Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Tuesday, 29 September 2015

MAKAMU WA RAIS DK. BILAL ACHANGISHA SHS. 105 MILIONI KUHIFADHI VYANZO VYA MAJI MILIMA YA TAO LA MASHARIKI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi Tuzo Maalum, Mshauri wa kampuni ya VIP Engineering & Marketing, Fr. James Rugemalira, wakati wa hafla ya Uchangishaji fedha kwa Uhifadhi wa vyanzo vya maji katika Mabwawa ya kuzalisha Umeme ya Mtera, Kihansi, Kidatu, Nyumba ya Mungu na Pangani, iliyofanyika jana usiku Sept 28, 2015 kwenye Hoteli ya Kilimanjaro, jijini Dar es Salaam. Picha zote na OMR

Na Daniel Mbega wa www.brotherdanny.com
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib Bilal, amewaomba wadau wa maendeleo na uhifadhi wa mazingira kuisaidia taasisi ya Mfuko wa Udhamini wa Hifadhi ya Milima ya Tao la Mashariki (EAMCEF) ili kufanikisha uhifadhi wa vyanzo vya maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme nchini.
Dk. Bilal aliyasema hayo jana usiku wakati wa Chakula cha Hisani cha uchangiaji wa mfuko huo wa EAMCEF katika Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro jijini Dar es Salaam ambapo alifanikiwa kuchangisha jumla ya Shs. 105.6 milioni.
“Napenda kuchukua nafasi hii kuwaomba wadau wote: taasisi mbalimbali, sekta binafsi, wafanya biashara na washirika wa maendeleo waendelee kuunga mkono uhudi hizi za kuhifadhi misitu ya Milima yaTao la Mashariki kwa kutoa michango ya hali na mali,” alisema.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akihutubia wakati wa hafla ya Uchangishaji fedha kwa Uhifadhi wa vyanzo vya maji katika Mabwawa ya kuzalisha Umeme ya Mtera, Kihansi, Kidatu, Nyumba ya Mungu na Pangani. Hafla hiyo ilifanyika jana usiku Sept 28, 2015 kwenye Hoteli ya Kilimanjaro, jijini Dar es Salaam. 

Makamu wa Rais alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuunga mkono juhudi za EAMCEF ili kuhakikisha kuwa misitu hiyo muhimu kitaifa na kimataifa inaendelea kuchangia ustawi na uboreshaji wa maisha ya jamii na ukuaji wa uchumi wa taifa.Aliwashukuru wadau wote waliochangia katika hafla hiyo na kuwaomba “wadau wengine waige mfano huu mzuri mliouonyesha jioni hii… napenda kuwaomba wale wote walioahidi kutimiza ahadi zao kwani kwa kufanya hivyo mtasaidia kufanikisha mipango iliyokwisha wekwa tayari.”
Katika chakula hicho cha hisani, wadau waliochangia na kiasi cha fedha kikiwa kwenye mabano ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania – TCRA (Shs. 5 milioni), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (Shs. 10 milioni), Wakala wa Nishati Vijijini – REA (Shs. 6 milioni), Kampuni ya IPTL-PAP (Shs. 10 milioni), Songas (Shs. 13 milioni), VIP Engineering & Marketing (Shs. 50 milioni) na waratibu wa shughuli hiyo kampuni ya Regalia Media Consult ambayo imechangisha Shs. 1.2 milioni.
Aidha, katika kufanikisha shughuli hiyo, kampuni ya Mabibo Beer, Wines and Spirits ilichangia vinywaji vyenye thamani ya Shs. 2.1 milioni, ITV na Radio One walichangia matangazo yenye thamani ya Shs. 640,000 na Hoteli ya Hyatt Regency walichangia ukumbi na chakula vyote vikiwa na thamani ya Dola 3,000 (takriban Shs. 6.6 milioni).
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi Cheti, Mwenyekiti wa Mabibo Beer, Wines & Spirits na Mkurugenzi wa VIP Engineering Marketing Ltd, Benedicta Rugemalira, wakati wa hafla ya Uchangishaji fedha kwa Uhifadhi wa vyanzo vya maji katika Mabwawa ya kuzalisha Umeme ya Mtera, Kihansi, Kidatu, Nyumba ya Mungu na Pangani, iliyofanyika jana usiku Sept 28, 2015 kwenye Hoteli ya Kilimanjaro, jijini Dar es Salaam. 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi Cheti, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya IPTL, Parthiban Chandrasakaran,  wakati wa hafla ya Uchangishaji fedha kwa Uhifadhi wa vyanzo vya maji katika Mabwawa ya kuzalisha Umeme ya Mtera, Kihansi, Kidatu, Nyumba ya Mungu na Pangani, iliyofanyika jana usiku Sept 28, 2015 kwenye Hoteli ya Kilimanjaro, jijini Dar es Salaam. 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi Cheti, Mkuu wa Idara ya Fedha na Utwala wa REA, George Nchwale,  wakati wa hafla ya Uchangishaji fedha kwa Uhifadhi wa vyanzo vya maji katika Mabwawa ya kuzalisha Umeme ya Mtera, Kihansi, Kidatu, Nyumba ya Mungu na Pangani, iliyofanyika jana usiku Sept 28, 2015 kwenye Hoteli ya Kilimanjaro, jijini Dar es Salaam. 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi Cheti, Mkurugenzi wa Sheria wa TCRA, Elizabeth Nzagi,  wakati wa hafla ya Uchangishaji fedha kwa Uhifadhi wa vyanzo vya maji katika Mabwawa ya kuzalisha Umeme ya Mtera, Kihansi, Kidatu, Nyumba ya Mungu na Pangani, iliyofanyika jana usiku Sept 28, 2015 kwenye Hoteli ya Kilimanjaro, jijini Dar es Salaam.

Katika tukio hilo, pia kulifanyika mnada wa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na jamii zinazozunguka misitu hiyo ambazo zimenufaika na miradi ya kijamii inayofadhiliwa na EAMCEF ambapo jumla ya Shs. 4.65 milioni zilikusanywa.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa EAMCEF, Francis Sabuni, alisema kwamba uhifadhi wa Misitu ya Milima ya Tao la Mashariki ni muhimu kijamii, kitaifa na hata kimataifa kwani ndiko kuliko na vyanzo vyote vya maji vinavyotegemewa na mabwawa makubwa matano yanayozalisha umeme nchini Tanzania ambayo ni Mtera, Kihansi, Kidatu, Nyumba ya Mungu, Hale na Pangani.
Sabuni alisema, Milima ya Tao la Mashariki ina eneo la ardhi lenye ukubwa wa takriban kilometa za mraba 5,350 ambalo liko kwenye wilaya 15 ndani ya mikoa mitano.
“Mkoa wa Kilimanjaro kuna Milima ya Upare Kaskazini na Kusini iliyoko katika wilaya za Mwanga na Same; Mkoa wa Tanga kuna Milima ya Usambara Magharibi na Mashariki pamoja na Milima ya Nguu katika wilaya za Lushoto, Korogwe, Muheza, Mkinga na Kilindi na Mkoa wa Dodoma kuna wilaya ya Mpwapwa iliko Milima ya Rubeho,” alisema.
Mikoa mingine ni Morogoro ambako kuna Milima ya Nguru, Uluguru, Ukaguru, Udzungwa, Malundwe, Mahenge na Rubeho ambayo iko katika wilaya za Morogoro, Mvomero, Kilosa, Kilombero, Ulanga na Manispaa ya Morogoro, pamoja na Mkoa wa Iringa wenye Milima ya Udzungwa iliyoko kwenye wilaya za Kilolo na Mufindi.
Kwa mujibu wa Sabuni, Milima ya Tao la Mashariki inaunda ukanda wa milima uliopo Mashariki mwa Afrika ambao unatambuliwa duniani kama moja ya maeneo 34 yenye utajiri mkubwa wa bioanuwai na kwa kuwa na viumbe ndwele wengi wanaokabiliwa na tishio la kutoweka.
Bioanuwai ya milimahiyo inatajwa kuwa na manufaa makubwa kijamii katika kupunguza athari za umaskini ambapo mazao ya misitu kama kuni, mbao, madawa ya asili, matunda pori na aina nyingine za vyakula yanakadiriwa kuchangia takriban asilimia 40 ya mahitaji yote ya kaya katika baadhi ya jamii zinazopakana na milima hiyo.
Misitu ya milima hiyo ndiyo vyanzo vikuu pia vya maji ambavyo kwa ujumla hutoa maji kwa matumizi ya viwanda vikubwa nchini pamoja na baadhi ya wananchi wanaokadiriwa kufikia asilimia 25 ya Watanzania wote wanaoishi katika miji ya Iringa, Kilolo, Mufindi, Mpwapwa, Morogoro, Kilosa, Gairo, Mvomero, Mahenge, Ifakara, Muheza, Chalinze, Korogwe, Lushoto, Mwanga, Same, Soni, Mikumi, Kilindi, Handeni, Kibaha pamoja na majiji ya Tanga na Dar es Salaam.
Uzalishaji wa umeme nchini Tanzania unategemea zaidi ustawi wa milima hiyo kwani maji yanayopatikana huko ndiyo hutumika kuzalisha asilimia 90 ya nishati hiyo inayotumia nguvu za maji, ambapo inakadiriwa kwamba asilimia 50 ya umeme wote unaotumika nchini Tanzania huzalishwa katika mabwawa hayo matano yaliyotajwa.
Sabuni anasema, kwa sababu ya kuwa na ardhi yenye rutuba pamoja na mvua za kutosha, milima hiyo ni maarufu kwa kilimo kikubwa cha mpunga, miwa, chai, na kahawa na hivyo kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kufikiwa kwa malengo ya mikakati ya Serikali ya Kilimo Kwanza, SAGCOT na Matokeo Makubwa Sasa (BRN), huku pia ikiwa kivutio kikubwa cha utalii kutokana na kuwa na viumbe ndwele wengi.
“Mto Ruvu ndicho chanzo kikubwa cha maji katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine, lakini chanzo chake ni Milima ya Uluguru mkoani Morogoro, hivyo bila kuilinda Dar es Salaam itakosa maji na hivyo kuikosesha Tanzania asilimia zaidi ya 70 ya pato lake la taifa kwani maji ya mto huo mbali ya kutumiwa na wanajamii kwa shughuli mbalimbali, lakini pia hutumika viwandani kwa uzalishaji mkubwa wa bidhaa,” anasema Sabuni.
Hata hivyo, inaelezwa kwamba, katika kipindi cha miaka 200 iliyopita, asilimia 70 ya misitu ya Milima ya Tao la Mashariki ilitoweka na kama hali hiyo haitadhibitiwa, kiasi cha misitu kilichobaki kinaweza kutoweka kabisa katika miaka 20 ijayo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi Cheti, Mwakilishi wa ITV na Radio One, wakati wa hafla ya Uchangishaji fedha kwa Uhifadhi wa vyanzo vya maji katika Mabwawa ya kuzalisha Umeme ya Mtera, Kihansi, Kidatu, Nyumba ya Mungu na Pangani, iliyofanyika jana usiku Sept 28, 2015 kwenye Hoteli ya Kilimanjaro, jijini Dar es Salaam.
Wageni mbalimbali waliohudhuria hafla ya Uchangishaji fedha kwa Uhifadhi wa vyanzo vya maji katika Mabwawa ya kuzalisha Umeme ya Mtera, Kihansi, Kidatu, Nyumba ya Mungu na Pangani, iliyofanyika jana usiku Sept 28, 2015 kwenye Hoteli ya Kilimanjaro, jijini Dar es Salaam. 

Katika kukabiliana na tishio hilo, EAMCEF inashirikisha jamii zinazoizunguka misitu hiyo katika uhifadhi ambapo hutenga asilimia 50 ya rasilimali zake za ufadhili kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya kijamii.
“Mfuko unafadhili miradi mbalimbali kwenye Halmashauri za Wilaya 11 ikilenga misitu 9 ya Hifadhi za Mazingira Asilia za Chome na Magamba (Same, Lushoto, Korogwe); Hifadhi za Mazingira Asili za Amani na Nilo (Korogwe, Muheza, Mkinga); Hifadhi za Mazingira Asili za Uluguru na Mkingu (Morogoro Manispaa, Morogoro na Mvomero); Hifadhi za Mazingira Asili za Udzungwa Scaep (Kilombero) na Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa (Mufindi, Kilolo na Kilombero),” anafafanua Sabuni.
Sabuni alieleza kwamba, tangu kuanzishwa kwake, EAMCEF imefadhili zaidi ya miradi 200 yenye thamani ya zaidi ya Shs.3.4bilioni ambapo miti zaidi ya milioni 18 imepandwa katika hekta zaidi ya 10,000 kwenye maeneo mbalimbali ya milima hiyo.
“Miradi hiyo katika vijiji zaidi ya 130 ni pamoja na ufugaji wa mbuzi wa maziwa zaidi ya 250, ng’ombe wa maziwa zaidi ya 30, kuku zaidi ya 1,000, nguruwe zaidi ya 100, ufugaji nyuki zaidi ya mizinga ya kisasa 800, majiko banifu zaidi ya 5,000, uwekaji na uimarishaji wa mipaka ya misitu ya hifadhi zaidi ya kilometa 2,000 na kadhalika,” anasema Sabuni.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya EAMCEF, Profesa Gerald Monela, aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kubuni na kuanzisha mfuko huo, kwani kulinda bioanwai zilizoko kwenye misitu ya milioma hiyo ni muhimu zaidi.
“Bioanwai zinazopatika kwenye misitu hii ni adimu na hazipatikani sehemu nyingine duniani, lakini misitu hii ni muhimu kwa upatikanaji wa maji, hivyo ni muhimu sana kuitunza na kuilinda,” alisema.
Profesa Monela aliwashukuru wadau wote waliochangia na kuwaomba wadau wengine kujitokeza ili kuunga mkono uhifadhi wa misitu hiyo muhimu kwa ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla.


No comments:

Post a Comment