Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday, 25 September 2015

LICHA YA VUGUVUGU KUBWA, HIZI NDIZO SABABU 10 ZA CCM KUSHINDA 2015

 
John Magufuli mara baada ya kupitishwa na CCM kugombea Urais Julai 12, 2015.
Na Daniel Mbega
KIMBUNGA kimepita ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na kwa kiasi kikubwa kimekitikisa chama hicho kikongwe barani Afrika.
Kuondoka kwa Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kwenda Chadema na hatimaye kuteuliwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumeitikisa CCM hasa kutokana na wimbi la makada wengi walioondoka pamoja naye.
Awali CCM iliamini kwamba, baada ya kumaliza zoezi la kumpata mgombea wake wa urais Julai 12 mjini Dodoma, basi kazi ingekuwa rahisi zaidi, lakini kwa uhakika imekuwa ngumu na kuiyumbisha ingawa badoina nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Blogu hii ya www.brotherdanny.com leo inachambua baadhi ya sababu 10 ambazo bado zinaipa nafasi kubwa CCM ya kushinda Oktoba licha ya vuguvugu kubwa la mabadiliko lililopo:

1. Ukongwe wake
Daima huwa napenda kusema; “Ukubwa wa umri, ni ujana wa umahiri”. Kwa kawaida kadiri mtu anavyozeeka ndivyo anavyozidi kuwa na busara na ndiyo sababu daima huwa tunakimbilia kwa wazee ili kupata ushauri.
Ukiacha Frelimo ya Msumbiji na ANC ya Afrika Kusini, CCM ndicho chama pekee kikongwe zaidi Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ambacho bado kipo madarakani.
Katika uhai wake chama hiki kimesaidia ukombozi wanchi nyingi barani Afrika, kimewapika na kuwatengeneza wanamapinduzi wengi ambao wamepata nab ado wanaendeelea kuongoza nchi zao.
Kimesaidia chaguzi nyingi barani humo, zikiwemo zile ambazo mageuzi yamefanyika, kutokana na kujua propaganda.
Ukongwe huo, wa kujua mbinu za jukwaani na za medani, bado unakipa kete nzuri zaidi za kushinda uchaguzi na wimbi la sasa la upinzani linaweza kukikomaza zaidi.

2. Kukubalika vijijini
Licha ya upinzani kuonekana kupata nguvu ghafla baada ya ujio wa Lowassa, lakini inaonekana vyama hivyo vina nguvu zaidi kwenye miji ambako wimbi la mabadiliko kwa vijana, hasa wasomi, ni kubwa.
Hata hivyo, CCM inakubalika zaidi vijijini ambako ndiko waliko Watanzania takriban asilimia 83. Sehemu nyingine huko vijijini bado wanaamini Rais wa Tanzaniani Mwalimu Julius Nyerere na chama pekee cha siasa ni CCM, hivyo linapokuja suala la upinzani hata hawajishughulishi nalo.
Nakumbuka safari moja Chadema katika operesheni zao nyingi walikwenda na helikopta katika Kijiji cha Songambele wilayani Kongwa katika Mkoa wa Dodoma. Umati mkubwa ulifika pale na kuizunguka helikopta. Haukujishughulisha kabisa na hotuba ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliyokuwa akiitoa.
Ikabidi aulize: “Mmekuja kunisikiliza au kutazama helikopta?” Wakamjibu: “Tumekuja kutazama helikopta!!” Akaingia kwenye helikopta na kuelekea Kibaigwa. Mkutano ukaishia hapo. Iko mikoa ambako upinzani hauwezi kugusa, miongoni mwake ni Mkoa wa Dodoma, ingawa kama watajitahidi safari hii wanaweza walau kupata hata jimbo moja.
Kwa hiyo ni wazi kwamba CCM, pamoja na mtikisiko uliotokea, siyo tu kwamba bado kina wanachama wengi, bali kinakubalika sana vijijini ambako wananchi wanatambua mchango wa chama hicho kuliko kelele nyingi za wapinzani, ambao wengi ama hawajawahi kufika huko kunadi sera zao au bado wananchi wana mashaka ya kuwakabidhi wapinzani serikali.

3. Ukigeugeu wa wapinzani
Hii ni silaha kubwa kwa CCM safari hii kuelekea uchaguzi mkuu na kitaitumia agenda hiyo kuwamaliza wapinzani kutokana na ukigeugeu wao.
Kama wapinzani ndio waliotangaza kwamba Lowassa ni fisadi, CCM wao watasema, pamoja na kutomshughulikia kwa kukosa ushahidi, lakini waliamua kumwengua kwenye mbio za urais kwa tuhuma hizo hizo zilizotajwa na wapinzani wenyewe.
Lakini kinyume chake, wapinzani waliomwita fisadi, leo hii wamemtakasa na kumuona anang’ara kama yakuti kiasi kwamba wameyageuka maneno na matamko yao wenyewe ambayo kwa miaka kadhaa ulikuwa ni wimbo usio na vina, urari, mizani wala kiitikio.
Ni silaha hiyo hiyo ambayo wapinzani wenyewe awali walikuwa wamepanga kuimaliza CCM ikiwa ingempitisha Lowassa kugombea.
Kwamba, kama wapinzani wenyewe walijiapiza kutopokea ‘makapi’ ya CCM, iweje sasa wamegeuka kuwa jalala ambalo mizoga na masazo yote yanatupwa humo?

4. Kujitenga kwa Slaa, Lipumba
Dk. Wilbrod Slaa, Katibu Mkuu wa Chadema, ametengwa rasmi na chama chake baada ya yeye mwenyewe kujitenga tangu chama hicho kilipotangaza kumkaribisha Lowassa. Hajaonekana na hajazungumza lolote licha ya mwenyekiti wake, Mbowe, kusikika akisema kwamba Ukawa utaendelea na kwamba Dk. Slaa amepumzika.
Kimya chake kinaonyesha kwamba mambo hayako sawa na inaelezwa kwamba Dk. Slaa alipinga sana kukaribishwa kwa Lowassa ndani ya chama hicho lakini Mbowe na wenzake wakamkatalia.
Nafsi inamsuta Dk. Slaa kwa sababu ni yeye ambaye Jumamosi ya Septemba 15, 2007 alisimama jukwaani pale Mwembeyanga, Temeke na kumtaja Lowassa katika ile Orodha ya Mafisadi kwamba ni fisadi anayeitafuna nchi, sasa akiwa ndani wanawezaje kuketi pamoja?
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Nguyulu Ibrahim Haruna Lipumba, naye amejivua wadhifa huo aliodumua nao tangu mwaka 1994 walipomtoa James Mapalala kwenye mkutano ule wa Mkonge Hotel, Tanga.
Sababu amezitaja, kwamba wenzake, hasa Chadema, wamekiuka makubaliano waliyojiwekea wakati wanaunda umoja huo wa kutowapokea mafisadi, ambao sasa wameonekana kunyenyekewa zaidi.
Kabla ya hapo alikuwa amejitenga baada ya kuona kuna dalili za kumkaribisha Lowassa, ndiyo maana akatangaza kwamba angegombea urais kupitia CUF, lakini alirejeshwa siku moja tu kabla ya Lowassa kutambulishwa rasmi.
Nafsi yake imemsuta, kama alivyosema mwenyewe, kwamba maazimio yalikuwa kutowapokea hao mafisadi, kinyume chake wanachama wengi wamekimbilia huko Ukawa, na hasa Chadema.
Dk. Slaa na Lipumba bado ni wanasiasa wenye nguvu na wana wafuasi wengi. Hoja alizozitoa Lipumba zinaweza kuwa na mantiki siyo tu kwa wanachama wa CUF, bali hata kwa Watanzania wengine ambao walikuwa wamezolewa na kimbunga hicho.
Slaa naye hajasema lolote, lakini ukimya wake umekwishaleta ufa mkubwa ndani ya Ukawa na hata kama leo atatokea na kutamka kwamba yuko pamoja na umoja huo, tayari atakuwa ameyumbisha harakati.

5. Nguvu ya fedha
Licha ya ukweli kwamba Chadema na Ukawa safari wako vizuri kifedha kutokana na ujio wa Lowassa ambaye bado anaweza kuwatumia ‘marafiki zake kumchangia’, lakini CCM bado ina nguvu ya fedha, ambacho ni kigezo muhimu katika kufanikisha kampeni na kupata ushindi katika siasa za ushindani.
Bila fedha katu huwezi kufika kila kona ya nchi, na maeneo mengi hayafikiki kirahisi ila kwa gharama kubwa.
Kama chama kinataka kuungwa mkono, ni lazima viongozi na wagombea watembelee maeneo mbalimbali nchini kujinadi kwa wananchi.
Vyama vyote vinavyoshiriki katika uchaguzi vinakidhi kigezo hiki, ingawa kuna tofauti kubwa. Vyama vitatu kati ya vinne vinavyounda Ukawa vinapata ruzuku kutoka serikalini kutokana na kuwa na wabunge.
Lakini CCM ndiyo inayoongoza kwa kupewa kiasi kikubwa cha fedha kama ruzuku, kwani inapata takriban Shs. 800 milioni kwa mwezi, Chadema inapata Shs. 203.6 milioni, CUF inapata Shs. 117.4 milioni na NCCR-Mageuzi Shs. 10 milioni.
Ukiachilia mbali fedha za ruzuku, bado CCM ina vitegauchumi vingi na wafadhili wengi wakiwamo wafanyabiashara wakubwa nchini, tofauti na wapinzani.

6. Mtandao wa wanachama
Pamoja na kwamba CCM bado inakubalika katika maeneo mengi vijijini na licha ya wanachama kuondoka, lakini chama hicho bado kina mtaji wa wanachama nchi nzima kutokana na mtandao wake imara uliojengwa tangu kipindi cha mfumo wa chama kimoja.
Mfumo wa CCM ni kuanzia ngazi ya shina (mabalozi wa nyumba kumi), mtindo unaokiwekea mazingira mazuri ya kujikusanyia wanachama wa uhakika katika maeneo mengi ya nchi, hususan vijijini ambako upinzani umeshindwa kupenya kwa kiasi kikubwa.
Japokuwa Chadema imeiga mfumo huo wa mashina, lakini mafanikio yake hayawezi kulinganishwa na CCM.

7. Demokrasia ndani ya vyama
Pamoja na madai ya matumizi makubwa ya fedha na vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi, mfumo wa uongozi wa CCM unaonekana kuwa wa kidemokrasia zaidi kulinganisha na ule wa vyama vya upinzani.
CCM pekee ndicho chama ambacho viongozi wake wana utamaduni wa kuachiana madaraka kwa njia ya kidemokrasia kila baada ya miaka fulani.
Wakati CCM ikiweka bayana katika Katiba yake vipindi viwili vya uongozi, kwa vyama vya upinzani hakuonekani kuwapo kwa demokrasia hiyo, baadhi yao tangu vianzishwe viongozi wa kitaifa ni walewale.
Vyama vyote vinavyounda Ukawa havina ukomo wa madaraka na viongozi wake wote wa taifa, wamedumu kwenye uongozi kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano.
Tazama CUF, ambako kama Ukawa wasingevuruga makubaliano, basi Lipumba angeendelea kuwa mwenyekiti kwa kipindi kirefu zaidi licha ya kuongoza chama hicho kwa miaka 16 sasa.
Ndani ya Chadema kumekuwa na tuhuma za ubabe na ‘u-kanda’ na inapotokea mtu mwingine anataka kugombea uongozi, huanza kushambuliwa kama ilivyotokea kwa Zitto Kabwe mwaka 2009. Tuhuma zilizotolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho aliyejiuzulu, Dk. Wilbrod Slaa, zimetia ufa mkubwa kwenye chama na umoja huo kwa ujumla, licha ya viongozi wa Chadema kufumba macho na kujibu hoja kwa 'masimango'. Hoja za Dk. Slaa hazijajibiwa mpaka sasa, wafuasi wa mageuzi wanatukana badala ya kujibu.
NCCR nako mambo ni yale yale. Makamu Mwenyekiti na Katibu Mkuu wameachia ngazi kwa sababu makubaliano ndani ya Ukawa yamekiukwa. Chadema imepewa majimbo mengi na chama hicho kina majimbo machache. 
Kama kawaida, kila anayeondoka ndani ya Ukawa, ama anayekosoa mwenendo mzima, ama ataambiwa amehongwa, amenunuliwa au anatumiwa na 'maCCM' kama wenyewe wanavyoita. Uhuru wa kidemokrasia haupo, na mtaji wanaojivunia wa vijana ambao wengi wao umri wao ni mdogo kuliko hata umri wa mfumo wa vyama vingi, ndio unawapa kiburi wapinzani hawa kiasi kwamba, hoja za msingi zinapuuzwa na wanachotaka ni mabadiliko tu - siyo kingine.
Hii ni turufu kwa CCM, kwa sababu wanaoondoka nao wana wafuasi wao, wanaweza kuwa wameondoka nao na hata kama hawataipigia kura CCM, bado watavipigia vyama vingine na hivyo kupunguza idadi ya kura za Ukawa.

8. Hakuna Tume huru
Kilio cha muda mrefu cha kuwepo kwa Tume huru ya Uchaguzi bado hakijapatiwa majibu na kwa vile CCM ndiyo imeshika Dola na Tume hiyo iko chini ya serikali yake, kushindwa kwa wapinzani kwenye urais itakuwa ndoto ambayo itahitaji miujiza ili iwe ya kweli.
Rais ni wa CCM na ndiye anayeteua viongozi wa Tume, ambao wanalipwa na serikali hiyo hiyo ingawa fedha hizo ni kodi za wananchi. Huwezi kutegemea kwamba kutakuwa na haki sawa kwa asilimia zote kamaambavyo ingekuwepo Tume huru. Hiki ni kitanzi kwa wapinzani linapokuja suala la kwenda Magogoni.

9. Mahusiano ya kimataifa
Ingawa zipo propaganda kwamba mataifa mengi, hasa ya Ulaya, ‘yameichoka’ CCM, bado hakuna ukweli wowote kwa sababu chama hicho kimejenga misingi ya muda mrefu ya mahusiano mazuri ya kimataifa.
Chadema au Ukawa wanaweza kuwa na vyama washirika katika baadhi ya mataifa ya Ulaya, lakini CCM ina ushirika mzuri na serikali, siyo vyama pekee, jambo ambalo ni mtaji mwingine mnono hasa linapokuja suala la uchaguzi kama hili.
Kama ilivyo kwa wapinzani, ambao vyama washirika lazima vitakuwa na maslahi fulani, vivyo hivyo kwa CCM kuna mataifa ambayo mpaka sasa yana maslahi ndani ya Tanzania kutokana na uwekezaji katika sekta mbalimbali, iwe serikali zamataifa hayo ama kampuni zinazotoka huko.
Urusi imewekeza kwenye Uranium, Canada imewekeza kwenye dhahabu, Afrika Kusini kwenye miradi mingi ikiwemo Tanzanite, Marekani na Uingereza kwenye mafuta na gesi kama ilivyo kwa China ambayo pia imewekeza kwenye chuma na makaa ya mawe.
Kwa kuzingatia uwekezaji huo, mataifa haya hayawezi kuwa na uhakika wa serikali ijayo ya wapinzani ikiwa maslahi yao yatakuwa salama au la, na kwa vile wapinzani wamekuwa wakipiga kelele kuhusu mikataba ya uwekezaji, siyo rahisi kwao kuamini kwamba watakuwa salama.

10. Muungano
Hoja ya kudumishwa kwa Muuungano itanadiwa zaidi na CCM hasa Zanzibar na kuwaeleza kwamba ikiwa wapinzani watachukua madaraka, basi Muungano utavunjika. Na ikiwa Muungano wa Zanzibar na Tanganyika utavunjika, basi hata Zanzibar haitakuwepo kwa sababu itagawanyika kuwa Pemba na Unguja!
Haya yako dhahiri na yangeweza kunadiwa zaidi kama zoezi la Kura ya Maoni kuhusu Katiba Pendekezwa lingekuwepo, kwani wapo wengi wanaotamani Serikali Tatu ndani ya Muungano lakini siyo muundo kama wa sasa.
Tusubiri na tuone kitakachotokea.


0656-331974

No comments:

Post a Comment