By Abducado Emmanuel
UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, kwa
kushirikiana na benchi la ufundi la timu hiyo hivi sasa upo kwenye mchakato wa
kukiongezea nguvu kikosi hicho.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni nia ya dhati kabisa ya Azam FC kutaka
kufanya vizuri zaidi kwenye mzunguko wa pili wa ligi, Kombe la Shirikisho (Azam
Sports Federation Cup) na michuano ya Kimataifa inayokuja kuanzia mwezi ujao na
mwakani (Kombe la Kagame na lile la Shirikisho Afrika).
Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii mwaka huu, tayari wamemaliza mzunguko wa
kwanza wa ligi wakiwa kwenye nafasi ya tatu kwenye msimamo wakijikusanyia jumla
ya pointi 25, wakizidiwa pointi 10 na kinara Simba aliyejizolea 35.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz juzi Kocha Msaidizi wa Azam FC, Yeray
Romero, alisema kuwa kuelekea mzunguko wa pili wa ligi wanatarajia kuangalia
mapungufu ya kikosi hicho kabla ya kuingiza sura mpya kwenye usajili ya dirisha
dogo kwa ajili ya kuinyanyua timu na kufika kwenye nafasi nzuri zaidi.
“Wakati wachezaji wapya wanaingia pia tunatarajia kuwaangalia wachezaji
ambao tunadhani kwa sasa kikosini hawawezi kuisaidia timu, ambao ndio
watawapisha wachezaji hao, lengo la yote haya ni kuweza kuipeleka mbele zaidi
timu zaidi ya hapa ilipo,” alisema.
Katika hatua nyingine, Romero aliwapongeza wachezaji kwa kazi waliyoweza
kuifanya mpaka sasa huku wao kama benchi la ufundi wakiahidi kufanya kazi nzuri
zaidi kwa asilimia 100 katika kuirekebisha zaidi timu na kuziba mapungufu
yaliyopo.
Matarajio yamefikiwa?
“Kiufupi matarajio hayakuwepo ya kumaliza nafasi ya tatu kwenye mzunguko
wa kwanza, hatukuwa tumepanga kufika nafasi hiyo lakini mazingira tuliyokuwa
nayo yametufanya kumaliza hapo, licha ya yote hii ni nafasi nzuri kwetu na
tunachoangalia kwenye raundi ijayo ni kufika nafasi pili na ya kwanza,”
alisema.
Kauli kwa mashabiki Azam FC
Kocha huyo wa zamani wa timu za CF Reale Juventud Laguna na CD Tenerife
zote za Hispania, aliwashukuru mashabiki wa Azam FC kwa sapoti kubwa
wanayoendelea kutoa kwenye mechi zao licha ya kupitia wakati mgumu kwenye
baadhi ya mechi.
“Kwa kweli nachukua fursa hii kuwapongeza mashabiki wa Azam FC, kwa yote
yaliyotokea wao wamekuwa pamoja nasi, timu inapofanya vibaya wapo na inapofanya
vizuri wapo na ambacho tunaweza kuwaahidi ni mashabiki wetu ni kwamba waendelee
kuwa na imani na timu yao kwa sababu nafasi tuliyofikia hivi sasa si mbaya
sana, lakini ingawaje si kama ndio tuliyokuwa tumepanga kufika.
“Hivyo tunategemea raundi ya pili itakapoanza kwa nguvu ambazo tutaziingiza
kikosini basi wakiwa wanaendelea kutusapoti kama mwanzo naamini ya kuwa
mashabiki watajikuta kwamba hawakukosea kuichagua Azam FC kwa sababu matokeo
yatakuwa ni mazuri kwa timu kuweza kupata ushindi,” alimalizia mtaalamu huyo.
Azam FC kuendelea kujifua
Wakati huo huo, mara baada ya kikosi cha Azam FC kurejea jana jioni
jijini Dar es Salaam kikitokea mkoani Shinyanga kilipocheza na Mwadui, taarifa
ni kuwa wachezaji wa timu hiyo wataendelea na mazoezi kama kawaida jioni ya
leo.
Kwa mujibu wa programu ya benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Zeben
Hernandez, mara baada ya mazoezi ya leo, kikosi hicho kinatarajia kucheza
mchezo wa kirafiki kesho Jumamosi kabla ya kupumzika Jumapili na Jumatatu
kitacheza mchezo mwingine wa kujipima ubavu.
Tathimini ya mzunguko wa kwanza
Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi ya Azam Cola kinachochangamsha
mwili na kuburudisha koo na Benki bora nchini kwa usalama wa fedha zako ya NMB,
imefanikiwa kucheza jumla ya mechi 15 kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi
ikifanikiwa kushinda jumla ya mechi saba, sare nne na kupoteza nne ikiwa
imekunja kibindoni pointi 25.
Takwimu pia zinaonyesha kuwa, Azam FC imeshinda robo tatu ya mechi zake
ilizocheza ugenini, ikiibuka na ushindi mara tano kati ya mechi nane za
ugenini, ikifungwa tatu, kati ya mechi saba ilizokuwa mwenyeji imefanikiwa
kuibuka kidedea mara mbili, sare nne na kuteleza mechi moja.
Hivyo takwimu hizo zinaeleza kuwa Azam FC imefanikiwa kupata alama 15
kwenye viwanja vya ugenini kati ya 24 ilizotakiwa kuvuna, ambapo imepoteza jumla
ya pointi tisa ugenini.
Mabingwa hao wamevuna jumla ya pointi 10 kati ya 21 katika uwanja wa
nyumbani, ikiwa imeacha uwanjani jumla ya pointi 11, nane katika uwanja wake wa
Azam Complex kutokana na sare nne ilizotoa ndani ya dimba hilo na tatu ikiziacha
ndani ya Uwanja wa Uhuru kufuatia kupoteza bao 1-0 dhidi ya Simba ambayo
inaongoza ligi ikiwa na pointi 35 pungufu ya pointi 10 na mabingwa hao.
Rekodi ya ufungaji wa mabao zinaonyesha kuwa mpaka sasa kikosi hicho
kimefunga 21, ukiwa ni wastani wa bao 1.4 kwenye kila mchezo katika mechi 15
ilizocheza huku pia ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 14 (yaani wastani wa
kufungwa bao 1.0 kwenye kila mchezo iliocheza).
Nahodha John Bocco ‘Adebayor’, ndiye ameonekana kinara wa kutupia mabao
msimu huu ndani ya Azam FC mpaka sasa akitupia sita akizidiwa mabao matatu na
Shiza Kichuya wa Simba aliyekuwa kileleni kwa mabao tisa, wengine wanaomzidi ni
Rashid Mandawa (Mtibwa Sugar), Simon Msuva, Amissi Tambwe (Yanga), ambao wote
wamefunga saba kila mmoja.
Bocco pia yupo kileleni kwenye utengenezaji wa mabao akiwa ametoa pasi
za mwisho nne, akifuatiwa kwa ukaribu na Khamis Mcha aliyechangia matatu ambaye
pia ametupia wavuni matatu, huku Shaaban Idd aliyeweka kambani matatu naye
akipika mawili.
Mpaka raundi ya kwanza inamalizika mchezaji wa Azam FC aliyecheza mechi
nyingi kuliko mwingine yoyote ni kipa namba moja, aliyecheza 14 sawa na dakika
1,260 kati ya 1,350, alizotakiwa kucheza hadi ligi inafikia katikati na hii ni
baada ya kupumzishwa mechi moja wakati kikosi hicho kikikabiliana Mbao, mchezo
ulioisha kwa Azam FC kuteleza kwa kufungwa mabao 2-1.
No comments:
Post a Comment