Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Wednesday, 24 September 2014

CHADEMA WAKOMAA NA MAANDAMANO 15 WAKITINGA KIZIMBANI



Wakati wafuasi 15 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika wilaya za Bunda na Dodoma wakifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kukusanyika kwa lengo la kutaka kufanya maandamano yasiyokuwa halali, chama hicho kimeendelea kupinga amri ya Jeshi la Polisi baada ya vijana wake kutangaza kufanya maandamano makubwa jijini Dar es Salaam leo.

Vijana hao wa Chadema kupitia baraza lao (Bavicha), wamewataka wafuasi wa chama hicho na wananchi kwa ujumla kujitokeza kushiriki maandamano hayo leo.

Akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana,

Mwenyekiti wa Bavicha, Patrobas Katambi, alisema maandamano ya leo ni sehemu ya maandalizi ya maandamano makubwa ya kitaifa yanayopangwa kufanywa nchi nzima baadaye.

“Katika mkutano mkuu wa chama, Mheshimiwa Mbowe (Freeman), alisema tutafanya maandamano yasiyokuwa na ukomo nchi nzima na kwamba viongozi wote waanze kuratibu...hali inayotokea hivi sasa ni maandalizi. Tunatoa taarifa polisi, lakini majibu ya polisi ni ya kufanana nchi nzima.” alisema.

Alisema inashangaza polisi wakizuia mikutano na maandamano ya vyama vya upinzani, kikiwamo Chadema, huku wakiruhusu mikutano ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana.

Alisema Kinana na viongozi wengine wa CCM wamekuwa wakifanya ziara na mikutano kwenye mikoa mbalimbali na polisi wanailinda wakati wakizuia ya upinzani.

“Tutaandamana kwa amani, iwe mchana au usiku kupinga ukiukwaji wa sheria. Tunaomba polisi wasikubali kutumika kukipendelea chama kimoja, waje walinde maandamano,” alisema.

Kuhusu uhalali wa Bunge Maalum la Katiba, Katambi alisema ni batili na kwamba, hakuna muujiza unaoweza kutokea ili akidi iweze kutimia, hivyo kinachofanyika ni kupoteza fedha za walipakodi.

Mratibu wa Uhamasishaji Vijana, Edward Simbeye, alisema maandamano hayo yatakuwa makubwa na ni mwanzo wa maandamano mengine yasiyo na kikomo.

Katibu wa Bavicha, Julius Mwita, alisema vijana wamejipanga kushiriki maandamano hayo na kuliomba Jeshi la Polisi kuyalinda kwa kuwa yatakuwa ya amani. Hata hivyo, hawakutangaza yatakapoanzia.

WAFUASI 10 WAFIKISHWA MAHAKAMANI BUNDA
Watu 10,  wakiwemo viongozi wa Chadema  wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, wakituhumiwa kufanya mkusanyiko usiokuwa wa lazima, kwa kile kinachodaiwa kuwa walitaka kufanya maandamano.

Waliofikishwa katika mahakama hiyo, ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema wilaya hiyo, Ismail Mwenula (62).

Wengine ni Mwenyekiti wa Jimbo la Bunda, Samwel Imanani; Diwani wa Kata Balili, iliyoko katika Mamlaka ya Mjimdogo wa Bunda, George Miyawa na Katibu Mwenezi wa Jimbo hilo, Emmanuel Malibwa.Wamo pia Loyce Ernest, Tausi Kazi, John Stephano, Chacha Mwita, Charles Shitobela na Masige Maregesi, ambao ni wafuasi wa Chadema.

Akiwasomea shitaka jana, Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Masuod Mohamed, alisema washitakiwa wote kwa pamoja wanashitakiwa kufanya mkusanyiko usiokuwa wa lazima, chini ya kifungu cha 74 cha kwanza na 75 cha kanuni ya adhabu sura ya 16.

Washitakiwa wote mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Said Hamad Kasonso, walikana mashitaka yao na kupelekwa mahabusu hadi Oktoba 7, mwaka huu, baada ya kukosa dhamana.

Walinyimwa dhamana na mahakama baada ya mwendesha mashitaka huyo kudai kuwa uchunguzi wa kina bado unafanyika na kwamba, iwapo watadhaminiwa wataharibu upelelezi wa kesi, ambayo ni ya uvunjifu wa amani.

Malibwa aliomba kupewa ufafanuzi wa kisheria kwa sababu kesho katika Mahakama ya Mwanzo ya mjini Bunda, atakuwa na shauri linalomhusu akiwa kama mlalamikaji.

Pia Miyawa aliiomba mahakama kumpa dhamana kwa sababu leo atakuwa na mkutano na wananchi wake kwa ajili ya kuhamasisha maendeleo katika kata hiyo.

Maombi yote ya watuhumiwa yalitupiliwa mbali na Hakimu Kasonso na hivyo wakaamriwa kupelekwa mahabusu katika gereza la Nyasura hadi Oktoba 7, mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani hapo.

Dalili za kuwapo maandamano zilianza kuonekana mapema asubuhi katika mji wa Bunda.Kufuatia hali hiyo, kila kona yalishuhudiwa magari ya polisi waliokuwa na sare na waliovalia kiraia wakiwa na silaha mbalimbali wakiimarisha ulinzi.

WAFUASI WATANO WAFIKISHWA MAHAKAMANI DODOMA
Wafuasi watano wa Chadema waliokamatwa mkoani Dodoma kwa tuhuma za kufanya mkusanyiko usio halali, jana walifikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.

Akisoma mashtaka mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya, Verynice Kawiche, Wakili wa Serikali, Chivanenda Luongo, alidai watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Septemba 18, mwaka huu, katika Manispaa ya Dodoma.

Alisema watuhumiwa wanashitakiwa kwa makosa mawili; la kufanya mkusanyiko usiokuwa halali na kukaidi amri halali ya Kamanda wa Polisi Wilaya (OCD) ya kutowataka kuandamana.

Wafuasi hao ni pamoja na Mratibu wa Chadema Kanda ya Magharibi, Christopher Nyawanji; Laurent Manguweshi, ambaye ni Katibu wa Chadema Mkoa wa Katavi; Agnes Stephano, ambaye ni mkazi wa jijini Dar es Salaam; Elisha Daudi, ambaye ni mkazi wa Tabora na Tuli Kiwanga, ambaye ni Katibu wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) Mkoa wa Dodoma.

Wanachama hao wanatetewa na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu.Wote kwa pamoja walikana mashitaka yao na wako nje kwa dhamana hadi Oktoba 22, mwaka huu, kesi itakapotajwa tena.

Akizungumza nje ya mahakama, Lissu alisema watuhumiwa hao walikamatwa wakati wakitokea jijini Dar es Salaam kwenye mkutano mkuu wa chama wakielekea Tabora . Alisema watu hao walikamatwa kwa sababu  walikuwa wanatumia gari la Chadema na walionekana kama wanafanya fujo wakati walikuwa sheli wakijaza mafuta kuelekea kwao.

Hata hivyo, alisema kwa mujibu wa vielelezo alivyo navyo vya majibishano kati ya uongozi wa Chadema Mkoa wa Dodoma na OCD ya kuomba kufanya maandamano kwa mujibu wa sheria, mkuu huyo wa polisi aliwajibu kwa kukataa wasiandamane.

“Barua hiyo, katibu wa Chadema mkoa akamjibu OCD siku hiyo hiyo kwamba, sababu za kukataa Chadema wasiandamane hazikuwa na mashiko, hivyo Jeshi la Polisi likaona majibu hayo ni kukaidi amri halali,” alisema Lissu.

Kuhusu maandamano ya Chadema, Lissu alisema polisi wakiondoka barabarani, maandamano yao yanaendelea kama kawaida, kwani wao wanataka kuandamana na siyo kupigwa.

“Hivi wewe ulishawahi kupigwa?...Kupigwa na polisi siyo jambo zuri, sisi tunataka kuandamana siyo kupigwa na polisi,” alisema Lissu.

POLISI TUNA HAMU NA CHADEMA
Polisi jijini Mwanza wamesema wana hamu kubwa na wafuasi wa Chadema watakaothubutu kuandamana kwa kukiuka agizo la jeshi hilo la kuwataka wasiandamane leo.

Akizungumza na NIPASHE jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola, alisema licha ya kupata barua kutoka chama hicho ya taarifa ya kuandamana, jeshi lake limeyapiga marufuku maandamano hayo kwa kutekeleza agizo kutoka ngazi za juu.

“Tumepewa maagizo ya kutoruhusu maandamano ya Chadema kwa sasa, kwanza Mwanza tuna wageni wengi kutokana na mbio za mwenge, hivyo kuruhusu kutatusababishia shida,” alisema Kamanda Mlowola.

Alisema Jeshi la Polisi jijini Mwanza, halioni sababu za chama hicho kufanya hivyo ndani ya mkoa huo kutokana na sababu walizozieleza zinatakiwa zielekezwe mkoani Dodoma.

Mlowola alisema polisi jijini huo wamejipanga kukabiliana na wafuasi wa chama hicho watakaokaidi agizo la kutoandamana na wana hamu kubwa ya kukabiliana nao.

Alisema kuruhusu maandamano hayo kutasababisha wakazi wa jiji hilo kutofanya shughuli za kuwaingizia kipato wanazozifanya kila siku.
Awali, akizungumza na NIPASHE, kiongozi wa operesheni wa Chadema Kanda ya Magharibi, Tungaraza Njugu, alisema wanatarajiwa kufanya maandamano hayo ili kutimiza wajibu wao kama chama.

“Tumepeleka taarifa kila kituo cha polisi cha wilaya ili kuwafahamisha kuhusu kuwapo kwa maandamano yetu ya kupinga mwenendo wa Bunge la Katiba linaloendelea mjini Dodoma,” alisema Njugu.

Alisema lengo la kuwasilisha barua hizo polisi, ni kuwataka wawalinde ili watimize agizo la mkutano mkuu wa chama hicho lilitolewa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.

“Kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa, hatuhitaji kuomba kibali cha kufanya maandamano, bali ni kutoa taarifa kituo cha polisi na wao kuweza kutulinda…haya ni maandamano ya amani na wala si vita,” alisema.
Alisema iwapo polisi wamejipanga kuzuia kufanyika kwa maandamano hayo, watakuwa wamekiuka sheria kutokana na wao kutakiwa kukutana na uongozi wa chama hicho kuelezea sababu ya kupinga maandamano hayo.
Hata hivyo, Njugu alisema kutofanyika kwa maanadamano hayo, wana hofu ya kuhukumiwa na wananchi, ambao walishaelezwa yatafanyika nchi nzima bila kikomo.

CHADEMA WASHINDWA KUANDAMANA RUVUMA
Chadema mkoani Ruvuma imegonga mwamba  kufanya maandamano yasiyo na kikomo baada ya Jeshi la Polisi mkoani humo kukataa kutoa kibali  kwa madai kuwa serikali imekataza maandamano hayo nchini kote.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Songea, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa huo, Erneus Ngwatula, alisema pamoja na kuwapo ghilba za kisiasa zinazofanywa na CCM kushinikiza Chadema kutofanya maandamano, bado chama hicho kitafanya maandamano yasiyokuwa na kikomo .

Alisema Chadema mkoani humo inatarajia kufanya maandamano, ambayo yatakuwa na ujumbe maalumu, ambao utawafikia wananchi wenyewe.

Ngwatula alisema wananchi wamekuwa wakidanganywa na watu wachache, ambao ni vigogo wa CCM wanaoendekeza ubadhirifu wa fedha za umma.
Alisema tayari wameshapitisha maazimio ya kufanya maandamano ya kupinga matumizi mabaya ya fedha zinazotumika kwenye Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea mjini Dodoma.

Ngwatula alisema maandamano ni haki ya msingi  kwa kila raia na kazi ya polisi ni kuhakikisha yanalindwa ili mradi tu taratibu zifuatwe.

Alisema CCM inaonekana imeshindwa na badala yake inalitumia Jeshi la Polisi kufanya mizengwe ili Chadema ishindwe kufanya maandamano.

Hata hivyo, NIPASHE ilishuhudia askari wengi wakirandaranda katika maeneo mbalimbali ya mji wa Songea wakidhibiti wafuasi wa Chadema kufanya maandamano.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Mihayo Misikhela, alisema jana ofisini kwake kuwa Chadema wanafahamu fika kuwa maandamano yamekatazwa, lakini wanalazimisha kutaka kuyafanya, hivyo akawataka waone umuhimu wa kutii amri.

Alisema maandamano na mikutano ya hadhara havipaswi kufanyika hivi sasa, kwani kuna tangazo la serikali la kuvipiga marufuku na kwamba, kama watashindwa kutii amri hiyo, watatumia nguvu.

Imeandikwa na Ahmed Makongo (Bunda); Augusta Njoji (Dodoma); Gedion Mwakanosya (Songea); Restuta James (Dar) na Daniel Mkate (Mwanza).
 
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

  1. POLISI WETU SIO WELEDI WANAFANYA KAZI KWA MAAGIZO YA CCM NA SIO UTAALAMU

    ReplyDelete