Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Saturday, 26 September 2015

HIFADHI YA MANYARA YAKABILIWA NA SIMBA WAJANE, YATIMA

 
Mwandishi wa makala haya akiwa kwenye geti la kuingilia ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Manyara. 
Simba majike wakiwa na watoto wao ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Manyara. 
Simba akiwa amejipumzisha juu ya mti.


Na Daniel Mbega, Manyara

HAWAFI kwa Ukimwi wala malaria, lakini Simba madume wametoweka katika Hifadhi ya Taifa ya Manyara. Matokeo yake wameacha wajane na yatima.
Hadi kufikia mwaka 2013, hifadhi nzima inadaiwa ilikuwa na Simba dume mmoja tu, wawili wengine walikimbia baada ya ‘kuzidiwa’ na utoaji wa huduma kwa Simba majike.
Naam. Hayo ndiyo matokeo ya ujangili, janga la kitaifa ambalo kwa hakika linatishia uwepo wa rasilimali za asili kwa faida ya wachache wanaotaka kuchuma mahali wasipopanda.
Hali hiyo imesababisha hata kivutio kile maarufu cha kuwaona Simba wanaokwea miti kutoweka, kwani walio wengi wanaogopa kukwea miti kwa hofu ya kupopolewa na majangili.
“Nimekuja hapa kutaka kuwaona hao Simba wanaokwea miti, lakini sijamuona hata mmoja,” anasema kwa masikitiko Sarah Evans, mtalii kutoka Uingereza.
Kwa miaka mingi, watalii kutoka ng’ambo wamekuwa wakivutiwa na tabia ya Simba wa Manyara kukwea miti, ambapo hufanya hivyo kutokana na eneo hilo kuwa na siafu wengi ambao wanawapa shida na hivyo kutafuta mahali salama juu ya miti kujihifadhi.
Manyara, ambayo ni hifadhi pekee barani Afrika kuwa na Simba wanaopanda miti, ipo ndani ya Bonde la Ufa ambalo kingo zake upande wa kaskazini na magharibi zinaongeza mandhari zaidi, achilia mbali Ziwa Manyara upande wa kusini.
Wanyama wanaopatikana ndani ya hifadhi hiyo ni pamoja na simba, nyati, tembo, nyani, chui, pundamilia na wanyama wengine wanaokula majani, huku ikisifika kwa wingi wa ndege hasa heroe na mnandi ambao huonekana katika makundi makubwa na kufanya eneo hili la utalii kuwa na aina 400 za ndege wanaovutia.
Chemchemi za maji moto ni maajabu mengine ndani ya hifadhi hiyo. Maji hayo yanayobubujika kutoka ardhini huonekana yakitoa moshi kama vile maji yanayochemka jikoni. Chemchem hizi za maji moto ya asili zimekuwa zikibubujika bila kukauka kwa kipindi cha mamilioni ya miaka.
Mji mdogo wa Mto wa Mbu, ambao upo jirani na lango la kuingilia hifadhini upande wa mashariki, ni kituo kikubwa cha biashara kinachotoa huduma kwa wageni wanaotembelea hifadhi hiyo iliyoanzishwa rasmi mwaka 1960 na yenye ukubwa wa kilometa za mraba 330 (kilometa za mraba 220 ni za eneo la Ziwa Manyara – lenye urefu wa kilometa 40 na upana wa kilometa 13 – na kilometa za mraba 110 ni  nchi  kavu), ikiwa umbali wa kilometa 126 kutoka Arusha mjini. Kipindi kizuri cha kutembelea hifadhi hiyo ni kuanzia mwezi Juni hadi Desemba baada ya mvua za masika.
Jina  la hifadhi ya Taifa  ya ziwa Manyara  limetokana na neno lililotoholewa  kutoka  katika lugha ya kabila la Wamaasai (Emanyara) lenye  kumaanisha  mmea wa asili  ujulikanao  Kiswahili kama ‘Mnyaa’ au kwa kisayansi na Kibotania Eurphorbia tirucalii na  kwa Kiingereza unafahamika kama Milk bush au Finger  Eurphorbia.
Hifadhi hiyo ina hadhi ya kimataifa na inatambuliwa na Shirika  la umoja  wa mataifa  linaloshughulikia  Elimu, Sayansi na utamaduni (Unesco).
Lakini hatari ya ujangili inayosababisha vivutio vingi vya asili – hasa wanyama – kutoweka, inaweza kuifanya hifadhi hiyo kuwa msitu usio na wanyama.
Meneja wa Program ya Ujirani Mwema wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Ahmed Mbugi, anasema ujangili limekuwa janga kubwa, siyo kwa Tembo tu, bali hata Simba.
Anasema, katika kipindi cha miaka mitatu tu (2008 hadi 2010), jumla ya Simba waliouawa kijangili kwenye Hifadhi ya Manyara ni 62, huku madume wakiwa ndio wengi.
“Mwaka 2008 waliuawa Simba 15, mwaka 2009 Simba waliouawa walikuwa 30 na mwaka 2010 jumla ya Simba 17 waliuawa kwenye hifadhi hiyo. Majangili wanawinda zaidi madume, matokeo yake hifadhi nzima ikabaki na Simba madume watatu tu, lakini kwa sasa wawili wamekimbia hifadhini kwa sababu ya kuzidiwa na utoaji wa huduma kwa majike, amebaki dume mmoja,” anasema Mbugi.
Hali hiyo, anasema, “…Imesababisha kuwepo kwa wajane na yatima wengi kwa wanyama hao, hali inayotishia kutokuwepo kwa ongezeko lao kwa miaka ijayo kwani dume mmoja naye anaweza kuchoka na hata kufa. Pengine hata wadogo waliopo sasa, watakapokua hawataweza kuzaliana kwa vile wanyama hao hawawezi kujamiiana kutoka familia moja.”
Lakini mauaji hayo hayakuwapata Simba tu, kwani katika kipindi hicho pia watu 58 waliuawa na wanyama hao wakali, “…wengi wakiwa katika harakati ya kuwawinda Simba kwenye makazi yao,” anaongeza Mbugi.
Hali inaonekana kuwa mbaya katika Hifadhi ya Manyara kuhusu uwepo wa Tembo ambapo katika kipindi cha mwaka 2007 hadi 2009, jumla Tembo 104 waliuawa kijangili.
“Binadamu waliojeruhiwa na Tembo katika kipindi hicho walikuwa  63,” anasema Mbugi na kuongeza kwamba wengi kati ya watu hao ni wale wanaofanya shughuli zao katika ushoroba wa Tembo.
Mbugi anasema hali hiyo imeifanya Tanapa kuongeza juhudi katika mpango wa ujirani mwema kwa kuwashirikisha wanajamii wanaoishi pembezoni mwa hifadhi zote huku shirika likisaidia miradi mbalimbali ya kijamii.
“Miradi hii wanaibua wananchi wenyewe, hatuwezi kwenda kuwajengea vyoo wakati mahitaji yao ni zahanati. Kwa kufanya hivi tunataka kujenga ushirikiano wa karibu na kuwaelimisha wanajamii kwamba maliasili hizi ni za Watanzania wote,” anasema.
Tanapa, kupitia program hiyo, inachangia asilimia 70 kwenye miradi yote ya kijamii, wakati asilimia 30 ni nguvukazi za wananchi husika na Mbugi anasema, “…Katika kipindi cha miaka 10, yaani kuanzia 2003/2004 – 2012/2013, shirika hilo limetoa jumla ya Shs. 13,848,784,463.19 kusaidia miradi 1,003 ya jamii. 
Katika mwaka wa fedha 2003/2004, Tanapa ilifadhili miradi 94 iliyogharimu Shs. 805,821,034.24; mwaka 2004/2005 jumla ya Shs. 618,502,682.95 zilitumika katika miradi 60; mwaka 2005/06 jumla ya Shs. 865,860,778 zilitumika katika miradi 65; mwaka 2006/07 jumla ya Shs. 1,212,619,300 zilitumika katika miradi 90; mwaka 2007/08 walitumia Shs. 3,447,154,353 katika miradi 141; na mwaka 2008/09 walitumia Shs. 1,736,751,235 katika miradi 87.
Aidha, kwa mwaka wa fedha 2009/10 walifadhili miradi 98 iliyogharimu Shs. 2,320,893,785; mwaka 2010/11 walitumia Shs. 536,136,868 kugharamia miradi 33; mwaka 2011/12 walitumia Shs. 744,244,212 kugharamia miradi 26 na mwaka 2012/13 walitumia Shs. 1,560,800,212 katika miradi 36 ya jamii.
Fedha hizo, anasema, zinatokana na asiliamia ya mapato yatokanayo na hifadhi hizo, “…hasa baada ya kutoa gharama za bajeti ya idara husika.”
Ufadhili huo wa Tanapa, anasema Mbugi, umesaidia kupunguza migogoro baina ya hifadhi na wananchi na pia umepromoti uhifadhi wa mazingira huku mpango ukisaidia kuibua ajira kwa kusaidia makundi mbalimbali ya jamii.
Mpango wa Ujirani Mwema, awali ukijulikana zaidi kama Huduma za Uhifadhi kwa Jamii (CCS) ulianzishwa mwaka 1985 kufuatia mkutano uliofanyika Seronera ambao ulikuwa na madhumuni ya kujadili masuala ya Mpango wa Ikolojia katika Hifadhi ya Serengeti.
Katika mkutano huo ilielezwa kwamba, wanyama wengi walikuwa wanatoweka kwa sababu ya uwindaji haramu ambapo ilibainishwa kwamba Nyati walikuwa wamepungua kutoka 70,000 hadi 40,000 katika hifadhi hiyo.
“Tembo walikuwa wamepungua kutoka 2,500 hadi 500 wakati Faru walipungua kutoka 1,000 hadi 20 tu,” anasema Mbugi na kuongeza kwamba hali hiyo ilichangiwa kwa kiasi kikubwa na ujangili uliofanywa na wananchi wa maeneo yanayozunguka hifadhi kwa matumizi ya nyumbani na biashara.
Anaongeza kwamba, malengo ya program hiyo ni kuongeza uhusiano mwema kati ya hifadhi na jamii na kuhakikisha maslahi ya Tanapa yanahubiriwa katika ngazi zote kwa kutoa taarifa katika vijiji husika.
Mpaka sasa Tanapa inasimamia hifadhi 15 ambazo ni Arusha, Gombe, Katavi, Kilimanjaro, Kitulo, Mahale, Lake Manyara, Mikumi, Mkomazi, Ruaha, Rubondo, Saadani, Serengeti, Tarangire, na Udzungwa.
Hifadhi zote hizo zinazungukwa na jumla ya mikoa 28, wilaya 52 na vijiji 536 huku hifadhi za Kilimanjaro na Serengeti zikizungukwa na vijiji 88 kila moja.


0656-331974

No comments:

Post a Comment