Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday, 2 January 2014

KATIBA MPYA YAWAKATAA WABUNGE DARASA LA SABA


Na Waandishi Wetu 

RASIMU mpya ya Katiba imekataa watu wenye elimu ya chini ya kidato cha nne kugombea ubunge.

Pia mbali na elimu, imependekeza miongoni mwa sifa za ubunge, mgombea awe na umri usiopungua miaka 21 na elimu isiyopungua kidato cha nne.
Aidha, aliyepata kuwa mbunge kwa vipindi vitatu vya miaka mitano, kulingana na mapendekezo hayo ya rasimu, hana sifa za kugombea.
Pia mtu anayeshika madaraka ya ofisa mwandamizi katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano au nchi washirika haruhusiwi kugombea kwa mujibu wa Rasimu hiyo.
Rasimu imeendelea kubariki, kwamba mbunge anapofukuzwa au kuvuliwa uanachama wa chama chake cha siasa, atakuwa amekosa sifa za kuendelea na ubunge.
Katika Rasimu hiyo kama ilivyokuwa ya awali, wapiga kura wamepewa mamlaka ya kuondoa madarakani mbunge atakayeacha kuishi au atakayehamisha makazi yake kutoka eneo la Jimbo la Uchaguzi kwa zaidi ya miezi sita bila sababu za msingi.
Sababu nyingine ambayo inaweza kuwa chanzo cha wananchi kumwondoa mbunge madarakani, ni kushindwa kuwasilisha au kutetea kwa dhati hoja zinazotokana na kero za wapiga kura wake.
Rasimu inaelekeza, kwamba Bunge litatunga sheria kuweka masharti ya kuendesha uchunguzi kwa mbunge atakayeshindwa kutekeleza majukumu yake kwa wapiga kura na utaratibu wa kumwondoa kwenye ubunge.
Akaunti nje Rasimu hiyo imependekeza iwe marufuku kwa kiongozi wa umma kufungua au kumiliki akaunti ya benki nje ya nchi isipokuwa sheria za nchi zinaporuhusu.
Hayo ni miongoni mwa mambo yaliyoongezwa katika Rasimu ya Pili ya Katiba katika eneo la maadili na miiko ya uongozi na utumishi wa umma.
Katika eneo hilo kiongozi wa umma hataomba au kupokea mkopo au faida yoyote kwa namna au mazingira ambayo yanashusha hadhi au heshima ya utumishi wa umma.
Pia asasi za kiraia ambazo zimekuwa mstari wa mbele kulalamika kuwa Tume ya Uchaguzi haiko huru, zimepewa mamlaka na Rasimu mpya ya Katiba kuwa zinaweza kupendekeza majina ya watu wanaoweza kuteuliwa kuwa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi.
Rasimu hiyo ambayo alikabidhiwa Rais Jakaya Kikwete juzi, imetaja asasi hizo zitawasilisha majina hayo kwa Kamati Maalumu ambayo itajadili na kuchambua majina hayo kabla ya hatua ya mwisho ya uteuzi utakaofanywa na Rais.
Kamati hiyo ya Uteuzi itachambua majina ya watu walioomba na waliopendekezwa kuwa wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi na kuwasilisha kwa Rais majina ya watu wanaofaa kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi.
Wajumbe wanaounda Kamati hiyo ya Uteuzi ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Spika wa Bunge, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Spika wa Bunge la Tanganyika, Jaji Mkuu wa Tanganyika na Jaji Mkuu wa Zanzibar.
Rais atateua Mwenyekiti, Makamu na wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi kutoka miongoni mwa majina yaliyowasilishwa na Kamati ya Uteuzi na atawasilisha majina hayo bungeni kwa ajili ya kuthibitishwa na Bunge.
Pia miongoni mwa mambo ambayo Tume imebadilisha kutoka Rasimu ya kwanza ni kuondoa mamlaka ya wakuu wa nchi washirika kuunda vikosi vya ulinzi au idara zitakazoshughulika na mambo ya kiusalama katika mamlaka zao.
Kwa upande wa Idara ya Usalama, inaeleza kuwa wakuu wa nchi washirika wanaweza kumwagiza kiongozi yeyote wa Jeshi la Polisi au Idara ya Usalama wa Taifa kuchukua hatua yoyote ambayo ni muhimu kwa ajili ya kulinda au kuimarisha usalama wa eneo lolote la nchi mshirika husika.
Awali Rasimu ilikuwa inawapa wakuu wa nchi washirika mamlaka ya kuanzisha idara au taasisi zitakazoshughulika na mambo ya kiusalama ambazo zitafanya na kutekeleza majukumu yao kwa kushirikiana na Idara ya Usalama ya Muungano.
Rasimu pia imeanzisha nafasi ya Waziri Mwandamizi wa Serikali ya Muungano ambaye atateuliwa na Rais na kuthibitishwa na Bunge. Kazi na mamlaka ya Waziri huyo itakuwa ni udhibiti na usimamizi wa utekelezaji wa shughuli za Serikali za siku hadi siku.
Waziri huyo atatekeleza majukumu yote atakayoelekezwa na Rais na katika utekelezaji wa majukumu yake atawajibika kwa Rais.
Shughuli kama hizo kwa sasa zinafanywa na Waziri Mkuu ambaye anateuliwa na Rais na kuthibitishwa na Bunge na ndiye msimamizi wa shughuli zote za kiserikali.
Pia kutakuwa na Tume ya Utumishi wa Bunge ambayo itaundwa na Spika, Naibu Spika, wabunge wawili, kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni na mwanasheria mkuu wa Serikali.
Tume hiyo ndiyo itaandaa na kupendekeza viwango vya mishahara, posho na marupurupu mengine kwa wabunge na watumishi wa Bunge kwa chombo chenye jukumu la kusimamia maslahi ya watumishi wa umma.
Wakati huo huo, Rasimu hiyo mpya imetambua Serikali ya Tanganyika. Rasimu ya awali, ilikuwa ikitaja Tanzania Bara lakini sasa inatamka Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambazo kwa Rasimu hiyo zinatambulika kama nchi washirika wa Jamhuri ya Muungano. Shughuli ya uendeshaji wa jumuiya za dini itakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya Serikali.
“Ni marufuku kwa mtu, kikundi au taasisi ya dini kutumia uhuru wa kutangaza dini kwa namna ambayo italeta uvunjifu wa amani, kujenga chuki au kuchochea vurugu na ghasia kwa madai ya kutetea imani au dini hiyo,” Rasimu inatamka.
Imani ya dini haitatumika kwa namna yoyote itakayogawa wananchi, kuleta uhasama au kuharibu amani miongoni mwa wananchi. Rasimu pia inataka vyombo vya habari viwe huru na kuwa na haki ya kupata, kutumia na kusambaza habari na taarifa vinazopata.
Hata hivyo, vitawajibika kuheshimu na kulinda utu, heshima, uhuru na staha ya wananchi dhidi ya habari na taarifa vinazotumia, zinazotayarisha na kusambaza.
Serikali na taasisi zake, asasi za kiraia na watu binafsi watakuwa na wajibu wa kutoa habari kwa umma juu ya shughuli na utekelezaji wao.Rasimu inaelekeza Bunge kutunga sheria kulinda haki na uhuru wa vyombo vya habari.

Kikwete ‘akuna’ wengi

Katika hatua nyingine, wasomi, viongozi wa dini na wananchi wa kawaida wamemwelezea Rais Kikwete kuwa shujaa aliyefungua mwaka 2014 kwa kudhihirisha ukomavu wa kisiasa katika uongozi.
Wamesema uvumilivu katika mambo mengi kwenye uongozi wake uliowezesha kukamilika kwa hatua ya kwanza ya kupata Rasimu ya Katiba mpya kwa amani, unadhihirisha alivyo shujaa.
Miongoni mwa waliopongeza na kumsifu Rais Kikwete, ni pamoja na Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini aliyemwelezea kuwa uvumilivu, utulivu na hekima ndivyo vimewezesha hayo.
“Lazima tumshukuru Rais Kikwete, kusema ukweli hakuwa na jazba, alitulia, alisikiliza na kuelekeza pale ilipobidi ili mambo yasiharibike, ameonesha ukomavu wa kiutawala na kisiasa,” alisema Kilaini.
Aliendelea: “ Kwa mwaka huu (2013) hiki (Rasimu) ni kitu cha pekee tumekipata Watanzania, tuzingatie alichosema jana (juzi) wakati alipokabidhiwa Rasimu, kwamba si kila kitu anachotaka mtu kitakuwemo kwenye Katiba, tuweke maslahi ya Taifa mbele.”
Askofu Kilaini akitoa maoni yake kama kiongozi wa kiroho kuhusu mchakato huo, alisema Watanzania watakuwa wachoyo wa fadhila wasipomshukuru Mungu kufika salama katika hatua ya kupata Rasimu ikiwa ni kuelekea ukingoni mwa kupata Katiba mpya.
Askofu huyo alisema, Tanzania imefanya vizuri katika eneo hilo ikilinganishwa na mataifa mengine yaliyokuwa na mchakato kama huo.
Wengine waliozungumzia mchakato huo wa Katiba, ni pamoja na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana ambaye pia alisema Rais Kikwete alivumilia mengi.
Katika maoni ya wengi, walisema kipindi cha kwanza cha mchakato wa Katiba mpya kabla ya kupatikana Rasimu ya pili juzi Desemba 30, Rais Kikwete alivumilia mengi magumu kwa maana kwamba hakuwa na jazba kama mtawala mkuu wa nchi kwa yote aliyokuwa akiyasikia ya kukatisha tamaa.
Dk Bana alisema pamoja na yote yaliyokuwa yakisemwa juu yake na Serikali yake kwa ujumla, alitulia na kusikiliza wananchi wanachotaka.
Alisema: “Kabla sijasema mengi nitoe pongezi za dhati kwa Rais Kikwete kuona mahitaji haya na kuruhusu mchakato wa Katiba mpya uanze …Tume ya Jaji Warioba pia imefanya kazi nzuri, Rasimu ni nzuri, huwezi kupata Katiba yenye kukidhi haja ya kila Mtanzania.
“Binafsi Rasimu hii ni nzuri, imezingatia maoni ya wananchi, katika Afrika ni Tanzania pekee imekwenda mpaka ngazi ya chini kabisa ya kata kuuliza wananchi kuhusu Katiba wanayoitaka, Kikwete anastahili pongezi kwa hili, mchakato wa Katiba ni jambo zuri sana na la kihistoria, kilikuwa kipindi kigumu kwa utawala, lakini umewezesha kwa hatua hii iliyofikiwa, kuandika historia nzuri,” alisema Dk Bana.
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Uhusiano wa Kanisa la Moravian, Jimbo la Misheni Mashariki, Mchungaji Emmaus Mwamakula alisema hatua iliyofikiwa inastahili pongezi kubwa kwa viongozi.
Baadhi ya madereva wa pikipiki, maarufu kama bodaboda wa Mbezi Louis, Kinondoni, Dar es Salaam, walimpongeza Rais Kikwete kwa kusimamia vizuri mchakato na kuwezesha hatua iliyofikia, huku baadhi wakimtaja kwa jina la mitaani kuwa Rais ni ‘Kidume’.
“Jambo muhimu hapa ni Katiba itakayojali wanyonge, kama mpaka sasa tunasikia Rasimu imepatikana, ambayo ni mwongozo wa kile Watanzania tulichotolea maoni, hapo Rais wetu ni ‘Kidume’ kwa kweli, amesimamia vizuri, tunaomba aendelee kusimamia mpaka Katiba kamili ipatikane,” alisema Mustafa Ismail.
Juzi, akihutubia baada ya kukabidhiwa ripoti ya Rasimu hiyo, Kikwete alisema kabla ya mchakato kuanza, kulikuwa na kipindi kigumu cha nyakati za misuguano, hisia, mawazo, maneno mengi makali kutoka pande mbalimbali kuhusu mahitaji ya Katiba na kuona ni busara kuwa na Katiba mpya.
Rais alisema hotuba yake ya kufunga mwaka 2010 ya Desemba 31 na kuukaribisha mwaka 2011, alieleza dhamira hiyo ya kuanza mchakato wa kupata Katiba mpya itakayohusisha Watanzania wengi jambo analomshukuru Mungu na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kwamba limefanikiwa kwa kiwango kikubwa ingawa kazi bado inaendelea.
Alisema ni nia yake hadi Februari 11, Bunge Maalumu la Katiba liwe limeanza ili Watanzania wawakilishwe kwa mara nyingine kuipitia Rasimu na kuipitisha kabla ya kuruhusu hatua ya Kura ya Maoni itakayohusisha nchi nzima.
Juzi, Mwenyekiti wa Tume, Jaji Warioba alimkabidhi Rais Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein Ripoti ya Tume na Rasimu ya Katiba mpya baada ya kukamilisha kazi ya kuiandaa kutokana na maoni ya wananchi.

Wakosoa NGOs

Nao baadhi ya watu waliotoa maoni kuhusu Rasimu, wamehadharisha juu ya kuzipa madaraka makubwa kikatiba asasi za kiraia ya kupendekeza majina ya kuunda Tume Huru ya Uchaguzi na Tume ya Haki za Binadamu.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema ni jambo la kujipongeza kwa Tanzania kupata Rasimu iliyokidhi matakwa ya wananchi kuhusu mfumo serikali tatu kwani suala hilo halipingiki na kueleza kuwa kama maslahi ya Taifa yatawekwa mbele, Rasimu hiyo ni nzuri.
Hata hivyo, alisema upo upungufu kwenye Rasimu hasa kuhusu asasi za kiraia kujitokeza sana kwenye Katiba kupendekeza majina ya Tume Huru ya Uchaguzi na ya Tume ya Haki za Binadamu.
“Asasi nyingi viongozi wao hawachaguliwi kidemokrasia, utawapaje nafasi katika masuala ya utawala wa nchi? Wafadhili wao wako nje na wana maslahi binafsi, nyingine ni za mifukoni, ni heri mwananchi yeyote akapata nafasi ya kupendekeza majina badala ya asasi zaidi,” alisema Dk Bana.
Alisema ripoti inahitaji kuhaririwa kwa kuonesha marekebisho ya Katiba yaweje, kipindi cha mpito kipewe umakini ili kuepuka ghasia.
Serikali tatu Mhadhiri wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Ayub Rioba alisema suala la Rasimu kupendekeza mfumo wa serikali tatu ni la Watanzania na si mtu binafsi ingawa yeye angependa serikali moja ili kuzuia kugawanywa na wenye kutaka kuliangamiza Bara la Afrika kwa rasilimali zake.
Mbunge wa Igunga, Dk Dalaly Kafumu alisema endapo Katiba ya mfumo wa serikali tatu itapitishwa na wananchi, mwaka mpya utaendelea kuwa na changamoto ikiwamo ya kusutwa na dhamira ya kukiuka mawazo ya waasisi wa Muungano na kutumia muda mrefu kuruhusu ianze kufanya kazi.
Akifafanua hoja hiyo, Kafumu alisema serikali tatu zitahitaji kuandaliwa Katiba tatu tofauti, kwa ajili ya kila nchi, jambo litakalogharimu fedha na muda wa miaka isiyopungua mitatu kabla ya Katiba kuu inayoandaliwa sasa kuanza kutumika.
“Kwa kuwa Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amaan Karume waliona mbali na kuanzisha Muungano uliozalisha serikali mbili, kuanzisha tatu ni kurudi nyuma na kutafuta gharama nyingine za michakato ya katiba za kila nchi. Kwa maana hiyo, mwaka mpya utakuwa na changamoto nzito hasa kuhusu suala la Katiba.
“Lakini, kwa sababu Rais amesema watu wasigawanyike kwa suala linalojadilika, mimi nikiwa mwanasiasa nitalazimika kukubali maoni ya wananchi ingawa msimamo wangu na wa wengine wengi ninaowafahamu ni serikali mbili.Tunamsikiliza na kumheshimu Rais kwamba yawekwe mbele maslahi ya Taifa lakini ni yapi hayo? Bado mimi Kafumu sijafahamu,” alisema.

Jukwaa la Katiba

Kutoka Dodoma, habari zinasema Jukwaa la Katiba nchini, limechagua wawakilishi 40 kutoka mitandao ya asasi za kiraia (azaki), ambao majina yao yatapelekwa kwa Rais Kikwete kwa ajili ya uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
Kesho ndio muda wa ukomo wa makundi kupeleka majina Ikulu kwa ajili hiyo. Asasi za kiraia nchini zimepewa nafasi 20 za uwakilishi katika Bunge hilo ambalo linatarajia kuanza Februari.
Kwenye uchaguzi huo wa Jukwaa la Katiba uliomalizika juzi saa 4 usiku, zaidi ya wagombea 100 walijinadi na kupigiwa kura na wawakilishi wa Azaki kutoka mikoa yote 30.
Wapiga kura hao ni wawakilishi wa mitandao ya Azaki wa wilaya 140, mikoa 30 , kisekta 20 ambapo wawakilishi hao walichaguliwa kwa kufuata kanda na uwakilishi wa kisekta.
Msimamizi wa uchaguzi huo, Deus Kibamba, alitaja waliochaguliwa kuwakilisha sekta ya Utawala Bora na Uwajibikaji na kura zao kwenye mabano ni Alban Marcossy (104) na Renatus Mkinga (78).
Katika Sekta ya Haki za Watoto ni Seif Mahumbi na James Marenya ambao walipata kura 47 kila mmoja. Sekta ya Uchumi na Maendeleo ni Martina Kabisan (95) na Gerald Ruhere (64).
Waliochaguliwa kwa upande wa habari ni Mwandishi wa New Habari 2006, Arodia Peter (108) na Mwandishi wa Mwananchi Communications, Burhan Yakoub (75).
Katika sekta ya wazee waliochaguliwa ni Charles Lwabulala (77) na Dk Joseph Saqware (56).
Aidha, sekta ya vijana waliochaguliwa ni Violet Edwin (58) na Jafari Yusuph (45) huku sekta ya Sheria na Haki za Binadamu wakichaguliwa Sarah Malingingwa (71) na Elias Machibya (67).
Pia Sekta ya Virusi vya Ukimwi na Ukimwi ni Alex Margery na Elita Chusi ambao walifungana kwa kura 72 kila mmoja. Sekta ya Jamii ni Happiness Sengi (66) na Dk Peter Bujari (43).
Kwenye sekta ya Mazingira na Maliasili ni Magreth Katanga (56) na Jecha Jecha (46). Jinsia na Wanawake ni Gemma Akilimali (93) na Grace Mkumbwa (61).
Kundi la uwakilishi wa kikanda, Kanda ya Kati ni Maliki Marupu (12) na Maendeleo Makoye (7) wakati Kanda ya Kaskazini ni Petro Ahham mwenye kura tisa na Saumu Swai kura nane.
Katika Kanda ya Magharibi waliochaguliwa ni Babyegeya Bitegeko (6) na Bihaga Simon (5), Kanda ya Kusini ni Michael Malucha (5) na Sharifu Kombo (4).
Kanda ya Pemba waliochaguliwa ni Mussa Kombo Mussa (4) na Fakih Hamad Ally (3) , Nyanda za Juu Kusini waliochaguliwa ni Paul Kita na Raphael Mtitu ambapo wote walipata kura saba kila mmoja.
Kutoka Kanda ya Ziwa waliochaguliwa ni Mariam Mkaka (13) na Nicas Nibengo (9) wakati Kanda ya Unguja ni Hassan Khamis Juma (4) na Hafidhi Hamid Soud (3), Kanda ya Pwani ni Shaib Lipwata (9) na Sofia Mwakagenza (8).
Kibamba alisema majina hayo yanatarajiwa kuwasilishwa kesho kwa Rais kabla ya saa 9 alasiri kwa ajili ya uchaguzi wa wabunge 20 watakaoingia katika Bunge Maalumu la Katiba.
Awali akizungumza juzi jioni, Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi huo, Juma Nyumayo, alisema Kamati ilipokea malalamiko kutoka Kanda ya Unguja kuwa mmoja wa wawakilishi aliyechaguliwa ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa hilo.
Nyumayo alisema aliyekata rufaa wa Kanda ya Kaskazini alidai kuwepo kwa idadi kubwa ya kura kuliko wapiga kura. Alisema wamepokea rufaa tatu kwa maandishi ambapo Kanda ya Unguja kuna rufaa moja na Kaskazini rufaa moja. Rufaa zote zitafanyiwa kazi.
Alisema rufaa ya tatu ilikuwa ni ya Kanda ya Ziwa lakini baadaye aliamua kujitoa. Alisema malalamiko hayo yatafanyiwa kazi na kisha kurejeshwa majibu kwa wajumbe wa mkutano huo wa uchaguzi.
Hata hivyo, Kibamba alisema wajumbe wa Bodi na kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Katiba, hawaruhusiwi kugombea nafasi za uwakilishi.
Bunge Maalumu la Katiba, litaundwa na wabunge wa Jamhuri ya Muungano, ambao ni 357, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar 76 na wajumbe wengine 201 watakaoteuliwa na Rais kutoka mashirika yasiyokuwa ya serikali na taasisi za kidini.
Mashirika yasiyo ya serikali na taasisi za kidini, yanatakiwa kupendekeza majina watu wanne hadi tisa, ambayo yatapelekwa kwa Rais, naye atateua matatu.
Chikawe Alipozungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe alisema makundi husika yanapaswa kuwasilisha majina yenye uoanisho wa dini, jinsi, kabila ili kuondoa uwezekano wa kuwa na wawakilishi wa kabila fulani au dini fulani pekee, hali inayoweza kusababisha kutengeneza uwakilishi usio na sifa ya utaifa.
Chikawe alishauri makundi hayo kuwasilisha majina mengi ili kumpa Rais nafasi ya kutengua upungufu huo kama utajitokeza kwenye mapendekezo ya majina yenu.
“Fanyeni hivyo kwa kumpa majina mengi, mfano kundi linalopaswa kuwa na wawakilishi 20 litume majina 80 ili kama la watu 20 wa kwanza litakuwa na Wasukuma watupu au kabila fulani pekee, aweze kutengua na kubadili baadhi kutoka majina ya ziada yaliyopendekezwa,” alisema Chikawe.
Rais kabla ya uteuzi huo, atakaa na vyombo vyake na kuteua majina ya wajumbe ndani ya mapendekezo ya mashirika na taasisi hizo. Uamuzi wa vipengele vya Katiba mpya ndani ya Bunge hilo, unatarajiwa kufanyika kwa kupigiwa kura.
Kila kipengele kitapita kwa kupata kura ya zaidi ya theluthi mbili ya wajumbe kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Habari hizi zimeandikwa na Shadrack Sagati,Namsembaeli Mduma, Gloria Tesha, Khatib Suleiman, Zanzibar na Sifa Lubasi, Dodoma.


Chanzo: Habarileo

No comments:

Post a Comment