UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC,
unayofuraha kuwaataarifu wapenzi wa soka kuwa jioni ya leo umefanikiwa kuingia
mkataba wa miaka mitatu na kiungo mshambuliaji kutoka Ghana, Enock Atta Agyei.
Agosti mwaka huu, Azam FC tuliingia makubaliano maalumu na
Medeama ya Ghana juu ya kumsajili kinda huyo anayetimiza umri wa miaka 18
mwakani baada ya benchi la ufundi kuridhishwa na uwezo wake na sasa amejiunga
rasmi kwenye viunga vya Azam Complex.
Agyei anasaini mkataba tayari kabisa kuanza kuitumikia Azam FC
katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) mwakani
pamoja na michuano mingine ikiwemo Kombe la Shirikisho Afrika.
Tunaamini ya kuwa ujio wa nyota huyo wa timu ya Taifa ya Vijana
ya Ghana chini ya miaka 17, utazidi kuipa nguvu timu yetu kuelekea kwenye
michuano inayotukabili mbeleni, hivyo tunapenda kumtakia mafanikio mema kwa
kipindi chote atakachokuwa akiipigania jezi ya Azam FC.
Azam FC tunapenda kuwafahamisha mashabiki wetu kuwa tutaendelea
kukifanyia marekebisho kikosi chetu kuelekea usajili wa dirisha dogo, lengo ni
kukipa nguvu kikosi hicho ili kifanye vizuri zaidi katika michuano ya hapa
nchini pamoja na ile ya Kimataifa.
Lengo kubwa la Azam FC ni kuendelea kuwafurahisha mashabiki wetu
kwa kupata matokeo bora uwanjani, na tunaamini ya kuwa, benchi zuri la ufundi
tulilokuwa nalo, wachezaji wazuri walioko kikosini na wengine watakaokuja
kuongeza nguvu, wote kwa pamoja wataweza kutuvusha kuelekea safari ya mafanikio
msimu huu.
Hivyo, tunawaomba mashabiki wetu kuvuta subira na kuendelea
kuisapoti timu kwani tunaamini ya kuwa nyie ndio nguzo muhimu ya 12 uwanjani
katika kuwapa hamasa wachezaji ya kupata matokeo bora pamoja na kuijenga timu
kiujumla.
Wakati huo huo, leo tumewapokea wachezaji saba waliokuja kwenye
majaribio ya kujiunga na Azam FC, ambao ni mabeki wa kati Mbimbe Aaron Nkot
(Cameroon), Kone Nabil Ibrahim (Ivory Coast), kiungo mkabaji Kingue Mpondo
Stephane (Cameroon), na washambuliaji Yaya Awaba Joel (Cameroon), Samuel
Afful, Benard Ofori (wote Ghana) na Konan Oussou kutoka Ivory Coast.
Imetolewa na Uongozi Azam FC
Novemba 11, 2016
No comments:
Post a Comment