Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe
BODI ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamaizi wa Bandari Tanzania (TPA), imemtaka Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe kusitisha mchakato wa kumpata mtendaji mkuu kutoka nje na badala yake imwache Kaimu Mkurugenzi wa sasa, Madeni Kipande ili azidi kuleta mabadiliko ya kiutendaji katika mamlaka hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Bodi ya PTA, Peter Msambichaka, alisema msimamo wa bodi yake unatokana na ufanisi wa bandari uliopo sasa ambao umetokana na mchango mkubwa wa Kipande.
Msambichaka alisema ushauri huo unalenga kumpa nafasi zaidi mtendaji mkuu wa sasa ili apate fursa ya kuyasimamia mabadiliko makubwa ya uongozi yaliyotokea chini yake na aweze kusimamia malengo ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN), kwa kasi, ufanisi na nguvu aliyoanza nayo mwaka jana.
“Katika kipindi cha mwaka mmoja, TPA imeweza kudhibiti kwa kiasi kikubwa wizi na upotevu wa shehena (zikiwemo kontena) ndani ya bandari, kurejesha imani ya wateja wa nje hasa kutoka DRC, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia na Malawi,” alisema Msambichaka.
Aliyataja mafanikio mengine kuwa ni kuvuka malengo kwa kuhudumia shehena zaidi ya tani milioni 13 mwaka jana ukilinganisha na tani 12,050,682 na tani 10,390,136 mwaka 2011.
Aidha, katika kuhakikisha kwamba utendaji wa menejimenti unakuwa na tija, bodi hiyo imeanzisha mchakato wa utaratibu mpya wa kuwapata wakurugenzi.
Alisema kuanzia sasa ajira za wakurugenzi hao zitakuwa za mkataba wa miaka mitano, tofauti na awali ambako ajira ya wakurugenzi ilikuwa ya kudumu.
Msambichaka alisema mkurugenzi atapata nafasi ya kuendelea baada ya mkataba wake kwisha kama tu utendaji wake utakuwa wa kuridhisha.
Aliongeza kuwa bodi hiyo imefanya uteuzi wa Naibu Mkurugenzi Mkuu (Miundombinu), Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, wakurugenzi wanne (Rasilimali watu), Mkuu wa Ulinzi, Meneja wa Gati la Mafuta na mameneja wawili wa Manunuzi na Ugavi.
Pia alisema bodi imeamua kumuongezea kipindi cha miezi sita Naibu Mkurugenzi Mkuu, Clemence Kiloyavaha ili kupata muda zaidi wa kumtafuta mrithi wa nafasi hiyo mwenye sifa stahiki.
CHANZO: TanzaniaDaima
No comments:
Post a Comment