Leo ni miaka miwili tangu mwanahabari Daudi Mwangosi alipouawa kinyama na askari polisi katika mkutano wa hadhara kwenye Kijiji cha Nyororo wilayani Mufindi.
Ni tukio la kuhuzunisha kwa sababu lilitendwa katika mazingira ambayo yangeweza kuzuia umwagaji damu, tena mbele ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda.
Tunakumbuka tu kwa majonzi, hatuna cha kusema zaidi kwa sababu kesi iko mahakamani na inasuasua kwa namna ilivyo, tusije tukashangaa tukiambiwa hata mhusika hana hatia.
Hata hivyo, ninainukuu habari hii, ambayo ndiyo iliyotoa taswira halisi na ukweli kuhusu mhusika wa mauaji pamoja na kukiri kwake. Habari hii ilichapwa kwenye gazeti la Kwanza Jamii Iringa, Jumatatu, Septemba 10, 2012 wakati huo mamlaka husika zikiendelea kusema kwamba marehemu Mwangosi aliuawa na wafuasi wa Chadema waliokwenda na bomu wakitokea Mbeya, wengine wakadai eti marehemu alikuwa na bomu kwenye koti lake!
Habari yenyewe hii hapa:
MAUAJI: Wakati inadaiwa kuwa ni
bomu la machozi, sasa yadhihirika…
Ni bomu la kivita lilimuua
Mwangosi
·
Aliyelifyatua
ajutia, ana miaka 23, ni askari wa Iringa
·
Yadai
walitumwa kuwakamata viongozi wa Chadema
Na Daniel
Mbega
WAKATI
ambapo dunia bado imezizima kutokana na kuuawa kwa mwandishi wa habari, Daudi
Mwangosi (40) mkoani Iringa, imeelezwa kwamba bomu la kishindo (kivita) ndilo
limekatiza uhai wake.
Habari za
awali, ambazo zimesambaa dunia nzima zimekuwa zikieleza kilichomuua ni bomu la
machozi, na sasa imegundulika tofauti.
Uchunguzi
wa kina uliofanywa na gazeti la Kwanza Jamii Iringa, umebaini kwamba bomu hilo
la kishindo lilifyatuliwa na mmoja wa askari kutoka Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU)
mkoani Iringa, aliyefahamika kwa jina la Pacificus Cleophase Simon (23) mwenye
namba G2573.
Taarifa za
awali zinasema kwamba, askari huyo anayedaiwa kukiri kuua (kwa bahati mbaya), tayari
ameshakula kiapo cha ungamo mbele ya Mlinzi wa Amani na kwamba anatarajiwa
kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa kusomewa mashtaka yake, ingawa
hatatakiwa kujibu kwa vile kesi za mauaji zinasikilizwa na Mahakama Kuu.
Vyanzo
mbalimbali vya habari vimebainisha kwamba, askari huyo, kabla ya kuondoka
Iringa kwenda Nyololo, Mufindi, alikuwa amepewa mabomu mawili – moja la machozi
na jingine la mlipuko – wakiwa wametumwa kuwakamata viongozi wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
“Tulitumwa
kuwakamata viongozi wa Chadema, lilikuwa ni agizo, kwa sababu walikuwa
wamekaidia amri ya Jeshi la Polisi ya kutoitisha mkutano, tulifanikiwa
kuwakamata viongozi watano wa chama hicho,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani
ya jeshi hilo.
Kabla ya
kuuawa, Mwangosi alikuwa amezingirwa na askari wanane huku mmoja wao, OCS
Mwambapa wa Mafinga, aliyekuwa ameshikiliwa na marehemu kiunoni, akiwataka
wasimpige kwa vile ni mwandishi.
Miongoni
mwa askari hao, wawili (akiwemo mtuhumiwa) walikuwa na bunduki maalum kwa
kufyatulia mabomu, mmoja aliyevaa kiraia alikuwa na bastola wakati wengine
walikuwa na virungu.
Inaelezwa
kwamba, askari huyo amekiri kwamba alifyatua bomu hilo la mlipuko kwa bahati
mbaya baada ya askari mwenzake kuugonga mtutu wake wakati wa purukushani na Mwangosi.
Taarifa za
ndani ya jeshi hilo zinadai kuwa, mtuhumiwa huyo aligundua kwamba alitumia bomu
la mlipuko baada ya kurejea kituoni kwake wakati wakikabidhi silaha.
Gazeti hili lilimtafuta Inspekta Jenerali wa
Polisi, Said Mwema, ili kuzungumzia suala hilo, lakini msaidizi wake ambaye
hakutaka hata kujitambulisha, alisema: “Huwezi kuongea naye kwa sasa, ana kazi
nyingi. Kwani wewe una shida gani?”
Hata hivyo, alipotafutwa Mkurugenzi wa Makosa ya
Jinai, DCI Robert Manumba, hakuwa tayari kuthibitisha wala kukanusha kuhusu
madai hayo.
Kwanza
Jamii:
Haloo afande DCI, shikamoo na habari za kazi.
DCI
Manumba:
Nzuri!
KJ: Mimi ni mwanahabari,
nataka kujua maelezo yako, kwamba askari aliyehusika kumfyatulia bomu mwandishi
Mwangosi ametambuliwa kuwa ni wa Iringa, na kwamba inaelezwa kuwa amekiri kwa
ungamo kufanya mauaji hayo akitumia bomu la mlipuko. Unalizungumziaje hili?
DCI
Manumba:
Jeshi la Polisi halijatoa ripoti yake, tunakamilisha ripoti na itatolewa na
mkuu wa jeshi. Kwanza wewe umezipata wapi taarifa hizo?
KJ: Mimi ni mwandishi wa
habari za uchunguzi naweza pia kutafuta vyanzo mbalimbali.
DCI
Manumba:
Basi mpaka tutakapokamilisha uchunguzi ndipo taarifa zitatolewa.
Awali, baadhi ya askari waliokuwepo siku ya
tukio walisema mtuhumiwa huyo alikuwa amekamatwa pamoja na askari wengine
watano ambao kwa mara ya mwisho walikuwa wamemzingira Mwangosi na kumpiga
virungu, kabla mwenzao hajafyatua bomu hilo.
Hata hivyo, taarifa hizo zinadaiwa kukanushwa na
Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Michael Kamhanda, aliyesema hakuwa na taarifa
za askari yeyote kushikiliwa na kuhojiwa kwa tukio hilo.
Kudhihirika
kwa silaha iliyomuua Mwangosi pamoja na kukiri kwa askari aliyehusika,
kumeondoa uvumi wa kupotosha uliokuwa unaenezwa sehemu mbalimbali kwamba, eti
bomu hilo lilirushwa na wafuasi wa Chadema huku wengine wakizusha kwamba huenda
marehemu alikuwa nalo mfukoni, bila taarifa hizo kueleza lilikotoka.
Mwili wa marehemu Mwangosi ulizikwa Jumanne
iliyopita (Septemba 4, 2012) kijijini kwao Busoka, Kata ya Itete, Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya
huku ndugu, waandishi wa habari, wachungaji na wananchi wengine wakililaumu
Jeshi la Polisi kwa mauaji hayo, na kwa kushindwa kuwachukulia hatua askari
polisi waliosababisha kifo hicho na jina baya la jeshi hilo.
Mashuhuda
Watu mbalimbali walioshuhudia tukio hilo,
hususan waandishi wa habari, walisema kwamba, baadhi walijitahidi kumwarifu RPC
Kamuhanda aliyekuwa anashuhudia, kwamba aliyekuwa akipigwa virungu na polisi ni
mwandishi na kiongozi wa Klabu ya Waandishi wa Habari Iringa (IPC).
Abdallah Said, mwandishi wa gazeti la Majira
jijini Dar es Salaam aliyekuwa eneo la tukio, alisema kwamba alimgongea kioo cha
gari alimokuwamo RPC Kamuhanda na kumwarifu kwamba, anayepigwa na mwanahabari,
lakini kamanda huyo wa mkoa ‘akampuuza’.
“Nilimgongea kioo akiwa ndani ya gari lake,
nikamwambia anayepigwa ni mwandishi wa habari na kiongozi wa wanahabari Iringa,
lakini RPC aliteremsha kioo, akanitazama kwa sekunde kadhaa, halafu akapandisha
kioo na kusogea karibu ya tukio kabla ya mipuko ule kusikika,” alisema Said.
Tume
yapingwa
Pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel
Nchimbi, kuunda tume kuchunguza mauaji hayo, lakini tume hiyo imepingwa
hadharani kwa maelezo kwamba inaweza isitoe ripoti iliyo sahihi, hivyo kutaka
iwepo tume huru zaidi.
Tayari
Chadema, kupitia kwa Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, kimesema, tume
hiyo ni batili kwa kuwa kwa mujibu Katiba, Dk. Nchimbi hana mamlaka ya kuunda
tume ya kuchunguza mauaji, na kwamba mwenye mamlaka hayo ni Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania pekee.
Nayo Klabu
ya Waandishi wa Habari Iringa (IPC) kimesema ni vyema tume hiyo ikamshirikisha
mwakilishi wa Umoja wa Klabu za Wanahabari Tanzania (UTPC) kwa vile marehemu
alikuwa Mwenyekiti wa IPC.
“Ili
kuweka uwiano, pamoja na kuwemo kwa wajumbe kutoka taasisi za habari, ni vyema
awepo mwakilishi wa UTPC,” alisema Frank Leonard, Katibu Mtendaji wa IPC.
Tume hiyo
inaundwa na wanahabari Pili Mtambalike kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT)
na Theophil Makunga kutoka Jukwaa la Wahariri (TEF) ambaye pia ni Mhariri
Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication inayochapisha magazeti ya
Mwananchi na Mwanaspoti.
Wengine ni Kanali Wema W. Wapo ambaye ni
mtaalamu wa milipuko kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Mkuu wa Kitengo
cha Ufuatiliaji na Tathmini, Naibu Kamishna wa Polisi, Issaya Mungulu na
Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mstaafu Pivel Ihema.
Matamko mbalimbali
Taasisi
mbalimbali za ndani na nje ya nchi zimejitokeza kulaani mauaji hayo ya kinyama
ambayo hayakuzingatia haki za binadamu.
Miongoni
mwa taasisi hizo ni Sikika, ambayo imesema: “…Uhai
ni haki ya kikatiba ya kila Mtanzania. Hivyo, ni jukumu la polisi kulinda
maisha na uhai wa wananchi wote bila kujali itikadi au kazi zao. Hakuna sheria
inayohalalisha kujeruhi, kutesa wala kuua mwananchi yeyote kwa sababu tu ati
amekataa kutii amri ya polisi. Sikika inasikitishwa zaidi na utamaduni
unaozoeleka ndani ya jeshi la polisi kwamba matukio ya kujeruhi, kutesa
au vifo ni halali iwapo wanasiasa au wananchi hawakutii amri...”
Jumuiya ya Wanahabari za Maendeleo Zanzibar (Wahamaza),
ilisema: “…Tunasikitika kuona kwamba serikali taratibu
inawarudi raia zake, na sasa inaua waandishi wa habari, siku chache tangu
alipouliwa kijana mbichi eneo la Msamvu, mjini Morogoro, katika mazingira
ambayo pia yenyewe yanatia shaka. Tena ni mwezi mmoja tu tokea serikali,
inayojinasibu kuwa inaheshimu utawala wa sheria na haki za binadamu, ithubutu
kutumia sheria mbaya kufungia gazeti la MwanaHALISI kwa muda usojulikana…”
Jukwaa la Wahariri (TEF), lilisema: “…Ieleweke wazi kwamba matukio haya siyo yanaondoa imani ya waandishi wa
habari kwa jeshi la polisi tu, bali yanaweza kuwa chanzo cha uhasama na ufa mkubwa
ambao utawanyima wananchi nafasi ya kutumikiwa na pande mbili ambazo
zinategemeana…”
Tasisi ya Vyombo vya Habari kwa Nchi za Kusini
mwa Afrika (MISA Tan), ilisema: “…Huu ni mwendelezo wa matumizi ya nguvu kupita
kiasi yanayofanywa na polisi kwa raia wa nchi hii. Ni lini polisi
watasimamia ulinzi wa raia na mali zao badala ya kugeuka kuwa jeshi la mauaji
kila wananchi wanapokusanyika kwa minajili ya kutimiza ndoto zao?”
Naye
Waziri Mkuu (mstaafu), Frederick Sumaye, amewaleza wahariri wa vyombo mbalimbali
vya habari mjini Morogoro mwishoni mwa wiki kwamba serikali, kupitia Jeshi la Polisi, inapaswa kutumia zaidi
busara katika kuzuia maandamano, badala ya silaha na nguvu za ziada za polisi.
Sumaye
amesema, kifo cha Mwangosi, pamoja na kusikitika sana, ameshauri kiwe chachu ya
kujifunza zaidi kwamba nguvu za ziada kuwakabili watu wasiokuwa na silaha,
zinaweza kuleta madhara makubwa badala ya kuponya au kuzuia.
CHANZO: KWANZAJAMII IRINGA, SEPTEMBA 10, 2012
No comments:
Post a Comment