NA GODFREY MUSHI
Mgombea udiwani wa Kata ya Bomang’ombe wilayani Hai kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Livingstone Nkya maarufu kama Ferefere, amefariki dunia ghafla muda mfupi baada ya kuzindua kampeni zake za kuwania nafasi hiyo.
Ferefere alifariki jana jioni baada ya kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ya mjini Moshi, kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Katibu wa CCM Wilaya ya Hai, Allan Kingazi, alilithibitishia Nipashe kwa njia ya simu jana kuwa, mgombea huyo aliaga dunia baada ya kuzindua kampeni za uchaguzi kwenye kata hiyo.
Alisema Ferefere alianza kuhisi afya yake inabadilika na kumfanya kushindwa kuendelea na jukumu la kujieleza, hivyo aliamua kuondoka baada ya mkutano huo na kwenda kutibiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi, kabla ya kuhamishiwa KCMC.
Kata ya Bomang’ombe ni miongoni mwa kata mpya tatu zilizogawanywa katika Jimbo la Hai, lililokuwa likiwakilishwa bungeni na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.
“Ni kweli mgombea wetu amefariki jana usiku katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC majira ya jioni; na hivi sasa tuko kwenye taratibu za kuandaa mazishi yake. Tunasubiri majibu ya daktari kujua amefariki dunia kutokana na tatizo gani, lakini sisi kama CCM tutasimamisha mgombea mwingine ili kutwaa kata hiyo,”alisema Kingazi.
Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Hai, Said Mderu alipotafutwa na NIPASHE ili kutoa ufafanuzi iwapo uchaguzi huo utaahirishwa au laa, alisema,” Mimi sina taarifa za kifo hicho na kwa sasa nipo njiani, siwezi kuzungumza lolote. Nitafute kesho (leo) nitakuwa na majibu.
Ferefere ambaye pia ni mfanyabiashara maarufu wa maduka ya vileo na vinywaji baridi mjini hapa, alikuwa akigombea kiti hicho, akishindana na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joe Nkya ambaye naye ni mfanyabiashara wa maduka ya pembejeo za kilimo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment