Na Joyce Joliga,Mwananchi
Songea. Mbunge wa zamani wa Mbinga Mashariki kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Erneus Ngwatula aliyehamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), juzi alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Ruvuma baada ya kumshinda, Joseph Fuime aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, msimamizi wa uchaguzi huo ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Uchaguzi Kanda ya Kusini wa Chadema, Mays Mkwembe alisema Fuime alikubaliana na matokeo.
Ngwatula aliibuka mshindi katika uchaguzi huo uliokuwa na mchuano mkali kwa tofauti ya kura moja. Alipata kura 28 wakati Fuime alipata kura 27 na kura moja iliharibika. Wanachama 56 walipiga kura.
Akizungumzia ushindi huo, Ngwatula alisema kusudio lake kubwa ni kuhakikisha Mkoa wa Ruvuma unakuwa na mizani ya usawa kisiasa ili wananchi waweze kusukuma gurudumu la maendeleo kwa pamoja.
“Tuna mpango kabambe wa kuwajengea uwezo wanachama wetu pamoja na wananchi ili wajue umuhimu wa mfumo wa siasa za vyama vingi na waelewe nini maana yake, kwa lengo la kuondoa dhana potofu kuwa siasa ni uongo,”alisema Ngwatula
Alisema changamoto kubwa iliyopo tangu chama hicho kianzishwe mkoani hapa ni ofisi... “Hakuna ofisi wala samani.”
Akizungumzia matokeo hayo, Fuime alisema ameridhika na kwamba amemkabidhi kijiti Ngwatula.
Aliahidi kumpa mwenyekiti mpya ushirikiano na ushauri pale atakapohitaji.
Aidha, Fuime alikanusha uvumi kuwa ana mpango wa kuhamia chama kingine cha siasa.
Katika uchaguzi huo, Mkwembe alisema nafasi ya Katibu wa Mkoa ilichukuliwa na Christopher Mapunda ambaye kwa kipindi cha nyuma alikuwa ni Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Peramiho.
Aliwataja wengine na nafasi zao kuwa ni Christian Ruta ambaye amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Mkoa. Kabla ya wadhifa huo, alikuwa ni Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Songea.
Mariam Mtamike amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (Bawacha). Awali, alikuwa Mwenyekiti wa Bawacha, Wilaya ya Songea.
Alisema nafasi ya Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) ilichukuliwa na Stuaty Kaking.
Wagombea wote walioshinda nafasi hizo hawajapata pingamizi na wamehaidi kutoa ushirikiano kwa wanachama.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment