Mmiliki wa blogu ya www.maendeleovijijini,blogspot.com,
Bw. Daniel Mbega, akipokea kadi ya uanachama wa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi
wa Umma – PSPF kutoka kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe.
Nape Nnauye baada ya kujiunga na mfuko huo leo hii jijini Dar es Salaam. Mhe. Nape
alikuwa mgeni rasmi wakati wa ufungaji wa semina na mkutano mkuu maalum wa
wamailiki wa blogu Tanzania – TBN, ambapo PSPF walikuwa miongoni mwa wadhamini.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko
wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma – PSPF, Bw. Adam Mayingu, akizungumza wakati
wa ufungaji wa semina na mkutano mkuu maalum wa wamiliki wa blogu Tanzania –
TBN leo hii. Katikati ni mgeni na kulia ni Mwenyekiti wa TBN, Bw. Joachim Mushi.
Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye - kulia – akipokea fomu ya kujiunga na Mfuko
wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma – PSPF, kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa mfuko
huo Bw. Adam Mayingu. Tukio hilo lilifanyika wakati wa ufungaji wa semina na
mkutano mkuu maalum wa wamiliki wa blogu Tanzania – TBN leo hii ambapo PSPF
walikuwa miongoni mwa wadhamini.
Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye - kulia – akitia saini ya dole gumba kwenye fomu
ya kujiunga na Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma – PSPF. Kushoto ni
Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo Bw. Adam Mayingu na aliyesimama ni Ofisa Uhusiano
Mwandamizi wa PSPF, Bw. Abdul Njaidi.
Mgeni rasmi Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye - kulia – akiwa katika picha ya pamoja na
wanachama wa TBN baada ya kufunga semina na mkutano mkuu maalum wa wamiliki wa
blogu Tanzania – TBN leo hii. PICHA ZOTE NA RAHEL PALLANGYO.
Na Daniel Mbega
WAZIRI wa
Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye, amekiri kwamba, mitandao ya
kijamii hususan blogu, ndiyo imekirudisha madarakani Chama cha Mapinduzi – CCM.
Akizungumza
wakati wa ufungaji wa semina na mkutano mkuu wa Chama cha Mabloggers Tanzania –
yaani Tanzania Bloggers Network – TBN , Nape amesema kwamba, katika kipindi
ambacho CCM ilikuwa inaonekana kuchukiwa na baadhi ya wananchi na kutishiwa
uwezekano wa kurudi madarakani, ni bloggers ndio walikuwa muhimili mkubwa wa
kurejesha imani kwa wananchi hata wakaichagua tena.
‘Wakati
nikiwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, na wakati ambao ulikuwa mgumu zaidi
kwa serikali ya CCM, ambapo ilikuwa ikishambuliwa na upinzani, ni bloggers
ambao walisimama imara na kuandika ukweli kuhusu serikali ya CCM kiasi cha
kurudisha imani ya wananchi na hatimaye tukampata Rais john Magufuli,’ alisema
Nape.
Waziri
Nape amebainisha kwamba, mitandao ya kijamii ni zaidi ya vyombo vya habari
vingine kwa kuwa ndiyo inayoanza kuchapisha taarifa kabla hata ya vyombo
vingine vya kawaida kuziripoti, hivyo akasema serikali inaitambua na kuiunga
mkono.
Aidha,
alisema kwamba, kwa kuwa hivi sasa Watanzania takriban milioni 21 wanatumia
mtandao wa internet, ni muhimu kutambua na kuipa kipaumbele mitandao mitandao
ya kijamii kama blogu, ambayo kwa kiasi kikubwa imeunganishwa na mitandao
mingine kama facebook na twitter.
‘Facebook
ina watumiaji karibu milioni tatu, twitter ina watumiaji zaidi ya milioni moja
na nusu pamoja na mitandao mingine, lakini hii yote imeunganishwa kwenye blogu,
hivyo kuna kila sababu ya kuthamini mchango wa mitandao ya kijamii na endapo
itatumiwa vyema, inaweza kuleta manufaa kwa umma kwa kusukuma mbele gurudumu la
maendeleo,’ alisema.
Aliwahakikishia
bloggers kwamba, serikali inawatambua, inawathamani na inaunga mkono juhudi zao
katika upashanaji habari na kwamba serikali iko tayari kuwasaidia kuhakikisha
wanafanya kazi zao kwa uhuru na kwa weledi.
Aliongeza kusema
kwamba, wanamitandao hao wako huru kuikosoa serikali katika kujenga na kwamba
taarifa nyingi wanazoziandika zinafanyiwa kazi na serikali japokuwa siyo rahisi
kuona moja kwa moja.
Katika kuthibitisha
kuwaunga kwake mkono, Waziri Nape ameuagiza uongozi wa TBN kuanzisha Tuzo za
Blog Bora kuanzia mwakani na kwamba zinaweza kuwekwa katika makundi mbalimbali,
hatua ambayo siyo tu itawahamasisha wanamitandao wenyewe, bali pia itawafanya wajikite
katika maeneo mbalimbali na kufanya kazi kwa makini zaidi badala ya sasa ambapo
walio wengi hawajajipambanua kwamba wako upande gani.
‘Ninawaagiza
muanzishe mara moja tuzo hizi kama wenzetu Wakenya, mkijipambanua maeneo yenu
mtafanya kazi kwa ufanisi na itasaidia kuleta maendeleo ya taifa,’ alisema na
kuongeza kwamba, wizara yake itasaidia kwa namna moja ama nyingine kuhimiza
hata baadhi ya taasisi za serikali ziweze kudhamini tuzo hizo.
Wanachama wa
TBN walikuwa katika semina na mkutano wao maalum wa mwaka ambao ulifanyika
jijini Dar es Salaam tangu Jumatatu Desemba 5 hadi Jumanne Desemba 6, 2016.
Wakati huo
huo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paulo Makonda, amesema anautambua mchango
mkubwa wa bloggers wa Tanzania na kwamba wanamsaidia katika kutekeleza majukumu
yake ya serikali.
‘Bloggers
wanajitahidi kuripoti habari nyingi na kwa wakati, zipo habari ambazo katika
vyombo vingine vya habari zinaweza zisiripotiwe, lakini bloggers wanaziandika
kwa mapana na kwa wakati, hivyo kwangu mimi vyombo hivi vya mitandao ni muhimu
na niko tayari kusaidia wakati wowote mtakaponihitaji,’ Makonda alimweleza
Mwenyekiti wa TBN, Joachim Mushi, kwa njia ya simu wakati mkutano huo
ukiendelea.
No comments:
Post a Comment