Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday 28 February 2016

WALIMU DAR KUPANDA DALADALA BURE!!

Paul Makonda

Walimu wa shule za msingi na sekondari za serikali mkoani Dar es Salaam wataanza kusafiri bure kwenye daladala kuanzia tarehe 7 Machi 2016.
Hayo yamesemwa leo hii na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, alipozungumza na wanahabari kwenye Hoteli ya Ramada jijini Dar es Salaam kueleza jitihada alizozifanya katika kutafuta namna ya kuwasaidia walimu kuondokana na adha ya usafiri ambayo husababisha wengi wao ama kuchelewa vipindi au kukosa kabisa kufika katika maeneo yao ya kazi.

"Tunatafuta mahali pa kuanzia walau kutatua kero za walimu, najua kuna mengi ambayo yanafanywa na serikali kwa sasa katika kuhakikisha maslahi (mishahara) yao yanaboreshwa, malimbikizo ya madeni yao yanalipwa pamoja na kuboresha mazingira ya kazi, hivyo nami kama msaidizi wa Rais katika ngazi ya wilaya, nimeona bora nifanye jambo ambalo linaweza kuwasaidia walimu wetu," alisema Makonda.
Aliongeza kwamba, awali wazo lake lilikuwa kuwaombea walimu wa wilaya yake, lakini katika mkutano wake na wamiliki wa vyombo vya usafiri jijini Dar es Salaam uliofanyika ofisini kwake jana Jumamosi, Februari 27, 2016, wamiliki hao wamesema watatoa huduma hiyo kwa walimu wa mkoa wote wa Dar es Salaam.
Alisema, huduma hiyo ya kuwasafirisha bure itaanzia saa 11.30 hadi 2 asubuhi na saa 9 hadi 12 jioni kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa.
"Tumezingatia muda ule ambao wote wanapaswa wafike kazini na kuondoka, lakini hapo katikati kama mwalimu huyo atakuwa anasafiri, itabidi ajigharamie maana hii ni hisani jamani," alisema.
Mkoa wa Dar es Salaam una walimu zaidi ya 15,000 wa sekondari na shule za msingi, huku Wilaya ya Kinondoni pekee ikiwa na walimu takriban 1,900 wa sekondari na zaidi ya 3,000 wa shule za msingi za umma.
DC Makonda amesema kwamba, walimu hao watatengenezwa vitambulisho maalum ambavyo vitakuwa na saini yake mwenyewe ili kuepuka udanganyifu.
"Nimemuelekeza ofisa elimu wa sekondari na shule za msingi kutoa maelekezo kwa wakuu wa shule zote za serikali zilizopo wilayani kwangu na wilaya nyinginezo za Jiji la Dar es Salaam, kutengeneza vitambulisho vya shule zao vitakavyokuwa na picha ya mwalimu, jila lake kamili, jina la shule anayofundisha, namba ya simu ya mkuu wa shule husika pamoja na saini yangu mimi mwenyewe Paul Makonda ili kuepuka udanganyifu," alisema.
Viongozi wa vyama hivyo vya usafirishaji abiria jijini Dar es Salaam wamesema kwamba wameamua kwa nia moja kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli ambaye serikali yake imefuta ada zote kwenye shule za umma kuanzia chekechea hadi kidato cha nne kwa lengo la kuhamasisha na kuboresha elimu.
Sabri Mabrouk, Mwenyekiti wa Darcoboa, amesema wanatambua mazingira magumu yanayowakabili walimu, hivyo wao na kama wanajamii hawana budi kuunga mkono jitihada za serikali katika kupunguza makali ya walimu.
"Walimu wanafanya kazi katika mazingira magumu, kubwa zaidi ni shida ya usafiri jijini Dar es Salaam, hivyo tumeamua kwa pamoja kutoa huduma hii kwao ili watambue kwamba hasa sisi kama wanajamii tunatambua umuhimu na mchango wao," alisema Mabrouk.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Uwadar, William Masanja, amesema dhana ya kwamba ualimu ni wito haipaswi kutumika kwa sababu adha wanazozipata walimu ni kubwa na jamii inapaswa kutambua kwamba ina wajibu wa kuwasaidia.
"Walimu wanasomea kwa gharama, wana familia hawa ambazo zinahitaji matunzo, lakini maslahi yao ni madogo, sasa hatuwezi kukaa na kuwaangalia, lazima nasi tufanye kitu kuonyesha kwamba tunaguswa na kazi wanayoifanya kwani bila wao hatuwezi kupata viongozi, masuala ya maslahi yao nadhani serikali itayashughulikia kikamilifu," alisema.
Naye Shaaban Mdemu, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Madereva Tanzania (TADWU) alisema wanaunga mkono uamuzi uliofikiwa na wamiliki hao na kubainisha kwamba hakuna dereva wala kondakta atakayewanyanyasa walimu.

Hii ni taarifa kamili ya DC Makonda:


Moja ya mambo ambayo serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi makini wa Mheshimiwa John Pombe Magufuli imefanya kuwa kipaumbele kikubwa kwenye mipango yake ya maendeleo ni suala la uboreshaji wa sekta ya elimu nchini na ndiyo maana serikali imeanza utekelezaji wa mpango huu kwa kufuta ada zote shuleni.
Kimsingi, ni ndoto hii ya Mheshimiwa Rais ambayo nina uhakika kila mmoja wetu anaelewa ukubwa wa faida zake kwenye ujenzi wa Tanzania mpya na yenye wasomi na wataalamu wa kila namna, tena wanaopatikana bila kuzingatia hali ya kipato cha familia anayotokea mwanafunzi, iliyonifanya mimi kama msaidizi wake katika nafasi ya ukuu wa wilaya nijiulize kila wakati juu ya ushiriki wangu wa kuhakikisha inatimia kimamilifu.
Maswali hayo yamenifikisha kwenye wazo la kuboresha sekta hii kwa kuchagua kufanya jambo ambalo wakati serikali ikiendelea kupigania changamoto nyinginezo za kuboresha ajira za walimu, ikiwemo upandishwaji wa madaraja na mishahara, basin a mimi katika nafasi yangu nishiriki kwenye mchakato huu mzima kwa kutoa motisha ya usafiri wa bure kwa walimu wote wanaotufundisha kwenye shule za serikali zilizopo jijini Dar es Salaam.
Kwa ufupi ni kwamba, wazo hili limejengwa juu ya msingi wa sababu kubwa tatu: Moja, kwa kuzingatia changamoto za nauli za mara kwa mara wanazolazimika kuzilipa walimu ili kuyafikia kwa wakati maeneo yao ya kufanyia kazi, na pili, ni kuhakikisha mimi na serikali yangu ya wilaya ya Kinondoni tunakuwa sehemu ya juhudi za Mheshimiwa Rais za kuboresha maslahi na mazingira ya walimu ya kufanyia kazi ili ndoto yake anayoipigania usiku na mchana ya kutaka kuiona sekta ya elimu nchini ikikua kwa kasi yanatimia.
Na tatu, ni kuwafanya walimu wa wilaya ya Kinondoni na Dar es Salaam kwa ujumla kama watumishi wenzangu wa serikali nao wanafaidi sehemu ya matunda ya serikali yao ambayo kwa dhati imedhamiria kubadilisha maisha yao ili na wao waweze kubadilisha maisha ya vijana wetu kupitia taaluma.
Kwa sababu hizo nilizoziainisha hapo juu, ninaomba kuwatangazia walimu wangu bwa shule zote za serikali kuanzia za msingi paka sekondari ya kwamba, sasa watasafiri bure wanapokwenda kutufundishia wadogo zetu na watoto wao.
Hii ni baada ya kufanya vikao na mazungumzo ya kina na wamiliki wa vyombo vya usafiri wa umma kupitia vyama vyao vya Darcoboa na Uwadar na hatimaye mazungumzo hayo kuhitimishwa na mkutano wa vyama vyote hivyo viwili vya wamiliki wa vyombo vya usafiri ambao kwa sauti moja wamekubali kuniunga mkono kwenye utekelezaji wa wazo langu hili.
Kipee na kwa unyenyekevu mkubwa, naomba kuchukua fursa hii kuwashukuru sana wamiliki hawa wa vyombo vya usafiri wa umma pamoja na viongozi wa vyama vya Darcoboa na Uwadar kwani walikuwa na kila sababu ya kukataa hasa ukizingatia kuwao wao ni wafanyabiashara na tena wanazo changamoto nyingi katika sekta yao ya usafirishaji, wengine wakiwa hata wamekopa kwenye mabenki ili wapate uwezo wa kufanya biashara, lakini kwenye jambo hili wote kwa umoja wao wamesema ndio na wako tayari kuanza haraka iwezekanavyo.
Utaratibu kwa walimu juu ya utumiaji wa fursa ambayo tumeipata utakuwa kama ifuatavyo: Moja, nimemuelekeza ofisa elimu wa sekondari na shule za msingi kutoa maelekezo kwa wakuu wa shule zote za serikali zilizopo wilayani kwangu na wilaya nyinginezo za Jiji la Dar es Salaam, kutengeneza vitambulisho vya shule zao vitakavyokuwa na picha ya mwalimu, jila lake kamili, jina la shule anayofundisha, namba ya simu ya mkuu wa shule husika pamoja na saini yangu mimi mwenyewe Paul Makonda ili kuepuka udanganyifu.
Nimewataka zoezi hili walifanye na kulikamilisha ndani ya wiki moja ambapo baada tu ya kukamilika itakuwa ni furaha yangu kuwatangazia walimu wote wa shule za serikali jijini Dar es Salaam kuwa, watakuwa wakipanda daladala bure ila tu kwa siku za Jumatatu mpaka Ijumaa na kwa muda was aa 11:30 mpaka saa 2:00 asubuhi, na kati ya saa 9:00 alasiri hadi saa 12:00 jioni.
Ingawa kila mwalimu atalazimika kuonyesha kitambulisho chake alichotengenezewa kwenye shule yake pamoja na kile cha ajira ya serikali.

Imetolewa na:

Paul Makonda
Mkuu wa Wilaya - Kinondoni


No comments:

Post a Comment