajwa pamoja na watendaji wengine serikali walipewa rushwa ya Dola 200,000 kila mmoja ili kufanikisha, lakini wapo wengine wazalendo, akiwemo Patrick Rutabanzibwa aliyekuwa Kamishna wa Nishati wakati huo, ambao walikataa rushwa hiyo.
Wakati mkataba huo unasainiwa mwaka 1995 ili IPTL izalishe umeme wa megawati 100 na kuliuzia Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco), Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikuwa Andrew Chenge wakati Waziri wa Maji, Nishati na Madini alikuwa Jakaya Kikwete, rais mstaafu wa awamu ya nne.
Kwa mujibu wa mkataba huo, IPTL ilijenga mtambo wa SSD Tegeta jijini Dar es Salaam kwa gharama ya Dola 163.5 milioni.
IPTL ilianzishwa mwaka 1994 ikiwa ni kampuni ya ubia baina ya Mechmar Corporation ya Malaysia iliyokuwa na hisa 70% na kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited inayomilikiwa na mzawa James Rugemalira iliyokuwa na hisa 30%.
Mchakato wenyewe wa kuipatia zabuni IPTL ulitandwa na rushwa kubwa na pamoja na ushauri kutolewa na wataalamu wa uchumi, bado viongozi wa serikali waliamua kuipatia zabuni hiyo bila hata kurekebisha baadhi ya vipengele kama ilivyoshauriwa.
Ripoti ya Profesa Mark Mwandosya, wakati huo akiwa Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Taasisi ya Nishati, Mazingira, sayansi na Teknolojia (CEEST – Centre for Energy, Environment, Science and Technology) kabla ya kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, iliyowasilishwa kwa Rais Benjamin Mkapa Januari 1998 ilibainisha kuwepo kwa rushwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za kiserikali katika kuipatia IPTL mradi huo mkubwa.
Katika ripoti hiyo ambayo haijawahi kuwekwa hadharani kutokana na kuwagusa moja kwa moja vigogo wa serikali, wakiwemo mawaziri wanne waliokuwa kwenye Serikali ya Awamu ya Tatu pamoja na mbunge mmoja, ilielezwa kwamba rushwa hiyo ndiyo iliyowafumba macho watendaji wa serikali na hivyo kuliingiza taifa mkenge katika mzigo huo mkubwa.
Kulingana na mkataba huo, Serikali/Tanesco ilikuwa inailipa IPTL Dola za Marekani 2,865,920 kila mwezi ambazo kama zitakokotolewa kwa thamani ya Shs. 1,500 kwa Dola moja kama ilivyokuwa miaka mitano iliyopita, ni sawa na Shs. 4,298,879,847 (bila Kodi ya Ongezeko la Thamani – VAT) hali inayomaanisha kwamba, katika kipindi cha miaka 20, Tanzania imekamuliwa jumla ya Dola 687,820,800 (kwa kiwango cha miaka mitano iliyopita, ni sawa na Shs. 1,031,732,000,000).
Inaelezwa katika ripoti hiyo kwamba, Wamalaysia walipowasili tu nchini, baada ya muda mfupi walipata baraka za kuanza kazi kwa kuwa inaaminika walitumia mwanya wa kufahamiana na ‘wakubwa’ kurahisisha kukubalika kwa IPTL.
Ripoti hiyo inaeleza kwamba, unzishwaji wa IPTL ulikuwa wa mashaka kwa sababu ilikosa ‘chanzo’ cha maana cha kupewa kazi hiyo kubwa, ikawa inabainishwa kwamba ‘mwenyeji’ wake hapa nchini, Rugemalira alikuwa na ufahamu mkubwa wa ‘kunusa’ mahali pa kupata fedha nyingi.
Aidha, ripoti inasema kukubalika na hatimaye kupewa kazi kwa IPTL kusingewezekana kama siyo kwa njia nyingine zilizojificha.
Itakumbukwa kwamba, taasisi ya Decision Strategies Fairfax International (DSFX) ya Marekani nayo ilieleza kutokana na ripoti ya Mwandosya kwamba, profesa huyo alibainisha namna baadhi ya viongozi wa serikali wasivyokuwa waaminifu.
DSFX ilipewa kazi na Serikali ya Rais Mkapa kupitia upya mradi mzima wa IPTL na kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia Rushwa (PCB wakati huo – sasa PCCB) ilibainisha kwamba baadhi ya watendaji wa serikali, wakiwemo mawaziri, waliwezesha IPTL kupata zabuni kubwa ya kufua umeme ulioelezwa kuwa wa dharura na kwamba walipewa rushwa ili kufanikisha kazi hiyo.
Licha ya taarifa zote hizo za uchunguzi na ushauri wa wataalamu wa uchumi, sheria za mikataba na wahandisi wa nishati, lakini serikali ilipuuza na hakuna kilichofanyika zaidi ya ripoti hiyo kuwekwa kabatini.
Mwaka 2002 suala hilo lilitua mikononi mwa PCB, na taarifa za baadaye zikasema tayari faili limepelekwa Polisi kwa ajili ya kushughulikiwa kisheria, ikiwemo kuwafikisha mahakamani wahusika, lakini mpaka nukta hii hakuna kilichofanyika.
Mtiririko mzima wa mchakato mzima hadi IPTL ikapewa mkataba wa kuzalisha umeme ghali upo, umeandaliwa vizuri, umehifadhiwa na unafahamika kwa viongozi wengi wa juu serikalini.

Mwanzoni mwa 1992
Tanzania inakabiliwa na uhaba wa umeme kutokana na ukame ulioikumba na kukausha maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme. Serikali ya Awamu ya Pili chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi inaanza kupitia mapendekezo kadhaa ya wataalamu kuhusu namna ya kukabiliana na tatizo hilo.

Novemba 1994
IPTL, kampuni iliyosajiliwa Tanzania kwa ubia kati ya Mechmar Corporation ya Malaysia na VIP Engineering and Marketing Limited ya Mtanzania James Rugemalira, inapeleka mapendekezo ya kutatua tatizo la umeme kwa kuanzisha mradi wa haraka wa kufua umeme.

Desemba 1994
Wawakilishi wa Mechmar wanaitembelea Tanzania na kufanya mazungumzo na viongozi wa Serikali ya Tanzania inayowakilishwa na viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Maji, Nishati na Madini, Tanesco na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wakati huo Andrew Chenge.

Januari 1995
Wizara ya Maji, Nishati na Madini inapeleka mapendekezo katika kikao cha Kamati ya Ufundi ya Baraza la Mawaziri (IMTC) na kupendekeza IPTL ipewe zabuni. IMTC inakataa mapendekezo ya Wizara ya Maji, Nishati na Madini kwa kuwa yalikosa tathmini ya kifedha na kiuchumi kuhusu mradi huo. Baada ya uamuzi wa IMTC, Tanesco chini ya Mkurugenzi Mtendaji wake wakati huo Baruany Luhanga inaipa zabuni kampuni ya Economics International ya London, Uingereza kufanya tathmini ya kina kuhusu mradi huo kifedha na kiuchumi. Economics International inasema mkataba utakuwa ni gharama kubwa kwa serikali ingawa inapendekeza IPTL itekeleze mradi. Economics International ilipendekeza vipengele vya mkataba vifanyiwe tathmini ya kina kabla ya kufanya mkataba wowote.

Mei 3, 1995
Bila kuzingatia ushauri wa Economics International juu ya masuala ya uchumi, Baraza la Mawaziri linapitisha uamuzi kuwa mkataba utiwe saini kama ulivyowasilishwa awali.

Mei 26, 1995
Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco inapitisha mkataba baada ya kupewa idhini na uongozi wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini. Mkataba wa kifisadi ulioliumiza taifa kwa miaka 20 mfululizo.

Julai 16, 1996
Wizara ya Nishati na Madini chini ya Waziri Dk. William Shija inatoa leseni kwa IPTL na Tanesco zishirikiane kuwaumiza watumiaji umeme kwa kuongeza gharama.

Februari 1997
IPTL inaweka mkataba wa kiufundi na kampuni iitwayo Stork-Wartsila ya Uholanzi. IPTL inakiuka vipengele vya mkataba na Tanesco/Serikali kwa kufunga mitambo ya kufua umeme wa bei ghali inayotumia kasi ya kati (Medium Speed Diesel – MSD) badala ya kasi ndogo (Slow Speed Diesel – SSD) iliyokubaliwa katika mkataba. IPTL inafanya hivyo bila hata kuitaarifu Tanesco wala serikali.

Septemba 1997
Rais Benjamin Mkapa anaagiza mkataba wa IPTL upitiwe upya na kuagiza Wizara ya Nishati na Madini kuanza majadiliano na wawakilishi wa IPTL.

Oktoba 13, 1997
Baraza la Mawaziri linapitisha uamuzi kwamba IPTL izingatie vipengele vyote vya mkataba na kuuza umeme kwa bei nafuu.

Januari 1998
Ripoti ya upitiaji upya mkataba huo inawasilishwa kwa Rais Mkapa na kubainisha kwamba kulikuwa na rushwa na ukiukwaji wa maadili katika kuipatia IPTL zabuni.

Machi 1998
Tanesco inapewa kibali cha serikali kuipa notisi IPTL kuhusu ukiukwaji wa mkataba. IPTL nayo inafungua madai Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam ikidai Tanesco iendelee kulipa gharama za umeme kila mwezi na kushinda, lakini uamuzi wa kesi ukasogezwa Mahakama ya Rufaa. Baadaye shauri linavuka mipaka ya nchi na kuamuliwa katika mahakama ya kimataifa iitwayo International Centre for the Settlement of Investment Disputes (ICSID) iliyoko London, Uingereza baada ya IPTL kushindwa kutoa vielelezo vya kuthibitisha madai yake.

Februari 2001
ICSID inatoa uamuzi kuwa IPTL ilionewa kkidogo na kwamba Tanesco ilitambua mabadiliko ya vipengele vya mkataba kutoka matumizi ya mitambo ya SSD hadi mitambo ya MSD.

2002 hadi 2013
Mbia wa IPTL – VIP Engineering and Marketing Limited ya Tanzania inafungua kesi ya madai Mahakama Kuu ikitaka kufungwa kwa kampuni ya IPTL. Hata hivyo, kesi hiyo ikarushwa tena hadi London kwa majaji wa Labour Court of International Arbitration (LCIA).
Wabia wa IPTL kutoka Malaysia, Mechmar Corporation wanasema uamuzi wa VIP Engineering ni ujanja tu wa kutaka kupandisha thamani ya hisa zake ndani ya IPTL.
Serikali ya Tanzania inaamriwa kulipa Dola 30 milioni kila mwaka kwa IPTL  hadi mwaka 2015 ambazo zinawekwa kwenye akaunti maalum ya Tegeta Escrow. Wamalaysia wanakataa kata kata kuuza mitambo yao ya IPTL kwa Tanesco au serikali kwa sababu za wazi kwamba walikuwa wanafaidi uhondo wa mamilioni hayo.
Wizara ya Nishati na Madini chini ya Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete inaamua kunyamazia suala hilo.
Mwaka 2013 VIP Engineering inashinda kesi, ndipo ufisadi mkubwa wa Shs. 240 bilioni kutoka akaunti ya Tegeta Escrow unafanyika, tena bila kuzingatia sheria za usimamizi wa fedha.

2014
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi) David Kafulila, anatoa hoja binafsi Bungeni kuhusu ufisadi wa akaunti ya Tegeta Escrow. Anapingwa lakini baadaye hoja hiyo inashika nguvu na kuikisa serikali.

Januari 2015
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, anajiuzulu kufuatia kashfa hiyo. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, akafukuzwa kazi baada ya kupokea Shs. 1 bilioni kutoka kwa Rugemalira huku maelezo yake yakishindwa kujitosheleza, lakini yeye akasema hizo zilikuwa ‘fedha za mboga’.


0656-331974

No comments:

Post a Comment