Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Awamu ya Pili wa Tanzania
Hatuwezi kujijengea utaratibu wo wote ambao utazuia kabisa makosa yasifanyike,
hasa makosa makubwa; lakini tunatazamia kuwa yakifanyika wanaohusika
watawajibika. Na katika makosa makubwa ya maadili na utendaji mwenye jukumu la
wazi wazi la kuwadhibiti wahusika ni Rais. Mawaziri wake wanapofanya makosa
makubwa, na badala yake kujiuzulu waanze kufanya hila na kutafuta visingizio
vya kutofanya hivyo, ni wajibu wa Rais kuwafukuza; na tunamtazamia kufanya
hivyo. Ni kazi yake mwenyewe, asiyoweza kusaidiwa na mtu mwingine. Mtu anaweza
kumsaidia Rais kumnong'oneza Waziri wake kujiuzulu; lakini hawezi kumsaidia
kufukuza Waziri wake. Hiyo ni kazi ya Rais peke yake. Asipoifanya kosa ni lake
peke yake.
Rais alikuwa na nafasi kadhaa za kumfukuza au kumshauri Waziri Mkuu
kujiuzulu. Kwanza, ni wakati Waziri Mkuu alipomshauri akubali hoja ya
Utanganyika. Nilisema awali kwamba Waziri Mkuu huyo huyo huwezi kumshauri Rais
wako akubali hoja, ambayo jana tu ulimshauri apinge, na badala ya kujiuzulu
uendelee na kazi yako. Lakini pia Rais huyo huyo huwezi kukubali ushauri fulani
leo, na kesho ukubali kinyume cha ushauri huo, kutoka kwa Waziri Mkuu huyo
huyo, bila kumfukuza au kumtaka ajiuzulu. Hata kama yeye ndiye angekuwa mkuu
wako ungepaswa kujiuzulu, badala ya kukubali ushauri wake. Lakini si mkuu wako,
ni mshauri wako tu. Kosa la kukushauri vibaya ni lake; lakini kosa la kukubali
ushauri wake mbaya badala ya kumfukuza au kumtaka ajiuzulu ni lako. Rais analo
kosa hilo.
Rais alipata nafasi ya pili baada ya Halmashauri Kuu ya Taifa kukataa
pendekezo la Serikali la kuitaka ikubali sera ya Serikali Tatu. Azimio la
Serikali Tatu lilifanya Bunge la Muungano na Serikali ya Muungano viwe na sera
moja na Chama Cha Mapinduzi kiwe na sera nyingine katika suala muhimu kabisa.
Halmashauri Kuu ya Taifa ilipokataa pendekezo la Serikali la kukubali hoja ya
Utanganyika, Rais alipaswa kutumia nafasi hiyo kukipa Chama na serikali uongozi
mpya wenye msimamo. Rais hakufanya hivyo. Alifanya kosa.
Nafasi ya tatu ni wakati kikao mchanganyiko cha Dodoma kilipokubali kuwa
utaratibu wa kutaka kubadili sera ya Chama ulikuwa umekosewa na kikapendekeza
lipelekwe kwa wanachama wa CCM. llikuwa ni dhahiri kwamba shughuli hiyo itataka
uongozi mpya wa Chama na Serikali. Kama nilivyokwisha kusema, viongozi wahusika
walinong'onezwa wajiuzulu, wakagoma; na Rais akashindwa kuwafukuza. Akabaki na
washauri wake wale wale. Hili lilikuwa kosa, tena la kushangaza!
Naamini kuwa wanachama wa CCM watakataa pendekezo la Bunge na Serikali la
kutaka SerikaIi ya Tanganyika. Hiyo itampa Rais nafasi nyingine tena ya
kubadili uongozi wa Chama na Serikali. Asipofanya hivyo atakuwa amepoteza
nafasi yake ya mwisho ya kuiondoa nchi hii katika mwelekeo wa hatari; na Nchi
yetu itaserereka haraka sana katika njia ya giza na wasi wasi; bila matumaini.
Na viongozi hawa wataachwa wamwongoze nani? Katika jambo gani? Na
kutupeleke wapi? Watageuka tena wawe watetezi wa Muungano wenye muundo wa
Serikali Mbili? Mpaka lini? Mpaka hapo watakapopata ndoto nzuri zaidi au
kutuzulia "muafaka" mpya?
Katika haIi ya kawaida, kama Rais kashindwa kubadili uongozi wa Serikali
tungetazamia Bunge au Chama kufanya hivyo. Uingereza kwa mfano Wabunge wa Chama
kinachotawala walipoona kuwa Mrs Margareth Thatcher alikuwa hafai tena
kuendelea kuwaongoza ni wao wenyewe walimwondoa na kuchagua kiongozi mwingine.
Bunge letu ni la chama kimoja; na Katiba ya sasa inawapa Wabunge uwezo
wa kuikataa Serikali kwa kupilisha Azimio la kutokuwa na imani nayo. Bunge
likifanya hivyo Rais atalazimika kuteua Serikali mpya itakayoomba upya kibali
cha Bunge. Lakini wabunge wetu hawatafanya hivyo. Kwa ghiliba za viongozi na
hasira za mkizi wamefanywa waonekane kuwa sasa wao wote, pamoja na viongozi
wetu, wamekuwa ni mbuya na makomredi wa kushuku Muungano. Badala ya kuwasaidia
wananchi wenzao kwa kuishughulikia Serikali yenyewe na ubovu wake, wanataka
kuongeza Serikali ya Tatu! Na baadhi yao wangependa kumwimpichi, au kumshtaki
Rais Bungeni! Hiyo kwao ni rahisi zaidi kuliko kuidhibiti SerikaIi.
NADHANI akilini mwao Muungano na Ramani ya-Zanzibar; na maadamu
"tumechoka na Wazanzibari", basi na waondoke warudi walikotoka,
wakifungasha na Muungano wao na Rais wao! Kwa hiyo, kama majuha au mazuge tunaendelea
kuimba wimbo wa Serikali tatu, na nchi inazidi kuserereka kuelekea gema la
hifaki.
Rais Mwinyi ni mtu mwema na mpole, lakini ni kiongozi dhaifu; au upole
wake na udhaifu wake unatumiwa na watu ambao wala si wema wala wapole
kuhatarisha umoja na amani ya nchi yetu, Kipindi chake cha pili kinakaribia
kwisha, kwa Taifa letu jambo muhimu zaidi kwa sasa ni uongozi wa Chama na
Serikali, na ni nani atakayechukua nafasi ya Rais baada ya Uchaguzi Mkuu
mwakani.
Kwa sababu ya minong'ononong'ono ya watu wasioona mbali kuhusu Rais, na
kubabaishwa anakobabaishwa na washauri wake wakuu, nililazimika kuiambia wazi
wazi Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi kwamba najiona kuwa ninao wajibu
wa kumsaidia Rais amaIize kipindi chake salama. Kipindi Cha mpito, cha kujaribu
kujenga utaratibu wa kikatiba wa kubadili uongozi wa nchi yetu kwa heshima na
amani hakitakamilika mpaka hapo Rais Mwinyi atakapomaliza kipindi chake
kilichobaki kwa usalama, na kumkabidhi madaraka Rais mpya kwa utaratibu ule ule
uliompa madaraka hayo.
Suala hili la kutaka kuvunja Muungano, watu wanaostahili kuwajibika ni
wale waliokuwa na wajibu wa moja kwa moja na ambao kwa makosa yao wamemfikisha
Rais katika hali hii ngumu; na kuitumbukiza nchi yetu katika hali ya hofu na
wasi wasi.
UHALALI
WA SERIKALI
Serikali ya sasa ni halali, kwa maana ya kwamba imeteuliwa na Rais
halali, kwa njia halali. Raia ye yote wa Tanzania hawezi kwenda Mahakamani na
kudai kuwa Serikali hii ni haramu, kwa maana ya kwamba haikuteuliwa kisheria.
Pamoja na kwamba Waziri Mkuu hakuteuliwa kwa kufuata utaratibu unaotakiwa na
Katiba ya sasa, kuteuliwa kwake nje ya utaratibu huo kulihalalishwa na Bunge.
Kwa hiyo, nasema, Serikali hii ni halali. Lakini ni halali kwa maana hiyo tu.
Ni uhalali wa sheria bila uhalali wa uwezo na mwenendo na vitendo.
Kwa maana moja sasa hatuna Serikali, tuna Mawaziri tu. Serikali ni timu;
na timu halisi ina dira na rubani. Mkusanyiko wa Mawaziri bila mwelekeo, bila
mwongozo, bila mshikamano na bila uongozi, kila Waziri na lwake, hauwezi
ukaitwa Serikali. Katika hali kama hiyo, hata hila ubovu mwingine wa nyongeza,
mambo muhimu ya nchi hayawezi kujadiliwa wala kushughulikiwa. Lakini hata kama
Serikali yetu ingekuwa na umoja na mshikamano wa kuiwezesha kushughulikia
masuala mengine muhimu ya Nchi yetu, kwa kukubali hoja ya kuwa na Serikali ya
Tanganyika, ingekuwa imejiondolea uwezo na uhalali wa kushughulikia na masuala
ya Muungano wenye Katiba ya sasa ya muundo wa Serikali mbili.
REJEA: NYERERE, J.K.; UONGOZI WETU NA HATMA YA TANZANIA (1994)
REJEA: NYERERE, J.K.; UONGOZI WETU NA HATMA YA TANZANIA (1994)
No comments:
Post a Comment