Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday 29 November 2015

UFISADI WA WABUNGE BALAA



Na Daniel Mbega

YALE madai ya ufisadi wa wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yameanza. Wamegomea mkopo wa Shilingi milini  90 kwa ajili ya kununulia magari ya kifahari aina ya Toyota Land Cruiser, ambayo ni vitendea kazi vyao.
Na wamefanya hivyo wakati Serikali ya Rais Dk. John Magufuli ikijitahidi kubana matumizi yasiyo ya lazima, ikiwemo kufuta posho za vikao na kuondoa safari za nje ili kuleta maendeleo ya taifa.
Rais Magufuli mwenyewe ameamua kutokwenda kwenye Mkutano wa Jumuiya ya Madola nchini Malta, huku akiwafyeka maofisa 50 ambao walipangwa kuwemo kwenye safari hiyo iliyopangwa kugharimu Shs. 700 milioni kwa nauli na posho.
Badala yake ameagiza Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Pater Kallaghe na maofisa wengine ndiyo wawakilishe katika mkutano huo wa 24 unaofanyika kwenye Ukumbi wa Fort St. Angelo mjini Birgu.
Lakini wabunge wanasema fedha hizo ni ndogo hivyo wanataka wapatiwe Shs. 130 milioni ambazo wanasema ndiyo bei halisi ya magari hayo kwa sasa baada ya kuporomoka kwa thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani.
Wabunge wanapaswa kulipa nusu ya mkopo wa magari hayo kutoka kwenye mishahara yao, wakati nusu nyingine hutolewa na serikali, lakini wao wanasema fedha hizo hazitoshi licha ya kwamba kiasi hicho cha Shs. 90 milioni ndicho kilichotolewa kwa wabunge wa Bunge la 10.
Siyo siri, watunga sheria hao wamekubuhu katika suala la ufisadi wakiwa wanalipwa fedha nyingi huku wananchi hohe hahe waliowachagua kuwawakilisha wengi wakiwa hawana uhakika wa milo miwili kwa siku, achilia mbali huduma duni za jamii wanazopata.
Wabunge wanakubali kulipwa posho ya vikao (sitting allowance) za Shs. 200,000 kwa siku wakati tayari wana mishahara na hawastahili kupokea posho hiyo, ambayo kimsingi haikatwi kodi na kubwa kuliko hata mshahara wa mwalimu anayeanza kazi leo.
Kwa kupokea posho hiyo, kila mbunge anakomba Shs. 36.4 milioni kwa mwaka, na kwa wabunge wote 396 watakaokuwemo kwenye Bunge la 11, ina maana serikali italipa Shs. 14.41 bilioni kwa mwaka kutokana na vikao 182 vinavyofanyika kila mwaka, sawa na Shs. 72.1 bilioni  katika kipindi cha miaka mitano.
Kama wabunge wangalikuwa na huruma na Watanzania, basi wangaliikataa posho hii ya vikao, ambapo fedha hizo zingeweza kulipia sehemu ya deni la walimu ambalo linatajwa kuwa Shs. 91 bilioni.
Pengine wangemuunga mkono Mbunge wa Singida Magharibi (CCM), Elibariki Kingu, ambaye amegoma kupokea posho hiyo, na kwa kipindi cha miaka mitano fedha hizo zikiokolewa, zinaweza kufanya kazi nyingi za maendeleo ya jamii ikiwemo kununua madawati 600,600 kwa gharama ya Shs. 120,000 kila moja.

Kiinua mgongo

Pamoja na kutambua hali ya uchumi wa Tanzania ni mbaya huku wastani wa pato la mtu mmoja mmoja (per capita) ni dola 998 kwa mwaka, lakini wabunge hao ambao ndiyo wanaopitisha bajeti za serikali, wameonyesha kutokuwa na huruma kwa Watanzania wenzao kwa kudai posho, mishahara na marupurupu makubwa kuliko kipato cha taifa.

Itakumbukwa kwamba, wakati wa Mkutano wa 20 wa Bunge la Kumi (Bunge la Bajeti), wabunge hao walizua tafrani kubwa wakitaka wapatiwe mafao ya Shs. 238 milioni kila mmoja baada ya Bunge kuvunjwa Julai 2015.
Tume ya Utumishi wa Bunge ilipendekeza kiwango hicho cha mafao kwa wabunge wote 357 waliokuwemo kikatiba katika Bunge la 10, ambapo pamoja na serikali kusita, lakini baadaye ikalipa jumla ya Shs. 85.024 bilioni, mafao ambayo yalilenga kuwanufaisha spika, naibu spika, wabunge, wajumbe wa tume na watumishi wanne wa kila mbunge.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeundwa kwa mujibu wa Ibara ya 62 ya Katiba ambapo mshahara na marupurupu mengine ya wabunge yameelekezwa katika Ibara ya 73 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Kutokana na msingi wa Katiba hiyo, Mafao ya Hitimisho la Kazi kwa spika, naibu spika, wabunge na wajumbe wa tume hulipwa kwa mujibu wa Sheria ya Hitimisho la Kazi ya Viongozi wa Kisiasa Sura Na. 225 ya mwaka 1999 pamoja na Sheria ya Marekebisho mbalimbali Na. 2 ya mwaka 2005.
Mchanganuo wa mafao hayo ambao wabunge walilipwa kwa awamu mbili ni; Kiinua mgongo ambayo ni asilimia 40 ya mshahara (Shs. 89,376,000), Posho ya Hitimisho la Kazi ambayo ni asilimia 85 ya kiinua mgongo (Shs. 75,969,600), Posho ya Usumbufu ambayo ni asilimia 40 ya kiinua mgongo (Shs. 35,750,400), Posho ya Mpito ambayo ni mshahara wa miezi nane (Shs. 11,760,000), na Mafao ya Watumishi wanne wa Mbunge (Shs. 25,187,500).

Stahili za wabunge
Katika taifa linalohangaika kukuza uchumi wake na kuhudumia jamii iliyo maskini zaidi, bado wabunge hawaoni umuhimu wa kubana matumizi, badala yake hata malipo wanayopata wanasema ni madogo mno.
Spika wa Bunge la 10, Anne Semamba Makinda, akizungumza jijini Dar es Salaam siku chache kabla ya Mkutano wa Kwanza wa Bunge la 11, alisema wabunge wa Tanzania wanalipwa kidogo sana kulinganisha na mabunge ya nchi jirani, huku akionyesha wasiwasi kwamba huenda wengi, hasa ambao wameshindwa kurudi bungeni, watapoteza maisha mapema kwa sababu hawana akiba.
“Nawaambia jamani, mimi ndiye najua malipo yao, hawana kitu kabisa, wengi hata hayo mafao yao walikwishayakopa na wameondoka mikono mitupu, malipo ya wabunge ni madogo tofauti na watu wanavyofikiria,” alisema Makinda ambaye ameamua kukaa pembeni.
Hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Makinda kulalamikia udogo wa mishahara ya wabunge, kwani Oktoba 23, 2013 wakati wa mazungumzo na Spika wa Bunge la Uswisi, Maya Graf, alisema mishahara ya wabunge wa Tanzania siyo mikubwa kulinganisha na wanayolipwa wabunge wa mabunge mengine duniani.
Kuweka akiba ya baadaye hakuhusiani na udogo au ukubwa wa mshahara, bali ni nidhamu ya fedha na vipaumbele ambavyo mhusika anapaswa kuviweka.
Wakati ambapo kima cha chini cha mshahara kimefikia Shs. 315,000 badala ya kile cha Shs. 720,000 kilichopendekezwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), wabunge wana stahili nyingi ambazo pamoja na mishahara zinafikia Shs. 11.3 milioni  kwa mwezi.
Katika Bunge la 10, mbunge alikuwa akilipwa Shs. 2,305,000 kwa mwezi, na baada ya kuondoa makato yote (Shs. 588,000), alikuwa anabakiwa na Shs. 1,717,000.
Kiasi hicho ni mbali na posho ya Shs. 330,000 anayolipwa mbunge kwa kuhudhuria kikao kimoja kwa siku. Posho ni Shs. 80,000 za kujikimu akiwa nje ya jimbo lake, posho ya vikao Shs. 200,000 kwa siku na mafuta ya gari Shs. 50,000, jumla kuwa Shs. 330,000 kwa siku.
Kwa kupokea posho ya vikao (sitting allowance) ambayo ni Shs. 200,000 kwa siku, serikali inatumia Shs. 76.2 milioni kwa siku pindi wabunge 396 wa sasa wanapokuwa kwenye kikao, na kwa kipindi cha mwaka mzima ambacho kinakuwa na vikao 182, inalipa Shs. 14.41 bilioni.
Hii maana yake ni kwamba, kwa kipindi cha miaka mitano, serikali inapoteza kiasi cha Shs. 72.1 bilioni kwa posho za vikao pekee (sitting allowance) kwa wabunge ambao bado wanalipwa mshahara.
Mbali ya stahili hizo, lakini mbunge bado analipwa Posho ya Ubunge (Jimbo), Posho ya Vikao vya Bunge na kamati zake, Posho ya madaraka kwa viongozi, Posho ya viburudisho kwa viongozi, Posho ya kujikimu ndani na nje ya nchi, Posho ya mavazi anaposafiri nje ya Tanzania, Posho ya msaidizi wa Ofisi ya Mbunge, na Posho ya usafiri wakati wa vikao vya kamati na mikutano ya Bunge.
Katika kuonyesha ufisadi zaidi, wanalipwa Posho ya mafuta lita 1,000 kwa mwezi na kwa takriban miaka 10 iliyopita, wabunge – kwa mujibu wa utaratibu huo – wamepigiwa hesabu ya Shs. 2,500 kwa lita moja.
Huu ni ufisadi, kwa sababu katika kipindi chote cha miaka 10, licha ya kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola pamoja na mtikisiko wa uchumi duniani, lita moja ya mafuta ya petroli haijwahi kuuzwa kwa Shs. 2,500. Siyo ajabu kesho wakaibuka na kusema waongezewe ifike Shs. 3,000 kwa lita kwa sababu posho hiyo imekaa muda mrefu!

Kujilinganisha na wengine
Wabunge wetu wamekuwa kama watoto wadogo, wanajilinganisha na ‘watoto wa jirani waliokula wali nyama’ bila kulinganisha pia uwezo wa ‘wazazi wao’.
Wanasema wenzao wa Uganda wanalipwa kwa mwezi UShs. 19 milioni (sawa na Shs. 11,759,600 za Tanzania) au wale wa Kenya wanaolipwa KShs. 1,305,000 (sawa na Shs. 26,559,800 za Tanzania).
Itakuwa ni ajabu kwa wabunge kuangalia maslahi binafsi na kuwasahau Watanzania wanaoogelea kwenye lindi la umaskini, huku huduma za jamii zikiwa duni. Ni ufisadi kama ulivyo ufisadi mwingine.
Bunge la 11 linaongozwa na Spika Job Ndugai na Naibu Spika ni Dk. Tulia Ackson Mwansasu.


0656-331974

No comments:

Post a Comment