Magufuli katika ziara wizara ya fedha
Na Daniel Mbega
WAKATI
uchumi wa Tanzania ni mdogo, baraza la mawaziri limeonekana kuwa kubwa na mzigo
kwa taifa, tofauti na mabaraza ya nchi ambazo uchumi wake ni mkubwa, kama
Marekani, China, Uingereza na hata nchi jirani ya Kenya, Uwazi Mizengwe linaandika.
Hali hiyo
inamlazimu Rais Dk. John Magufuli alifyeke baraza hilo lenye jumla ya mawaziri
30 na naibu mawaziri 26 na kuunda wizara 15 tu ili kuakisi hali halisi ya
uchumi wa taifa na wananchi kwa ujumla.
Pato la Ndani la Tanzania (Gross Domestic Product –
GDP) kwa mwaka ni Dola za Marekani 49.18 bilioni (Sawa na Shs. 130.3 trilioni).
Uchunguzi
unaonyesha kwamba, kwa kasi iliyopo, Rais Magufuli anahitaji wizara 15 tu na
kuteua naibu mawaziri watano, ambapo pia yeye mwenyewe anaweza kuongoza wizara
mojawapo kati ya hizo, hususan Wizara ya Fedha, Uchumi na Mipango.
Wizara
nyingine ambazo zinapaswa kuwa chini ya Ofisi ya Rais ni Mambo ya Nje na
Uhusiano wa Afrika Mashariki; Miundombinu, Uchukuzi na Mawasiliano; Utumishi,
Ajira na Maendeleo ya Vijana; Mambo ya Ndani; na Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Wizara ambazo zinapaswa kuwa chini
ya Makamu wa Rais ni Maliasili, Utalii, Mazingira, Maji na Umwagiliaji; Katiba, Sheria
na Masuala ya Muungano; Afya na Ustawi wa Jamii; na Viwanda, Biashara na Masoko.
Ofisi ya
Waziri Mkuu inapaswa kuongoza wizara sita ambazo Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi); Ardhi na Maendeleo ya Makazi; Habari, Utamaduni na Michezo; Kilimo,
Mifugo na Uvuvi; Elimu, Sayansi na Teknolojia; na Nishati na Madini.
Naibu
mawaziri wanaotakiwa kwenye baraza hilo ni katika wizara za Fedha, Uchumi na Mipango;
Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki; Katiba, Sheria na Masuala ya
Muungano; Viwanda, Biashara na Masoko; na Elimu, Sayansi na Teknolojia huku
makatibu wakuu wakipewa majukumu ya kusimamia utekelezaji wa wizara hizo.
Kwa kuteua
baraza hilo, atakuwa amepunguza mawaziri 15 na naibu mawaziri 21 wa sasa, hivyo
kuokoa Shs. 17.3 bilioni ambazo zingelipwa kwa mishahara na posho kwa miaka
mitano.
Katika awamu iliyopita kumekuwepo na wastani wa
wizara 30 huku naibu mawaziri wakiwa 26 kutokana na kubadilika mara kwa mara,
ambao katika kipindi cha miaka 10 iliyopita wameigharimu serikali takriban Shs.
54.8 bilioni kwa mishahara, posho na marupurupu mengine.
Hiyo inatokana na wastani wa Shs. 8 milioni kama
jumla ya malipo ya mshahara, posho na marupurupu mengine kwa ngazi ya waziri
kwa mwezi, lakini hauhusishi fedha zilizotumika kwa safari za mawaziri hao
ndani ya nchi kukagua miradi ama nje ya nchi kwa ziara za mafunzo ambazo
ziliwahusisha hata watendaji wa idara nyingine za serikali.
Aidha, kiasi hicho hakihusishi stahili nyingine kama kiinua mgongo
kinachokokotolewa, pensheni ya kila mwezi, posho ya hitimisho la kazi
(winding-up allowance) pamoja na stahili nyinginezo, na kwa kuwa waziri ni
Mbunge, pia anastahili kulipwa posho nyinginezo kadiri itakavyoamuliwa na
mamlaka husika.
Gharama hizo
hazihusishi pia ununuzi wa mashangingi kwa kila waziri na naibu waziri, ambayo
gharama za mafuta na matengenezo ni kubwa.
Gharama ambazo serikali inawalipa watumishi wake
hasa katika ngazi hiyo ya uwaziri ni kubwa wakati wastani wa pato la Mtanzania
wa kawaida (per capita), kwa mujibu wa Benki ya Dunia, ni Dola 998.1 (Shs. 2.09
milioni) tu kwa mwaka, huku Tanzania ikitajwa kuwa mojawapo ya nchi maskini
zaidi duniani.
Hata hivyo, kipato hicho kinaonekana kiko zaidi
kitakwimu kuliko uhalisia, kwani wananchi walio wengi, hasa wa vijijini,
wanaishi katika hali duni huku wakikabiliwa na ukosefu wa huduma muhimu za
kijamii licha ya nchi hiyo kuwa na rasilimali nyingi.
Nigeria, ambayo inaongoza kiuchumi barani Afrika huku
pato lake la mwaka likiwa Dola 534.7 milioni (Shs.
1,123 trilioni), ina jumla ya mawaziri na naibu mawaziri 35 tu baada ya Rais
Muhammadu Buhari wa nchi hiyo kuwafyeka saba na yeye mwenyewe kuongoza Wizara
ya Petroli.
Marekani,
ambayo pato lake kwa mwaka ni Dola 17.42 trilioni (Shs. 36,582 trilioni) na
idadi ya watu milioni 351.5, inaongozwa na mawaziri 16, wakati China, nchi ya
pili kwa utajiri duniani ikiwa na pato la Dola 10.4 trilioni (Shs. 21,840
trilioni) kwa mwaka na watu bilioni 1.36, baraza lake linaundwa na mawaziri 25
tu.
Baraza la Mawaziri la Marekani linahusisha
Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Fedha, Wizara ya Ulinzi, Wizara ya Sheria,
Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Biashara, Wizara ya Kazi,
Wizara ya Afya na Huduma za Jamii, Wizara ya Nyumba na Maendeleo Mijini, Wizara
ya Usafirishaji, Wizara ya Nishati, Wizara ya Elimu, Wizara ya Masuala ya
Wazee, na Wizara ya Usalama wa Ndani.
India,
ambayo ni ya pili kwa wingi wa watu duniani ikiwa na watu 1.24 Pato lake la
ndani ni Dola 2.07 trilioni, lakini idadi ya mawaziri ni 27 tu.
Nchi
jirani ya Rwanda ambayo pato lake la taifa ni Dola 7.9 bilioni (Shs. 16,590
trilioni) tu kwa mwaka, baraza lake linaundwa na mawaziri 20 chini ya Rais Paul
Kagame na Waziri Mkuu Anastase Murekezi, huku wakuu wa majimbo 16 ambao
wamepewa hadhi ya Waziri wa Nchi, wakiwa na jukumu la kusimamia majimbo hayo
kwa bidii na kuifanya nchi hiyo ndogo kupiga hatua kimaendeleo ambapo kwa sasa
uchumi wake, hadi kufikia robo ya kwanza ya mwaka 2015, umefikia asilimia 7.6.
Uingereza, ambayo ni nchi ya tano kwa
uchumi imara duniani pato lake likiwa Dola 2.95 trilioni (Shs. 6,195 trilioni),
ina mawaziri 19 na maspika wawili – wa Bunge la Makabwela na Bunge la
Mabwanyenye – na Chancellor wa Duchy of Lancaster.
Hata hivyo, wapo wajumbe wengine nane
wanaohudhuria vikao vya baraza la mawaziri, hivyo kufanya wajumbe halisi kuwa 31
tu, akiwemo Waziri Mkuu David Cameroon.
Baraza la mawaziri la Rais Uhuru Kenyatta
wa Kenya kwa sasa lina mawaziri 18 tu huku Makatibu Wakuu 26 wakiwasaidia
mawaziri hao katika idara mbalimbali. Awali kulikuwa na wizara 33.
Kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 2010 ya nchi
hiyo, ambayo pato lake ni Dola 60.72 bilioni (Shs. 127.5 trilioni) kwa mwaka,
baraza la mawaziri linapaswa kuwa na mawaziri 22, ambapo mawaziri hao siyo
wabunge na wanapaswa kuomba kazi kabla ya kuthibitishwa na Bunge lenyewe.
Utaratibu huo umeondoa ukiritimba wa mtu
mmoja kuwa na vyeo viwili – uwaziri na ubunge – hivyo kunusuru mapato ya
serikali na kukuza kipato cha mwananchi mmoja mmoja kutoka Dola 1,012.9 mwaka
2011 hadi Dola 1,358.3 mwaka 2014.
Tanzania haiwezi kujilinganisha na Afrika
Kusini wala Uganda, ambazo mabaraza yao yana utitiri wa mawaziri japokuwa
uchumi unatofautiana.
Afrika Kusini, ambayo pato lake ni Dola
350.1 bilioni (Shs. 735.2 trilioni) kwa mwaka, baraza lake chini ya Rais Jacob
Zuma lina mawaziri 35 na naibu mawaziri 37 huku kipato cha mwananchi mmoja
mmoja kikiwa kimeporomoka kutoka Dola 8,080.9 mwaka 2011 hadi Dola 6,477.9
mwaka 2014.
Baraza la Mawaziri la Uganda Rais Yoweri
Museveni na Waziri Mkuu Ruhakana Rugunda, lina jumla ya mawaziri 33 na mawaziri
wa nchi 38 kufanya jumla ya mawaziri wote kuwa 71, likiwa ndilo baraza kubwa
zaidi katika Afrika Mashariki na Kati.
Hata hivyo, pato la Uganda ni dogo
kulinganisha na Tanzania ambapo kwa sasa ni Dola 26.09 bilioni kwa mwaka, huku
kipato cha mwananchi mmoja mmoja kikiwa Dola 696.4 kwa mwaka.
Ingawa
muundo wa utawala wa Marekani ni wa shirikisho (federal) ukihusisha majimbo
tofauti na Tanzania, lakini ili kuhakikisha serikali ya Rais Magufuli inabana
matumizi, kuhimiza uwajibikaji na kuleta maendeleo, lazima wakuu wa mikoa
wapewe majukumu ya kusimamia maendeleo katika mikoa yao huku wizara zikitoa
usimamizi wa jumla kwa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Wachambuzi
wa masuala ya utawala na maendeleo wanaeleza kwamba, mipango yote ya maendeleo
inaanzia kwenye halmashauri, hivyo madiwani wana jukumu kubwa la kusimamia
miradi ya maendeleo pamoja na fedha za miradi hiyo.
Kwa mujibu
wa utaratibu wa sasa, bajeti kuu ya serikali inaanzia kwenye halmashauri, hivyo
madiwani wana wajibu mkubwa wa kusimamia miradi ya maendeleo na endapo serikali
itashindwa, basi madiwani watakuwa hawakutimiza wajibu wao.
Katika
kipindi hiki cha uwajibikaji, wakuu wa mikoa husika wanatakiwa wasimamie
halmashauri zao kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa wananchi zikiwemo huduma
muhimu na bora za kijamii kama afya, maji, elimu na miundombinu.
0656-331974
CHANZO: UWAZI MIZENGWE
No comments:
Post a Comment