Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Saturday 27 February 2016

BURIANI SAJINI KASSIM SAID MAPILI

Mzee Kassim Mapili wakati akiwa amelazwa kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili. Kulia ni Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Addo November. 
Kassim Mapili akipiga gitaa la solo kwenye jukwaa la bendi ya Mjomba Mrisho Mpoto.


Na Daniel Mbega
“KIFO oooh kifoo, kifooo kifoooo, kifo hakina huruma!” Naam. Ndivyo alivyoimba marehemu Ramazan Mtoro Ongalla ‘Dk. Remmy’ wakati akiwa na bendi yake ya Super Matimila ‘Wana Bongo Beats’ akiomboleza kuhusu ‘kifo’, Fikra Pevu inaripoti.
Kweli kifo hakina huruma, kwa sababu kinaweza kumchukua yule umpendaye katika wakati ambao bado unamhitaji.
Katika albamu yao ya Nippon Banzai ya mwaka 1994, Zaiko Langa Langa ‘Nkolo Mboka’ wanasema ‘Liwa yo Moyibi’, yaani ‘Wewe kifo ni mwizi’! Hakika kifo ni mwizi kwa sababu kinatokea bila taarifa, hakipigi hodi, kinashambulia na kuwaacha watu wakiwa na majonzi na mpendwa wao.

Hakika ndivyo ilivyotokea kwa mkongwe wa muziki nchini Tanzania, al-marhum Kassim Said Mapili (79), ambaye amefikwa na mauti Februari 24, 2016 akiwa amelala mwenyewe nyumbani kwake maeneo ya Tabata TIOT jijini Dar es Salaam, tena baada ya kurejea kutoka kuangalia mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baina ya Arsenal na Barcelona.
Kifo hakikumpa nafasi Mzee Mapili hata kuwaaga wapendwa wake. Tasnia ya muziki wa dansi ikiwa imetetereka, hakika ilikuwa inamhitaji mkongwe huyu japo kwa ushauri tu.
Anazikwa leo Ijumaa, Februari 26, 2016 saa 10:00 jioni katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.
Kwa wadau wa muziki, hakuna asiyemfahamu Mzee Mapili, afande aliyevua magwanda ya Polisi akiwa na cheo cha Sajini na kuanza kuzitumikia bendi za muziki wa dansi za uraiani.
Alikuwa hakosekani katika matukio mengi yaliyohusu jamii, na ndiyo maana hata wakati wa mazishi ya mtangazaji na mchambuzi wa masuala ya muziki wa kituo cha Radio Tumaini, Fred Mosha ‘Mkuu’, Jumatatu Februari 21, 2016 pale kwenye makaburi ya Kinondoni, Mzee Mapili alipewa fursa ya kuzungumza machache na akamuimbia akisikitika kuondoka kwake mapema.
Kinachosikitisha zaidi ni kwamba, ilichukua takriban siku mbili kabla ya kubaini kwamba mwanamuziki huyo alikuwa amefariki dunia.
Taarifa za awali zilieleza kwamba, tangu aliporejea chumbani kwake Jumanne usiku baada ya kutazama mechi ya Arsenal na Barcelona kwenye luninga, hakuweza kutoka nje hadi Alhamisi Februari 25, 2016 wakati majirani walipolazimika kutoa taarifa polisi ambao walivunja mlango wa chumba cha Mzee Mapili na kukuta amekwishafariki.
Miezi michache iliyopita Mzee Mapili alilazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na kusumbuliwa na tatizo la moyo, lakini baadaye mwenyewe akasema alikuwa anaendelea vizuri kutokana na kusaidiwa na msanii mkongwe anayeishi Marekani, Salma Moshi, ambaye alimlipia Bima ya Afya na hivyo kusaidia kupata dawa zote zinazohitajika bila ya matatizo.
“Lakini Mola, eee, kazi yake haina makosa, na wala hairekebishwi na binadamu yeyote…” ndivyo alipopata kuimba ‘Bulldozer’ Marijani Rajabu Marijani katika kibao cha ‘Rufaa ya Kifo’. Mungu alitenda kazi yake kwa Mzee Mapili na kuwaachia wapendwa wake simanzi kubwa.
Binafsi namkumbuka Mzee Mapili kwa mengi, nikiwa nimefahamiana naye tangu mwaka 1994 hasa wakati wa maandalizi ya mashindano ya ‘Mkali wa Solo’ nchini Tanzania, nilitambua kwamba mzee huyo alikuwa mcheshi, mchangamfu na mzungumzaji hasa, wakati huo akiwa Mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (Chamudata).
Ni wakati huo aliponieleza kwamba, wimbo alioutunga akiwa na bendi ya Polisi Jazz ‘Wana Vangavanga’ mwaka 1978 ndio uliomtambulisha mwanamuziki aliyekuja kuwa mahiri nchini Tanzania, Shaban Ally Mhoja Kishiwa, ambaye alijulikana zaidi kwa jina la TX Moshi William.
“Nilikuwa kiongozi na mpiga solo, si kwamba sikuweza kuuimba, lakini niliona nikimpa kijana yule kutokana na sauti yake ilivyokuwa, wakati huo akiwa kijana wa miaka 20,” nakumbuka alinieleza hivyo Mzee Mapili wakati wakiwa wanafanya mazoezi kwa ajili ya mashindano ya ‘Mkali wa Solo’ yaliyokuwa yakiratibiwa na Juma Mbizo. Wapiga solo wengine walikuwa Remmy Ongala, Komandoo Hamza Kalala, Michael Bilal, Shaaban Yohana ‘Wanted’ na wengineo.
Mzee Mapili alianza muziki kabla hata Tanganyika haijapata uhuru na alikuwa na mwingi wa vipaji kuanzia kutunga, kuimba na kupiga gitaa.
Alizaliwa katika Kijiji cha Lipuyu kilichopo Tarafa ya Lionya, Wilaya Nachingwea mkoani Lindi mwaka 1937 ambako alipata elimu ya msingi sambamba na ya Qur’an.
Ni wakati akiwa madrasa ndipo alipoibuka kuwa mahiri wa kughani kaswida katika Madrasa yake na ndiko alikoyapata mapenzi ya kuimba.
Jina lake lilianza kutajwa Zaidi kwenye ulimwengu wa muziki mara tu alipojiunga na bendi ya White Jazz iliyokuwa mjini Lindi mwaka 1958 chini ya uongozi wa Hamisi Seif Mayocha. Muda mfupi baadaye sifa zake zikazagaa sehemu mbalimbali hadi mikoa ya jirani. Mwaka 1959 akajiunga na bendi ya Mtwara Jazz wakati huo.
Ushindani wa bendi katika kumuwania mwanamuziki huyo ulikuwa mkubwa, kwani bendi ya Holulu ya mjini Mtwara, nayo ikaona ni bora inyakue ‘kifaa’ hicho. Mapili akashawishika na maslahi aliyoahidiwa, akajiunga nayo mwaka 1962.
Wakati huo tayari Tanganyika ilikuwa imepata uhuru, hivyo chama tawala cha TANU kikaanzisha vikundi vya vijana ili kukitangaza zaidi. Mwaka 1963 Mzee Mapili akachukuliwa na bendi ya Jamhuri Jazz ya mjini Lindi iliyokuwa inamilikiwa na Umoja wa Vijana wa TANU (TANU Youth League -TYL).
Kazi nzuri aliyoifanya kwenye bendi ya Jamhuri ikawashawishi viongozi wa TYL wamechukue akaasisi bendi nyingine ya vijana huko Tunduru mkoani Ruvuma mwaka 1964.
Lakini mwaka 1965 maslahi yakampeleka kwenye bendi ya Luck Star iliyokuwa na maskani yake Kilwa Masoko mkoani Lindi. Hakudumu na bendi hiyo, miezi michache baadaye akanyakuliwa na Kilwa Jazz iliyokuwa ikiongozwa na Ahmed Kipande ambako aliibuka na nyimbo kama ‘Ewe Mola Tunakuomba Ubariki Afrika’, ‘Dunia Kukaa Wawili Wawili’, ‘Dolie Mimi Nakwambia’, ‘Sikutegemea’ na ‘Yatanikabili’.
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) lilianzisha bendi mbili za muziki wa dansi za JKT Mgulani ‘Kimbunga Stereo’ na JKT Mafinga ‘Kimulimuli Jazz’. Kutokana na sifa za Mzee Mapili kuenea sana, JKT wakamchukua kuwa muasisi wa bendi ya JKT Mgulani, jijini Dar es Salaam mwaka huo wa 1965 akiwa na akina Athumani Omari, Msenda Saidi, Vinyama Kiss Rajabu.
Ushindani wa bendi katika Majeshi, ukaanza. Jeshi la Polisi nalo likamhitaji ajiunge nalo. Alikubali kwenda kuasisi bendi yao ya Polisi Jazz ‘Wana Vangavanga’ baada ya kupata ajira rasmi Desemba 15, 1965 na kupewa namba ya kazi B 3710 ambako alikuwa na akina Ali Omari Kayanda, Kassim Mponda, Manzi Matumla, Abdu Ali Mwalugembe, Plimo Gandam, Bosco Mfundiri, Juma Ubao na Kitwana Majaliwa. Polisi Jazz ilikuwa ikipiga muziki wake katika ukumbi wa Polisi Barracks, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya nyimbo alizotunga akiwa na Polisi Jazz ni pamoja na ‘Dunia ni Watu’, ‘Kashinagali Ugupina’, ‘Lijelalwa Ngwamba’, ‘Ashijajani Mweshimajani Mwe’ na ‘Nataka Uoe Mke Uwe Mume wa Nyumbani’.
Wakati akiwa ndani ya Jeshi la Polisi, Mzee Mapili aliteuliwa kufundisha bendi ya Wanawake iliyojulikana kama Woman Jazz Band Desemba 23, 1965. Bendi hiyo ilikuwa inamilikiwa na TYL ambapo alisafiri nayo kwenda Kenya, kwenye sherehe za siku ya Kenyatta (Kenyatta Day). Jomo Kenyatta ndiye alikuwa rais wa kwanza wa Kenya.
Mei 1966 Mzee Mapili alipata pigo baada ya kuondokewa na baba yake mzazi Mzee Said Amri Makolela, aliyeuawa wakati akipambana na Nyati porini.
Kuvunjika kwa bendi ya Woman Jazz  mwaka 1974, ndio ulikuwa mwanzo wa kuanzishwa kwa Vijana Jazz  baada ya kuwakusanya vijana wa wakati huo akina Hemed Maneti (Kilosa Jazz),  Hassan Dalali (Mwenyekiti wa zamani wa Simba), Manitu Mussa, ‘Komandoo’ Hamza Kalala Chakupele,  Abdallah Kwesa, Agrey Ndumbaro na wengineo.
Kassim Mapili alistaafu Jeshi la Polisi Mei 5, 1981 akiwa na cheo cha Sajini na mara baada ya kustaafu akajiunga na bendi ya Tanzania Stars Ushirika Jazz iliyokuwa inamilikiwa na Muungano wa Vyama vya Ushirika Tanzania (CUT).
Baada ya kuingia uraiani ndipo alianza kuongoza vyama mbalimbali vya muziki nchini ambapo baada ya kuhudhuria semina ya Baraza la Muziki Tanzania (Bamuta) mwaka 1982 alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa mpito wa chama kipya kilichoanzishwa yaani Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (Chamudata) kabla ya kuchaguliwa na kuwa mwenyekiti wake wa kwanza mwaka 1984.
Chini ya uongozi wake ndipo walikusanywa wanamuziki 57 kuunda bendi ya Tanzania All Stars mwaka 1986 ambao walitunda nyimbo zilizokuwa na mafanikio ya kisiasa siyo tu Tanzania bali hata Afrika kwa ujumla. Wanamuziki hao walitunga nyimbo kama ‘Hayati Samora Machel’, ‘Azimio la Arusha’ wimbo uliokuja kujulikana nchini Tanzania kama fagio la chuma uliokuwa ukimsifu Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi ukiwaonya wazembe kwamba wangepitiwa na ‘fagio la chuma’.
Kila panapofanyika jambo la manufaa katika muziki hapa nchini, Mzee Mapili amekuwa akishirikishwa kikamilifu. Amekuwa akitoa michango ya mawazo yenye busara katika tasnia ya muziki kwa nyakati tofauti.
Kwa ujumla historia ya mwanamuziki huyo aliyeitwa mbele za haki ni ndefu, akiwa ameshiriki kuanzishwa kwa bendi kadhaa ikiwemo Shikamoo Jazz inayoongozwa na Salum Zahoro.

Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahai pema peponi. AMINA.
CREDIT SOURCE: FIKRA PEVU

No comments:

Post a Comment