Na Daniel Mbega
Alhamisi
ya Septemba 18, 2014 wananchi wa Uskochi (Scotland) wamepiga kura ya ‘HAPANA’
kupinga nchi hiyo kujitoa katika Himaya ya Kifalme ya Uingereza (United
Kingdom) na kutaka kuwa taifa huru linalojitegemea.
Hadi kufikia
hatua hiyo, kulikuwepo na mivutano mingi ya kisiasa iliyochochewa na wanasiasa
ambao walitaka Scotland liwe taifa huru kwa mara ya kwanza
baada ya kudumu kwenye Himaya ya Kifalme ya Uingereza kwa zaidi ya miaka 300.
baada ya kudumu kwenye Himaya ya Kifalme ya Uingereza kwa zaidi ya miaka 300.
Katika kura
hiyo ya maoni (referendum) wananchi waliosema HAPANA walikuwa 1,914,187 sawa na
asilimia 55, wakati waliosema NDIYO walikuwa 1,539,920 sawa na asilimia 45.
Waziri
Kiongozi wa Scotland, Alex Salmond kiongozi wa chama cha Scottish National
Party, ambaye alikuwa kinara wa kudai mabadiliko hayo ya kujitenga, hatimaye
alisema ameridhia kuanguka katika mchakato wa kura ya maoni, huku akikiri
kwamba tukio hilo tayari limebadilisha mfumo wa maisha eneo la Scotland.
Idadi kubwa
ya wapiga kura walikuwa wamesajiliwa na kwa mara ya kwanza vijana wenye umri wa
miaka 16 na 17 waliruhusiwa kupiga kura.
Kimsingi,
tukio la kura ya maoni huko Scotland linaleta taswira inayoendana na hali
halisi ya mambo yanayoendelea nchini Tanzania, hasa katika mchakato wa Katiba
Mpya, japokuwa muundo wa muungano wa Uingereza ni tofauti na ule wa Tanzania.
Bunge la
Katiba linaendelea huko Dodoma kuhitimisha majadiliano ya kuichambua Rasimu ya
Pili ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji
mstaafu Joseph Sinde Warioba.
Ingawa hakuna
dalili za kupatikana kwa Katiba mpya mpaka sasa baada ya mvutano wa wajumbe
huku wengine wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakisusia vikao
tangu Aprili mwaka huu, lakini imedhihirika wazi kwamba kipengele cha muundo wa
Muungano ndicho hasa kilichozua nongwa.
Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, ambayo iliongozwa na wasomi, wanasheria na wajuzi wa
masuala ya katiba, ilipendekeza – baada ya kukusanya maoni ya wananchi – kwamba
muundo huo uwe wa Shirikisho la Serikali Tatu – Tanganyika nayo ikizaliwa upya
baada ya kuzikwa tangu Aprili 26, 1964.
Kundi la
wajumbe walio wengi, ambalo zaidi limejaza wajumbe wa Chama cha Mapinduzi (CCM)
lilipinga vikali muundo huo kwa visingizio vingi ambavyo sina haja ya kuvirudia,
lakini ukweli ni kwamba wananusuru migongo yao katika kuulinda Muungano kwa
gharama yoyote. Ndiyo maana haikushangaza kwa jinsi walivyokuwa wakitumia lugha
za maudhi, kebehi na dharau dhidi ya wale wote waliokuwa wanaunga mkono
serikali tatu.
Tume ya Jaji
Warioba siyo ya kwanza kuzungumzia Serikali ya Shirikisho, kwani hata Tume ya
Jaji mstaafu Franncis Nyalali nayo ilipendekeza hivyo mwaka 1992 lakini Mwalimu
Julius Nyerere akasimama kidete kupinga jitihada zozote zilizolenga kuanzishwa
kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano.
Hofu iliyopo
katika muundo wa shirikisho ni kwamba, kwa nadharia utakuwepo, lakini kivitendo
utakuwa umekufa na hiyo Zanzibar itakuwa imejitenga na kuwa taifa huru, ndoto
ambazo wamekuwa nazo Wazanzibari kwa miaka mingi sasa.
Ikiongezwa
na uchu wa madaraka wa wanasiasa ambao sasa wataona kuna fursa nyingi za
uongozi, ni dhahiri muundo huo ulikuwa unawasukuma wengi kufanya kila wawezalo –
kwa mitazamo yao – kuhakikisha ama zinakuwepo serikali tatu na vyeo viongezeke
au zibakie serikali mbili na CCM iendelee kutawala.
Kwa nini? Kwa
sababu Tanzania ilizaliwa kwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar – kuanzishwa kwa
Tanganyika tena kunaashiria kifo cha CCM ambayo nayo ilizaliwa kwa muungano wa
TANU na ASP. Zanzibar ikijitenga maana yake hakutakuwa na haja ya CCM na
yawezekana wakataka ama ASP irudi au waanzishe vyama ingine vya siasa.
Upande wa
Tanganyika nako kutakuwa hakuna haja ya CCM kwa sababu mantiki yake
haitakuwepo. Ama wengine wataifufua TANU kama alivyokuwa amefanya marehemu
Joseph Nyerere mwaka 1993 au kitaanzishwa chama kingine tofauti.
Naam. Hata
wakati huu ambapo imethibitika rasmi kwamba katiba mpya haitapatikana mpaka
baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, hiyo rasimu yenyewe tu imebakia mifupa
mitupu baada ya wajumbe walio wengi kuondoa hata vipengele vyenye maslahi kwa
umma.
Lililo dhahiri
hapa ni kwamba, ikiwa Scotland, taifa kubwa lenye nguvu kuzidi Tanzania,
imeshindwa kujitenga na Uingereza, sembuse Tanzania!
Hapana shaka
kwamba suala la kujitenga kwa Zanzibar ama Tanganyika haliwezi kutokea kwa sasa
wala kesho. Siwaamulii wajumbe wa Bunge la Katiba, lakini ikumbukwe kwamba
baada ya rasimu hiyo kutoka Bungeni, hata kama serikali ya shirikisho itapita,
bado inaweza kupingwa kwenye kura ya maoni ya wananchi kama Waskochi
walivyofanya!
Ni mtazamo
wangu tu.
0656-331974
No comments:
Post a Comment