Na Abushehe Nondo na
Immaculate Makilika - MAELEZO
Dar es Salaam
11.8.2016
Serikali imesema
kwamba inaendelea kushirikiana na Serikali ya Uturuki ili kupata taarifa zaidi
kuhusu wamiliki wa shule za Feza kuhusishwa na jaribio la kuipindua serikali ya
Uturuki kama ambavyo imeripotiwa na baadhi
ya vyombo vya habari.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Waziri
wa Mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga
alisema wanaendelea
kuwasiliana na Serikali ya Uturuki kuhusu taarifa hizo ili kupata ukweli.
Balozi Mahiga alisema kuwa
kumekuwepo na taarifa zinazohusisha wamiliki wa shule hizo na baadhi ya
wafanyabiashara ambao walifadhili
na kuongoza jaribio la mapinduzi lililoshindwa Julai 15, mwaka huu nchini humo.
“ Serikali inaendelea
kufanya mawasiliano na Serikali ya Uturuki kupitia ubalozi wake hapa nchini ili
tuweze kupata taarifa kuhusu kuhusishwa kwa wamiliki wa shule za Feza na baadhi
ya wafanyabiashara katika jaribio la kuipindua serikali ya uturuki,” alisema Balozi Mahiga.
Aliongeza kuwa kwa
sasa serikali ya Tanzania haiwezi kufanya uamuzi
wowote kuhusu wamiliki wa shule ya Feza na wafanyabiashara wa uturuki
waliopo hapa nchini.
Kuhusu wanafunzi wa kitanzania wanaosoma nchini humo, Balozi
Mahiga alisema kuwa wamemuagiza afisa ubalozi wa Tanzania aliyepo Roma nchini Italia kufuatilia hatma ya wanafunzi
katika vyuo vilivyopo kwenye miji ya Ankara na Instanbul baada ya kufungwa kwa shule na vyuo
kufuatia jaribio hilo la mapinduzi.
Kwa upande wake, Balozi wa Uturuki
nchini Bw. Yasemin Eralp, hivi karibuni alisema kuwa wanafunzi wa Tanzania
wanaosoma nchini mwake katika
vyuo na shule zilizofungwa watahamishiwa vyuo vingine kuendelea na masomo yao.
Balozi Eralp alisema kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya kufungwa kwa baadhi ya
vyuo na taasisi za kielimu zilizobainika kuwa na uhusiano na kikundi cha
kigaidi cha Fetullah Terrorist Organization(FTO) kinachotajwa kufadhili na
kuongoza jaribio la mapinduzi lililoshindwa hivi karibuni nchini humo.
Hivi karibuni Serikali inatarajia kukutana na balozi wa Uturuki
nchini ili kujua ni vyuo vingapi vilivyofungwa nchini humo ikiwa ni pamoja
na idadi ya wanafunzi wa kitanzania wanaosoma katika vyuo hivyo ili kupatiwa
msaada zaidi.
No comments:
Post a Comment