Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Saturday 20 February 2016

YANGA KAMA 1996 KWA MKAPA, YAANZA KWA NEEMA UTAWALA WA MAGUFULI KWA KUIMINYA SIMBA 2-0




Na Daniel Mbega

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga, wamerejea kile walichokifanya mwaka 1996 katika utawala mpya wa Serikali baada ya kuwachapa mahasimu wao Simba kwa mabao 2-0 na kurejea kileleni.
Hii ni mechi yao ya kwanza tangu Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli kuingia madarakani na wameupata ushindi kama ule ule wa mwaka 1996.
Rekodi zinaonyesha kwamba, Februari 25, 1996 katika mechi yao ya kwanza katika utawala mpya wa Awamu ya Tatu chini ya Benjamin Mkapa, Yanga iliitandika Simba mabao 2-0 kwenye Ligi Daraja la Kwanza (kabla haijawa Ligi Kuu).

Bao la Donald Ngoma la dakika ya 39 na lile na Amissi Tambwe katika dakika ya 72 yalitosha kuipa Yanga ushindi wa mabao 2-0 kama ule ilioupata siku 112 zilizopita, yaani Septemba 26, 2015.
Simba walicheza wakiwa pungufu baada ya mchezaji wake Abdi Banda kupigwa kadi nyekundu, hatua iliyodhoofisha zaidi nguvu ya Wekundu wa Msimbazi.
Kwa kawaida Yanga imekuwa na bahati ya kuanza vyema mechi dhidi ya watani wao wa jadi katika utawala mpya wa serikali, kwani kumbukumbu zinaonyesha kwamba, mechi yao ya kwanza kabisa kwenye Ligi ya Taifa katika utawala wa Rais Julius Nyerere Juni 7, 1965, Yanga ilishinda kwa bao 1-0, mechi ambayo hata hivyo ilivunjika dakika ya 80 kutokana na kutanda kwa giza kwenye Uwanja wa Ilala (sasa Kumbukumbu ya Karume).
Katika awamu ya pili ya Alhaj Ali Hassan Mwinyi, mechi ya kwanza ya mahasimu hao ilishuhudia sare ya bao 1-1 Machi 15, 1986 na mechi yao ya kwanza ya ligi chini ya Jakaya Kikwete katika awamu ya nne Machi 26, 2006 timu hizo zilitoka suluhu.
Hata hivyo, timu hizo ziko nguvu sawa katika ‘kumaliza na Serikali’ kwani Yanga ilimaliza utawala wa Mwalimu Nyerere kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Simba Agosti 10, 1985 na ikaupata ushindi kama huo katika mechi ya mwisho chini ya utawala wa Kikwete Septemba 26, 2015.
Simba nayo ilimaliza utawala wa Mwinyi kwa ushindi wa mabao 2-1 Oktoba 4, 1995 na ikamaliza utawala wa Mkapa kwa ushindi wa mabao 2-0 Agosti 21, 2005.
Kwa ushindi huo wa leo, Yanga imerejea kileleni kwa kufikisha pointi 46 dhidi ya 45 za Simba, lakini ikiwa na mechi moja mkononi.
Aidha, vijana hao wa Jangwani wamefikisha mabao 44 ya kufungwa na kufungwa mabao 9 tu, wakati Simba wamefunga mabao 35 na kufungwa 13.


No comments:

Post a Comment