Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Saturday 27 February 2016

YANGA YASONGA MBELE LIGI YA MABINGWA AFRIKA, YAITUNGUA CERCLE DE JOACHIM 2-0


Mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga, leo wamefanikiwa kusonga mbele kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuitandika klabu ya Cercle de Joachim ya Mauritius kwa mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Yanga imefuzu raundi ya kwanza kwa ushindi wa jumla ya mabao 3-0 kufuatia ushindi wake wa bao 1-0 ugenini wiki mbili zilizopita.
Mshambuliaji hatari Mrundi Amisi Tambwe ndiye aliyeanza kuiandikia Yanga bao la kwanza kwa kichwa katika dakika ya tatu ya mchezo akiunganisha krosi ya Simon Msuva.
Dakika ya 56 Thabani Kamusoko aliifungia Yanga bao la pili kwa mkwaju wa faulo baada ya Msuva kumuachia mpira Haji Mwinyi aliyempasia Kamusoko ambaye naye alifumua shuti kutoka umbali wa meta 21 na kujaa kimiani.
Yanga sasa inasubiri mshindi wa mechi ya Mbambane Swallows ya Swaziland na APR ya Rwanda ambayo inapigwa kwenye Uwanja wa Amahoro jijini Kigali. Katika mechi ya kwanza APR ilifungwa 1-0.
Yanga ilianza kupeleka mashambulizi mapema kuanzia dakika ya kwanza baada ya Msuva kuachia shuti lililopanguliwa na kipa wa Cercle de Joachim.
Katika dakika ya pili, Emerson wa Cercle de Joachim aliingia vizuri kwenye eneo la Yanga lakini kipa Ally Mustapha alitoka na kuokoa.
Shambulizi hilo kama liliwachongea Wamauritius hao, kwani dakika iliyofuata walishangaa kuona nyavu zao zikitisika kufuatia bao la Tambwe, ambaye alicheza vizuri.
Malimi Busungu aliingia vizuri kwenye eneo la Cercle de Joachim katika dakika ya 8 huku mabeki wa timu hiyo wakidhani ameotea, lakini akashindwa kulenga lango. Hata hivyo, mashambulizi ya Yanga yaliendelea mfululizo hadi dakika ya 12 ingawa hayakuleta mabadiliko ya matokeo.
Katika dakika ya 18, Cercle de Joachim  walifanya shambulizi jingine la kushitukiza, lakini beki Kelvin Yondani alikuwa mwepesi kuwahi na kuokoa mpira.
Yanga iliongeza mashambulizi na kuumiliki zaidi mpira ambapo Kamusoko alionekana kutamba peke yake akifanya anavyotaka huku Cercle de Joachim akiwa wamejazana nyuma kwenye lango lao katika hali ya kuzuia kasi ya Yanga, ambayo iliathiriwa na mipango mibovu ya umaliziaji.
Yanga ilipata kona katika dakika 26 lakini haikuzaa matunda. Katika daika ya 28 pasi ya Kaseke ilimkuta Juma Abdul aliyepiga shuti kali lakini likatoka pembeni mwa lango. Tambwe naye akapoteza nafasi ya wazi katika dakika ya 31.
Katika dakika ya 37 Cercle de Joachim walipata kona baada ya Bossou kuutoa mpira nje, hata hivyo walipiga kona dhaifu iliyookolewa kilaini.
Kunako dakika ya 45, Yanga walipata kona yao ya pili, lakini kipa wa Cercle de Joachim akaikumbatia.
Hadi mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa bao hilo 1-0.
Yanga walimtoa Busungu katika dakika ya 46 na nafasi yake kuchukuliwa na Paul Nonga, Mbuyu Twite naye alipumzishwa na akaingia Pato Ngonyani.
Mabadiliko hayo yaliendelea uhai wa timu hiyo ambapo katika dakika ya 52 Nonga alipata nafasi akiwa yeye na kipa, lakini akapata kigugumizi cha miguu na kushindwa kuleta lango.
Hatimaye wakasahihisha makosa yao baada ya kupata faulo katika dakika ya 56, ambapo Kamusoko bila ajizi akafumua shuti la nguvu lililozama kimiani.
Bao hilo lilionekana kuwapa nguvu zaidi Yanga wakitafuta ushindi mnono, lakini Cercle de Joachim wakapaki basi na kuondosha hatari badala ya kushambulia.
Mashambulizi yalionekana kuwa ya upande mmoja huku wageni wakishambulia kwa kushtukiza, ambapo Yanga walipoteza nafasi nyingi za wazi, makosa ambayo kocha wa timu hiyo Hans van de Pluijim anapaswa kuyarekebisha mapema kabla ya hatua inayofuata.
Kikosi cha Yanga kilikuwa na:
1. Ally Mustapha 'Barthez'
2. Juma Abdul
3. Haji Mwinyi
4. Kelvin Yondani
5. Vicent Bossou
6. Mbuyu Twite
7. Simon Msuva
8. Thabani Kamusoko
9. Amissi Tambwe
10. Malimi Busungu
11. Deus Kaseke

Sub:
12. Deo Munishi
13. Oscar Joshua
14. Pato Ngonyani
15. Matheo Simon
16. Paul Nonga

No comments:

Post a Comment