IGP Ernest Mangu
Taarifa zilizoifikia www.brotherdanny.com dakika chache zilizopita zinaeleza kwamba takriban watu saba wameuawa katika mapigano kati ya wafugaji wa kabila la Wamasai na wakulima kwenye vijiji vya Laitimi, Mbumbuseseni na vitongoji vyake wilayani Kiteto mkoani Manyara.Kwa mujibu wa taarifa hizo, mauaji hayo yamefanyika kati ya jana Jumamosi na leo Jumapili na mpaka sasa mapigano bado yanaendelea.
Vyanzo vya habari kutoka eneo hilo vimeeleza kwamba, chanzo cha mapigano hayo ni baadhi ya wafugaji wa Kimasai kulisha mifugo kwenye mashamba ya watu na kwamba wenye mashamba walipohoji kisa cha wao kufanya hivyo, Wamasai hao wakawaua wakulima wawili kwa kuwakata kwa mapanga.
Inaelezwa kwamba, wakulima hao wakishirikiana na kikundi maarufu kwa upigaji wa mishale cha Jenga kutoka kabila la Wakaguru, leo hii nao wamekwenda kufanya mashambulizi ambapo inaelezwa kuwa watu watano wameuawa.
"Hali ni mbaya sana huku, watu wameyakimbia makazi yao na mapigano yanaendelea kuanzia kwenye Kitongoji za Mtanzania kuelekea mashariki katika maeneo ya Mbumbuseseni (Seseni)," alisema mmoja wa wakulima hao ambaye alieleza kuwa alikuwa akikimbia mapigano hayo.
Wakulima hao wameiomba serikali ifanye haraka kutuliza vurugu hizo ambazo zinaweza kuleta uvunjifu wa amani katika maeneo hayo.
Maeneo hayo yamekuwa na mgogoro kwa takriban miaka 10 sasa na zaidi ya watu 50 wanahofiwa kuuawa kutokana na mapigano tangu migogoro ya ardhi ilipoanza.
Mwaka 2006 wafugaji hao walizusha vurugu kubwa zilizosababisha mauaji dhidi ya wakulima, ambapo serikali ya wilaya ya Kiteto ilituma askari polisi kuwahamisha kwa nguvu wakulima kwa madai kwamba ni 'wavamizi' wa maeneo hayo ambayo yalikuwa mapori.
Katika operesheni hiyo wananchi wengi walichomewa nyumba zao pamoja na mazao na wengine kuwekwa rumande, ingawa baadaye waliachiliwa.
Wakulima hao walifungua kesi ya ardhi wakidai kuachiwa waendelee kulima kwa maelezo kwamba wao ni Watanzania na wanayo haki kuitumia ardhi hiyo ambayo haikuwa ikitumiwa na yeyote. Walishinda kesi hiyo, lakini wafugaji wakakata rufaa kupinga hukumu hiyo na wakashinda.
Hata hivyo, wakulima hao waliamua kukata rufaa tena katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi ambapo mwaka 2012 walishinda kesi hiyo huku wakiwa tayari wameamriwa na serikali kutolima kwenye maeneo hayo.
Blog hii itawaletea kwa kina taarifa kutoka huko na kiini hasa cha mgogoro huo.
No comments:
Post a Comment