Rais Dkt. John Pombe Magufuli
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO, Dodoma
Rais Dkt. John Pombe Magufuli ametimiza siku ya 365 Watanzania wameona, kushuhudia utendaji na mwelekeo wake wa kuiongoza Serikali ya Awamu ya Tano kwa mafanikio.
Kauli hiyo imetolewa na leo Bungeni mjini Dodoma na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa kabla ya kuanza kujibu maswali ya papo kwa papo ambayo huulizwa na Wabunge kwa Waziri Mkuu kwa kumwomba Naibu Spika Dkt. Tulia Akson kuridhia kuwakumbusha Watanzania kuhusu muda wa uongozi tangu Rais Dkt. Magufuli aingie madarakani.
“Jukumu letu, ni kumwombea Mhe. Rais aweze kuendelea vizuri na kazi ya kuiongoza nchi yetu na wananchi wote tuungane pamoja kila moja kwa dhehebu lake kuweza kuiombea Serikali hii ili iweze kupata mafanikio makubwa” amesema Waziri Mkuu.
Akijibu swali lililoulizwa na Munde Tambwe Abdallah (Mb) juu ya mifumo ya Serikali ya kupeleka fedha za maendeleo katika halmashauri kwa kuzingatia mifumo, sheria, taratibu na miongozo ambayo husababisha halmashauri kuchelewa kupelekewa fedha mara baada ya bajeti kukamilika, Waziri Mkuu amesema kuwa baada ya Bunge la Bajeti kukamilisha kazi yake, Serikali inawajibika kutekeleza maamuzi ya Bunge kwa kupeleka fedha zilizopangwa kulingana na bajeti hiyo.
Akifafanua suala hilo, Waziri Mkuu amesema kuwa baada ya Bunge kuridhia na kutoa mamlaka ya matumizi ya fedha, Serikali ya Awamu ta Tano ilianza na majukumu muhimu ya kujiridhisha na uwepo wa mifumo sahihi ya makusanyo ya mapato na matumizi yake, kupeleka watumishi watakaosimamia shughuli za usimamizi wa ukusanyaji wa mapato na matumizi yake kwenye halmashauri zote nchini na kuratibu na kutathmini miradi yote iliyokuwa imeanza halafu kutokuendelezwa pamoja na miradi mipya ili kutambua pamoja na thamani zake.
Baada ya kujiridhisha juu ya mambo hayo, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imeanza kupeleka kwenye halmashauri zote nchini ambapo kufikia mwezi Oktoba kwa mujibu wa Hazina, jumla ya zaidi ya shilingi Bilioni 177 za miradi ya maendeleo zimepelekwa kwenye halmashauri.
Kwa kudhihirisha masuala hayo, Waziri Mkuu amesema kuwa hivi karibuni vyombo vya habari ikiwemo magazeti kwa wiki tatu yameanza kutoa matangazo ya zabuni kutoka kwenye halmashauri mbalimbali juu ya miradi iliyokuwepo na ile inayoendelea na miradi mipya imeanza kutengewa fedha na ambayo imeanza kutangaza kwa ajili ya kuetekeleza miradi hiyo.
Aidha, Waziri Mkuu amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kupeleka fedha kwenye halmashauri kwa ajili ya shughuli za maendeleo na kuzisisitiza halmashauri ziendelee kukusanya mapato ya ndani ili kuongezea bajeti fedha za Serikali zinazopelekwa na kuongeza kuwa ukusanyaji wa mapato hayo uwe wa mfumo wa kielekroniki ili kudhibiti mapato yanayopatikana.
Akijibu swali la nyongeza juu halmashauri zote kutumia mashine za kielekroniki, Waziri Mkuu amewaagiza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Watendaji wote wa Halmashauri wakiwemo Wakurugenzi kuhakikisha kila eneo la makusanyo vifaa vya kielekriniki vinatumika na matumizi ya vifaa hivyo yaendelee ili kuboresha ukusanyaji wa mapato nchini.
Zaidi ya hayo Waziri Mkuu ameendelea kusisitiza kuwa matumizi sahihi ya fedha ambazo zinapelekwa kwenye halmashauri ni lazima zitumike kulingana na malengo yaliyokusidiwa katika kutekeleza miradi iliyoandaliwa kwenye halmashauri na kuwasihi Wabunge wakiwa wajumbe wa baraza la madiwani katika halmashauri zao waendelee kusimamia na kufuatilia matumizi ya fedha zinazopelekwa ili zitekeleze miradi hiyo kikamilifu.
Kuhusu swali la Mbunge wa Ukonga Mwita Witara juu ya Mfuko wa Jimbo, Waziri Mkuu Majaliwa amemhakikishia Mbunge huyo kuwa Serikali haijafilisika, na kusisitiza kuwa suala la Mfuko wa Jimbo bado unatambulika na fedha zitapelekwa kwenye majimbo na wabunge wote watajulishwa ni kiasi gani cha fedha kimepelekwa kwenye majimbo yao ili sheria ziendelee kutumika na kutekelezwa na Mbunge akiwa mwenyekiti wa Mfuko huo anatakiwa kuendelee kuratibu fedha hizo.
Waziri Mkuu amesema kuwa fedha za Mfuko wa Jimbo ni miongoni mwa fedha inayotengwa kwenye Bajeti na kukumbusha kuwa tangu Bunge la bajeti limalize kazi yake miezi mitatu, bado kuna miezi saba ya kutekeleza bajeti hiyo ambapo fedha hizo zitapelekwa kwenye miradi iliyokusudiwa kwenye majimbo mbalimbali nchini.
Kwa upande wa Wafanyabishara kunyanyaswa na Maafisa wa Kodi nchini swali lililoulizwa na Ritha Kabati Mbunge wa Iringoa, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali inaheshimu na kuwathamini wafanyabiashara wote nchini, wawekezaji, wadau na walipa kodi wote wa ndani ya nchi kwa kuzingatia kuwa maendeleo katika nchi yataletwa na sekta ya wafanyabiashara na wawekezaji wakiwa ndio walipa kodi wakubwa nchini.
Kuhusu suala la nidhamu ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Mpato Tanzania (TRA), Waziri Mkuu amewaonya wafanyakazi hao kuwa watumie lugha nzuri na busara wanapokwenda kutimiza majukumu yao kwa kutumia sheria na kanuni na taratibu za kufanya kazi yao.
Kwa upande wa wafanyabiashara, Wairi Mkuu amewataka wafanyabishara hao kutoa taarifa juu ya jambo linalowakwaza kwenye vyombo vya usalama ikiwemo kitengo cha nidhamu kilichopo TRA ili kutafuta dawa sahihi juu ya wafanyakazi ambao hawaendani na nidhamu ya watumishi wa umma.
Swali lingine lililoelekezwa kwa Waziri Mkuu liliulizwa na mbunge wa jimbo la Liwale Zuberi Kuchauka ambalo lilihusu uwepo wa Sera ya wafanyakazi kutoka nje ya nchi (TX) kupitia makampuni mbalimbali, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa Sera hiyo bado ipo na Serikali inaisimamia kwa kuzingatia msingi wa kuwapa muda mfupi wataalamu hao wenye ufundi maalumu katika sekta ya kazi ili kujenga wigo mpana kwa Watanzania kupata ajira na kuweza kusimamia maeneo yanayohitaji utaalamu.
“Tumetoa nafasi kwa watumishi wa nchi za nje kuja nchini Tanzania kufanya kazi ambazo hapa ndani sisi tunakosa utaalamu ndio tunafuata msingi huo, tunawapa miaka miwili ya mwanzo, tukiamini Watanzania waambata watakuwa wamejifunza utaalamu ule kwa miaka miwili hadi mitano ambapo baada ya hapo wataalamu wa nje ya nchi wanaweza kuondoka, tunamini Watanzania watakuwa wamepata taaluma hiyo na kusimamia sekta ya kazi” amesisitiza Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amewahakikishia Watanzania kuwa makakati wa Serikali wa kufugua milango ya ajira katika sekta zote ikiwemo utalamu, utaratibu huo utaendelea kusimamiwa wa kupokea utaalamu kutoka nje ambao Tanzania haupo ili kutoa nafasi kwa Wanzania kujifunza.
Kuhusu swali la ruzuku ya pembejeo kwenye sekta ya kilimo kuwafikia wakulima kwa wakati ambalo liliulizwa na Mbunge wa Mbeya vijijini Oran Njeza, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeweka utaratibu wa kusambaza pembejeo nchini kwa kutumia Kampuni ijulikanayo Tanzania Fertilizer Cooperation ili kupeleka mbolea kwa wakulima wakati taasisi nyingine zimepewa kazi kusambaza pembejeo nyingine.
Ili kuhakikisha wananchi wanapata mbolea na pembejeo nyingine kwa wakati, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imetoa fedhakwa ajili ya kununua pembejeo kwa kampuni hizo na zitatumia mawakala waliopo hadi ngazi za vijiji na kuhakikisha pembejeo hizo zinzwafikia walengwa zinazohitajika katika musimu wa kilimo unapoanza.
Maswali ya papo kwa papo ya Wabunge ambayo huelekezwa kwa Waziri Mkuu yapo kwenye utaratibu kulingana na ratiba ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kila siku ya Alhamisi ili kutoa majibu ya maswali hayo yanayoelekezwa kwenye sekta mbalimbali nchini kwa musatakabali wa kuboresha maisha ya Watanzania na taifa kwa ujumla ili kuwa na maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2025 kulingana na Dira ya Maendeleo ya Taifa.
No comments:
Post a Comment