Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Saturday 27 February 2016

YANGA KATIKA MTIHANI WA AFRIKA, APR, GOR MAHIA NA MAFUNZO KAZI NGUMU



Na Daniel Mbega
WAKATI ambapo Yanga ya Tanzania na Vital’O ya Burundi zinacheza nyumbani Jumamosi hii Februari 27, 2016 zikihitaji sare tu kutokana na ushindi katika mechi zao za kwanza za Ligi ya Mabingwa Afrika, klabu za APR ya Rwanda, Gor Mahia ya Kenya na Mafunzo ya Zanzibar ziko katika wakati mgumu.
Gor Mahia ilikubali kipigo cha nyumbani Nairobi cha mabao 2-1 kutoka kwa CNaPS Sports ya Madagascar katika mechi ya kwanza ya raundi ya awali, na sasa inahitaji miujiza ili isonge mbele wakati zitakaporudiana mjini Antananarivo.
Mafunzo yenyewe ina wakati mgumu Zaidi wa kuvuka mbele ya AS Vita Club baada ya kipigo cha mabao 3-0 mjini Unguja na kuwang’oa wakongwe hao wa soka Afrika ni sawa na kupanda mlima Kilimanjaro wakikimbia.

Yanga wao wanacheza nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam dhidi ya Cercle de Joachim wakijivunia ushindi wao wa bao 1-0 mjini Curepipe, lakini kama hawatakuwa makini, wanaweza kuadhiriwa na mabingwa hao wa Mauritius.
Mabingwa hao wa Tanzania Bara watawakosa wachezaji kadhaa mahiri akiwemo mfungaji wa bao hilo pekee Mzimbabwe Donald Ngoma ambaye yuko Harare kwenda kumzika mdogo wake aliyefariki kwa ajali ya gari.
Vital’O watakuwa mjini Bujumbura kuwakaribisha Lioli ya Lesotho wakijivunia ushindi wao wa ugenini wa mabao 2-1 ambapo sare yoyote itawavusha kwenda hatua inayofuata.
Mabingwa wa Rwanda, maafande wa APR walilazwa kwa bao 1-0 na wenyeji Mbambane Swallows nchini Swaziland, kwa hiyo kesho wanahitaji kushinda kwa Zaidi ya bao moja na wasiruhusu bao ili waweze kusonga mbele.
Nao mabingwa wa Uganda, Bunamwaya au Vipers, licha ya kushinda bao 1-0 jijini Kampala, watakuwa na wakati mgumu mbele ya Enyimba ya Nigeria watakaporudiana kesho mjini Aba.
Kama hakutakuwa na namna ya jitihada, kuna uwezekano mkubwa wa Afrika Mashariki kupoteza timu zaidi ya tatu ambazo hazitafuzu kwa raundi ya kwanza ya mashindano hayo.
Wakati ambapo Ferroviario de Maputo ya Msumbiji imefuzu moja kwa moja raundi ya kwanza baada ya wapinzani wao Centre Chiefs ya Botswana kujitoa, mechi nyingine za Ligi ya Mabingwa Afrika wiki hii zinaonyesha kwamba, Warri ya Nigeria itakuwa na kazi ndogo dhidi ya Praia Cruz ya Sao Tome & Princepe kutokana na ushindi wake wa mabao 3-0 ugenini.
Aidha, Wydad Casablanca ya Morocco inatakiwa kulinda ushindi wake wa mabao 2-0 ilioupata nyumbani wiki mbili zilizopita dhidi ya Douanes Niamey ya Niger huku wakongwe Union Douala kutoka Cameroon wakiwa nyumbani kwao mjini Douala watahitaji sare tu kusonga mbele dhidi ya Nimba ya Liberia kwani katika mechi ya kwanza Wacameroon hao walishinda 3-1 mjini Monrovia.
Al Ahly Tripoli ya Libya inajivunia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Once Createurs (Viumbe 11) ya Mali na zitakaporudiana katika uwanja huru Walibya watakuwa wanataka kulinda ushindi wao ili wasonge mbele. Mechi yao ilichezwa jana Ijumaa, Februari 26, 2016.
Klabu kongwe ya Ghana, Ashanti, iko ugenini wikiendi hii kukabiliana na MO Bejaia ya Algeria na licha ya ushindi wao wa bao 1-0 ilioupata wiki mbili zilizopita, bado ina kibarua kigumu dhidi ya Waarabu hao.
Asec Mimoas wako nyumbani Abidjan kuwakabili Cotton Tchad ya Chad wakiwa na ushindi wa bao 1-0 katika mechi yao ya kwanza, lakini hilo haliwapia nafasi ya kutosha kujihakikishia kusonga mbele kwenye mashindano hayo makubwa kabisa ya klabu barani Afrika.
Tanda ya Ivory Coast nayo iko nyumbani na leo hii Ijumaa inarudiana na Club Africain ya Tunisia. Katika mechi ya kwanza, Tanda ilifungwa 2-0 ugenini.
St. Georges ya Ethiopia iliyopata ushindi wa mabao 3-0, sasa itakuwa ugenini kuwakabili St. Michel United ya Shelisheli wakati Zesco ya Zambia Ijumaa Februari 26, 2016 inacheza mjini Juba na wenyeji Al-Ghazal ya Sudan Kusini huku ikitambia ushindi wake wa mabao 2-0.
Volcan Club ya Comoro inakwenda kukamilisha ratiba mjini Johannesburg baada ya kukubali kipigo cha mabao 4-0 nyumbani dhidi ya Kaizer Chiefs wakati Douanes ya Senegal itakuwa na kazi ngumu ugenini mjini Conakry, Guinea dhidi ya Horoya baada ya miamba hiyo kutoka sare tasa wiki mbili zilizopita.
Bobo-Dioulasso watakuwa nyumbani Burkina Faso kukabiliana na Stade Malien ya Mali ambapo licha ya kufungwa 3-1, wanajivunia bao lao la ugenini na hivyo wanahitaji ushindi wa mabao 2-0 tu wasonge mbele.
Kazi ni ngumu kwa Mangasport ya Gabon itakayokuwa ugenini huko Brazzaville kuwakabili Etoile du Congo baada ya kutoka suluhu mechi ya kwanza, lakini kwa klabu ya CRD Libolo ya Angola, kazi yao itakuwa rahisi dhidi ya Micomeseng ya Guinea ya Ikweta mjini Malabo kufuatia ushindi wao wamabao 5-1.
Chicken Inn ya Zimbabwe ilishinda 1-0 dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, lakini inahitaji kukaza msuli kuitoa timu hiyo ngumu ya Afrika Kusini ambayo itakuwa na faida ya kucheza nyumbani, kama ilivyo kwa Olympique Khouribga ya Morocco inayocheza na Gamtel ya Gambia. Olympique ilishinda 2-1 mchezo wa kwanza.
Katika Kombe la Shirikisho, hali ni ngumu kwa Bandari ya Kenya, Atletico Olympic ya Burundi n ahata SC Villa ya Uganda licha ya timu hiyo kushinda bao 1-0 ugenini wiki mbili zilizopita.
Villa itakuwa nyumbani kucheza na al-Khartoum ya Sudan, wakati Bandari iliyokubali kipigo cha mabao 2-0, sasa itahitaji kuifunga mabao mengi St. Eloi Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Atletico Olympic ya Burundi ilipigwa bao 1-0 na Fomboni ya Comoro mjini Moroni, lakini sasa inapocheza nyumbani inahitaji ushindi ili isonge mbele.
Polisi ya Rwanda ndiyo iko kwenye nafasi nzuri ya kuvuka dhidi ya Atlabara ya Sudan Kusini kufuatia ushindi wake wa mabao 3-1. Timu hizo zitacheza mjini Juba.
Kawkab Marrakech ya Morocco itakuwa ugenini kwa USFA ya Burkina Faso, lakini ushindi wake wa mabao 3-0 katika mechi ya kwanza unawaweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele ikiwa hawatafanya mzaha kwenye mechi hiyo ya marudiano.
Mechi nyingine zinaonyesha kwamba Nasarawa ya Nigeria itakumbana na Generation ugenini huko Senegal. Katika mechi ya kwanza Nasarawa ilishinda 2-1.
Africa Sports ya Ivory Coast, ikichagizwa na ushindi wake wa ugenini wa mabao 2-1, itaikaribisha Diables Noirs ya Congo, wakati USFAS Bamako ya Mali itakuwa inagangamala kutafuta ushindi wa nyumbani dhidi ya Sporting Gagnoa ya Ivory Coast baada ya kufungwa 2-0.
USM de Loum ya Cameroon na Deportivo Mongomo ya Guinea ya Ikweta zina kibarua kigumu baada ya kutoka sare tasa katika mechi ya kwanza, wakati Vita Club Mokanda ya Congo Brazzaville inahitaji miujiza ugenini kwa Akwa ya Nigeria baada ya kuruhusu kipigo cha bao 1-0 katika mechi ya kwanza.
Renaissance ya Chad iko ugenini kwa New Star ya Cameroon, lakini inajivunia ushindi wake wa bao 1-0, wakati Ajax Cape Town itakuwa nyumbani kucheza na Sagrada ya Angola huku ikiwa na ushindi wa mabao 2-1 wa ugenini.
Defence ya Ethiopia iliruhusu kufungwa nyumbani mabao 3-1 na Misr Elmaqasah, sasa inahitaji nguvu za ziada kushinda ugenini huku Harare City ikihitaji sare ugenini kwa Adema ya Magadascar kufuatia ushindi wake wa mabao 3-2. Ikizembea tu na jamaa wakapata bao moja, basi itakuwa imetolewa.
Kazi inaonekana kuwa mteremko kwa Bidvest Wits ya Afrika Kusini inayocheza nyumbani dhidi ya Lightstars ya Shelisheli, kwani katika mechi ya kwanza Wasauzi hao walishinda mabao 3-0 ugenini.
 CREDIT SOURCE: FIKRA PEVU

No comments:

Post a Comment